Somo la 9: Vifungu Vinavyokinzana?

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Luka 16 & 23, Yohana 20, 1 Petro 3, Ufunuo 6)
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
4
Lesson Number: 
9

Somo la 9: Vifungu Vinavyokinzana?

(Luka 16 & 23, Yohana 20, 1 Petro 3, Ufunuo 6)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kila ninapojiandaa kwenda kujenga hoja mbele ya mahakama, huwa ninajaribu kufikiria maswali yote ambayo ninaweza kuulizwa na majaji. Huwa ninatafakari kwa makini juu ya lile linaloweza kuwa jibu sahihi, kisha ninalifanyia kazi jibu hilo kwa kurudiarudia. Lengo ni kuepuka kuulizwa swali ambalo sijalifikiria, na kisha, mambo yanapopamba moto, ninajaribu kuja na jibu lenye ushawishi. Tunapaswa kufanya vivyo hivyo linapokuja suala la imani zetu za Kikristo. Tunatakiwa kuyatafakari maswali magumu na kuandaa kwa umakini mkubwa jibu madhubuti la kuvutia. Kama ilivyo kwa mambo mengine, Roho Mtakatifu huniongoza kwenye tafakari bora. Katika somo letu juma hili, hebu tuungane na Roho Mtakatifu, tutafakari maswali magumu juu ya hali ya wafu, na tuchimbue kwa kina majibu madhubuti ya Biblia!

I.  Visa Visivyo vya Kawaida

A.  Soma Luka 16:1-2. Kwa nini meneja anafukuzwa kazi? (Ameshindwa kusimamia mali za bwana wake.)

B.  Soma Luka 16:3. Tatizo gani la msingi lipo mawazoni mwa meneja? (Nitaishije? Nitajipatiaje mahitaji?)

C.  Soma Luka 16:5-7. Unalizungumziaje suluhisho la meneja? (Sio la uaminifu hata kidogo. Linaakisi sababu ya kufukuzwa kwake kazi – hayaweki mbele maslahi ya bwana wake.)

D.  Soma Luka 16:8-9. Nani anazungumza hapa? (Yesu!)

1.  Umejifunza nini kutokana na kisa hiki? (Kwamba kutokuwa mwaminifu na mbinafsi, hususani kama una ustadi wa kufanya hivyo, ndicho anachokitukuza Mungu.)

E.  Soma Luka 16:10. Je, hitimisho hili linaendana na kisa? (Hapana. Ukisoma Luka 16:11-13 Yesu anasisitiza hitimisho lake kwamba ukweli na uaminifu ni mambo ya msingi. Lazima “tuutumikie” ukweli badala ya kutumikia msukumo wa kuwa tajiri.)

1.  Je, ni kwa bahati tu Yesu anaelezea kisa ambacho kinakinzana kabisa na kile anachokisema? (Yesu anatutaka tuangalie zaidi mambo ya dhahiri ili kuelewa anachokimaanisha. Anachokimaanisha ni kwamba tunatakiwa kuwa werevu zaidi ya ulimwengu na kutumia zana za ulimwengu kuutangaza Ufalme wa Mungu. Usipotumia njia bora, unamwibia Mungu.)

F.  Soma Luka 16:19-23. Umejifunza nini kutokana na kisa hiki? (Maskini mgonjwa anakwenda mbinguni. Tajiri mwenye lishe bora anakwenda kuzimu.)

1.  Je, hilo linaendana na mafundishi ya Biblia? Dhana hiyo ikitumiwa leo, je, watu wasio na makazi na wagonjwa wanakwenda mbinguni moja kwa moja? Je, tunaweza kupata taswira ndogo ya mbingu kwa kwenda Los Angeles na kutembelea kambi za watu wasio na makazi?

G.  Soma Luka 16:24-25. Katika kisa hiki Ibrahimu anasema wale waliokuwa na maisha mazuri wanateseka na wale waliopitia uzoefu wa mambo mabaya wanaifurahia mbingu. Ibrahimu aliishiaje na kujikuta yupo mbinguni? Alikuwa mtu tajiri mwenye mafanikio! Kati ya watu wote, hapaswi kuwa kuzimu? (Hiki ni kisa kingine kisicholeta mantiki. Kinakinzana na mafundisho ya Musa anayehusianisha utii na baraka na kutokutii na laana. Kumbukumbu la Torati 28.)

