Somo la 11: Kusubiria Tanurini (Kalibuni) 

Wagalatia 5, Yakobo 1, Luka 12, 1 Samweli 26
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
3
Lesson Number: 
11

Somo la 11: Kusubiria Tanurini (Kalibuni) 

(Wagalatia 5, Yakobo 1, Luka 12, 1 Samweli 26) 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza. 

Utangulizi: Je, unapenda kusubiri? Je, jibu lako linafanana na asili ya kusubiri kwako? Kwa mfano, mimi na mke wangu tumekubaliana kwamba bora tupitie njia ndefu kwenda tunapokwenda endapo hakuna msongamano wa magari kwenye barabara hiyo tofauti na kupita njia fupi ambapo tutasubiria kwa muda mrefu kwenye msururu mrefu wa magari. Katika mazingira yote haya mawili tunasubiria (tunachelewa kufika kule tunapokwenda), lakini aina mojawapo ya kusubiria inakubalika. Je, hii pia ni kweli katika maisha ya Mkristo? Au, je, fundisho la Biblia juu ya uvumilivu ni mjadala mwingine tofauti kabisa? Je, kujifunza kusubiria ni jambo la kimaadili, tofauti na kujifunza jinsi ya kufanya kusubiria huko kusiwe na maumivu? Hebu tuone kile Biblia inachotufundisha juu ya uvumilivu! 

I.  Uvumilivu ni Maadili ya Vitunguu 

A.  Soma Wagalatia 5:19-21. Kwa nini Biblia inaiita mitazamo hii na matendo haya kama “matendo ya mwili?” (Hayatoki kwa Mungu. Yanatoka kwenye mitazamo yetu ya ubinafsi.) 

B.  Soma Wagalatia 5:22-23. Haya ni “matunda ya roho.” Jinsi haya yalivyoandikwa katika kitabu cha Wagalatia yanaonekana kuwa ujumbe unaojibu “matendo ya mwili.” Unapoyatafakari matendo ya mwili, ni nini kinyume cha uvumilivu? (Tunapoitafakari orodha, inaonekana matendo kadhaa yanatokana na kutokuwa na uvumilivu: uadui, ugomvi, wivu, hasira, na tamaa. Uhusiano ni kwamba endapo tutasubiria, inawezekana tusipitie uzoefu wa hisia hizi.) 

1.  Je, hii inatufundisha kwamba uvumilivu unafananishwa na kitunguu, kina matabaka mengi tofauti tofauti? 

C.  Soma Wagalatia 5:24. Chukulia kwamba tunaokolewa kwa imani pekee, hii inatuambia tufanye nini? (Soma Warumi 6:6 na Warumi 8:13. Hii inaonekana kuwa na sehemu mbili. Kwanza, tulipobatizwa tuliungana na Yesu katika mateso yake. Utu wetu wa kale ulikufa. Wakati huo huo katika Warumi 7:15 tunaona kwamba mapambano dhidi ya dhambi bado yapo na hivyo Warumi 8:13 inatuambia tufanye uchaguzi wa jinsi tutakavyoishi.) 

D.  Soma Wagalatia 5:25. Roho Mtakatifu anahusianaje na hili? (Tunaambiwa “tuenende” kwa Roho Mtakatifu. Nadhani hiyo inamaanisha kuzingatia na kutenda kile ambacho Roho anatuambia tukifanye.) 

1.  Je, huu uzingativu unahusiana na uvumilivu? 

II.  Njia Kuuelekea Uvumilivu 

A.  Soma Yakobo 1:2-3. Tafsiri ya ESV inatafsiri neno la Kiebrania kama “ustahimilivu” wakati tafsiri nyingine zinalitafsiri neno hilo kama “uvumilivu.” Tafsiri ya Strong inapendekeza “saburi.” Kwa nini majaribu maishani “huleta” saburi? (Haya ni maelekezo kwa Wakristo. Kama tunamtumaini Mungu, tunajua kwamba mambo yataenda vizuri.) 

1.  Huu ni uvumilivu wa namna gani? (Hili ni tabaka tofauti la kitunguu: uvumilivu katika mazingira magumu, tofauti na uvumilivu kwa mtu tunayejaribu kumfundisha.) 

