Somo la 7: Rehema Zako Hufika Hadi Mbinguni

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Zaburi 51, 136 & 103
Swahili
Year: 
2024
Quarter: 
1
Lesson Number: 
7

Somo la 7: Rehema Zako Hufika Hadi Mbinguni

(Zaburi 51, 136 & 103)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, umewahi kutamani kama polisi angekuwepo ili amwadhibu dereva anayeendesha kwa mwendokasi? Vipi kuhusu mtu aliyeshindwa kusimama kwenye alama ya barabarani inayomtaka kusimama? Kwa upande mwingine, pale polisi anapokusimamisha huwa una matumaini ya kupata rehema zake? Je, hivyo sivyo mambo yalivyo maishani kwa ujumla? Tunawaona watu wengine wakitenda dhambi na tunataka haki itendeke. Hili ni kweli hususan pale matajiri na wenye nguvu wanapotenda dhambi, na ni dhambi kubwa! Lakini pale inapokuwa kwamba sisi ndio tumetenda dhambi tunataka kurehemiwa. Somo letu la Zaburi juma hili linahusu rehema. Sio tu rehema kwa dhambi za kawaida, bali rehema kwa mtu tajiri mwenye nguvu na ushawishi mkubwa ambaye ametenda dhambi ya kutisha. Hebu tuzame kwenye Zaburi na tujifunze zaidi kuhusu taswira kamili ya upendo na rehema ya Mungu!

I.  Upendo Thabiti – na Hatari

A.  Soma Zaburi 136:1-6. Uwezo wa Mungu unaelezewaje kwenye vifungu hivi? (Yeye ni Bwana wa vyote, Mungu wa miungu, na Muumbaji wa mbingu na nchi. Yeye ndiye mwenye mamlaka makuu katika ulimwengu!)

1.  Utaona kwamba kila kauli inaanza kwa kusema “mshukuruni” na inaishia kwa kusema “kwa maana fadhili zake ni za milele.” Je, unadhani watu wenye nguvu wana “upendo thabiti?” (Kwa ujumla huwa tunadhani kuwa matajiri na watu wenye nguvu ni wabinafsi, na hawana upendo.)

a.  Je, hiyo ndio sababu mtunga Zaburi anaanza kwa kusema “mshukuruni?” Tunapaswa kushukuru kwamba mtazamo wa kawaida tunaouona kwa wanadamu haupo kwa Mungu wetu.)

b.  Au, unadhani ana sababu tofauti?

B.  Soma Zaburi 136:10-15. Hebu subiri kidogo! Je, ni “upendo thabiti” kumuua mzaliwa wa kwanza wa kila familia nchini Misri? Vipi kuhusu kumzamisha majini Farao na jeshi lake? Tunaposema “jeshi” tunazungumzia kuhusu wana, akina baba, na waume.

1.  Nimekutana na walimu wa Biblia wanaodai kuwa uangamivu huu wa Wamisri hauendani na upendo wa Mungu. Wanasema kuwa tetemeko la ardhi, au kujongea fulani hivi kwa dunia kwa nguvu za asili, ndiko kulikosababisha Bahari ya Shamu kugawanyika kama ilivyotokea ili kuwaokoa Waebrania na kuwaua Wamisri. Je, hilo linaendana na hii Zaburi? (Hoja juu ya janga la asili ni ya kipumbavu. Vifungu vya mwanzoni vya Zaburi 136 vinasema kuwa Mungu ndiye mwenye mamlaka kamili ulimwenguni. Mambo yaliyoelezewa ni sahihi sana kiasi kwamba hili haliwezi kuwa jambo la bahati. Na hata kama ingekuwa bahati, asili inaongozwa na kudhibitiwa na Mungu.)