H.  Soma Luka 16:27-28. Tajiri anataka nini? (Lazaro asafiri kwenda duniani na kuwaonya ndugu zake watano. Ninachokibashiri ni kuwa onyo lile ni kwamba wanatakiwa waache mara moja kuwa matajiri.)

I.  Soma Luka 16:29-31. Je, kwa mara nyingine Yesu anatutaka tuangalie viashiria vya dhahiri (na makosa ya wazi) vya kisa hiki ili kubaini anachokimaanisha? (Kama ambavyo Yesu alikuwa hatukuzi vitendo visivyo vya uaminifu katika kisa cha kwanza, haashirii kipimo cha hukumu au kufundisha juu ya hali ya wafu katika kisa hiki.)

1.  Yesu anamaanisha nini? (Wale “wasioisikia” Biblia “hawatamsikia” Yesu mfufuka. Kisa hiki hakihusu hali ya wafu.)

II.  Sarufi na Vituo vya Uandishi (Punctuation)

A.  Soma Luka 23:39-43. Ni nani atakayekwenda “peponi” leo? (Yesu na mmojawapo wa wahalifu aliyesulubiwa pamoja naye.)

1.  Je, utetezi wetu juu ya hali ya wafu unahusiana na vituo vya uandishi (punctuation) – ambavyo lugha ya asili ya Kiyunani haikuwa navyo? Je, tuhamishe alama ya koma (,) kutoka kabla ya “leo” hadi baada ya “leo?” (Ninadhani hoja ya kuhamisha alama ya koma haina ushawishi. Kama ungekuwa unazungumza na mtu, je ungesema, “Leo ninazungumza?” Kimsingi hapana. Ni dhahiri kwamba unazungumza sasa hivi.)

B.  Soma Yohana 20:15-17. Hii inazungumzia nini juu ya Yesu kumtembelea Baba yake Peponi siku ya Ijumaa (siku ya kusulubiwa kwake)? (Hii haigeukii kwenye vituo vya uandishi. Yesu anamwambia Mariamu kwamba bado hajapaa kwenda kwa Baba yake na Peponi.)

C.  Tuna ukinzani wa dhahiri kati ya kauli mbili za Yesu. Unalitatuaje hili? (Kwanza, alichokizungumza Yesu msalabani haikuhusiana na muda, kilihusu wokovu. Wakati alichokimaanisha kwa Mariamu kwa mahsusi kilihusu kurejea kwa Yesu mbinguni. Pili, kwenye mjadala wa Kiyunani niliona kuwa “nakuambia leo” ni lahaja ya Kiebrania ikielezea uhakika wa jambo. Ni sawa na kusema katika Kiingereza cha kisasa “Unaweza kuipeleka benki” (you can take this to the bank). Hakuna atakayedhani kuwa unapaswa kusafiri kwenda benki. Usemi huo unahusu kuaminika. Anachokisema Yesu hasa kwa mhalifu ni “Unaweza kuwa na uhakika wa wokovu.” Uelewa huu unatatua mgongano kati ya kile Yesu alichomwambia mwizi na kile alichomwambia Mariamu.)

III.  Kuzihubiri Roho

A.  Soma 1 Petro 3:18-20. Hawa “roho waliokaa kifungoni” ni akina nani? (Wale waliokataa kuyatii maonyo ya Nuhu.)

1.  Jela hii iko wapi? (Lazima ni kule kuzimu.)

B.  Je, Yesu alikwenda mbinguni na kisha kuzimu? (Kuna watu wanajenga hoja kwamba Yesu alikwenda kuzimu kuhubiri baada ya kifo chake, lakini kabla ya ufufuo wake.) 

