Somo la 9: Utume kwa Wenye Mamlaka

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Danieli 1-3, 2 Wafalme 5, Yohana 3
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
4
Lesson Number: 
9

Somo la 9: Utume kwa Wenye Mamlaka

(Danieli 1-3, 2 Wafalme 5, Yohana 3)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, umewahi kumwongoa mtu mwenye hadhi ya juu kumwamini Yesu? Agano la Kale lina maonyo mengi juu ya kutowalaghai au kuwawonea masikini, na kuwasaidia pale wanapohitaji msaada. Kwa namna fulani nadhani hilo linawasababisha Wakristo wajikite kwenye kuongoa roho za wale wenye mamlaka madogo. Hiyo haina maana yoyote kiuhalisia au Kibiblia (Mambo ya Walawi 19:15). Kama ungekuwa na kampuni ya kompyuta, je, ungependa kukusanya vikokotoo (calculators) vyenye uwezo mdogo au kompyuta zenye uwezo wa hali ya juu? Ingawa kila roho ina hadhi sawa mbele za Mungu, watu wenye mamlaka wana ushawishi mkubwa ambao masikini atapata ugumu sana kuendana nao. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuangalie jinsi Mungu alivyowatumia watu wenye ushawishi mkubwa kuendeleza kazi yake!

I. Danieli

A. Soma Danieli 1:1-2. Nini kimeitokea Yuda? (Imeanguka mikononi mwa Babeli.)

B. Soma Danieli 1:3-4 na Danieli 1:6. Je, Danieli alikuwa mtu wa hadhi ya juu kabla Yuda haijashindwa? (Ndiyo. Ama alikuwa mtu wa jamaa ya kifalme au alikuwa mtu wa daraja la malodi (nobility). Alikuwa mwerevu na aliyeelimika.)

C. Kisa cha Danieli kinaendelea kwa kufafanua kuwa Danieli anapewa mafunzo maalumu na watu wa Babeli. Matokeo yake ni kwamba, Danieli sura ya 2 inabainisha kuwa Danieli ni miongoni mwa kundi la watu wanaotarajiwa kufichua yaliyomo kwenye ndoto ya Mfalme Nebukadreza na maana yake. Soma Danieli 2:31-35. Unafahamu nini kuhusu hii ndoto? (Ukisoma Danieli 2:37-45 utaona kwamba ndoto hii inatoa taswira ya mustakabali wa ulimwengu ikiwemo ujio wa Yesu Mara ya Pili.)

D. Soma Danieli 3:1-2. Jambo gani limeitokea ile ndoto? (Sasa inaakisiwa isivyo sahihi kwenye hii sanamu kubwa ambayo watu kutoka pande zote za ufalme wataiona.)

1. Chukulia kwamba Mungu alimpa mtu asiye na makao ndoto hii na Danieli akamtafsiria ndoto hiyo. Ingeenda mbali kiasi gani? (Uwezekano mkubwa ni kwamba isingefika popote. Kwa sababu Nebukadreza ndiye mlengwa wa ujumbe wa Mungu, mfalme anausambaza ujumbe huo kila mahali.)

a. Je, umegundua kwenye kisa hiki tatizo la kuwalenga matajiri na wenye mamlaka kuhusiana na injili? Tatizo hilo ni lipi? (Uwezekano mkubwa ni kwamba mtu mwenye mamlaka na nguvu na majivuno. Kutokana na majivuno yake, Nebukadreza anatafsiri vibaya ndoto kwa kutengeneza sanamu.)

II. Naamani

A. Soma 2 Wafalme 5:1-2. Nani aliyeipatia Shamu ushindi? (Kifungu kinasema kuwa Mungu ndiye aliyewapatia ushindi.)

1. Tunamwona nani kwenye kifungu hiki anayekukumbusha juu ya Danieli? (Mwanamke kijana asiye na jina.)

a. Je, kuna ishara yoyote kwamba binti huyu, kama ilivyo kwa Danieli, alikuwa mtu mwenye hadhi ya juu na maarifa makubwa? (Hapana.)

