Somo la 7: Ushindi wa Kristo Dhidi ya Kifo
Somo la 7: Ushindi wa Kristo Dhidi ya Kifo
(Yohana 20, Mathayo 27, 1 Wathesalonike 4)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mimi sio mpenzi wa besiboli (aina ya mchezo wa mpira wa gongo unaochezwa na timu mbili za watu tisa kila upande). Mchezo huu unaonekana kuchezeka pole pole bila kuwa na mwisho. Bila shaka wasomaji wengi hawatakubaliana nami. Fikiria mchezo wa besiboli (au mpira wa miguu, au mpira wa magongo (hockey), au ndondi) usiofikia mwisho. Je, utaridhishwa na hilo? Tumia fikra hiyo kwenye pambano kati ya wema na uovu. Kama wafu wenye haki wanakwenda mbinguni moja kwa moja, kwa nini basi tuhitaji ufufuo? Kama jibu ni kwamba unahitaji kuwa na mwili mbinguni ili uende na roho yako, kwa nini usipewe mwili huo huko mbinguni? Sio kana kwamba unapewa mwili wako uliooza. Kuna mantiki ya “ushindi” inayounga mkono dhana ya kwamba kulala kwa roho tutakayoichunguza juma hili. Ushindi huo unaanza na ufufuo wa Yesu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia!
I. Tomaso Mwenye Mashaka
A. Soma Yohana 20:19. Wanafunzi wa Yesu wana mtazamo gani baada ya kusulubiwa kwake? (Ni mtazamo wa kushindwa. Wanaogopa kwamba wao pia watauawa na mamlaka.)
B. Soma Matendo 1:6. Wakati Yesu akikaribia kabisa kurudi mbinguni, baada ya kufufuka kwake, wanafunzi wanaliuliza swali hili. Hebu niambie, hili linaongezea nini kwenye mtazamo wako kiakili juu ya wanafunzi katika Yohana 20:19? (Lazima walikuwa wameteketea kabisa kimwili na kiakili. Walikuwa na maono ya kuwa watawala katika ufalme wa Yesu hapa duniani. Sasa wamekusanyika pamoja wakiwa na hofu kwamba ufalme wa sasa utawaua.)
C. Soma Yohana 20:20-21. Wanafunzi wanapelekwa kufanya nini? (Wanatumwa kupeleka taarifa ya ushindi! Ushindi wa Yesu dhidi ya kifo. Amani ya injili.)
D. Soma Yohana 20:22. Kwa nini Yesu aliwapatia wanafunzi Roho Mtakatifu mara tu baada ya kuwatuma kazi? (Roho Mtakatifu alikuwa wa muhimu kwenye kazi yao.)
E. Soma Yohana 20:24-25. Kwa nini Tomaso haamini? Je, anadhani kuwa wanafunzi wenzake ni waongo?
F. Soma Yohana 20:26-27. Kwa nini Yesu alichukua juhudi za ziada ili kumshawihi Tomaso?
G. Soma Yohana 20:28-29. Hebu tuangalie umuhimu wa kujitokeza kwa Yesu. Je, unadhani wanafunzi wengine wangekuwa na mtazamo huo huo kama wa Tomaso kama wao pia wasingekuwepo wakati Yesu alipojitokeza mara ya kwanza?
1. Hebu tubadili kisa chote. Chukulia kwamba baada ya Yesu kufa Roho yake ilirejea mbinguni kwa ushindi na hivyo Shetani alishindwa. Je, wanafunzi wote wangekuwa kama Tomaso? (Inaonekana kuwa haiwezekani kuwa na madai tofauti na hayo. Kujitokeza kwa Yesu ndiko kulikowabadilisha kutoka mafichoni nyuma ya milango iliyofungwa.)
2. Kama kufufuka kwa Yesu ni muhimu kwenye mustakabali wa imani, ufufuo wetu ujao ni wa muhimu kiasi gani kwenye imani? (Kama Ukristo ulikuwa mfululizo wa roho nyingi zipenyazo kuingia mbinguni, ingekuwa vigumu kuyachukulia madai hayo kwa dhati.)
II. Wengine Wafufuka
A. Soma Mathayo 27:50-53. Utaona kwamba hili lilitokea mara tu baada ya kifo cha Yesu. Kwa nini? (Huu wote ni uthibitisho kwamba Yesu ni Masihi na amekishinda kifo. Pazia la hekalu linalotenganisha Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu linapasuka. Mfumo wa kutoa kafara unafikia ukingoni. Watu wanafufuliwa. Madai ya Shetani juu ya maisha yetu yanafikia ukingoni.)
B. Soma Mathayo 27:54. Ni nini athari ya matukio haya kwa askari wa kidunia? (Waliamini kwamba Yesu alikuwa Mungu.)
C. Angalia tena Mathayo 27:51-52. Ikiwa watakatifu hawa walifufuliwa mara tu baada ya kifo cha Yesu, kwa nini Yesu hakuruka kutoka msalabani na Kwenda mbinguni huku akiwa amezungukwa na malaika katika utukufu? (Pumziko la Yesu kaburini halina mantiki yoyote isipokuwa kwenye suala la ushindi wa pumziko la Sabato. Kama ambavyo Yesu alipumzika ili kuadhimisha uumbaji wake wa ulimwengu (Mwanzo 2:1-3), vivyo hivyo Yesu anaadhimisha ushindi wa kuukomboa uumbaji.)