B.  Soma Yakobo 1:4-5. “Kazi kamili” ya uvumilivu ni ipi? (Tunakua kitabia. Hii inaashiria kuwa uvumilivu ni njia ya kuelekea kwenye “kutopungukiwa na neno.”) 

1.  Hekima inahusianaje na hili? 

C.  Soma 2 Petro 3:8-9. Tunajifunza nini juu ya muda wa Mungu? (Ana kipimo tofauti cha muda tofauti na kipimo chetu.) 

1.  Utaona kwamba hii inazungumzia juu ya uvumilivu wa Mungu. Nini inayoweza kuwa sababu ya kwa nini tunapaswa kumsubiria Mungu kwa uvumilivu? (Kuchelewa kwake ni kwa manufaa yetu! Tunamsubiria Mungu na Mungu anatusubiria.) 

2.  Unganisha hili na kile tulichokijadili awali kuhusu uvumilivu kuwa tiba ya mitazamo kadhaa ya dhambi. Sasa tunaona kuwa lengo la uvumilivu wa Mungu kwetu pia linahusu mitazamo yetu ya dhambi. 

D.  Hapo juu nimebainisha kuwa Stronmg anaangalia mtazamo wa saburi kama sehemu ya uvumilivu. Wakati huo huo, nilisoma maoni yaliyopendekeza kwamba kama unafurahia kusubiri (kama ilivyo kwenye utangulizi wangu juu ya kupita njia nzuri zaidi), basi huu sio uvumilivu. Je, kusubiri kunapaswa kukera ili kukusaidia kukuza uvumilivu? (Angalia tena Yakobo 1:2. Anatuambia kuwa njia ya kuuelekea uvumilivu inapaswa kuwa ya furaha. Nadhani lengo ni kupata furaha katika kusubiri.) 

E.  Kwa uwepo wa simu za mkononi nilikuwa na uwezekano wa kufanya mambo mbalimbali ya kuburudisha au mambo ya msingi wakati nikisubiria. Je, simu za mkononi ni msingi wa kupata furaha wakati wa kusubiria? (Soma 1 Wathesalonike 5:16-18. Huu ni ushauri wa Mungu uliotolewa kabla ya kuwepo kwa simu ya mkononi. Tunaweza kuwa na furaha wakati tunasubiria kwa kuomba [kusali] na kumshukuru Mungu.) 

1.  Je, umewahi kujaribu hilo wakati ukisubiria kwenye foleni? 

III.  Taswira Sahihi ya Uvumilivu 

A.  Mimi na mke wangu tunapokubaliana kwenda mahali fulani, kwa kawaida huwa ninakwenda kwenye gari mara moja, naliondoa kwenye eneo la maegesho (gereji), nashusha kioo cha dirisha na kujipumzisha huku nikiangalia mazingira ya nyumbani kwangu na maeneo ya jirani. Je, hii ndio aina ya uvumilivu ambayo Mungu anataka tuwe nayo? 

B.  Soma Waebrania 6:11-12. Hii inaashiria kwamba kuwa “wavivu” wakati tukisubiria kwa uvumilivu ni tatizo. Kwa nini hilo ni kweli? (Kifungu kinasema kuwa tunapaswa “kuwaiga” wale wasio wavivu wakati tukisubiri kwa sababu wanarithi ahadi.) 

1.  Tunaepukaje kuwa wavivu? (Taswira iliyopo hapa ni ile ya kuwa na “ari,” “matumaini,” na “imani” wakati tukiitazamia thawabu. Ni taswira ya matendo.) 

a.  Hii inaonekana kuwa ni mitazamo. Tunapaswa kufanya nini kwa umahsusi ili kuepuka kuitwa “wavivu?” (Tutaliangalia hilo katika sehemu inayofuata.) 

C.  Soma Luka 12:35-37. Tunapaswa kufanya nini tunapokuwa tunasubiria? 

D.  Soma Luka 12:42-43. Hapa tunaona maelekezo gani ya ziada kuhusu majukumu yetu wakati tukisubiri kwa uvumilivu? (Meneja anasimamia kaya [familia].) 

