Somo la 4: Sadaka kwa Ajili ya Yesu

2 Wakorintho 9, Marko 12
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
4

Somo la 4: Sadaka kwa Ajili ya Yesu

(2 Wakorintho 9, Marko 12)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Miaka mingi iliyopita nilikuwa ninajitolea kufanya kazi za mikono zinazotumia nguvu kanisani. Nilikuwa mdogo na mmojawapo wa washiriki wa kanisa aliyekuwa mtu mzima alikuwa anajadiliana nami juu ya masuala ya fedha katika ngazi ya familia. Alipojua kwamba mimi na mke wangu tulikuwa na akaunti moja ya benki alishangaa, “Vipi kama mkeo akikimbia na fedha zako?” Kiukweli, sikuwa nimeliwaza hilo kabla. Nilimjibu kwamba ningewaza zaidi kuhusu kumpoteza mke wangu kuliko kupoteza fedha. Alistaajabishwa na jibu langu. Kwa upande wake, fedha zilikuwa na kipaumbele kuliko mke wake. Mazungumzo yale yanafanana na somo letu la juma hili. Kama kazi yangu ya kuandika somo hili ni kukushawishi utoe sadaka za hiari, basi tatizo lililopo sio fedha, bali mtazamo wako kwa Mungu. Juma hili tunapoendelea kujifunza Biblia hebu tujikite zaidi kwenye mtazamo wetu kwa Yesu!

I.  Upendo ni nini?

A.  Soma 2 Wakorintho 9:1. Paulo anapowaandikia Wakorintho na kusema “hana haja” ya kuwaandikia juu ya mambo ya fedha, anazungumzia nini? (Anasema kuwa hakuna umuhimu wa yeye kuandika.)

1.  Je, anamaanisha hicho alichokisema? Kama anamaanisha, kwa nini anawaandikia kuhusu fedha?

B.  Soma 2 Wakorintho 9:2. Paulo amewaambia nini Wakristo wa Makedonia juu ya Wakristo wa Korintho? (Amekuwa akijivunia juu ya ari yao (furaha yao) katika kutoa fedha.)

C.  Soma 2 Wakorintho 9:3-4. Je, kuna tatizo lolote? Kwa nini Paulo anawaza juu ya kufedheheshwa atakapokuja, hususani kama ataongozana na Wamakedonia? (Kwa dhahiri Paulo anaamini anaweza kukumbana na tatizo. Ana wasiwasi kwamba inawezekana Wakristo hawajachangia fedha ambazo alijigamba kuwa zilikuwa zinachangwa.)

D.  Soma 2 Wakorintho 9:5. Paulo amechukua uamuzi wa kufanya nini ili kuepuka kuaibika? (Anawatanguliza watendakazi wenzake ili kuhakikisha kuwa Wakorintho wanatoa zawadi walizoahidi kuzitoa.)

1.  Angalia maneno ya mwisho, “ili iwe tayari, na hivi iwe kama kipawa, wala si kama kitu kitolewacho kwa unyimivu.” Unaweza kuelezea ni kwa jinsi gani kutanguliza timu ili kuhakikisha kuwa fedha ziko tayari kunaepusha jambo hili kuwa “unyimivu?”

2.  Tuchukulie kwamba umeahidi kuninunulia gari jipya. Ninakuambia kwamba ninawatuma vijana kadhaa ili kuhakikisha kuwa gari hilo jipya liko tayari kwa ajili yangu. Una maoni gani? Je, utaichukulia hii kama “kipawa cha hiari?”

E.  Soma 2 Wakorintho 9:6. Jambo hili linawashawishije Wakorintho kutoa kwa ukarimu?

1.  Je, hii ni sawa na kusema, “maana najua utayari wenu wa kutoa?” (Hapana. Paulo anasema kuwa ukitoa kidogo, utabarikiwa kidogo. Ukitoa zaidi, utapokea zaidi.)

