Somo la 8: Hekima kwa Ajili ya Kuishi Maisha ya Haki
Somo la 8: Hekima kwa Ajili ya Kuishi Maisha ya Haki
(Zaburi 119, 90, 81, 141)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: “Mkumbuke mwizi msalabani!” Kwenye mjadala juu ya nini maana yakuhesabiwa haki kwa imani, uzoefu wa yule mwizi unatupatia uhakika kwamba matendo yetu hayatatuokoa. Je, umewahi kumsikia Mkristo anayejenga hoja juu ya umuhimu wa kuishi maisha makamilifu akisema, “Unamkumbuka mwizi msalabani?” Ukitafakari juu ya hili, mwizi yule ni fundisho kubwa kuhusu jinsi ambavyo maisha yetu yanaweza kuwa kama tutapuuzia mafundisho ya Biblia juu ya kuishi maisha makamilifu. Mwisho yule alihitimisha maisha ya hapa duniani kwa kifo cha aibu na kichungu sana. Hebu tuzame kwenye somo letu la Zaburi ili tujifunze zaidi kuhusu ambavyo maisha ni mazuri kama tutafuata kanuni za Mungu!
I. Kwenda
A. Soma Zaburi 119:1-3. Vifungu hivi vinatumia neno “waendao” mara mbili. Inamaanisha nini kwenda “katika sharia,” na “kwenda katika njia zake?” (Kwenda inarejelea mwelekeo wa maisha yako. Mtu aliyebarikiwa anasonga mbele kwa namna inayoendana na sheria ya Mungu.)
B. Soma Zaburi 119:4-6. Je, unapenda kuaibika? Hii inatufundisha nini kuhusu jinsi ya kuepuka aibu? (“Hatutaaibika” ikiwa tutajikita kwenye sheria za Mungu.)
1. Fikiria kipindi ambacho ulijiona kuwa umeaibika sana. Je, ilikuwa ni kwa sababu ulikuwa unazitii amri za Mungu?
C. Soma Zaburi 119:7-9. Tunawezaje kujua jinsi ya kuishika sheria ya Mungu? Je, kuna hatua za kujifunza? (Kuna hatua za kujifunza. Mtunga Zaburi anaandika kuhusu kujifunza “hukumu za haki.” Hukumu hizo zinapatikana kwenye neno la Mungu – Biblia.)
D. Hebu turuke hadi chini na tusome Zaburi 119:32-34. Kifungu cha 32 kina maneno yasiyo ya kawaida: “utakaponikunjua moyo wangu.” Unadhani inamaanisha nini kwa Mungu kukunjua moyo wetu kwa kuzingatia sheria yake? (Moyo wetu wa asili hauendani na sheria ya Mungu. Sio tu kwamba tunatakiwa kujifunza sheria ya Mungu, bali pia tunahitaji badiliko la moyo. Tunamhitaji Roho Mtakatifu ili abadili moyo wetu ili tuweze “kukimbia” kwa “moyo wetu wote.”)
1. Je, umewahi kuwa kwenye mazingira ambayo ulitaka Mungu apuuzie sehemu moja ya maisha yako? Mungu angeweza kuyamiliki maisha yako, isipokuwa hii sehemu moja ndogo ambayo ungependa kubaki nayo? (Mtunga Zaburi anatuambia kuwa lengo ni kugeuza moyo wetu wote kufuata maelekezo ya Mungu.)
E. Angalia tena Zaburi 119:34. Mtunga Zaburi anahusianisha “uelewa” na kuishika kwa “moyo wote.” Je, unawaona Wakristo wanaopotosha maana ya amri?
1. Soma Mathayo 5:27-28. Hapa Yesu anafanya nini? Anatusaidiaje kuielewa vizuri amri ya saba? (Yesu anatupatia uelewa wa kina wa kile ambacho Mungu anakiwaza akilini mwake kwa ajili ya maisha mazuri.)