1.  Hebu tujikite katika 1 Petro 3:18-19. Huyo “he” (aliyewaendea…… akawahubiri) ni nani katika kifungu cha 19? (Rejea ya awali inamrejelea Roho Mtakatifu. Usomaji wa kawaida wa kifungu hiki unabainisha kuwa Yesu alihubiri kwa njia ya Roho Mtakatifu.)

2.  Swali linalofuata ni kwa nini baadhi ya watu wanadhani kuwa hili lilitokea Yesu alipokuwa kaburini? (Kifungu hakisemi hivyo.)

C.  Soma tena 1 Petro 3:20. Je, hii inajibu swali la “ilikuwa lini?” (Ndiyo, kifungu kinasema katika siku za Nuhu Mungu alikuwa mvumilivu.)

D.  Soma Isaya 14:16-17. Je, wadhambi wapo gerezani? (Ndiyo. Hii inalibainisha hilo. Yesu hakwenda kuzimu. Kabla ya kufanyika kuwa mwanadamu Yesu alitenda kazi kwa njia ya Roho ili kuiongoa hadhira ya Nuhu.)

IV.  Roho Zilizo Chini ya Madhabahu

A.  Soma Ufunuo 6:9-11. Haya ni mojawapo ya maneno magumu kabisa, angalao kwa haraka haraka, kwa sababu kwa umahsusi yanarejelea “roho” zenye ufahamu mbinguni ambazo ziliifia dini kwa ajili ya imani yao. Je, roho hizi zinaweza kufanya mazungumzo ya busara? (Ndiyo, kwa mujibu wa kifungu.)

1.  Je, roho hizi zina miili? (Lazima zinayo, vinginevyo wangekuwa wanafanya nini wakiwa wamevaa mavazi meupe?)

2.  Ikiwa zina miili, je, hiyo inamaanisha kuwa walifufuliwa? (Muktadha unatuambia kuwa hii ni kabla ya ujio wa Mara ya Pili, vinginevyo wasingekuwa wanalalamikia juu ya kutokuwepo kwa hukumu. Hivyo, ufufuo wao ni kabla ya ujio wa Yesu Mara ya Pili.)

3.  Kama tukikomea hapa, je kisa hiki hakiendani na fundisho la kulala kwa roho – wafu wanasubiria ufufuo wakati wa ujio wa Mara ya Pili? (Hapana, kwa sababu inaakisi jambo lisilo la kawaida tulilolijadili hapo awali: ufufuo wa Musa (Yuda 9). Kama Mungu alimfufua Musa na kumchukua mbinguni, kwa hakika angeweza kufanya hivyo kwa wengine.)

B.  Hebu tuchunguze taarifa kadhaa kwa kina. Soma Ufunuo 6:10. Je, inaonekana kuleta mantiki kwamba watu wanalalamika mbinguni? Je, watakuwa wanatafuta kulipiza kisasi? Linganisha Luka 23:34 na Matendo 7:59-60.

C.  Soma tena Ufunuo 6:9. Kama una malalamiko mbinguni, je, itaeleweka kwa malalamiko hayo kutoka kwa wale waliolazimishwa kuishi “chini ya madhabahu?”

1.  Soma Mambo ya Walawi 4:18. Je, hii ni ishara ya mahali roho hizi zinapoishi? (Ndiyo. Hii haionekani kuwa mahali pa kuishi kule mbinguni.)

D.  Soma tena Ufunuo 6:11. Tafakari jibu la malalamiko yao: rudini mkalale. Je, hiyo inaonekana kuleta mantiki, au kuendana na kuishi peponi?

E.  Kuna matatizo mengi kwenye maelezo haya endapo yatachukuliwa kiuhalisia. Hiyo inatupatia sababu ya kuamini kuwa hili ni jambo la kiishara – na hivyo taarifa za kina hazizungumzii chochote kuhusu hali ya wafu.

F.  Rafiki, tutajua jibu la kweli tutakapofika mbinguni, lakini upande huu wa mbingu ninadhani Biblia inafundisha kwamba wafu wenye haki wanalala hadi ujio wa Yesu Mara ya Pili. Je, unakubaliana?

V.  Juma lijalo: Mioto ya Kuzimu.