B. Soma 2 Wafalme 5:3-5. Kwa nini Naamani anamwamini binti huyu? (Lazima patakuwepo na taarifa za ziada kwenye kisa hiki. Ingawa inawezekana Naamani alikuwa tayari kufanya lolote (desperate), lazima binti huyu alionesha sifa za pekee. Mojawapo ya sifa hizo ni kwamba alikuwa mtu anayeaminika.)

C. Soma 2 Wafalme 5:6-7. Mfalme wa Israeli alilichukuliaje ombi la Mfalme wa Shamu? (Alidhani kuwa lilikuwa ni jaribio la kuanzisha vita.)

1. Mfalme wa Israeli ni mtu muhimu na mwenye nguvu/mamlaka. Kimantiki alikuwa mtu sahihi wa kupeleka habari za Mungu kwa Naamani na kwa Mfalme wa Shamu. Kwa nini asimtumie? Kwa nini amtumie binti huyu asiye na uwezo wala ushawishi wowote?

D. Soma 2 Wafalme 5:8-10. Mfalme wa Israeli amekosea wapi? (Hayuko makini kwenye fursa za kupeleka injili kwa wengine.)

1. Elisha amekosea wapi? Kwa nini asitumie fursa hii kumuinjilisha mtu mwenye mamlaka makubwa badala ya kumdhihaki?

E. Soma 2 Wafalme 5:11-13. Nani anayeokoa jahazi kwa Naamani? (Watumishi wake.)

1. Tunaona changamoto gani nyingine tena ya kuwashuhudia watu wenye mamlaka? (Majivuno yao ni tatizo.)

2. Je, unadhani Elisha alilitarajia hili hivyo kufanya majivuno kuwa kipimo kwa Naamani? Je, hiyo ndio sababu Elisha hakumpokea Naamani?

F. Soma 2 Wafalme 5:14. Je, majivuno haya yanakuzuia kupokea fursa nyingi zaidi na manufaa kutoka kwa Mungu?

G. Soma 2 Wafalme 5:15-16. Jambo gani limetokea ambalo litautangaza Ufalme wa Mungu kwa kiasi kikubwa? (Mojawapo ya watu wenye mamlaka makubwa kabisa katika nchi ya Shamu sasa anamkiri Mungu wa kweli.)

H. Soma 2 Wafalme 5:17. Jambo gani linaendelea hapa? Kwa nini Naamani anatoa ombi hili la kushangaza? (Dhana maarufu iliyokuwepo ni kwamba mungu alikuwa mtawala juu ya nchi yake. Sasa Naamani anaamini kuwa Mungu wa Israeli ni mtawala juu ya mamlaka zote, lakini anadhani kuwa anahitaji udongo kutoka Israeli ili aweze kumwabudu Mungu kikamilifu atakaporejea katika nchi ya Shamu.)

I. Soma 2 Wafalme 5:18. Naamani anahofia nini? (Kwamba ataonekana kama anamwabudu Rimoni kwa kumwinamia mungu huyo.)

1. Naamani anamwomba nini Elisha? (Anamwomba Mungu msamaha, sio Elisha, anapomwinamia Rimoni.)

J. Soma 2 Wafalme 5:19. Unalielewaje jibu la Elisha? Je, anaidhinisha suala la kumsujudia Rimoni? Je, anamwambia tu Naamani kwamba asiwe na wasiwasi juu ya suala hilo kwa sasa, atafanyia kazi kupata jibu sahihi katika siku zijazo? (Watoa maoni wa Biblia wako kinyume na usomaji unaoidhinisha kuisujudia miungu ya uongo.)

K. Hebu turejee kwenye visa vyetu vya Danieli na Naamani na tuangalie jinsi watu wenye mamlaka walivyoendewa ili kujifunza habari za Mungu wa kweli. Unajifunza nini? (Watu hawa wenye mamlaka hawakuendewa na wenye mamlaka wenzao. Bali, waliendewa na waliokuwa watumwa.)

