Somo la 10: Yakobo-Israeli

Mwanzo 32–35
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
2
Lesson Number: 
10

Somo la 10: Yakobo-Israeli

(Mwanzo 32–35)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mmojawapo wa watu wanaojitolea kutafsiri masomo haya ya GoBible, Shirley Babienco, anabandika (post) masomo haya mtandaoni kwa kutumia mfumo wa e-Sword. (Kwa sasa mfumo wa e-Sword ndio programu yangu ya msingi ya Biblia ya kielektroniki.) Shirley aliniandikia siku chache zilizopita kunifahamisha juu ya umri mkubwa wa Yakobo. Nilianza kuliangalia suala hilo na kugundua kuwa Biblia inatupatia taarifa za kutosha kutusaidia kufikia hitimisho lifuatalo: Yakobo alipokimbia kutoka nyumbani kwao alikuwa na umri wa miaka 71. Alipomuacha Labani ili kurudi nyumbani kwao alikuwa na umri wa miaka 91. Juma hili tunaendelea na kisa chetu na mtu aliye katika umri wa miaka ya 90 akipambana na Mungu! Hebu tuzame ulingoni na tujifunze zaidi!

  1.    Pambano
    1.    Soma Mwanzo 32:22-23. Tumeruka vifungu vinavyotuhabarisha kuwa bado Yakobo anamwogopa Esau. Kimsingi mkakati wa Yakobo ni kutanguliza kila anachokimiliki, ikiwemo familia yake. Yakobo anaongoza kutokea nyuma kwenye huku kukutana na Esau. Je, Yakobo ni mwoga? Au, huku ni kuwa tu na uhalisia?
    1.    Soma Mwanzo 32:9. Nani aliyemwambia Yakobo kurudi? (Mungu!)
      1.    Je, Mungu alidhamiria kumwadhibu Yakobo? (Hapana. Kifungu hiki kinamwonyesha Mungu akimwambia Yakobo kuwa anapaswa kurejea ili “nami nitakutendea mema.” Kuongoza akiwa nyuma ni kushindwa kwingine kumtumaini Mungu.)
    1.    Soma Mwanzo 32:1-2. Watu gani wa kufurahisha walikutana na Yakobo mwanzoni kabisa mwa safari yake? (Malaika walikutana naye!)
      1.    Yakobo anawezaje kutilia mashaka ulinzi wa Mungu?
    1.    Soma Mwanzo 32:24-25. Je, kushindwa kwa Yakobo kumtumaini Mungu kunamwepusha na hatari? (Hapana. Kwa dhahiri mtu wa ajabu (mgeni) anamshambulia wakati akiwa amelala. Cha kustaajabisha, Yakobo anapambana naye usiku kucha – na si yeyote kati yao anayeshinda! Maoni ya John MacArthur yanaashiria kuwa Yakobo ana umri wa miaka 97 katika kipindi hiki.)
      1.    Kama ungekuwa Yakobo halafu mtu akakushambulia wakati wa usiku, unadhani ungemhisi nani kuwa ndiye aliyemtuma mshambuliaji? (Ningedhani kuwa Esau ndiye amemtuma mtu kuja kuniua.)
    1.    Soma Mwanzo 32:26-28. Hii inatuambia kuwa Mungu ndiye aliyemshambulia Yakobo. Jambo gani linaendelea? Kwa nini Mungu hamshindi Yakobo?
      1.    Shambulizi hili lina maana gani? (Yakobo ana hofu. Hamtuaini Mungu. Yakobo anaposhambuliwa mara ya kwanza, ninadhani anaamini kuwa Esau yuko nyuma ya tukio hili. Lakini, wakati fulani anaelewa kuwa Mungu ndiye mshambuliaji kwa sababu Yakobo anadai baraka ya mshambulizi wake.)
      1.    Je, Mungu anafanyia kazi ili kukuza imani ya Yakobo? Je, unadhani kwamba kupambana na Mungu huongeza imani yako?
      1.    Kubadili jina kunamaanisha nini? (Maoni ya John MacArthur’s yanataarifu kuwa jina lake linatoka kwenye maana ya “mdanganyifu” au “mshika kisigino” hadi kuwa “mshindana na Mungu.”)
    1.    Soma Mwanzo 32:29-31. Je, unadhani kuchechemea kwa Yakobo kuna sababu? (Yakobo anabadilika jina na jeraha lililotokana na mpambano. Yote mawili yanamkumbusha kukutana kwake na Mungu. Yanampatia ujasiri.)
  1.   Kutaniko
    1.    Soma Mwanzo 33:1-3. Kitu gani kimebadilika kwenye mpango wa pambano wa Yakobo? (Wale anaotaka wawe salama bado wanawekwa nyuma. Unaweza kujua unapendwa kiasi gani kwa kuzingatia umewekwa nyuma sana kiasi gani katika kundi. Kilicho tofauti sasa ni kwamba “Akapita mwenyewe mbele yao.” Yakobo anaongoza kutokea mbele. Anaonyesha ujasiri.)
      1.    Je, unadhani jeshi la Esau la watu 400 linamtia hofu Yakobo?
    1.    Soma Mwanzo 33:4. Kukutana bora namna gani! Fikiria mambo yangekuwa tofauti kiasi gani endapo Yakobo angemtumaini Mungu tangu awali!
