Somo la 1: Yesu Anashinda – Shetani Anashindwa
Somo la 1: Yesu Anashinda – Shetani Anashindwa
(Ufunuo 12)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, una matumaini mema juu ya siku zijazo? Ninasoma kitabu kilichoandikwa na Jonathan Cahn kiitwacho “The Return of the Gods” (Kurejea kwa Miungu.) Cahn anajenga hoja kwamba miungu ya kipagani iliyokuwa ikitawala katika kipindi cha Agano la Kale na ambayo wafuasi wake walisababisha matatizo mengi sana kwa Kanisa la awali la Kikristo ilitokomezwa kutokana na kuibuka kwa Ukristo. Kwa zaidi ya miaka mia mbili miungu hiyo pamoja na mahekalu yao vimekuwa nje ya utendaji kazi. Sasa, kutokana na kuporomoka kwa Ukristo katika nchi za Magharibi, sasa vimeanza kurejea. Kimsingi, sanamu iliyotengenezwa kwa mkono wa mwanadamu si lolote wala chochote. Hata hivyo, tafakari jinsi wafuasi wa Shetani wa kimiujiza wanapoamua kuzitumia sanamu hizi, miungu hii, kwa malengo yao wenyewe. Mgongano huu ni sehemu ya msingi ya pambano la kilimwengu kati ya wema na uovu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
I. Shetani Anaanguka
A. Soma Ufunuo 12:7-9. Nyumbani kwao Shetani na malaika wake ni wapi? (Mbinguni! Wote walianzia mbinguni.)
1. Sababu ya mgogoro ni ipi? (Hatuambiwi kwenye vifungu hivi. Tutaliangalia hilo baadaye.)
2. Nani anayeonekana kuanzisha pambano? (Mikaeli na malaika wema. Kwa sababu gani? Kwa sababu kifungu kinasema kuwa joka na malaika wake walijibu mapigo.)
3. Nani alishinda? (Mikaeli na malaika wake walimshinda Shetani na malaika wake.)
4. Matokeo ya kushindwa huku ni yepi? (Shetani na malaika wake walifukuzwa na kutupwa duniani.)
5. Katika maeneo yote yaliyokuwepo, kwa nini walitupwa duniani? (Wanadamu walikubali kubadili utiifu wao na kumpa Shetani. Angalia Mwanzo 3.)
B. Soma Ufunuo 12:3-4. Unadhani kitu gani kinawakilishwa na “nyota za mbinguni?” (Utaona kwamba nyota hizo zinaangushwa duniani. Hiki ndicho kwa hakika kile tulichosoma kuwa kilimtokea Shetani (aliyeitwa joka) na wafuasi wake. Hivyo, tunapaswa kuelewa kuwa nyota hizi ni malaika walioanguka.)
1. Tunapewa taarifa gani ya ziada kuhusu pambano hili la kutisha mbinguni? (Tunaambiwa kuwa theluthi ya malaika waliasi. Mikaeli alikuwa na idadi ya malaika mara mbili zaidi upande wake.)
C. Soma Isaya 14:12-14. Hii inahusianisha kufukuzwa kwa Shetani kutoka mbinguni na sababu ya kufukuzwa huko. Kwa nini Shetani alitupwa kutoka mbinguni? Kitu gani kilisababisha pambano litokee? (Ilikuwa ni kiburi. Ilikuwa ni uhaini. Shetani alitaka kujifanya kuwa kama Mungu.)
1. Tunapoamua kukubali sehemu ya Biblia na kuzikataa sehemu nyingine kwa sababu “tunafahamu zaidi,” je, huko ni kujiweka kwenye nafasi ya Mungu?
II. Mwanamke na Mtoto
A. Soma Ufunuo 12:1-2. Kifungu kinaposema hii ni “ishara,” hiyo inamaanisha nini? (Ishara inakuelezea kuhusu uhalisia wa namna fulani. Ishara ya Mgahawa wa McDonald inakuambia kuwa mgahawa halisi upo karibu.)
1. Ishara hii inahusu nini? (Soma Isaya 54:5-6. Mwanamke ni ishara ya watu wa Mungu.)
B. Soma Ufunuo 12:5. Huyu “mtoto mwanamume” ni nani? (Yesu. Israeli ilikuwa taifa teule la watu wa Mungu na mamaye Yesu alikuwa Myahudi. Hiyo inafanya rejea ya “mama” iwe na mantiki. Lazima hii ni rejea ya kuzaliwa kwa Yesu duniani. Kufanywa kwake kuwa na mwili wa kibinadamu na kurejea kwake mbinguni.)
C. Hapo awali tuligundua kwamba joka na wafuasi wake ni Shetani na malaika walioanguka na kufukuzwa na kutupwa duniani. Sasa ongezea kifungu cha sita: soma Ufunuo 12:5-6. Hiyo inatuambia nini kuhusu pambano? (Kwamba liliendelea duniani. Na Shetani aliendelea kushindwa duniani.)