1. Utatumiaje fundisho hili pale unapofanya kazi ya kuwaongoa wenye mamlaka ili wamwamini Yesu? Je, unapaswa kuanza kwa kuwaongoa wafanyakazi wao?

III. Nikodemo

A. Soma Yohana 3:1-2. Nikodemo aliposema, “twajua,” anazungumza kwa niaba ya nani? (Inaonekana kama anazungumza kwa niaba ya watawala. Sio muda mrefu uliopita nilisoma juu ya ugunduzi wa kiakiolojia ulioashiria kuwa familia ya Nikodemo ilikuwa ya kimamlaka na yenye utajiri mkubwa.)

1. Je, ujumbe huu ni wa taadhima (unatoa sifa)? (Lazima Nikodemo alidhani hivyo. Hata hivyo, sio ujumbe ambao Yesu aliutaka. Hakutoka kwa Mungu au hakuwa na Mungu, alikuwa Mungu mwenye umbo la binadamu.)

B. Soma Yohana 3:3. Vipi kuhusu mazungumzo mafupi yasiyo rasmi kwanza? Vipi kuhusu kurejesha taadhima/sifa? Unadhani Nikodemo aliielewaje kauli ya Yesu? (Yesu anasema kuwa Nikodemo asingeweza kwenda mbinguni isipokuwa tu kama angezaliwa mara ya pili. Yumkini Nikodemo alidhani hii ilimaanisha kuwa asingeweza kwenda mbinguni.)

1. Hebu tulitafakari hili. Nikodemo anamsifia Yesu kwa kusema kuwa Yesu ni mwalimu “aliyetoka kwa Mungu,” na kimsingi Yesu anajibu, “hutaingia mbinguni isipokuwa tu kama utabadilika.” Je, hiyo ndio njia ya kuwaendea wenye majivuno?

C. Soma Yohana 3:4. Nikodemo anamwambia Yesu kuwa jambo hili halina mantiki yoyote. Je, unadhani Yesu alikusudia Nikodemo aelewe? (Katika Yohana 3:5-8 Yesu anatoa ufafanuzi. Huenda Nikodemo alielewa kipengele cha ubatizo, kwa kuwa hii ilikuwa kawaida ya Kiyahudi, lakini kuzaliwa kwa Roho Mtakatifu ni kipengele ambacho hakikueleweka.)

D. Soma Yohana 3:9-10. Sasa Nikodemo anasema kuwa haelewi mambo haya na Yesu anamdhihaki. Kwa nini? (Ninahisi hakuna aliyemtukana Nikodemo. Jambo hili lilivuta usikivu wake. Lilimfanya atafakari.)

E. Soma Yohana 3:11-15. Yesu anamtaka Nikodemo aamini nini? (Kwamba Yesu ni Masihi. Yeye ni Mungu. Yeye ni “nyoka” ambaye watu walimwangalia na kupona.)

1. Utaielezeaje njia aliyoitumia Yesu kwa Nikodemo? Je, anamheshimu? (Hapana. Nina uhakika siyafahamu masuala ya kiutamaduni, lakini Yesu anaonekana kudhihaki.)

2. Je, hivi ndivyo tunavyopaswa kuwaendea wenye mamlaka? (Zingatia kwamba sisi sio Mungu. Elisha pia alimdhihaki Naamani. Kitabu cha Warumi kinatufundisha kuwaheshimu na kuwatii wale wanaostahili heshima na utii (Warumi 13:7). Petro anatuambia tuwaheshimu watu wote (1 Petro 2:17). Kuna nyakati kutikisa majivuno ya watu huwafanya watafakari upya msimamo wao.)

F. Rafiki, je, una mawazo mapya ya namna ya kupeleka injili kwa watu wenye mamlaka? Kwa kuwa sisi si Mungu, bali Roho Mtakatifu ni Mungu, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu kukupatia njia sahihi pale unapowashuhudia wenye mamlaka na nguvu?

IV. Juma lijalo: Utume kwa Wasiofikika: Sehemu ya 1.