Uinjilisti na Ushuhudiaji wa Mtu Mmoja Mmoja (Binafsi)

(1 Petro 2 & 3, Yohana 1)
Swahili
Year: 
2012
Quarter: 
2
Lesson Number: 
6

Utangulizi: Kati ya watu ambao ungependa kuwaleta kwa Kristo, je, ni nani aliye wa umuhimu kwako? Ubashiri wangu ni kuwa jibu lako ni kuwa atakuwa mmojawapo wa watu kutoka kwenye familia yako. Mara nyingine huwa ninabaini kuwa watu huwa wema zaidi kwa watu ambao sio wa familia zao kuliko wale wa familia zao. Je, hiyo inaleta mantiki yoyote? Katika somo hili tutaangalia jinsi tunavyoweza kuwa mashuhuda kwa familia zetu, na kisha kuangalia kama kanuni hizo ndizo zitakazotumika kwenye ushuhudiaji binafsi kwa wale wanaotuzunguka. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

  1. Kubadili Mtazamo
    1. Soma 1 Petro 2:18-21. Je, wewe na mimi tumeitwa ili tupigwe? (Hivyo ndivyo fungu linavyosema! Kimsingi, linasema kuwa tumeitwa “kustahimili” tunapopigwa kwa kutenda mema.)
    2. Soma 1 Petro 2:23-24. Kwa nini tunaitwa kupigwa? (Kwa sababu Yesu, akiwa kama mfano kwetu, alipigwa kwa ajili ya dhambi zetu! Makovu yake yalituponya.)
    3. Soma 1 Petro 3:1-2. Je, Paulo anamaanisha nini anaposema “kadhalika?” (Petro anarejea kile alichokisema hivi punde; watumwa wanapaswa kukubali kupigwa kwa sababu Yesu alipigwa makofi kwa ajili yetu.)
      1. Kwa wazi kabisa ninajisikia vibaya (na watu wengine wengi pia wanajisikia hivyo). Ninaposikia kuwa mwanamume anampiga mkewe au wanawe, ninajisikia kumpiga ngumi. Wanaume wanaowapiga au kuwanyanyasa wake zao ni watu wanaostahili kudharauliwa. Unapompiga mtu ambaye hawezi kujibu mapigo, kama vile mkeo, wanao, wafanyakazi wako, watumishi walio chini yako au mhudumu kwenye mgahawa, basi wewe ni mwonevu/mkatili. Ni kwa jinsi gani basi Petro anapendekeza kuwa wake wapigwe?
    4. Hebu tumwangalie Yesu, ambaye ndio mfano wetu, kwa ukaribu zaidi, ili tuweze kuuelewa huu mtazamo vizuri zaidi. Soma tena 1 Petro 2:24. Kwa nini Yesu alipigwa? (Alichukua dhambi zetu. Alikuwa Mwana-kondoo wa Mungu.)
      1. Je, Yesu alikuwa akipigiwa mara kwa mara maishani mwake? (Hapana. Alipigwa mwishoni tu.)
      2. Petro anapoandika kuwa “kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu,” je, hii inamaanisha kustahimili kupigwa mara kwa mara? (Hapana. Hayo sio mateso aliyoyapitia Yesu. Kitu cha muhimu zaidi ni kuwa, Yesu alikuwa na lengo la msingi mawazoni mwake, kutuokoa. Mke akipigwa ili kumwokoa mumewe, basi hapo nitaelewa. Lakini mke akipigwa kwa lengo la kupigwa tu, basi hii sio kama ile kauli ya “kadhalika!”)
    5. Kama Petro hazungumzii kuhusu mapigo, je, anazungumzia kitu gani? (Kiini cha utume wa Yesu kilikuwa ni kujitoa kwa ajili yetu. Nadhani huo ndio mtazamo ambao Petro anauzungumzia. Kujikana nafsi.)
