Bwana wa Sabato

(Mwanzo 2, Kutoka 20, Kumbukumbu la Torati 5, Marko 15)
Swahili
Year: 
2012
Quarter: 
1
Lesson Number: 
7

Utangulizi: Juma lililopita tulijadiliana kwamba sheria ya Mungu inadhamiria kuwa mbaraka kwa wanadamu, sio kitu cha kutufanya tujikwae. Mojawapo ya mbaraka mkubwa wa sheria ni Sabato. Nilipokuwa kwenye shule ya sheria, mpambano ulikuwa mkali. Sio tu kuwa shule ya sheria ilihitajika mtu kusoma kwa bidii, bali pia wanafunzi walifahamu kuwa ubora wa kazi ambayo wangeipata baada ya kumaliza masomo ya shule ya sheria ulitegemea na nafasi yao kimasomo darasani. Baada ya kumaliza mwaka wa kwanza, shule ilikabiliana na shinikizo kubwa kwa kutotoa matokeo kulingana na nafasi aliyoishika mwanafunzi darasani! Nilikuwa na mahala pangu salama pa kujihifadhi, Sabato. Katika siku hiyo sikufanya kazi yoyote ya shule – na niliweza kupata pumziko bila kujisikia hatia! Kwa hakika nilijisikia vizuri sana. Mungu alibariki uaminifu wangu na akanipatia alama nzuri sana. Hetu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi kuhusu Sabato.

  1. Alama za Sabato
    1. Soma Mwanzo 2:1-3. Hapo awali tulijadili mafungu haya kwenye somo letu lililohusu utakatifu wa Mungu. Je, tulisema kitu gani kuhusiana na Sabato kuwa takatifu? (Kuwa takatifu ilimaanisha kuwa iliwekwa wakfu kinyume na siku nyingine zote. Ilibarikiwa. Utakatifu wake ulitokana na kitu kilichofanywa na Mungu, sio kitu chochote tulichokifanya sisi.)
    2. Soma Marko 2:27. Je, unadhani ni kwa nini Mungu aliifanya Sabato? (Ilifanywa kwa ajili yetu. Kimsingi, ilifanywa kuwa siku ya pumziko kwa ajili yetu.)
    3. Soma Kutoka 20:8-11. Je, ni sababu gani nyingine tunayoiona kwa Mungu kuifanya Sabato kuwa takatifu? (Ukumbusho wa uumbaji wa Mungu wa “mbingu na nchi.”)
    4. Soma Kumbukumbu la Torati 5:12-15. Je, ni sababu gani tunayoiona hapa ya kuitunza Sabato? (Mungu aliwaokoa watu wake kutoka kwenye kutendewa kusikokuwa kwa haki. Kwa hiyo tunapaswa kuwatendea wale walio chini yetu mambo ya haki kwa kuwapatia pumziko la Sabato.)
      1. Je, hiyo ndio sababu ya kutufanya tuamini kuwa Sabato ilifanywa kwa ajili ya Wayahudi pekee? (Hapana. Ulikuwa tu ni mfano wa “kuokoa.” Mungu aliingilia kati ili kuweza kuleta haki. Hivi leo Mungu anatuokoa kutoka kuwa watumwa wa dhambi na kifo.)
  2. Sabato Inayofananishwa na Mpira wa Kimarekani
    1. Soma Marko 15:33-34, Marko 15:37-39 na Marko 15:42-43. Je, Yesu alisulubiwa siku gani? (Ijumaa, kabla ya Sabato.)
    2. Soma Marko 16:1-3 na Marko 16:5-9. Je, Yesu alifufuka kutoka kaburini siku gani? (Jumapili.)
      1. Kwa nini ucheleweshaji huu? Hebu jiweke kwenye nafasi ya Mungu Baba. Ni punde tu Mwanao amepigwa hadi mauti kumkuta. Kabla Mwanao hajafa anakwambia, “Kwa nini umeniacha?” Kwa kuongezea, ni punde tu Mwanao ameshinda “Mpira wa Kimarekani (American Football)” wa hapa duniani – ameishinda dhambi na kuuleta ushindi katika Ufalme. Je, utachukua muda gani kumkumbatia Mwanao? Je, utachukua muda gani kusema, “Sijakuacha!” (Sitasubiri! Kwa hakika kabisa, sitasubiri.)
        1. Je, kwa nini Mungu alifanya kile ambacho hakuna hata mtu mmoja angeweza kukifanya? (Mungu alisubiria kwa sababu ile ile ambayo alisherehekea uumbaji wa dunia katika siku ya Sabato. Alisubiria kwa sababu ile ile aliyosherehekea ukombozi wa watu wake kutoka Misri siku ya Sabato. Yesu alipumzika siku ya Sabato ikiwa ni kusherehekea kile alichokitimiza!)