      1.    Ni mara ngapi umekuwa na wasiwasi juu ya jambo baya kutokea na kamwe halikutokea?
  1.      Fedheha
    1.    Soma Mwanzo 34:1-4. Shekemu ni mwana wa mkuu wa nchi. Je, anajaribu kurekebisha mambo aliyokosea?
    1.    Soma Mwanzo 34:5. Unadhani kwa nini Yakobo alinyamaza? Je, hana uhakika juu ya jambo sahihi kulitenda? (Ruka vifungu kadhaa na usome Mwanzo 34:30. Tunaweza kuona kwamba mazingira ya Yakobo yanatatizika.)
      1.    Je, mazingira ya Yakobo yanatatizika kwa sababu tu hamtumaini Mungu katika kuilinda familia yake?
    1.    Soma Mwanzo 34:6-8. Ungechukua uamuzi gani?
      1.    Je, Hamori na Shekemu wanajaribu kutenda jambo sahihi?
      1.    Je, kaka zake Dina wako sahihi kwamba kitendo hiki ni cha kifisadi/kikatili dhidi ya dada yao? Au, je, jambo hili “ni la kipumbavu katika Israeli” pekee na wao hawako Israeli?
      1.    Soma Mwanzo 28:1. Je, kuoleana ndilo jibu sahihi?
    1.    Hebu twende nyuma ya pazia la fikra ya Hamori. Soma Mwanzo 34:16 na Mwanzo 34:23. Lengo halisi la Hamori ni lipi? (Hamori anawazia muunganiko wenye ushirika. Anadhani kuwa wakiungana, basi atamiliki mali zote za Yakobo. Tunaona kwamba Hamori anaamini kuwa atapata faida kutokana na tatizo hili.)
    1.    Soma Mwanzo 34:13-16. Je, hii ni kweli kwamba Dina (dada) hapaswi kuolewa na mwanaume ambaye hajatahiriwa? (Kuna kiasi kidogo cha ukweli katika hili. Tohara ni ishara tu ya tatizo. Tatizo halisi ni kuoleana na wapagani, na tohara pekee haitibu tatizo hilo.)
    1.    Soma Mwanzo 34:17. Je, unadhani hii ni ahadi ya kweli? (Sidhani. Cha muhimu zaidi, “kitisho” hiki kinaniambia kuwa wana wa Yakobo wanatambua nia ya kweli ya Hamori kwenye makubaliano haya.)
    1.    Soma Mwanzo 34:24-29. Hii inakuambia nini juu ya tabia ya wana wa Yakobo? (Ni wabaya kuliko Hamori. Inawezekana Hamori alikuwa na lengo hilo hilo, lakini hakudhamiria kulitimiza kwa njia ya mauaji na wizi.)
    1.    Soma Mwanzo 34:30. Je, huu ni mjibizo (reaction) sahihi? (Hapana. Yakobo halaani mauaji wala wizi. Anawaza kwamba yeye pamoja na nyumba yake “wataangamizwa.” Kama angemtumaini Mungu, angetambua kuwa matokeo hayo yasingetokea.)
      1.    Kwa kuwa Yakobo ni mwakilishi wa Mungu Kaanani, hiyo inawaambia nini wapagani kuhusu Mungu? (Hii ni hali ya kutisha. Wawakilishi wa Mungu wanaenenda kwa namna ovu kabisa. Hata Yakobo hajali juu ya uovu na jinsi unavyomuakisi Mungu.)
    1.    Soma Mwanzo 34:31. Je, wanawe Yakobo wana hoja ya msingi? Je, hii inahalalisha kile walichokifanya? (Hapana. Dada yao angekuwa mke. Walimuua mumewe mtarajiwa.)
  1.   Kurejea
    1.    Baada ya hili tukio la kutisha Mungu anaamua kwamba ni bora Yakobo asikae mahali pale, bali arejee nyumbani kwao kwa mababu zake. Soma Mwanzo 35:1-4. Kwa nini Yakobo anaamrisha mabadiliko haya sasa hivi?
      1.    Je, hii ni sawa na kusafisha matendo yako ili uende kanisani? Kuwatembelea wazazi wako?
      1.    Kwa nini Yakobo anaizika tu miungu ya kigeni badala ya kuiangamiza? (Anaificha tu. Kama angetaka kuachana nayo angeiangamiza au kuiacha mahali ambapo mtu mwingine angeichukua.)
    1.    Soma Mwanzo 35:9 na Mwanzo 35:16-19. Je, Yakobo anafanana nasi? Anachukua hatua nusunusu juu ya uabudu miungu, lakini Mungu anambariki. Anabarikiwa, lakini mkewe kipenzi anafariki wakati anajifungua. (Ninapokiangalia kisa hiki ninamwona Mungu mwenye upendo na rehema. Yakobo sio mtu anayepaswa kuwa hivyo. Wakati huo huo, Mungu hamkingi Yakobo na Raheli dhidi ya majanga yote.)
    1.    Rafiki, ninajisikia kama vile tunasoma riwaya juu ya watu maalumu wa Mungu hapa duniani. Mungu alitaka tusome habari zao, zinazojumuisha dhambi zao za kutisha. Mungu anatufundisha nini? Ninadhani anatufundisha kuwa hatupaswi kuhuzunika juu ya dhambi zetu za zamani. Wakati huo huo, tunapaswa kumwomba Roho Mtakatifu kuwa wawakilishi wazuri wa Mungu Mkuu wa Mbinguni. Anastahili kilicho bora kutoka kwetu!
  1.    Juma lijalo: Yusufu, Mjuzi wa Ndoto.