Somo la 3: Kaini na Hiba (Legacy) Yake

Mwanzo 4
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
2
Lesson Number: 
3

Somo la 3: Kaini na Hiba (Legacy) Yake

 

(Mwanzo 4)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Kisa cha Kaini kinavunja moyo. Kama wewe ni mzazi, au unapanga kuwa mzazi, una matumaini makubwa na ndoto kubwa kwa ajili ya watoto wako. Kama wataanguka, unaweza kujilaumu. Mungu ni Muumbaji - baba wa Adamu na Eva. Walianguka. Adamu na Eva, huku wakiwa wameumbwa wakiwa wakamilifu, wanaona maafa makubwa kwa vijana wao wawili wa kwanza wa kiume. Hebu tuzame kwa kina kwenye kisa cha Kaini katika kitabu cha Mwanzo ili tuone tunaweza kupata mafunzo gani!

 

    I. Tumaini

 

        A. Soma Mwanzo 4:1 na Mwanzo 3:15-16. Fikiria wewe ni Adamu na Hawa, na hii ndio mara ya kwanza mtoto amezaliwa. Utakuwa na mwitiko (reaction) gani?

 

            1. Angalia tena Mwanzo 3:15. Ahadi gani ilitolewa juu ya “uzao” wa Eva? (Kwamba “utakiponda” kichwa cha Shetani.)

 

            2. Angalia tena Mwanzo 4:1. Kuna mabishano juu ya namna kifungu hiki kinavyopaswa kutafsiriwa. Jinsi tafsiri ya ESV (tafsiri ya Biblia ninayoitumia kwa sasa kwa ajili ya masomo haya) inavyokitafsiri kifungu hicho ni kawaida miongoni mwa tafsiri nyinginezo – dhana iliyopo ni kwamba Mungu alimsaidia Eva alipokuwa anamzaa Kaini. Albert Barnes anabainisha kuwa kinaweza kutafsiriwa kama “nimempata mtoto mwanamume, jina lake Yahweh.” Tafsiri hii mbadala inaashiria nini? (Kwamba Kaini alikuwa Masihi aliyeahidiwa ambaye angekiponda kichwa cha Shetani.)

 

                a. Jiweke kwenye nafasi ya Eva. Je, yumkini, au inawezekana kwamba aliamini kuwa Kaini ndiye yule aliyeahidiwa? (Ingeendana na tumaini kusahihisha dhambi yake mapema iwezekanavyo.)

 

                b. Barnes anajenga hoja dhidi ya tafsiri inayoashiria kwamba Eva alidhani kuwa mwanaye ni Masihi, kwa sababu anasema kuwa Eva angemwita “Yahweh” au tofauti na Yahweh. Badala yake, jina la Kaini linamaanisha jambo tofauti. Hivyo, Barnes anakubaliana na tafsiri ya ESV na tafsiri nyinginezo nyingi zinazofikisha ujumbe ule ule.)

 

        B. Soma Mwanzo 4:2 na uilinganishe na Mwanzo 3:17-19. Nani anayefanya kazi iliyoelezewa na Mungu? (Kaini anailima ardhi. Habili si mkulima.)

 

            1. Jina la Habili linamaanisha “pumzi, kisicho muhimu” kwa mujibu wa Barnes. Kazi ya Habili inachangia nini katika kuitegemeza familia? (Haichangii sana. Walikuwa wala mbogamboga (vegetarians), wala mimea! Linganisha Mwanzo 1:29 na Mwanzo 9:3. Habili alikuwa anatengeneza mavazi. Angalia Mwanzo 3:21.)

 

            2. Kama ungekuwa Kaini, je, ungekubaliana kwamba jina la Habili (Pumzi, kisicho muhimu) linaendana na kazi yake? Hafanyi kazi ngumu ya kukwatua ardhi na halishi familia?

 

            3. Unadhani Adamu na Eva waliwachukuliaje Kaini na Habili? (Kitabu cha Mwanzo kinatoa taswira inayoimarisha dhana ya kwamba tumaini lao lilikuwa kwa Kaini.)