II. Kuzihesabu
A. Soma Zaburi 90:10-12. Musa (aliyeishi miaka mingi Zaidi) anatuambia kuwa umri wetu wa kuishi ni miaka 70, au miaka 80 ikiwa tuna nguvu. Hizo ni habari za kutia wasiwasi kwa upande wangu! Unadhani Musa anamaanisha nini anapotuambia kutafakari nguvu ya hasira na ghadhabu ya Mungu? (Ukiangalia umri wa kuishi wanadamu kabla ya Gharika, utaona kwamba waliishi kwa miaka mingi Zaidi. Anachokimaanisha Musa ni kwamba Mungu ndiye anayeshikilia ufunguo wa maisha marefu. Hizo ni nguvu.)
1. Maelekezo ya “utujulishe kuzihesabu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima” yanaendanaje na kauli ya Musa kuhusu maisha marefu? (Tuna muda mfupi hapa duniani. Tunatakiwa kuutumia vizuri muda huo. Sehemu ya lengo letu katika muda wetu mfupi ni kuwa na busara.)
2. Unadhani Musa anamaanisha nini anapotuambia “tujipatie moyo wa hekima?” “Hekima” inamaanisha nini? Je, anazungumzia akili yetu ya kawaida? (Hapana. Anatuambia kuwa kuyaelewa mapenzi ya Mungu, na kuenenda kwa mujibu wa mapenzi hayo, ni hekima. Hekima inaweza kujifunzwa. Hii inaweza kuathiri urefu wa maisha yetu.)
3. Babu yangu wa kambo alikuwa mtu mwema kwa kipindi kifupi nilichomfahamu. Hata hivyo, miongo kadhaa hapo kabla alikuwa mlevi. Jeshi la wokovu na Roho Mtakatifu vilimwokoa na akaanza kuhubiri na kufundisha. Ninakumbuka alivyoniambia jinsi alivyojutia miaka yote aliyoipoteza kwenye ulevi wa pombe. Je, unaichukulia miaka yako kwa uzito na umakini mkubwa?
B. Soma Zaburi 81:6-7. Pitia kwa haraka haraka vifungu vilivyotangulia katika Zaburi 81 na uniambie kifungu cha 6 kinamaanisha nini? (Mungu anazungumzia kipindi amacho watu wake walikuwa watumwa nchini Misri.)
1. Rejea ya Meriba katika kifungu cha 7 inamaanisha nini? (Soma Kutoka 17:4-7. Rejea hii ni katika kipindi ambacho watu hawakumtumaini Mungu kwa kiasi kikubwa sana kiasi kwamba walitishia kumpiga Musa kwa mawe.)
2. Zaburi 81:7 inaporejelea watu “kujaribiwa” pale Meriba, unadhani Mungu aliwanyima maji ili kuwajaribu? (Ukisoma Kutoka 17:2 Musa anasema kuwa watu wanamjaribu Mungu.)
3. Kwa mashtaka yote haya yanayotolewa kuhusu “kumjaribu,” unadhani suala halisi ni lipi? (Kumtumaini Mungu.)
4. Hebu rudi nyuma kidogo. Ukimtumaini Mungu, je, maisha yako yatakuwa mazuri? (Yatakuwa na Amani Zaidi.)
C. Soma Zaburi 81:11-16. Kipengele gani cha kuzihesabu siku zetu kinaelezewa kwenye vifungu hivi? (Tunapozihesabu siku zetu, sio tu kwamba tunatafakari jinsi tunavyotumia muda wetu, bali pia tunayo fursa ya kuongeza furaha ya maisha. Je, ungependa siku zako zilizosalia kuwa bora sana (excellent)?
D. Soma Zaburi 112:7-8. Linganisha ufafanuzi huu wa wenye haki na tatizo lililotokea pale Meriba. Jambo gani linaleta utofauti? (Kumtumaini Mungu. Ufafanuzi mzuri kiasi gani wa kimtazamo tunaotakiwa kujipatia kutoka kwa Mungu. Hatuziogopi habari mbaya. Moyo wetu uko imara. Hatimaye tunatazamia kushinda.)