1. Hilo lina umuhimu gani kwetu leo? (Soma Waebrania 1:2-3 na Waebrania 1:8. Waebrania inatuambia kuwa alifanya utakaso wa dhambi zetu! Inaonekana kwamba fimbo ya chuma inayorejelewa katika Ufunuo 12:5 ni “fimbo yake ya adili” inayorejelewa katika Waebrania 1:8. Hii sio tu kwamba inaimarisha dhana ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee, bali pia inatuambia kuwa nguvu ya ufalme wa Mungu ni haki inayotangazwa na sheria yake.)
a. Hiyo inatufundisha nini leo miungu ya kale inaporejea katika jamii yetu? (Tunamtegemea Yesu kwa ajili ya haki yetu. Tunaelewa kuwa hatuwezi kuishika sheria kikamilifu. Kwa upande mwingine, udhaifu wetu hautuzuii kuishika na kuing’ang’ania sheria ya Mungu kama kipimo sahihi cha maisha.)
III. Ushindi
A. Soma Ufunuo 12:10. Kitu gani cha kwanza kinatajwa kinachopaswa kutupatia furaha katika ushindi? (Wokovu. Ushindi wa Yesu hutupatia wokovu endapo tutamkiri na kumpokea.)
1. Kitu gani kingine kinaongezeka kwetu kwa njia ya ushindi wa Yesu? (Nguvu ya ufalme wa Mungu, mamlaka ya Yesu (kama Mshindi), na kushindwa kwa mshtaki wetu.)
2. Unadhani kauli ya mshtaki wetu “ametupwa chini” inamaanisha nini kwa kuzingatia mashtaka yake? Je, hana tena usikivu wa Mungu ili kutoa mashtaka dhidi yetu? (Inaonekana kama vile Shetani hana tena nafasi mbinguni ya kutushtaki mbele za Mungu. Hata hivyo, suala hili linakuwa gumu unapoitafakari Ayubu 1:6-9. Muktadha unatuambia kuwa mazungumzo haya yalifanyika baada ya Shetani kutupwa duniani, lakini kwa dhahiri bado Shetani alikuwa na fursa ya kumshtaki Ayubu mbele ya Mungu.)
B. Soma Zekaria 3:1-2. Hii inatuambia nini kuhusu uwezo wa Shetani kutushtaki mbele za Mungu? (Bado alikuwa akifanya hivyo katika nyakati za Agano la Kale.)
C. Soma Yohana 12:31-32 na uilinganishe na Wafilipi 2:9-11. Hii inatuambia nini kuhusu muda wa Shetani kuondoshwa kabisa mbinguni? (Yesu aliishinda dhambi msalabani na akachukua nafasi ya Shetani kama mtawala wa dunia. Ama kwa hakika, Yesu alikuwa mtawala wa ulimwengu wote. Shetani hakuweza kudai tena kwamba alikuwa mtawala wa dunia na hiyo ilihitimisha mamlaka yake ya kuingia mbinguni na kutushtaki.)
1. Ikiwa uwezo wa Shetani kutushtaki mbele ya Mungu sasa umedhoofishwa, unadhani anafanya nini? Je, sasa yuko nje ya kazi yake ya mashtaka? (Anatushtaki kupitia kwa wapagani. Anatushtaki kupitia kwa Wakristo wenzetu. Anatushtaki mawazoni mwetu.)
a. Jibu ni lipi? (Ameshindwa! Yesu alipata ushindi kwa ajili yetu.)
IV. Pambano Linaendelea
A. Soma tena Ufunuo 12:10-11. Msingi wa kudai ushindi wa Yesu ni upi? (Tunautazama msalaba. Tunatazama kile ambacho Mungu ametutendea. Tunaenenda kana kwamba haya sio maisha yetu pekee.)
B. Soma Ufunuo 12:12. Shetani anachukuliaje kushindwa kwake?
C. Soma Ufunuo 12:17. Shetani anamlenga nani? (Wale wazishikao amri za Mungu na wanaomwangalia Yesu kama chanzo cha wokovu.)
1. Unatarajia wapagani waenende vipi kwa kuzingatia mtazamo wa kiongozi wao? (Kifungu hiki kinasema kuwa Shetani “amekasirika” na anachokiwaza ni “vita.”)
2. Je, tunaliona hili leo? (Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Marekani, Stuart Kyle Duncan, ninayefundisha naye katika shule ya sheria ya Chuo Kikuu cha Regent, alikaribishwa kuzungumza katika mojawapo ya shule za sheria zinazoongoza nchini Marekani. Kundi la wanafunzi lilimvurumishia matusi jaji alipojaribu kuongea. Jaji Duncan anataarifu kuwa mwandamanaji mmojawapo alisema, “Natumai mabinti wako watabakwa.” Je, hili ni jambo tofauti na ushetani?
D. Yesu alipata ushindi dhidi ya Shetani na malaika wake walioanguka. Ushindi umepatikana vitani. Lakini, bado tunatakiwa kupambana na washindwa wenye chuki na washirika wao wa kibinadamu. Tunatakiwa kuwajibuje? (Soma Luka 23:34. Mfano wa Yesu ni kuwasamehe. Ingawa muda umeshapita kabisa kwa Shetani na malaika walioanguka pamoja naye, washirika wao wa kibinadamu bado hawajachelewa. Tafakari suala la wanafunzi niliowabainisha hivi punde, wangapi kati yenu mnayaangalia na kuyachukulia mambo kwa mwanga tofauti kuliko mlivyokuwa mkiyachukulia mlipokuwa wadogo?)
E. Rafiki, Yesu alishinda! Upande wetu ulishinda! Miungu ya kale inaweza kuwa inarejea, lakini lengo lao limepotea. Kama bado haujachukua uamuzi thabiti, kwa nini usiudai ushindi wa Yesu na kuwa mshindi sasa hivi?
V. Juma lijalo: Kipindi cha Majaliwa.