 

    II. Mjadala Juu ya Tumaini

 

        A. Soma Mwanzo 4:3-4. Nani anayemtolea Mungu kitu cha thamani kabisa? (Kwa haraka haraka, kutoa chakula unachoweza kukila ni jambo la thamani zaidi. Familia isingeweza kula (au kuvaa) “sehemu zilizonona.”)

 

            1. Litafakari hili kidogo. Kaini anatoa uzima, Habili anatoa mauti, sadaka ya uzima. Jambo gani lina mantiki zaidi kwa mtazamo wa kibinadamu?

 

        B. Soma Waebrania 11:4. Kwa nini kifungu kinasema, “Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora?” (Yumkini Adamu na Eva walidhani kwamba Kaini atakuwa Masihi. Bila shaka ndio maana walimwambia Kaini jambo hili. Lakini ndugu Pumzi na Kisicho Muhimu aliielewa injili na akatoa “dhabihu iliyo bora.”)

 

        C. Soma Mwanzo 4:5. Unadhani hasira ya Kaini inahalalishwa? Tumetoka kujadili sababu zilizoonyesha kuwa dhabihu yake ni bora zaidi. Je, ingekuwa na mantiki kwake kuamini kwamba Mungu ameikataa kazi yake – kazi, kwa mujibu wa wazazi wa Kaini, ya aliyeahidiwa?

 

        D. Soma Mwanzo 4:6-7. Mungu anamuuliza Kaini, “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali?” Mungu anamtaka Kaini afanye nini? Hii inatuambia nini kuhusu mazungumzo ambayo hayakuandikwa katika kitabu cha Mwanzo? (Mungu anamtaka Kaini kutafakari juu ya kilicho sahihi kukitenda. Kutokana na mjadala wetu wa uhalisia wa jambo jema, hilo linatuacha na ushawishi thabiti kwamba Mungu alinena na Adamu, Eva, Kaini, na Habili kuhusu mpango wa wokovu na hitaji la dhabihu za wanyama.)

 

            1. Utaona Mungu anamwambia Kaini kuwa “dhambi iko, inakuotea mlangoni” kwenye hili suala la kutoa dhabihu sahihi. Taarifa hii ya ziada inatuhabarisha nini juu ya uchaguzi wa Kaini? (Hili sio tu suala la Mungu kuelezea dhabihu bora, hili ni suala la dhambi.)

 

            2. Kama tungekuwa na mjadala kwenye kikundi, upande mmoja ungejenga hoja juu ya ahadi ya Kaini, ukweli kwamba kazi yake inaendana na ufafanuzi wa Mungu wa kazi sahihi, na kipengele halisi cha kutoa uhai cha dhabihu yake. Tunapaswa kujifunza nini kutokana na Habili kutajwa katika kitabu cha Waebrania 11 kama shujaa wa imani? (Hii ni taswira inayofaa ya mjadala kati ya matendo na imani. Mengi yanaweza kusemwa katika kuunga mkono kazi ya Kaini, lakini imani katika ahadi ya Mungu inashinda. Kuunga mkono kazi na kuikataa imani ni dhambi.)

 

            3. Angalia tena sehemu ya mwisho ya Mwanzo 4:7. Kaini anaambiwa afanye nini? (Aishinde tamaa yake. Hatuokolewi kwa matendo yetu, bali kufanya uamuzi sahihi ni jambo la muhimu.)

 

    III. Tumaini Limevunjwa

 

        A. Soma Mwanzo 4:8. Unadhani Kaini alimwambia nini Habili? Kaini hana ugonvi na Habili, bali ana ugomvi na Mungu, kwa mujibu wa Mwanzo 4:5-6.

 

            1. Je, umegundua kwamba watu walio mbali na mapenzi ya Mungu wana hasira na wale wanaoenenda kufuatana na mapenzi ya Mungu?

 

        B. Soma 1 Yohana 3:12-13. Hii inatuambia nini kuhusu nia ya Kaini katika kumuua Habili? (Ni kwa sababu Kaini aliamua kutenda uovu kwamba alimchukia Habili kwa kuyatenda mapenzi ya Mungu.)