  3. . Sabato na Kanisa la Awali
    1. Padre wa kanisa la awali, Ignatius wa Antiokia, kwenye barua yake kwa “Magnesians 9-10” anasema, “Kama wale waliokuzwa kupitia kwenye mfumo wa kale hivi sasa wana matumaini mapya, hawaitunzi tena Sabato, lakini wanaishi kwa kuishika/kuitunza Siku ya Bwana, ambapo maisha yetu yamechipushwa tena na Yeye na ufufuo Wake….. Ni upuuzi kumkiri Kristo Yesu, na kufanya mambo ya Kiyahudi. Kwa maana Ukristo haukuikumbatia dini ya Kiyahudi, bali dini ya Kiyahudi iliukumbatia Ukristo.”
      1. Je, ni sababu ipi/zipi ambazo Ignatius anazitoa za kuabudu siku ya Jumapili? (Ufufuo wa Yesu siku ya Jumapili. Uhasama dhidi ya dini ya Kiyahudi.)
        1. Je, Wayahudi walikuwa maarufu kwa kiwango gani kipindi ambacho Rumi iliiharibu Yerusalemu na hekalu mwaka wa 70 BK?
        2. Je, dini ya Kiyahudi ina ugomvi na Ukristo? (Hii inatupatia mtazamo wa wazi kabisa wa sababu za kuitunza siku ya Jumapili hapo awali. Imejengwa kwenye hoja ya “kimantiki” ambayo sio bora zaidi kuliko mantiki ya Yesu kupumzika siku ya Sabato baada ya kuteswa kwake. Kwa kuongezea, ina upande wa pili wa chuki kubwa ya Wayahudi. Ilikuwa ni baada ya kujiingiza kwenye mjadala wa dhati wa kiteolojia na mmojawapo wa mafariki wangu wa Kiyahudi ndipo nilipoelimishwa kuhusu uhusiano wa karibu wa historia kati ya uhasama/chuki/uadui dhidi ya Wayahudi na ukataaji wa Sabato ya Kibiblia. Uhasama dhidi ya Wayahudi (mfikirie Musa, Petro, Paulo) hauna msingi wa kiteolojia, na hauna nafasi sahihi kwenye fikra zetu. Yesu alikuja kutimiliza, sio kutangua, unabii na matendo ya Agano la Kale. (Mathayo 5:17.)
    2. Mfalme Konstatino wa Rumi katika mwaka wa 321 BK alitangaza rasmi Jumapili kuwa siku mpya ya mapumziko kwenye himaya yake. Hivi sasa ninasoma kitabu maarufu sana kuhusu historia ya Yerusalemu. Kinasema kuwa Konstatino alikuwa na matamanio mawili makubwa, uwezo/nguvu ya jua na Ukristo. Alitengeneza sarafu zenye sanamu ya msalaba na nyingine zenye sanamuya jua. Je, hii inapendekeza nini kwenye mtazamo wake wa ibada ya Jumapili? (Alitaka Wakristo wajumuishe ibada ya jua kwenye ibada zao za kidini.)
      1. Baadhi ya Wakristo wanasema kuwa hawaijali Krismasi au Pasaka kwa sababu zina mizizi ya “kipagani.” Ninakataa hoja hizi kwa sababu ya umuhimu wa hizi sherehe za kidini kwa Wakristo hivi leo. Je, tunapaswa pia kuwa na mtazamo huo huo kuhusiana na ibada ya kila juma wa Sabato ya Jumapili? (Huo ungekuwa mtazamo wangu kama isingekuwa ni kwa ajili ya amri ya Biblia iliyo wazi kabisa na isiyoyumba kwamba siku ya saba ndio pekee iliyofanywa na Mungu kuwa takatifu. Krismasi na Pasaka kamwe hazikudhihirishwa kuwa takatifu katika Biblia, kwa hiyo nipo huru kudai umuhimu wao wa sasa kwa Wakristo wote waliopo duniani.)
  4. Siku Yetu ya Bwana
    1. Jina la kawaida la Jumapili ni kuiita kuwa siku ya Bwana. Je, Yesu aliabudu siku ya Jumapili au alitoa ishara yoyote kuwa aliikana/aliikataa Sabato? Hebu tusome Mathayo 12:1-2. Kama Yesu alitaka kutoa ishara ya kubadili ibada kutoka Sabato kwenda kwenye siku nyingine, je, hii ingekuwa fursa nzuri sana kufanya hivyo?