2.  Kuna fundisho gani kuhusu rehema za Mungu na upendo wake thabiti? (Anawaonesha rehema na upendo thabiti wale wanaomchagua. Farao alikuwa kwenye uasi dhidi ya Mungu.)

a.  Je, hiki ndicho kielelezo cha rehema yetu? Au madai yetu ya kukamatwa kwa waendeshao kwa mwendokasi – isipokuwa sisi – yanaonesha kuwa sisi ni mahakimu tusioaminika?

II.  Upendo Thabiti – na Dhambi

A.  Soma Zaburi 51:1. Angalia kipindi (timing) Zaburi hii ilipoandikwa. Jambo gani limetokea? (Nathani ametoka kumkabili Daudi kuhusiana na dhambi yake ya uzinzi na mauaji yaliyodhamiriwa.)

B.  Soma 2 Samweli 12:1-5 na 2 Samweli 12:7-9. Mfalme Daudi anasema kuwa haki ni ipi pale anaposikia kisa kuhusu mtu aliyetenda kile alichokitenda? (Daudi alitamka vikali kwamba mtu huyo anastahili kifo! Kitendo hicho kilimkasirisha Daudi.)

1.  Je, Daudi ni kipofu wa dhambi yake mwenyewe?  Je, sisi tu vipofu wa dhambi zetu wenyewe?

C.  Soma Zaburi 51:2-4. Sasa Daudi anasema kuwa “anajua” dhambi zake. Je, Mungu atakabiliana nasi kwa dhambi zetu ili “tuzijue?” (Mungu alimtumia nabii Nathani kumkabili Daudi. Ninadhani Roho Mtakatifu anatukabili kwa dhambi zetu.)

1.  Utaona kuwa Daudi pia anasema kuwa dhambi yake “i mbele yangu daima.” Wakati huo huo the Bible Knowledge Coommentary inasema kuwa Nathani alimkabili Daudi takriban mwaka mmoja baada ya dhambi. Je, Daudi aliitafakari dhambi yake kabla Nathani hajamwendea?

D.  Angalia tena Zaburi 51:4. Je, ni kweli kwamba Daudi alimtenda dhambi Mungu peke yake? Utaona kwamba Daudi anasisitiza kuwa dhambi yake ni dhidi ya Mungu “peke yake.” (Dhambi ya Daudi ya kumuua Uria, iliiharibu familia ya Daudi, na kuweka mfano mbaya kwa nchi. Lakini dhambi ni dhidi ya Mungu peke yake na tunapaswa kutubu dhambi zetu kwa Mungu. Tunatakiwa kusahihisha mambo na wale tuliowadhuru, lakini dhambi ni dhidi ya Mungu peke yake.)

E.  Soma Zaburi 51:5-7. Daudi anasema kuwa “mimba yake ilitungwa hatiani” na “aliumbwa katika hali ya uovu.” Je, tunazaliwa katika mwelekeo wa dhambi? Je, sisi tu wadhambi wakati tunazaliwa? (Ikiwa Daudi anazungumza jambo la kiteolojia, basi tunazaliwa tukiwa wadhambi.)

1.  Tunapaswa kufikia hitimisho gani jingine kutokana na alichokisema Daudi? Kwamba Daudi hana hatia kwa kuwa alizaliwa akiwa mdhambi?

2.  Ikiwa Daudi hana hatia, nani mwenye hatia? (Wengine wanaweza kusema, “Mungu,” lakini angalia kifungu cha 6 kinachosema kuwa Daudi anajua Mungu anapendezwa na kweli na “anafundisha hekima kwa siri.” Ninadhani Daudi anasema tu kwamba ameoza sana na Mungu anataka kumbadilisha.)

F.  Angalia tena Zaburi 51:7. Ni nini mtazamo wa Daudi juu ya kuhesabiwa haki kwa imani? (Mungu ndiye anayetufanya tuwe wenye haki.)

G.  Soma Zaburi 51:9-12. Je, Daudi anatafuta tu kutangazwa mwenye haki? Je, anatafuta rehema kwa ajili tu ya msamaha wa dhambi zake? (Hapana. Anataka utakaso wa kina. Anataka Roho Mtakatifu aifanye upya “roho iliyotulia” ndani yake. Anataka furaha na “roho ya wepesi.”)