 

        C. Soma Waebrania 12:24. Damu ya Habili iliyonyunyizwa inalinganishwa moja kwa moja na damu ya Yesu iliyonyunyizwa. Unaona mfanano gani kati ya dhabihu ya Yesu na ile ya Habili? (Wote walikuwa wafiadini (mashahidi) waliouawa na ndugu zao. Habili alikufa kutokana na imani yake katika neno la Mungu. Yeye ni mfano wa uaminifu. Hata hivyo, Yesu, kwa damu yake iliyomwagika anatupatia fursa ya kutambua mustakabali mzuri tulionao kama matokeo ya imani.)

 

        D. Soma Mwanzo 4:9 na Mwanzo 3:9. Utaona kwamba Mungu anawauliza swali Kaini na Adamu anapodhamiria kukabiliana na dhambi zao. Unaichukuliaje njia hii? Je, hii ndio njia tunayopaswa kuifuata?

 

            1. Angalia jibu la Kaini katika sehemu ya mwisho ya Mwanzo 4:9. Jibu hilo linaakisi mtazamo gani? (Kaini hatubu. Anadanganya. Wazazi wake walipotenda dhambi mara ya kwanza, waliwalaumu wengine, lakini hawakukwepa suala la dhambi.)

 

        E. Soma Mwanzo 4:10-12. Unaichukuliaje adhabu ya Mungu kutokana na mauaji? Mauaji ya kwanza! (Ni vigumu kwa Kaini kusema kuwa watu wengine walimshawishi kufanya mauaji. Badala ya kumuua Kaini kwa mauaji aliyoyafanya, Mungu anamzuia asiendelee na kazi yake.)

 

            1. Unadhani maneno “ardhi haitakupa mazao yake” yanamaanisha nini? (Nadhani yanamaanisha kwamba Kaini hataweza tena kukuza mazao, hata akifanya kazi kwa bidii kiasi gani.)

 

            2. Kuna athari gani halisi za Kaini kuwa “mtoro na mtu asiye na kikao duniani?” (Lazima aondoke nyumbani kwao, awaache wazazi wake, na kuacha kila anachokijua, pamoja na kupoteza kazi yake.)

 

        F. Soma Mwanzo 4:13-14. Kaini anaogopa kuuawa, ingawa hakuna kitangulizi (precedent) cha wanadamu kuwaua wenzao. Je, Kaini alihitimisha kuwa atauawa kwa haki kwa sababu aliweka mfano (kitangulizi)?

 

            1. Hii inaashiria kuwa sasa watu wangapi wanaishi duniani? (Soma Mwanzo 1:27-28. Mungu aliwaagiza Adamu na Eva “kuijaza dunia” kwa kuzaa watoto. Kwa dhahiri walikuwa wakifanya hivyo.)

 

            2. Kwa nini Kaini anataka aendelee kuona sura ya Mungu? Je, hiyo isingemkumbusha dhambi yake? (Kaini alifahamu kwamba kuwa na uhusiano na Mungu ilikuwa jambo la thamani sana, hata kama Kaini alikuwa ametenda dhambi ya kutisha. Hii inaashiria kwamba Kaini anaelewa kuwa uwepo wa Mungu huzuia dhambi.)

 

        G. Soma Mwanzo 4:15-16. Kifungu hiki kinazungumzia nini kuhusu Mungu wetu kwamba anamlinda Kaini? (Kwa dhahiri Mungu ni mwenye upendo awapendaye wale walioyakataa mapenzi yake. Mungu anaahidi kisasi kamili (mara saba zaidi) dhidi ya yeyote atakayemuua Kaini.)

 

        H. Soma Mwanzo 4:25. Ni nini ulio mtazamo wa wazazi Adamu na Eva? (Wana tumaini.)

 

        I. Rafiki, kisa cha Kaini kinaonyesha jinsi matumaini makubwa yanavyoweza kupotea kwa haraka sana tena bila sababu za msingi. Kwa kuzingatia dhambi hii kubwa, Mungu anaendelea kuonyesha rehema na kuwapa wanadamu tumaini. Je, utaikumbatia rehema ya Mungu na kushiriki tumaini lake na watu wengine?

 

    IV. Juma lijalo: Gharika.