F.  Sura ya 8 ya kitabu cha 2 Wakorintho inatoa muktadha mkubwa kuelekea Sura ya 9. Hebu tusome 2 Wakorintho 13-14. Hapa Paulo anajenga hoja gani kwa Wakorintho inayoendana na ukarimu? (Huu unaonekana kama mpango wa bima! Unapokuwa na ziada, unawapatia. Unapokuwa na uhitaji, watakupatia ziada yao.)

G.  Kama sisi ni waaminifu, na mara zote tunapaswa kuwa waaminifu, je, hoja za Paulo zinaonekana kujengwa juu ya upendo?

1.  Sabato iliyopita, nilipofundisha darasa langu la kujifunza Biblia tulijadili Malaki 3, na baadhi ya wanadarasa walikuwa wanahoji hoja yangu kwamba Mungu alikuwa anatoa zawadi ya usitawi kwa wanaotoa zaka. Mmojawapo wa wanadarasa alitoa maoni kwamba hoja ya usitawi ilikuwa ni kwa ajili wa waongofu wapya. Kwa Wakristo wakomavu nia ni kubwa zaidi, ambayo ni upendo. Je, unakubaliana naye? (Ninakubaliana kwamba hili ni jambo la msingi. Lakini, ni suala gumu.)

H.  Hebu tupitie sehemu yangu ya Utangulizi kuhusiana na mshiriki wa kanisa wa zamani ambaye alijali sana fedha zake kuliko mkewe. Unadhani kwa nini nilikuwa ninamjali zaidi mke wangu kuliko fedha,  na kwa nini mshiriki huyu alizijali zaidi fedha zake kuliko mkewe? (Mke wangu alithibitika kuwa wa muhimu zaidi kuliko fedha.)

1.  Unadhani kwamba tulipooana, alijiambia, “bora nithibitishe thamani yangu?” Unadhani nilisema, “Hebu tuone kama mke wangu mpya ni bora kuliko fedha?” (Kimsingi, Hapana. Tulipendana, na upendo huo ukatuhamasisha kuenenda kwa namna iliyoonesha tulikuwa na thamani kwa sababu nyingine tofauti na upendo.)

I.  Paulo anaponadika katika 2 Wakorintho 9 kwamba amekuwa akijivunia juu ya Wakorintho, na hataki wamdhalilishe. Anapoandika katika 2 Wakorintho 8 kwamba utoaji ni sawa na bima, je, hii inahusiana na upendo? (Nitajenga hoja kwamba, “ndiyo.” Kipengele kimojawapo cha upendo wangu kwa mke wangu ni kwamba hanidhalilishi mbele za watu. Kumpenda kumetokea kuwa na manufaa makubwa nje ya huba pekee.)

1.  Je, tunaweza kuhitimisha kwamba Paulo anapoandika juu ya mambo yaliyo kwenye taswira ya upendo, lakini ambayo kwa yenyewe sio upendo, kwamba bado anazungumzia upendo?

2.  Hebu tujaribishe dhana hii. Kwa nini unampenda Yesu ambaye kamwe hujawahi kumwona? Je, hii inahusiana na kile ambacho amekutendea wewe na wale unaowapenda? (Tunatakiwa kuelewa kwamba upendo sio jambo dhahania, upendo wa mwanadamu unatokana na uzoefu.)

II.  Kipimo cha Upendo

A.  Soma 2 Wakorintho 9:7. Kwa nini mtu awe na ukarimu kwenye suala la kutoa fedha? (Je, unapenda kuwapatia zawadi watu wengine? Ikiwa ndivyo, unaelewa jinsi unavyoweza kujisikia furaha katika kuwasaidia wengine.)

1.  Unadhani maneno “atende kama alivyokusudia moyoni mwake” yanamaanisha nini? (Inamaanisha kwamba tunapaswa kutoa kwa kudhamiria kama msemo wa sasa, “matendo ya wema yasiyo na utaratibu maalumu” yanayoakisi fikra za kibwege. Kwa nini usiwe na utaratibu maalumu wakati una fursa ya kutenda mema kwa kutumia fedha zako kwa upeo wa juu?

