Somo la 4: Kuuona Uso wa Mfua Dhahabu

Mwanzo 1, Warumi 8, 1 Wakorintho 3, Ayubu 1 % 23
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
3
Lesson Number: 
4

Somo la 4: Kuuona Uso wa Mfua Dhahabu

(Mwanzo 1, Warumi 8, 1 Wakorintho 3, Ayubu 1 % 23)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kutumia muda mwingi kujifikiria ni jambo la kawaida. Ni kawaida kutafakari jinsi baadhi ya mabadiliko yatakavyokuathiri. Ama kwa hakika, huenda unatumia sehemu kubwa ya muda wako kutafakari juu ya mabadiliko na jinsi yanavyokuathiri. Ninaogopa kwamba tunaruhusu jambo hili kujipenyeza kwenye teolojia yetu – kwamba tunaanza kufikiria matatizo kama njia ya kutuboresha. Lengo letu, wanasema, ni kuwa dhahabu iliyosafishwa, hivyo acha magumu yatujie. Tafakari jambo hili, kama Mungu alitaka tusafishwe kwa njia ya matatizo, kwa nini alitupatia Amri zake na ushauri wake kwenye Biblia? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi juu ya uhalali wa dhana ya kusafisha/kutakasa!

  1.    Watawala wa Mungu
    1.    Soma Mwanzo 1:26-27. Kwa nini Mungu aliwaumba wanadamu kwa mfano wake? (Aliwaumba ili wawe watawala. Aliwaumba ili wawe na mamlaka. Ingekuwa vigumu kwa mbuzi kuwa mtawala.)
    1.    Soma Warumi 8:18. Je, hii inaashiria kwamba mateso huleta utukufu? (Kifungu kinasema kuwa utukufu upo katika siku zijazo. Utukufu utafunuliwa. Lakini, kifungu hakisemi kwa dhahiri kwamba utukufu hutokana na mateso.)
    1.    Soma Warumi 8:19-21. Je, uumbaji unapitia mateso? (Ndiyo, “ulitiishwa chini ya ubatili.” Uko “katika utumwa wa uharibifu.”)
      1.    Nani atakayeuweka huru uumbaji dhidi ya mateso? (Tunaambiwa kuwa “utaingia katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.”)
        1.    Je, hiyo inamaanisha kuwa matokeo ya uhuru wetu ni uumbaji kuwa huru?
        1.    Hiyo inaendanaje na kifungu chetu cha kwanza, kwamba tuliumbwa kwa mfano wa Mungu ili kuutawala uumbaji? (Inaashiria kwamba ubinadamu kwa ujumla umepoteza sura ya Mungu na hivyo haujawa mtawala mwenye ukarimu kwa uumbaji.)
    1.    Soma Warumi 8:22-23. Wengi kati ya wale waliosoma vifungu vilivyotangulia huenda walikuwa wanadhani kuwa wanadamu wameyaharibu mazingira. Je, hicho ndicho kinachozungumziwa? (Hapana. “Ukombozi wa miili yetu” unarejelea ujio wa Yesu Mara ya Pili. Yesu atakapokuja atatuweka huru sisi pamoja na uumbaji dhidi ya utumwa wa dhambi.)
    1.    Hebu turukie chini na tusome Warumi 8:28-30. Lengo letu ni lipi? (“Tufananishwe na sura ya [Yesu].” Tafakari mantiki ya kile tulichokijadili hadi kufikia hapa. Je, “kufananishwa” na sura ya Yesu kutautendea nini uumbaji? (Kunafanya mambo yote kuwa mazuri. Kunaturejesha kwenye uhusiano wetu wa asili na Mangu.)
    1.    Soma Warumi 8:33-34. Hii inatuambia nini juu ya asili ya kuhesabiwa kwetu haki? Je, ni jambo linalotokana na uchafu/takataka zinazochomwa kutoka kwetu? (“Mungu ndiye mwenye kutuhesabia haki.” Mungu “ndiye anayetuombea.”)
    1.    Soma Warumi 8:35-39. Hii inaashiria kuwa lengo la mateso ni nini? (Kututenganisha na Mungu.)
      1.    Hii inazungumzia nini kuhusu madai kwamba Mungu huleta mateso ili kutufanya tufanane naye? (Inaashiria kwamba mateso hayatoki kwa Mungu na malengo yake ni kutufanya tusifanane na Mungu, kututenganisha naye.)
    1.    Soma 2 Wakorintho 3:14-18. Kifungu hiki kinasema kuwa tunabadilishwaje ili kufanana na sura ya Mungu? (Tunaposhikilia kile ambacho Mungu ametutendea. Tunapoishi ndani ya uwezo wa Roho Mtakatifu.)
    1.    Hebu tulijadili hili kwa kina zaidi kama ni muhimu kufanya hivyo. Je, kurejea kwenye sura ya Mungu ni jambo jema kwetu na kwa uumbaji?
      1.    Je, tunarejeshwa kwenye sura ya Mungu kwa njia ya mateso? (Vifungu hivi haviashirii hivyo.)
      1.    Je, Wakristo wanateseka? (Ndiyo. Lakini lengo letu ni kuishikilia imani yetu katika Yesu.)
      1.    Sote tumeona mfululizo wa vitabu “dummies.” “Word for dummies.” Dhana iliyopo ni kufanya kujifunza jambo kwa urahisi kadiri inavyowezekana. Ni kwa jinsi gani tulipoteza sura yetu ya Mungu mkamilifu? (Tulichagua kumgeuka na kumwacha Mungu. Tulijiletea mateso.)