1.  Linganisha hili na jinsi baadhi ya watu wanavyolitazama fundisho la kuhesabiwa haki kwa imani. Niliwahi kumsikia mtu akizungumza kuhusu dhambi, “Hilo ni sawa tu, Mungu atasamehe.” Lengo sio tu kupata kibali, lengo ni kuwa na moyo uliobadilika ili usitake kutenda dhambi. Lengo sio kuendelea “kufurahia” dhambi kwa uelewa wa msamaha ujao.)

H.  Soma Zaburi 51:13. Ni nini lengo la Daudi kwa siku zijazo? Je, nawe una lengo kama hilo? (Anataka kumtukuza Mungu kwa kuwasaidia wengine kumgeukia Mungu.)

III.  Upendo Thabiti – na Maisha Bora

A.  Soma Zaburi 130:3. Nani mwenye hitaji la rehema ya Mungu? (Kila mtu. Hakuna anayeweza kuhimili.)

B.  Soma Zaburi 103:2-4. Mungu atafanya nini kwenye udhalimu wetu? (Atasamehe dhambi zetu na kuukomboa “uhai wetu na kaburi.”)

C.  Soma Zaburi 103:5. Je, Mungu ana ukomo wa kutusamehe dhambi? (Hapana. Kifungu kinasema kuwa ujana wetu “unarejezwa.”)

1.  Je, hiyo inaleta mantiki? Kuna uhusiano gani kati ya kusamehewa na ujana? (Tunapoelewa kwamba dhambi zetu zinasamehewa, hiyo inatufanya tujisikie vizuri tena.)

2.  Rejea nyuma kwenye Zaburi 103:3. Je, unadhani kuwa msamaha wa dhambi pia unaponya magonjwa tuliyonayo? (Ninaamini, na pia nimesoma, kwamba kuna uhusiano kati ya mitazamo ya kiakili na magonjwa. Jambo la uhakika ni kwamba Mungu atatufanya kuwa wapya kabisa, kiakili na kimwili, tutakapokuwa pamoja naye mbinguni.)

D.  Soma Zaburi 103:6. Je, unajihisi kwamba unakandamizwa? Ikiwa ndivyo, Mungu atakutendea nini utakapomgeukia? (Analeta usawa na haki kwa wanaokandamizwa.)

E.  Soma Zaburi 103:7. Kwa nini anamrejelea Musa wakati tunajadili anachokifanya Mungu ili kuyaboresha maisha yetu? (Tafakari miujiza yote aliyoitenda Mungu kumwezesha Musa kuwatoa watumwa wa Kiebrania kutoka Misri.)

1.  Kuna fundisho gani kubwa kwenye kisa hicho? (Licha ya kuona miujiza yote ile, bado watu hawakumtumaini Mungu. Angalia Kumbukumbu la Torati 1.)

F.  Soma Zaburi 103:13-14. Kama unawapenda watoto wako, kama wazazi wako wanakupenda, unapaswa kuuangaliaje mtazamo wa Mungu kwako? (Mungu anafanana na mzazi mwenye upendo. Hii inajumuisha uelewa alio nao mzazi wa jinsi watoto wanavyotakiwa kulindwa kwa sababu bado hawana ukomavu wa kutosha kukabiliana na ulimwengu.)

G.  Rafiki, hatari imetuzunguka. Sote tumeandamana na hatari ya mwelekeo wa kutenda dhambi. Mungu, kwa rehema zake, anatuokoa kutoka hatarini, na anatuokoa kutoka kwenye asili yetu ya dhambi. Kwa rehema, tukimtumaini Mungu, atayabariki maisha yetu. Je, utamgeukia Mungu sasa hivi? Je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie kumtumaini Mungu katika hali na mazingira yote?

IV.  Juma lijalo: Hekima kwa Ajili ya Kuishi Maisha ya Haki.