III. Tafakari
A. Soma Zaburi 141:3-4. Vipi kuhusu midomo yetu, je, tunaiangalia? Je, tunajitahidi kutoapa? Je, tunajitahidi kutodanganya? (Ingawa hayo ni muhimu, nadhani suala kubwa limeakisiwa katika kifungu cha nne. Tunatakiwa kuangalia ushawishi wetu. Je, ushawishi wetu unawaelekeza wengine uovuni?
B. Soma Zaburi 141:5. Je, ungependa kupigwa kichwani kwa kushtukizwa bila kutarajia? Nilipokuwa nikifanya kazi za ujenzi nilichukia pale nilipogonga kichwa bila kutarajia kwenye ubao ambao sikuwa nimeuona.
1. Mafuta kichwani ni jambo zuri. Ni kwa jinsi gani kupigwa kichwani kwa karipio la mwenye haki kunafananishwa na mafuta? (Daudi anakiri kuwa wakati mwingine anahitaji tu kupigwa kwa karipio.)
2. Je, hili linaibua utamaduni wa kisasa dhidi ya suala la Biblia? Kama mtu yeyote anaikaripia dhambi, hususan kanisani, hii inachukuliwa na wengi kuwa kosa la kutisha. Tunaambiwa kuwa watu “wanaoingilika kiurahisi (welcoming).” Una maoni gani?
3. Mimi ni kiongozi katika kanisa ambalo ni “welcoming.” Tunaamini katika kuwa wema kwa wadhambi, na kuepuka kuwagongagonga. Binafsi, ninajisikia vizuri kuwa mwema kuliko kuwa mkali/katili. Vipi kuhusu wewe?
4. Je, kuna namna ya kutatua mgogoro huu? (Huyu ni Mfalme Daudi akijiandikia mwenyewe. Daudi ni mtu aliyekuwa karibu na Mungu na hakupaswa kuwa na visingizio vya kuwa na tabia mbaya mara kwa mara. Yesu alikuwa mwema kwa wadhambi. Tunahitajika kumwomba Roho Mtakatifu atupatie njia sahihi ya kuwaendea wadhambi.)
C. Soma Zaburi 141:6. Daudi anawaza nini juu ya mahakimu waovu? (Wanapaswa warushwe kutoka kwenye mnara/jabali.)
D. Soma Zaburi 141:8-10. Tuna mjadala mrefu hapa kuhusu vitu vya hatari. Daudi anasema kuwa waovu wanamuwazia mabaya. Je, ni sahihi kutumia siku zetu za mwisho kuwatafutia madhara maadui wetu na usalama kwa ajili yetu? Isipokuwa, kimsingi, pale tunapohitajika kupigwa ili kutusaidia kurejeshwa kwenye msitari? (Kwa kawaida tunatafuta usalama. Kinachomaanishwa na Daudi ni kwamba Mungu ndiye bandari yetu salama. Anaweza kutuokoa na kuwapa waovu kile walichokiwazia kuwadhuru wenye haki.)
E. Rafiki, wakati ambapo hatma ya wokovu wetu ndilo lengo la muhimu zaidi, je, unataka kutumia miaka 70-80 huku ukiwa na kipindi kibaya na kisichofurahisha? Je, unataka kuwa mtu mwenye wasiwasi na asiye na furaha? Kuwa mlalamishi kila mara kuhusu jinsi ambavyo Mungu na watu wengine wamekuangusha? Hatutaki kuishi maisha yaliyomfanya mwizi aishie msalabani. Badala yake, tunatakiwa kufuata amri za Mungu na kuishi maisha ya kujiamini, tumainifu, busara, na yenye furaha. Je, utafanya uchaguzi wa kufuata amri za Mungu?
IV. Juma lijalo: Amebarikiwa Yeye Ajaye kwa Jina la Bwana.