Uinjilisti na Ushuhuda wa Kundi (Watu Wengi)

(Mhubiri 4, Wafilipi 1, Matendo 15)
Swahili
Year: 
2012
Quarter: 
2
Lesson Number: 
7

Utangulizi: Adam Smith alizaliwa takriban miaka 200 iliyopita. Alianza maisha yake kama waziri, lakini aliishia kuandika mojawapo ya kitabu cha muhimu sana kinachohusu masuala ya uchumi: “the Wealth of Nations.” Kwa wazi kabisa, tasnifu yake inaelezea kuwa matamanio yako ya ubinafsi wa kutafuta fedha nyingi zaidi yanaboresha hali ya kiuchumi ya watu wanaokuzunguka. Je, wivu, ulafi/uroho na tamaa sio dhambi? Huku nikiwa sina shaka kabisa kuwa Adam Smith yuko sahihi, mara zote nimekuwa nikitafakari jinsi nadharia yake inavyoweza kuhusianishwa na imani. Kinachofanya suala hili liwe gumu zaidi ni kwamba Mungu, aliyetuambia tusiwe na tamaa, amekuwa akiendelea kuweka thawabu/ujira mbele yetu. Anafanya hivyo kwa kutumia fedha zetu (Malaki 3:10) na anafanya hivyo kwa kutumia matendo yetu (Mathayo 25:34-36). Je, wivu, ulafi/uroho na tamaa vinapaswa kuwa sehemu ya mafanikio ya uinjilisti wa kundi/kikundi (wa watu wengi)? Je, majivuno ya mawazo kuhusu uguswaji wetu wa kidini yana nafasi gani kwenye uinjilisti? Hebu tuzame kwenye Biblia zetu ili tujifunze zaidi!

  1. Hamasa/Nia
    1. Soma Mhubiri 4:4-6. Je, Sulemani anasema nini kuhusu mtazamo wa Adam Smith kuhusu masuala ya uchumi? (Anakubaliana na Smith! “Amali zote, na kila kazi ya ustadi, inatoka katika mtu kupingana na mwenzake.”)
    2. Soma Wafilipi 1:15-18. Je, Paulo anawaonaje wale wanaoieneza injili kwa husuda/wivu na ushindani? (Anasema kuwa haijalishi!)
    3. Soma Mathayo 6:2, Mathayo 6:5 na Mathayo 6:16. Je, thawabu/ujira kwa wale wanaoiendeleza injili kwa husuda na ushindani ni ipi? (Wanapata kile wanachokitafuta – wanajiendeleza wao wenyewe – na hicho tu ndicho wanachoweza kukifanya.)
    4. Soma Ufunuo 22:12-14. Je, ni ujira gani tunaoutafuta? (Uzima wa milele. Kuingia kwenye huo uzima kupitia kwenye malango ya mji mtakatifu.)
    5. Kama sote tunatafuta kupata thawabu/ujira wa namna fulani, je tofauti ya mitazamo yetu inahusika kwa namna yoyote ile?
    6. Hebu tupitie Wafilipi 1:15-16. Je, tunapaswa kuwa na nia gani? (Upendo na mapenzi mema.)
      1. Vipi kama nia zetu zina mkanganyiko? (Bado tunaiendeleza injili (kitu chema), lakini tunatakiwa tuwe makini na nia zetu kwa sababu ya tofauti kubwa iliyopo kwenye ujira.)
  2. Kanuni za Kujihusisha: Teolojia ya Mbili na Tatu
    1. Soma Mhubiri 4:9-12. Ninatumia hii kwenye ndoa, na ninadhani hapa ndipo mahala inapotumika kikamilifu. Hata hivyo, je, hii inahusikaje kwenye uinjilisti? (Soma Luka 10:1-3. Kwa wazi kabisa, Yesu anapendekeza kufanya kazi katika kundi la watu wawili wawili.)
    2. Soma Mathayo 18:19-20. Je, ipo “teolojia ya wawili,” na kwa hiyo kuna tatizo na “mmoja?” (Kwa hakika kabisa kuna faida kwenye wawili. Katika ushuhudiaji na katika maombi.)