        1.    Kama tumejiletea mateso, je, inaleta mantiki yoyote kudhani kuwa mateso yataturejesha kwa Yesu? Je, hiyo sio sawa na kujitandika viboko ili kuondoa dhambi?
  1.   Fundisho la Ayubu
    1.    Soma Ayubu 1:1. Je, Ayubu alihitaji kutakaswa? (Hapana. Kifungu hiki kinazungumzia mambo mazuri ya Ayubu, ikiwemo kwamba yeye ni “mwelekevu.”)
    1.    Soma Ayubu 1:8-12. Hii ni sehemu moja ambayo tunajua kwa uhakika sababu ya mateso. Chanzo cha mateso ya Ayubu ni kipi?
      1. Je, Ayubu alikuwa anatakaswa kwa mateso yatakayomjia?
    1.    Soma Ayubu 23:1-5. Ayubu anakata rufaa kwa nani ili kupata haki? (Mungu. Anasema kuwa kama angempata Mungu ili kufungua mashtaka, Mungu angemsikiliza.)
    1.    Soma Ayubu 23:6-9. Ayubu anakabiliana na tatizo gani halisi katika kufungua mashtaka yake dhidi ya Mungu? (Anashindwa kumpata Mungu.)
    1.    Soma Ayubu 23:10-12. Je, Ayubu anasema kuwa katika mateso yake atasafishwa kama dhahabu? (Sio kwa kiasi kikubwa. Anasema kuwa kama anaweza kumpata Mungu ili amsikilize, kwamba Mungu atakapokuwa anasikiliza kesi yake “atatoka kama dhahabu.” Yakobo anadai katika vifungu vya 11-12 kwamba amefanya kila lililo jema. Atafanywa kufikia kiwango cha dhahabu cha Mungu.)
      1.    Je, Ayubu anajidanganya? Je, ana kiburi? (Hapana. Tunafahamu kutoka katika kitabu cha Ayubu 1 kwamba Mungu anamchukulia Ayubu kuwa “mwelekevu” na mateso hayahusiani kivyovyote vile na kumtakasa Ayubu, na linahusiana kwa hali zote na kumpa Mungu utukufu.)
    1.    Hebu tusome tena Ayubu 1:11. Lengo la Shetani katika mateso ya Ayubu ni lipi? (Kumtenganisha na Mungu. Utaona kwamba hiki ndicho hasa ambacho Warumi 8:35 inatufundisha – lengo la Shetani katika mateso ni kutufanya tuiache imani yetu kwa Mungu.)
  1.      Mitume na Mateso
    1.    Soma 1 Wakorintho 4:9-13. Je, Paulo anateseka? Je, anayafurahia mateso? (Hayafurahii mateso.)
      1.    Unadhani kwa nini Paulo anajilinganisha na washiriki wenzake wa kanisa? (Paulo anaonekana kusema kuwa washiriki wa kanisa hawapaswi kumdharau kutokana na mateso yake. Hawana hadhi kubwa kuliko yeye kwa kuwa hawapitii mateso.)
    1.    Angalia tena 1 Wakorintho 4:9. Paulo anasema kuwa mitume wamekuwa “tamasha kwa dunia, kwa Malaika, na wanadamu.” Hii inaashiria kuwa sababu ya mateso yao ya kipekee ni ipi? (Hii inaonekana kuwa kama kwa Ayubu – ulimwengu unashuhudia uaminifu wa mitume.)
      1.    Matokeo ya uaminifu wao ni yapi, na uaminifu wa Yakobo? (Mungu anatukuzwa. Ana watu fulani waaminifu watakaosimama imara katika mazingira yote.)
        1.    Je, kuna pendekezo lolote kwamba mitume wanatakaswa kwa mateso haya?
    1.    Soma 1 Wakorintho 4:14-15. Paulo anasema kuwa wale wanaosoma barua yake wanaweza kujifunza jambo fulani kutokana na uzoefu wa mitume. Ni jambo gani hilo? (Inahusiana na kumchagua mwongozaji sahihi. Wanachopaswa kujifunza ni kwamba kiongozi anayeteseka anaweza kupitia uzoefu huo kwa sababu Mungu anamtumia kiongozi huyo kwa ajili ya utukufu wake. Sio lazima imaanishe kuwa kiongozi anastahili kuteseka.)
  1.   Jinsi ya Kutakaswa
    1.    Soma Waefeso 4:11-14. Kanuni ya Mungu ya kuwatakasa watu wake ni ipi? (Kanisa! Mungu anatutaka tuwe kwenye mfumo unaotufundisha na kutujenga!)
    1.    Soma Waefeso 4:15-16. Mungu anatutaka tutakaswe kwa njia gani? (Kwa kusema ukweli na kuwasikiliza wale wanaosema ukweli.)
    1.    Soma Waefeso 4:30. Roho Mtakatifu ana nafasi gani katika utakaso wetu? (Roho “hututia muhuri” kwa ajili ya wokovu.)
    1.    Rafiki, hii inatufikisha kwenye hitimisho kwamba kila mtu mwenye ukomavu ana uelewa. Kuna njia mbili za kujifunza. Unaweza kugonga kichwa chako kwenye ukweli, au unaweza kusikiliza, kujifunza, na kuufuata ukweli. Vifungu tulivyojifunza leo vinaonesha kuwa njia ya Mungu ni ya uerevu. Hata hivyo, uovu upo na tunapoingia kwenye mateso bila sisi kuwa chanzo cha mateso hayo, tunayo fursa ya kumpa Mungu utukufu!
  1.    Juma lijalo: Joto Kali Sana.