    6. Soma 1 Petro 3:3-6. Kwa utangulizi huu, je, Yesu anazungumzia kitu gani kuhusu urembo, mapambo, nywele na mavazi? (Sidhani kama anasema sana kuhusu kile ambacho mwanamke anakivaa. Anasema kuwa urembo wa kweli unatokana na kuwa na mtazamo huo huo dhidi ya mumeo ambao Yesu anao dhidi yetu.)
      1. Utabaini kuwa mke wa Ibrahimu, Sara, anatajwa kwa jina lake. Je, fungu hili linasema nini kumhusu Sara na urembo? (Soma Mwanzo 24:51-53. Kama Ibrahimu anatoa vyombo vya fedha na dhahabu (mapambo) kwa mkwewe (mkamwana) mtarajiwa, haionekani kwamba mkewe havai mapambo. Badala yake, hii inathibitisha kuwa Paulo anazungumzia kuhusu umuhimu wa urembo kuwa utokane na mtazamo, badala ya mapambo.)
      2. Je, mapambo yetu yanaweza kuwa na ujumbe gani kuhusu mtazamo wetu dhidi ya watu wengine? (Kwa kiwango kikubwa kabisa kile kinachoitwa “mapambo” hapa Marekani hivi leo sio mapambo. Ni metali ya bei nafuu na kitu cha plastiki ambacho mtu yeyote anaweza kuvimudu. Hata hivyo, kama unavaa mapambo kwa lengo la kusema kuwa wewe ni bora kuliko watu wengine, basi hii ni kinyume na kujitoa binafsi.)
  2. Uinjilisti Binafsi wa Kifamilia
    1. Hadi hivi sasa tumeona kuwa mke anapaswa kumshuhudia mumewe kwa kuwa na mtazamo wa kujikana nafsi. Soma 1 Petro 3:7. Je, ni mtazamo wa aina gani unaohitajika kwa mume anayetaka kumshuhudia mkewe?
      1. Utabaini kuwa Petro anaanza kwa kusena “kadhalika.” Je, ni kadhalika gani hiyo? (Njia ile ile ambayo Yesu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Njia hiyo hiyo ambayo mke anakuwa hana ubinafsi kwa mumewe. Waume wana jukumu hilo hilo la “kadhalika.”)
    2. Soma Wakolosai 3:19. Je, waume wanatakiwa kufanya nini? (Petro anawaambia waume kuwa wawachukulie wake zao na kuwaheshimu. Paulo anawaambia wawapende wake zao. Maelekezo dhidi ya kuwa “wakali,” kwa wazi kabisa yanazuia kumpiga mke.)
    3. Soma Wakolosai 3:21 na Waefeso 6:4. Je, ni mtazamo wa aina gani ambao wazazi wanapaswa kuwa nao dhidi ya watoto wao? (Chochote kile akifanyacho mzazi hakipaswi kuwa cha kumchokoza na kumchukiza mtoto (kumfanya aumie) au kumuudhi/kumkasirisha/kumghadhibisha/kumkera. Nadhani mtazamo ule ule wa kujikana nafsi alionao Yesu dhidi yetu ndio zana bora ya uinjilisti kwa wanafamilia, wakiwemo watoto.)
  3. . Uinjilisti Binafsi wa Kijamii
    1. Soma 1 Petro 2:11-12. Je, ni kitu gani kilicho cha msingi katika kupeleka injili ulimwenguni? (Maisha makamilifu.)
      1. Je, hii inamaanisha kuwa wapagani hawatatushtaki kwa matendo mabaya? (Hapana. Wataleta mashtaka ya uongo, lakini tutathibitisha kuwa kile wanachokisema ni cha uongo kutokana na matendo yetu.)
    2. Soma 1 Petro 2:13-17. Je, ni mtazamo wa aina gani tunaopaswa kuwa nao dhidi ya ulimwengu? (Tujitoe kwa mamlaka. Kupitia kwenye maisha yetu tunaonyesha kuwa Mungu anastahili kupewa sifa.)
    3. Unapokuwa ukitafakari kile tulichokijadili, je, kuna kitu cha kufanana katika kupeleka uinjilisti kwenye familia zetu na kupeleka uinjilisti ulimwenguni? (Ndiyo! Kitu cha kufanana ni kujikana nafsi. Maisha yako yanapaswa kuwabariki watu wengine.)
