Somo la 8: Ahadi

Mwanzo 22–24
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
2
Lesson Number: 
8

Somo la 8: Ahadi

(Mwanzo 22–24)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Katika masomo yetu yaliyotufikisha kwenye somo hili mara kwa mara tumeangalia maanguko ya Abramu kiimani. Agano Jipya linasifia imani ya Abramu kwenye mazingira ya kutatanisha, na tunadhani hiyo ni habari njema kwetu. Juma hili yote hayo yanabadilika. Ibrahimu anadhihirisha imani ya kustaajabisha kwa Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi.

  1.    Kipimo/Jaribu (The Test)
    1.    Soma Mwanzo 22:1-2. Kwa nini Mungu anataka kumjaribu Ibrahimu?
      1.    Kama imani ya Ibrahimu (iliyodhihirishwa hadi kufikia hapa) “ilihesabiwa kuwa jambo la haki kwake” (Mwanzo 15:6), kwa nini jaribu hilo la kutisha liwe la kufaa?
      1.    Jaribu hili haliko sahihi kwa namna nyingi. Linaamrisha kutolewa kwa sadaka ya mtoto mlimani. Linakinzana na ahadi ya agano la Mungu kutimizwa kupitia kwa Isaka (Mwanzo 17:21). Unaweza kulielezea jaribu hili?
    1.    Soma Yakobo 1:2-4. Je, hili ndilo lengo la Mungu, kuweka saburi kwa Ibrahimu?
    1.    Soma Luka 24:27 na Yohana 5:39. Hii inafundisha nini juu ya uhusiano kati ya Agano la Kale na Yesu? (Yesu anasema kuwa Agano la Kale linamhusu. Sio muda mrefu sana huko nyuma nilianza kuchunguza visa maarufu vya Agano la Kale ili kuona kile vilichofundisha kumhusu Yesu. Utambuzi (mafunuo) mpya ulikuwa wa kuvutia sana. Nadhani jaribu la Ibrahimu kwa sehemu fulani linahusu kushindwa kwake kiimani huko nyuma, lakini zaidi sana ni kutuhusu sisi. Ni jaribu la kukuza uelewa wetu juu ya kile ambacho Mungu Baba na Yesu walikitenda kwa ajili yetu msalabani.)
    1.    Soma Mwanzo 22:3. Unadhani kwa nini Ibrahimu ana haraka? Kwa nini anaondoka alfajiri na mapema? (Ninahisi hakumwambia Sara alichokuwa anakifanya.)
      1.    Je, ungemwambia mkeo? Kama ungekuwa na umri wa zaidi ya miaka 100, je, ungewashirikisha watu wengine? (Ningekuwa na hofu kwamba nilikuwa ninachanganyikiwa! Ningependa kuwakusanya watu ili kushauriana nao. Sababu ya Ibrahimu kutofanya hivyo ni kwamba aliisikia sauti ya Mungu na alikuwa na uhakika wa kile alichokiamuru Mungu.)
    1.    Soma Mwanzo 22:4-6. Kwa nini kuwaacha wasaidizi na usafiri nyuma? (Inawezekana Ibrahimu alidhani kuwa wangejaribu kumzuia.)
      1.    Ibrahimu anapowaambia wasaidizi (kuwafanya wabaki) “tutawarudia tena,” je, anasema uongo? (Soma Waebrania 11:17-19. Ibrahimu hadanganyi, anaamini Mungu atamfufua Isaka kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo.)
      1.    Fikiria jambo hili kwa ajili ya maisha yako. Ibrahimu ana maamrisho/ahadi zenye mkanganyiko kutoka kwa Mungu. Njia pekee ya kuzipatanisha ni kwa njia ya muujiza. Hivyo ndivyo Ibrahimu alivyotatua jambo hili. Je, hili ni fundisho kwetu?
    1.    Soma Mwanzo 22:7-8. Kwa nini asimwambie Isaka kile hasa ambacho Mungu amekiamuru? (Hii inatuambia jambo fulani kwamba Ibrahimu hakumwambia mtu yeyote jambo hili.)
      1.    Je, siri hii ndio njia ambayo nawe ungeichukua? (Ningekuwa na matumaini kwamba mtu aliyenizuia angeniambia, “Mungu, nimejaribu kutekeleza, lakini [fulani (andika jina lake)] alinizuia.”)
      1.    Tafakari pendekezo langu kwamba agano la Kale linamhusu Yesu, kisha utumie pendekezo hilo kwenye kile anachokisema Ibrahimu katika Mwanzo 22:8.
    1.    Soma Mwanzo 22:9-10. Kwa nini anamfunga Isaka?
    1.    Soma Mwanzo 22:11-12. Malaika anaposema “Sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu,” una uelewa gani juu ya neno “kumcha?” (Ninadhani “kujitoa kwa dhati” ndio uelewa sahihi. Ibrahimu amejitoa kwa Mungu.)
      1.    Je, Mungu haufahamu mustakabali? Malaika anawezaje kusema “sasa ninajua” kwa niaba ya Mungu? (Ibrahimu ana uhuru hadi kipindi cha kuweka kisu chake chini. Hapo awali, Ibrahimu hakuwa mtu wa kuaminika kwenye suala la kumtumaini Mungu.)