    3. Kwa nini basi Mungu yupo kwenye “tatu” (utatu) kama faida hiyo ipo kwenye wawili? (Soma tena Mathayo 18:20. Unawaona wangapi hapa? Unaona angalao wawili na Mungu. Hiyo inafanya kuwa watatu. Wawili kwa pamoja wanamhitaji Roho Mtakatifu ili kukamilisha juhudi zao.)
    4. Soma Warumi 12:4-5. Je, ni namba gani inayokujia akilini unapofikiria umbo la mwili? (Mbili. Macho mawili, masikio mawili, viganja viwili, mikono miwili, miguu miwili, makanyagio mawili. Hata pua letu moja lina matundu mawili.)
      1. Je, unadhani ni kwa nini Mungu alituumba kwa namna hiyo?
      2. Je, unadhani ni kwa nini Roho Mtakatifu alimvuvia Paulo kulielezea kanisa kuwa kama mwili? (Katika mwili kuna ubora wa “uwili.”)
      3. Je, umewahi kuwaona Wakristo walio “mbwa mwitu wa kipekee?” (Katika madai ya uhuru wa dini yangu mahakamani, wale ambao hawajihusishi na kanisa (mwili) kwa ujumla ni wale ambao wapo kwenye mienendo mibaya, au ambao hawana udhati na imani zao za kidini.)
    5. Hebu tutafakari kanuni ya kujihusisha ya “wawili kwa wawili” na tatizo la kuhamasishwa na husuda na ushindani. Je, kanuni ya wawili kwa wawili ina athari gani kwenye tatizo la uhamasishaji? (Inasaidia kuponya tatizo. Kama wawili wanatenda kazi pamoja, basi ni vigumu kutafuta sifa kwa mtu mmoja binafsi. Mwenzako anaweza kutambua na kusahihisha hamasa ya ubinafsi ambayo unaweza usiione.)
  3. . Uinjilisti na Kanisa
    1. Soma Matendo 15:1. Je, huu ni uinjilisti? Au, je, haya ni majivuno ya mawazo? (Kwa hakika huo ni uinjilisti katika macho ya Wakristo wengi. Kanisa langu lina fundisho ambalo bado hujalikubali, kwa hiyo nitakushuhudia na kukupa injili kuhusiana na suala hili lenye maarifa makubwa.)
      1. Je, makanisa mangapi ya kiprotestanti yana majina yaliyoanzishwa kutokana na mafundisho wanayodhani kuwa Wakristo wengine wanapaswa kuyafahamu au kiongozi wa kidini wanayedhani kuwa ni bora kuliko wengine?
    2. Soma Matendo 15:2. Je, Paulo na Barnaba walifikiria nini kuhusu ushuhuda wa wale “ndugu?” (Hawakukubaliana kwamba huo ulikuwa ni ushuhuda sahihi. Yalikuwa ni “makubaliano ya haraka haraka.”)
      1. Je, waumini waliamua kwamba suala hili litatuliweje? (Watashauriana na na “mitume na wazee kwa habari ya swali hili.”)
        1. Je, hii inatufundisha nini kuhusu kufanya uinjilisti nje ya mipaka ya kanuni ya wawili na watatu? (Inaonyesha kuwa tunapaswa kushauriana na mamlaka ya juu ya waamini.)
    3. Soma Matendo 15:4-5. Je, palikuwepo na makubaliano kati ya Paulo na baadhi ya viongozi pale Makao Makuu? (Walikaribishwa, lakini palikuwepo na mabishano pale Makao Mkuu.)
    4. Soma Matendo 15:6-11. Je, unaweza kuelezeaje mchakato wa kutatua huu mgogoro kuhusu ushuhudiaji? (Watu wanasema kile wanachokifikiri. Petro anatumia matendo ya Mungu kujenga hoja yake.)
      1. Soma Matendo 1:8-9. Maelekezo ya mwisho kwa wanafunzi wake yalikuwa ni kwamba wapeleke injili ulimwenguni. Je, palikuwa na shaka yoyote kuhusu kuwaendea Mataifa?
      2. Je, Kuna jambo analolikosea Petro? Je, suala si ni tohara badala ya kupeleka injili kwa Mataifa? (Petro anasema kwa usahihi zaidi kuliko hata huko kuwaendea Mataifa. Anasema kuwa Mungu aliwakubali watu wa Mataifa kwa kuwapatia Roho Mtakatifu na kuwahesabia haki kwa imani - hata kama walikuwa hawajatahiriwa.)