B.  Soma 2 Wakorintho 9:8. Sasa Paulo anatupatia sababu ya kutafakari kwa umakini kiasi tunachokitoa kama sadaka. Ni sababu gani hiyo? (Mungu atakurehemu kwa maana ya kwamba mna “riziki za kila namna siku zote.”)

C.  Soma 2 Wakorintho 9:10. Hapa mtu mkarimu anapitia uzoefu wa aina gani ya mazao? (Paulo anatuambia kuwa sababu nyingine ya kuwa mkarimu ni kwamba inatufanya tuwe watu bora zaidi. Tunavuna “haki.” tunatenda mema.)

D.  Soma 2 Wakorintho 9:11-14. Jambo gani jingine jema linatokana na ukarimu? (Utoaji hutusitawisha na hata kutufanya kuwa wakarimu zaidi. Huduma yako inawafanya watu wamshukuru Mungu. Unautangaza Ufalme wa Mungu. Unampa Mungu utukufu.)

III.  Kipimo cha Mungu

A.  Soma Marko 12:41. Je, huu ni mchezo wa kutazama kiasi ambacho watu wanamtolea Mungu? (Ukweli kwamba Yesu na wanafunzi wake waliweza kulitazama hili inatuambia kuwa mamlaka zilitaka utoaji uwe jambo la wazi.)

1.  Unadhani matajiri walijisikiaje kuonekana wakitoa kiasi kikubwa cha sadaka?

B.  Soma Marko 12:42. Unadhani mwanamke huyu alijisikiaje? Je, alijisikia kufedheheka kutoa kiasi kidogo sana cha fedha? Je, watu wanapenda kutangaza kwamba wao ni masikini?

C.  Soma Marko 12:43. Yesu anawezaje kutoa kauli hii? Kwa dhahiri alichangia kiasi kidogo sana kuliko watu wote.

D.  Soma Marko 12:44. Yesu anatoa ufafanuzi gani juu ya maoni yake kwenye kiasi kilichotolewa? (Anasema kuwa alitoa kila alichokuwa nacho. Alitoa “riziki yake yote.”)

1.  Je, mjane huyu atakufa njaa? Je, hilo ndilo lengo la utoaji? (Isipokuwa kama kila tulichokuwa tukijifunza juu ya utoaji na matokeo yake ni baraka ni uongo, mwanamke huyu hatakufa njaa. Atabarikiwa.)

2.  Tutafakari mtazamo wa mjane juu ya utoaji. Ni kwa namna gani basi yuko kwenye hali hii? Haiendani na kile tulichojifunza. Kwa mtazamo huo juu ya utoaji anapaswa kuwa tajiri! (Yesu anaonekana kumaanisha jambo dogo - kwamba haijalishi kiasi unachokitoa, bali ni endapo kipawa kinamaanisha jambo lolote kwako.)

3.  Yesu anamaanisha nini kwenye suala la matajiri kutoa “mali iliyowazidi” na mjane kutoa “riziki yake yote?” (Anachokimaanisha ni kwamba matajiri wanaweza (na walifanya hivyo) kuzitumaini fedha zao. Mjane alimtumaini Mungu.)

E.  Rafiki, Mungu anakupenda. Matokeo ya upendo wako kwake ni tamaa ya kuwa mkarimu kwa wengine. Lakini hiyo tamaa ya awali ni mwanzo tu wa mambo. Unapokuwa unatoa, unabarikiwa kwa namna zote zinazokuhamasisha kutoa zaidi. Kwa nini usifanye uamuzi leo wa kumtumaini Mungu na kuwa mkarimu kwa kazi ya Mungu?

III.  Juma lijalo: Kukabiliana na Deni.