E.  Soma Luka 12:45-47. Tunapaswa kujiepusha kufanya nini wakati tukisubiri? (Kuwadhuru watumishi wenzetu.) 

F.  Taswira hizi za haraka haraka (snapshots) kutoka Luka 12 zinaonekana kuwahusu watawala matajiri wa kaya. Utatumiaje fundisho hili kama hauna mtumishi uliyemwajiri katika kaya yako? (Nadhani hii inatumika kwa Wakristo wenzetu. Hii ni kaya [familia] ya Mungu. Tunapaswa kutumia muda wetu wa kusubiria kutenda mambo mema ili kuwasaidia waamini wenzetu.) 

IV.  Daudi, Taswira ya Uvumilivu? 

A.  Soma 1 Samweli 26:1-2. Kwa nini Mfalme Sauli alikuwa anamtafuta Daudi? Je, alikuwa anataka kumpa zawadi yake ya siku ya kuzaliwa? (1 Samweli 23:15 inabainisha kwamba Mfalme Sauli alitaka kumkamata na kumuua Daudi. Hapo awali Sauli alifanya majaribio kadhaa ya kumuua Daudi.) 

B.  Soma 1 Samweli 26:3-4. Je, Daudi alikuwa anamsubiria Sauli kwa uvumilivu? (Hapana. Aliwatuma wapelelezi ili kuwa na tahadhari ya kuja kwa Mfalme Sauli.) 

C.  Soma 1 Samweli 26:5-6. Je, hii ni taswira ya uvumilivu? (Sidhani. Kwa haraka haraka Daudi anasonga mbele na mpango wake.) 

D.  Soma 1 Samweli 26:7-9. Je, Daudi anasubiri? Kama umesema, “ndiyo,” Daudi anasubiria nini? (Anamsubiria Mungu. Ilikuwa Dhahiri kwamba Daudi atakuwa mfalme atakayefuatia (1 Samweli 23:17). Daudi aliamua kwamba badala ya kufanya mabadiliko haya yatokee, atasubiria hadi Mungu atakaposonga mbele.) 

E.  Soma 1 Samweli 31:3-5. Utaona kwamba mchukua silaha alikuwa na shaka ile ile kama ya Daudi. Soma 1 Samweli 31:6-9 na 1 Samweli 31:12. Je, uvumilivu wa Daudi ulikuwa jambo jema? 

1.  Kama umesema, “ndiyo,” rejea nyuma na usome 1 Samweli 23:16-17. Kama Daudi angemuua Sauli pale alipoweza kufanya hivyo, rafiki yake Yonathani angeishi na angemsaidia Daudi. Mwili wa Mfalme Sauli usingeondolewa kiungo na kutundikwa. Je, kuchelewa kwa Daudi ni udhihirisho wa uvumilivu au kushindwa kufuata maelekezo ya Mungu kwa uthabiti? 

a.  Je, lingekuwa tukio la mauaji endapo Daudi angemuua Sauli usiku ule? 

F.  Tafakari kwamba baada ya Daudi kuwa mfalme, kijana mdogo alimwendea na kutoa taarifa kwamba alimuua Mfalme Sauli, baada ya Sauli kuomba kufanyiwa hivyo, ili kumwokoa na adui. Maelezo haya yanatofautiana na kile tulichokisoma hivi punde, na inawezekana hii sio kweli. Soma 2 Samweli 1:14-16 ili kuona mwitiko wa Daudi. Je, suala kubwa la kiuadilifu lilihusika Daudi alipokataa kumuua Mfalme Sauli? 

G.  Rafiki, somo letu linabainisha upande wa kufurahisha wa kuwa na uvumilivu ambao siwezi kusema kwamba nimelitafakari hilo kabla. Kuwa mvumilivu kunakufanya ujiepusha kushiriki kwenye uovu. Katika kila jambo tuliloliangalia, uvumilivu uliwekwa kama mbadala wa matendo maovu. Je, utajitahidi kuwa mvumilivu, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu? 

V.  Juma lijalo: Kufa Kama Mbegu.