        1. Je, kuna lolote la kujifunza katika hili: kwamba Wakristo wenzetu wanaweza wasikubali mtazamo wetu wa kipekee juu ya kile Biblia inachokitaka, lakini jaribio la asidi ni endapo Mungu anawapatia Roho Mtakatifu na kuwahesabia haki kwa neema?
    5. Soma Matendo 15:12. Je, watu wenye mitazamo mbalimbali walichukulianaje kwenye huu mjadala? (Kwa kuheshimiana.)
    6. Soma Matendo 15:13-21. Je, msingi wa “hukumu” ya Yakobo ni upi? (Mwongozo wa Mungu kwenye suala hili, kutoka kwenye Biblia na kwenye maisha ya watu.)
      1. Je, ni sababu gani anayoitoa Yakobo kwenye kanuni (fungu la 20) zinazosalia? (Mungu, akizungumza kupitia kwa Musa, angalao anahitaji mambo haya!)
        1. Kimsingi Musa na Mungu waliwahitaji watu wengi zaidi wa Mataifa. Soma Kutoka 12:48 na Ezekieli 44:9. Je, Yakobo anasema kitu gani? (Maneno ya Yakobo yatawaudhi Wakristo wenye asili ya Kiyahudi. Ubashiri wangu ni kuwa anajaribu kupunguza kiwango cha maudhi.)
      2. Je, hii inapendekeza nini kuhusu mamlaka ya kanisa? Je, unachukulia kuelewa kwamba Yakobo alikuwa anatoa uamuzi wa kanisa kuhusu ujumbe wa uinjilisti?
    7. Soma 1 Wakorintho 8:7-13. Maswali mawili. Kama Paulo anatoa msimamo wa kanisa, je, ni punde tu Paulo amemdhibiti kwa sehemu fulani? Au, je, kauli za Paulo na Yakobo zinakubaliana kikamilifu, na sababu pekee ambayo Yakobo aliepuka mambo yaliyoorodheshwa katika Matendo 15:20 ni kuepuka kuwaudhi waumini wa Kiyahudi wenye imani “changa?” (Jibu linaloweza kuwa na mantiki kubwa linaonekana kuwa ni kwamba Yakobo na Paulo wanakubali kuwa kimsingi kusababisha maudhi ndio tatizo. Hata hivyo, mantiki hiyo inayeyuka pale unapobaini kuwa Matendo 15:20 inajumuisha “uasherati.” Nashindwa kuchukulia kwamba uzinzi ni sawa tu kwa Wakristo “thabiti.”)
    8. Soma Matendo 15:22-29. Je, barua hii inasema nini kuhusu mamlaka ya Yakobo? (Mamlaka kwenye hiyo barua ni ya “mitume na wazee.” Hii inaonyesha kuwa kundi ndilo lililokuwa na mamlaka kwenye hayo maamuzi. Barua yenyewe inaonyesha kuwa ilikuwa imekusudia kuwa ndio iwe mwongozo.)
    9. Hatujaelewa (au angalao mimi binasi) kikamilifu kabisa sura yote ya Matendo 15. Je, tunaweza kuelewa kitu gani kutoka kwenye somo letu? (Kwamba Mungu anapendekeza kuwa jukumu letu la uinjilisti wa kundi uwe ni juhudi za kundi. Kundi linaweza kuwa dogo kabisa la watu wawili, lakini tunatiwa nguvu tukitenda kazi pamoja. Kutenda kazi kwa pamoja ni dawa ya kupoza nguvu ya sumu ya majivuno/kiburi.)
    10. Rafiki, je, utadhamiria hivi leo kumtafuta mwenza na kikundi kwa ajili ya juhudi zako za kiinjilisti? Bado unapaswa kuwang’ang’aniza wale wanaokuzunguka kwenye injili katika maisha yako ya kila siku. Lakini, unapojiingiza/unapojihusisha kwenye ushuhudiaji rasmi wa kuwaendea watu, basi angalao unahitaji kuwa na mwenza.
  4. Juma lijalo: Kujiandaa kwa Ajili ya Uinjilisti na Ushuhudiaji.