    2. Soma Mathayo 12:3-5. Je, kuna wazo gani lililopo kuhusu utakatifu wa Sabato kwenye haya mafungu? (Analinganisha kula mikate ya wonyesho na wanafunzi wake kula siku ya Sabato – hakuna hata kimojawapo kilicho halali. Analinganisha makuhani kufanya kazi siku ya Sabato na wanafunzi wake “kufanya kazi” siku ya Sabato. Anasema kuwa “hawana hatia,” lakini sio kwa sababu ya tatizo lolote lililopo dhidi ya Sabato.)
    3. Soma Mathayo 12:6-8. Kwa nini Daudi hakuwa na hatia, makuhani hekaluni hawakuwa na hatia, na wanafunzi wa Yesu hawakuwa na hatia kwa kuivunja Sabato? (Lengo kuu. Daudi kwa dhati kabisa alikuwa na haki ya kufanya hivi kwa kuwa alikuwa mtiwa mafuta wa Mungu. Makuhani walikuwa wakifanya kazi kwa ajili ya Mungu. Yesu alikuwa Mungu na wanafunzi wake walikuwa pamoja naye katika kuuendeleza Ufalme wa Mungu.)
      1. Je, Yesu anamaanisha nini anaposema, “Nataka rehema, wala si sadaka?” (Soma Hosea 6:6. Dhana ya kutembea kwetu na Mungu sio kutoa wanyama sadaka (kutubu dhambi), ni kumpenda na kumtii Mungu. Washtaki wa wanafunzi walikuwa mbele za Mungu, lakini macho yao bado yalikuwa kwenye jambo dogo (lisilo la msingi). Yesu alikuwa hashushi umuhimu wa Sabato. Alikuwa akiwaelekeza wafuasi wake kujikita kwenye jambo la muhimu katika suala lolote lile.)
        1. Je, watunzaji wa Sabato watalitumiaje somo hili hivi leo?
    4. Soma Yohana 9:10-11 na Yohana 9:13-16. (Niliwahi kuwa na mshiriki wa darasa ambaye alimshutumu kwa nguvu zote Billy Graham kwa kutoitunza Sabato. Haya ndio mashtaka yaliyofanywa na baadhi ya Mafarisayo.)
    5. Soma Yohana 9:35-41. Je, Yesu anamaanisha nini anaposema kuwa amekuja ili vipofu wapate kuona? (Kwa mara nyingine tena Yesu anazungumzia kuhusu kuwa na mtazamo sahihi juu ya Sabato na asili ya umuhimu wake. Graham aliwaongoa mamia kwa maelfu ya watu maishani mwake. Huenda zaidi ya mtu mwingine yeyote yule, alikuwa uso (kioo) cha Wakristo wa Kiprotestati kwa miongo kadhaa. Mshiriki mwenzangu wa darasa, ambaye huenda kamwe hajawahi kumwongoa mtu yeyote, hakujikita kwenye Ufalme wa Mungu. Yesu anatuita tujikite kuuendeleza Ufalme wa Mungu.)
    6. Soma Mathayo 12:9-12. Je, Yesu anaukataa utakatifu wa Sabato? (Hapana.)
      1. Je, Yesu anasema nini kuhusiana na Sabato? (Kwa mara nyingine, anasema kuwa tunatakiwa kuiangalia vizuri - zana ya kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Kuwaponya na kuwasaidia watu wengine kunaendana na Sabato.)
    7. Soma Mathayo 12:13-14. Je, ingejalisha kitu chochote kwa yule mtu kama Yesu angesubiria hadi muda wa jua kuzama ili aweze kumponya? (Hapana.)
      1. Je, kwa nini Yesu alimponya siku ya Sabato? (Kusisitiza dhana yake ya jinsi ambavyo Sabato inapaswa kueleweka.)
      2. Kama Yesu alikuwa anakaribia kuifuta Sabato, kwa nini alifanya juhudi hizi za kubainisha jinsi Sabato inavyoingia kwenye mpambano kwa ajili ya Ufalme wa Mungu?
    8. Rafiki, Sabato ni ukumbusho wa kile ambacho Yesu amekifanya kwa ajili yetu – Alituumba, alituokoa kutoka dhambini, alikufa kwa ajili yetu na alifufuka kwa ajili yetu. Kamwe hatutakiwi kuacha kusherehekea siku takatifu aliyotupatia na kamwe haijabadilika. Lakini, lazima pia tuwe na mtazamo sahihi juu ya Sabato katika kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Je, utakubali hivi leo kuitunza Sabato kama sehemu ya kazi yako ya kuuendeleza ufalme wa Mungu?
  5. Juma lijalo: Utunzaji wa Viumbe