    1.    Soma Mwanzo 22:13-17. Mungu anatoa mbadala, kama ambavyo Ibrahimu alibashiri (Mwanzo 22:8). Ibrahimu anapata fundisho gani kutokana na huu uzoefu mkubwa kupita maelezo? (Mungu atajipatia.)
      1.    Je, hii ni sehemu ya ahadi za Mungu unazozijumuisha maishani mwako?
      1.    Je, hiki ndicho tunachokiona msalabani?
  1.   Sara
    1.    Soma Mwanzo 23:1. Hii ni miaka thelathini na saba baada ya kuzaliwa kwa Isaka. Unadhani alikuwa anawazia nini kuhusu kisa tulichokijadili hivi punde (cha kumtoa Isaka sadaka)? (Sara ni mwanamke pekee, kwa mujibu wa wanamaoni kadhaa, ambao umri wake wakati anafariki unaandikwa katika Agano la Kale. Kwa upande wangu hiyo inaashiria kwamba Mungu anamheshimisha na mwitiko wake kwenye kisa chetu unaheshimika.)
    1.    Soma Mwanzo 23:2. Kiriath-arba, mahali alipofia Sara, pana ukweli muhimu uliofichwa kwenye jina lake. Soma Yoshua 15:13. Tunajifunza nini juu ya watu walioishi Kiriath-arba? (Hawa ni wana wa Anaki – majitu ya nchi.)
      1.    Hiyo inazungumzia nini kuhusu imani ya Ibrahimu na Sara? (Hawakuyaogopa majitu – tofauti na uzao wao. Angalia Hesabu 13:33.)
  1.      Mke wa Isaka
    1.    Soma Mwanzo 24:7 na Mwanzo 24:10-12. Ibrahimu na Elieza wanatumia njia gani kumtafutia Isaka mke? (Maombi na zawadi!)
    1.    Soma Mwanzo 24:14. Unauchukuliaje mpango huu?
      1.    Unachukuliaje suala la Elieza kudhibiti binti gani anayestahili? Kwa nini asiombe kwamba yeyote atakayewapa ngamia maji ndiye awe mke mtarajiwa? (Soma Mwanzo 24:16. Elieza alitaka kuchagua mwanamke “mzuri sana.”)
      1.    Una maoni gani juu ya Elieza kutengeneza kipimo cha kuchagua mke mtarajiwa?
      1.    Kwa mtazamo wako, je, wanawake “wazuri sana” ni wake bora? Au, ujumuishaji uliojengwa juu ya mwonekano haufai? (Hiki ni kipimo kilichotafakariwa vizuri. Mara nyingi, wanawake warembo sana (na wanaume) ni wabinafsi. Kwa kujaribu kama mke mtarajiwa alikuwa tayari “kuwazingatia ngamia” – ikimaanisha hata kujali ustawi wa Wanyama – Elieza alikuwa anapima uzuri wa sura na moyo wa mke mtarajiwa.)
    1.    Soma Mwanzo 24:15-19. Je, Mungu anajibu maombi yako moja kwa moja?
    1.    Soma Mwanzo 24:20. Tunajifunza nini kingine kumhusu Rebeka, mke mtarajiwa? (Ni mtu mwenye juhudi ya kazi. Akafanya “haraka” na “akapiga mbio” kuteka maji kwa ajili ya ngamia kumi (Mwanzo 24:10).)
      1.    Kuoa mwenza mwenye bidi ya kazi ni muhimu kiasi gani? (Hili ni suala la muhimu sana. Mwenza mmoja analalamika kwamba anafanya kazi zote. Kama wenza wote wanafanya kazi kwa bidi, jambo hilo kamwe haliibuki.)
    1.    Soma Mwanzo 24:22. Baadaye Biblia (Mwanzo 24:47) inatuambia kuwa pete ni ya puani. Dhahabu imezidi kwa mbali sana malipo ya kawaida kwa kazi hii. Elieza anafanya nini?
      1.    Je, kuna fundisho kwenye jambo hili kwa vijana wa leo wanaotafuta wake?
    1.    Soma Mwanzo 24:29-31. Mkufu huu unaleta athari gani kwenye safari hii?
    1.    Katika Mwanzo 24:33-48 Elieza anaelezea matukio ya safari yote. Soma Mwanzo 24:49-53. Je, kazi maalumu (mission) imefanikiwa kwa wote wanaohusika? Vipi kuhusu Rebeka?
      1.    Soma Mwanzo 24:5. Ibrahimu na Elieza walikuwa wanatafuta makubaliano ya ndoa kwa nani? (Walitaka mke mtarajiwa akubaliane na ndoa.)
    1.    Soma Mwanzo 24:58-61. Hatimaye Rebeka anaulizwa na anakubaliana na ndoa. Unadhani kwa nini alikubali?
      1.    Tunapaswa kujifunza nini kutokana na kisa hiki kwa ajili ya ndoa katika zama za leo? (Maombi ni muhimu. Ibrahimu alifuata neno la Mungu katika kuoa mtu kutoka kwenye familia yake. Kuyafuata maelekezo ya Mungu ni muhimu. Kutafuta mtu anayevutia, mwenye bidi ya kazi, na asiye mbinafsi ni muhimu. Kutoa zawadi ni muhimu.)
    1.    Soma Mwanzo 24:67. Je, kisa hiki kinahusu “furaha tele baadaye?”
    1.    Rafiki, unadhani kwa nini kisa hiki kina mwisho mzuri? Ninasema ni kwa sababu ya kujitoa kwa Mungu. Ibrahimu alijitoa. Familia yake ilijitoa. Kujitoa huku kunaishia kuwa na baraka. Je, utadhamiria, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kujitoa kwa Mungu?
  1.   Juma Lijalo: Yakobo Mtwaa Mahali pa Wengine