      1. Je, hii inafananaje na mtazamo wa ulimwengu? (Ulimwengu unafanya mambo ya kujiongezea vitu yenyewe. Wakristo wanapata nadhari (attention) ya wale wanaowazunguka kwa kuwa kinyume na ulimwengu. “Kinyume” kinachowabariki wale wanaokuzunguka. Hiyo inawang’ang’aniza kwenye sababu ya mtazamo wako.)
  4. Mfano
    1. Soma Yohana 1:32-34. Yohana Mbatizaji anamzungumzia Yesu. Je, ni ushuhuda gani anaoutoa Yohana kumhusu Yesu? (Kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.)
      1. Je, kuna kujikana nafsi kokote kwenye kauli ya Yohana?
    2. Soma Yohana 1:35-37. Je, ni kitu gani kilichowahamasisha hawa wanafunzi wawili kuhitaji kujifunza zaidi kumhusu Yesu? (Kile alichokisema Yohana.)
    3. Soma Yohana 1:38-42. Je, kipaumbele cha kwanza cha Andrea ni kipi? (Kumwambia mwanafamilia mwenzake kuhusu habari za Yesu.)
      1. Je, kitendo cha Andrea kinaendanaje na mjadala wetu wa kujikana nafsi? (Badala ya kukaa na Yesu kwa muda mrefu, Andrea anamtafuta ndugu yake na kushiriki naye habari njema.)
    4. Soma Yohana 1:43-46. Chukulia kwamba Nathanaeli alilisema hili kuhusu uvumbuzi wako muhimu. Je, jibu binafsi la muhimu ni lipi? (Kuhojiana na Nathanaeli ili kumwonyesha kuwa uko sahihi. Badala yake, Filipo alisema kwa ufupi tu kuwa, “Njoo uone.”)
    5. Soma Yohana 1:47-48. Tunaweza kuchukulia kuwa Yesu pia alijua kile alichokisema Nathanaeli. Je, utajisikiaje mtu fulani alikwambia kuwa “Hakuna jambo zuri litokalo kwenye familia yako, mji wako, nk?” Je, aina gani ya jibu binafsi la muhimu utakalolitoa?
    6. Badala ya kusema jambo chanya kuhusu yeye mwenyewe au jambo hasi kumhusu Nathanaeli, je, Yesu anasema jambo gani? (Anampongeza Nathanaeli. Badala ya kufikiria kumfedhehesha/kumtukana, Yesu anamwinua Nathanaeli. Huku ndiko kujikana nafsi.)
    7. Soma Yohana 1:49. Je, ni kwa namna gani njia ya kujikana nafsi kuhusu uinjilisti inafanya kazi? (Nathanaeli anabadilishwa (kuwa mfuasi) mara moja.)
    8. Soma Yohana 1:50-51. Hebu subiri kidogo! Je, Yesu anatuambia kuwa “maajabu” ndio yaliyombadilisha Nathanaeli badala ya kujikana nafsi? (Njia aliyoitumia Yesu kwa Nathanaeli ilikuwa ni ya kushughulika naye. “Maajabu” (uwezo wa Mungu) yalifuatia na kusaidia mabadiliko.)
    9. Rafiki, je, unajishughulisha na watu wengine, au anajiangalia wewe mwenyewe? Ninapokuwa ninajishughulisha na masuala ya ndoa, huwa ninajumuisha nukuu ya sentensi kutoka kwenye harusi yangu mwenyewe: “Kila siku unapoamka sema kuwa, “Je, ninaweza kufanya kitu gani kwa mwenzi wangu?’” Je, utamwomba Roho Mtakatifu ili akupatie mtazamo sahihi wa kujikana nafsi, mtazamo utakaokufanya uivute familia yako, marafiki na ulimwengu kwa Yesu?
  5. Juma lijalo: Uinjilisti na Ushuhuda wa Kundi (Watu Wengi).