III. Kusherehekea Ushindi
A. Soma 1 Wathesalonike 4:16-18. Ni nini sababu ya kuwepo kwa vifungu hivi? (Kifungu cha 18 kinasema kuwa wanatakiwa kutufariji.)
1. Kutufariji juu ya nini? (Soma 1 Wathesalonike 4:13-14. Tunapewa tumaini kwamba waliokufa watafufuka tena. Kwa kuwa Yesu alifufuka, tunaweza kuwa na uhakika kwamba tutafufuka kutoka kaburini.)
a. Kwa nini Wakristo wahitaji farijiko hili ikiwa roho za walioondoka tayari zilikuwa mbinguni? (Ama dhana ya roho zenye ufahamu kuwa mbinguni si ya kweli, au ni vigumu sana kuendelea kushikilia imani kama hiyo kiasi cha kuhitaji neno la faraja.)
B. Soma Waebrania 9:28 na Ufunuo 1:7. Je, hii inaonekana kama hitimisho – ambapo tuna washindi na washindwa wa dhahiri?
1. Fikiria nyuma kwenye sehemu ya utangulizi. Je, ufufuo wa mwisho unafanana na mwisho wa mchezo ambapo tuna mshindi na mshindwa wa dhahiri?
2. Watakatifu tuliowajadili katika sehemu iliyotangulia walipofufuka wakati Yesu alipokufa, je, hicho kilikuwa kionjo cha ushindi wa mwisho?
C. Soma Yohana 14:3. Kama roho yako kule mbinguni ina ufahamu kamili na inaweza kuzungumza na Yesu, je, hii kauli juu ya Yesu kuja tena “kutuchukua mwenyewe” ina mantiki yoyote?
D. Soma Ufunuo 22:12 na Mathayo 16:27. Vifungu hivi vinasema kuwa angalao jambo gani ni sehemu ya sababu ya ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Kushughulikia mambo ambayo wanadamu wameyatenda.)
1. Je, hii inaonekana kama matokeo sare baada ya mchezo kukamilika?
2. Hii inatuambia nini juu ya imani ya kwamba wanadamu wanakwenda mbinguni au jehanamu kabla ya matokeo ya mwisho kufahamika? (Hii inahafifisha dhana hiyo.)
E. Soma Yohana 6:39-40. “Kila” ambaye Yesu alipewa ni kitu gani? (Yesu anawazungumzia wafuasi wake.)
1. Kitu gani sasa kinafufuliwa “siku ya mwisho?” (Wafuasi wa Yesu.)
a. Ikiwa roho za wafuasi wa Yesu zinakwenda mbinguni moja kwa moja, je, inaleta mantiki gani kuzizungumzia zikifufuliwa katika siku za mwisho?
F. Soma Ufunuo 20:11. Inamaanisha nini kusema “mbingu na nchi zikakimbia?” (Soma Ufunuo 21:1. Inatuambia kuwa katika kipindi fulani mbingu na nchi “zitapita.”)
G. Soma Ufunuo 20:12. Je, wafu hawa ni pamoja na wenye haki? (Kutajwa kwa Kitabu cha Uzima kunajenga hoja juu ya hilo.)
H. Soma Ufunuo 20:13-15. Je, hapa ndio “mwisho wa mchezo” kwenye pambano kati ya wema na uovu? (Naam.)
1. Je, maelezo ya “kusimama mbele ya kiti cha enzi” yanaonekana kama ufafanuzi wa roho, au miili? (Miili ya dhahiri.)
2. Kama tangazo la hukumu ya mwisho linafanyika wakati wa (au mara tu baada ya) ujio wa Yesu Mara ya Pili, je, hilo linaendana na roho za watakatifu ambao tayari wanaishi mbinguni, na wameishi mbinguni kwa maelfu ya miaka? (Haliendani na madai ya roho zilizopo mbinguni.)
I. Soma Ufunuo 20:4-6. Kipindi hiki cha miaka kinaendanaje na dhana nzima? (Lazima hapa ni kabla ya tukio tulilolisoma hivi punde katika Ufunuo 20:13-15.)
1. Tuna ufufuo wa aina ngapi? (Mbili. Ufufuo wa kwanza kwa ajili ya wenye haki na ufufuo wa pili kwa ajili ya waovu.)
2. Hiyo inahusianaje na ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Waumini kabla ya Milenia, ambao mimi ni mmoja wao, wanaelewa kwamba wakati wa ujio wa Yesu Mara ya Pili wenye haki waliokufa watafufuliwa, na wenye haki walio hai watachukuliwa mbinguni (1 Wathesalonike 4:16-17) na kuishi miaka elfu moja. Baada ya hapo Yerusalemu Mpya itashuka duniani, waovu watafufuliwa na hukumu yao kutangazwa. Mungu ataiangamiza dunia ya kale na kuumba dunia mpya ambayo Yerusalemu Mpya itakuwa juu yake.)
J. Rafiki, pambano kuu kati ya wema na uovu linafikia ukingoni. Pambano hilo lina hitimisho la kuvutia. Kwa kuwa Yesu alifufuka tunafahamu kwamba katika ujio wake Mara ya Pili tutafufuka na kwenda pamoja naye mbinguni. Je, utamchagua Yesu sasa hivi? Kwa nini unachelewa?
IV. Juma lijalo: Tumaini la Agano Jipya.