Somo la 1: Usuli na Kuzaliwa kwa Musa

Kutoka 1-2
Swahili
Year: 
2025
Quarter: 
3
Lesson Number: 
1

Somo la 1: Usuli na Kuzaliwa kwa Musa

(Kutoka 1-2)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Hivi karibuni tulijifunza kisa cha Ruthu na Naomi. Naomi aliondoka Yuda kutokana na njaa na akaenda Moabu ambapo mwanaye alimwoa Ruthu. Kitabu cha Kutoka kinaanza na kisa kama hicho. Yakobo na familia yake wanakwenda Misri kwa sababu ya njaa katika nchi yao, nchi ambayo Mungu alimuahidi Ibrahimu na uzao wake. Walikwenda kwa sababu palikuwepo na chakula Misri, na chakula hiki kilikuwa ni matokeo ya Mungu kumbariki Yusufu, mwana wa Yakobo. (Angalia Mwanzo 41.) Maswali ya kujiuliza ni, “Kwa nini waliamua kukaa Misri?” Baada ya njaa kwisha, “Kwa nini wasirudi katika nchi waliyoahidiwa na Mungu?” Kama tutakavyoona, ilitokea kwamba kubaki lilikuwa kosa kubwa ambalo liliviingiza vizazi vingi utumwani. Hebu tuzame kwenye somo letu la Kutoka na tujifunze zaidi!

  1.    Kwenda
    1.    Soma Kutoka 1:1-5. Familia ya Yakobo iliyokwenda Misri ilikuwa na ukubwa gani? (Watu sabini.)
    1.    Soma Kutoka 1:6. Kwa nini Yusufu anatajwa kimashuhuri? (Ukisoma kitabu cha Mwanzo kuanzia sura ya 41 hadi 50 utaona kwamba Yusufu, kutokana na uhusiano wake wa karibu na Mungu, aliwaokoa Wamisri dhidi ya njaa. Matokeo yake ni kwamba alipandishwa cheo na kuwa mtu wa pili kwa umashuhuri nchini Misri.)
      1.    Je, ushirika wake na mtu mashuhuri ndio uliofanya uzao wa Yakobo usalie Misri?
    1.    Soma Kutoka 1:7. Hii inaashiria kwamba sababu ya kusalia Misri ni ipi? (Walikuwa wanasitawi. Walikuwa wanatengeneza fedha.)
  1.   Kosa
    1.    Soma Kutoka 1:8-10. Lilikuwa tatizo kubwa kiasi gani kwa Misri kuwa na uzao wa Yakobo wakiishi katika nchi yao? (Walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuishinda Misri na utamaduni wao. Walikuwa “wengi tena wana nguvu [kwa Wamisri].”)
      1.    Unayaelewaje maneno “na kutoka [kutoroka] katika nchi hii?” Je, Wamisri hawakutaka wana wa Israeli waondoke? (Hii inaonesha mawazo yao yaliyovurugwa. Waliogopa idadi ya Waisraeli, lakini waliwahitaji kama vibarua. Walikuwa wachungaji, hivyo bila shaka walikuwa chanzo cha chakula nchini Misri.)
    1.    Soma Kutoka 1:11-13. Wamisri “wanawatendeaje kwa akili” (kifungu cha 10) wana wa Israeli? (Wanawafanya kuwa watumwa.)
      1.    Ikiwa hawa walikuwa watu wa Mungu, kwa nini Mungu hakuwafunulia hatari iliyokuwa mbele yao na kuwahamasisha kurejea katika nchi aliyoahidiwa Ibrahimu?
    1.    Soma Mwanzo 37:25-28. Nduguze Yusufu walimwuza utumwani. Je, utumwa wa uzao wa nduguze ni malipo? Je, hiyo ndio sababu hakuna kumbukumbu ya Mungu kujaribu kuepusha hali yao ya utumwa nchini Misri katika siku zijazo? (Marekani ilikuwa mojawapo ya mataifa mengi yaliyowafanya Waafrika kuwa watumwa. Matokeo ya utumwa huo ni kwamba kati ya Wamarekani 620,000 na 750,000 walifariki kwenye vita miongoni mwa majimbo ili kukomesha utumwa. Haya yalikuwa maafa makubwa kwa Wamarekani ikilinganishwa na vita vyote walivyowahi kupigana. Hii inaweza kuonekana kama aina mojawapo ya malipo kutokana na kuruhusu utumwa.)
  1.      Uovu
    1.    Soma Kutoka 1:15-16. Farao alitekeleza uovu gani wa ziada ili kupunguza nguvu ya wana wa Israeli? (Aliwaelekeza viongozi wa wakunga wa Kiebrania kumwua mtoto ikiwa alikuwa wa kiume.)
      1.    Je, hii ni mada tunayoiona ikijirudia baadaye katika historia? (Ujerumani ilidhamiria kuwamaliza Wayahudi. Hata katika nyakati za sasa, Margaret Sanger ni shujaa kwa wale wanaoamini katika sayansi ya uzalishaji watoto wenye afya (kwa nia ya kustawisha hazina ya jeni ya watu), dhana ya kwamba tunapaswa kusimamia kwa dhati uaviaji mimba wa watu “dhaifu.” Hii inaakisi mawazo ya Farao.)
    1.    Soma Kutoka 1:17-21. Je, wakunga wanamdanganya Farao? (Walichomwambia Farao kinakinzana na kauli iliyopo katika kifungu cha 17 kwamba hawakufanya kama walivyoamriwa na Farao.)
      1.    Mungu anawatunuku wakunga. Kwa nini? (Waliyalinda maisha ya watoto wa kiume.)
    1.    Soma Kutoka 1:22. Mpango wa Farao unaofuata ni upi wa kuiepusha Misri na watoto wa kiume wa Kiebrania wasiotakiwa?
  1.   Musa
    1.    Soma Kutoka 2:1-3. Je, hii inaendana na amri ya Farao kwamba watoto wa kiume wa Kiebrania “mta[wa]tupa motoni?” Angalia Kutoka 1:22.
      1.    Utaona kwamba mtoto huyu wa kiume alikuwa Mlawi. Je, kuna umuhimu katika hilo? (Tutalijadili hili baadaye.)
    1.    Soma Kutoka 2:4-6. Je, ungetarajia mwitiko (reaction) kama huu wa binti wa mtu aliyeamuru mauaji ya watoto wa kiume wa Kiebrania?
    1.    Soma Kutoka 2:7-8. Ni wazo la nani kwa binti Farao kumuasili Musa?
    1.    Soma Kutoka 2:9-10. Musa ni mtoto wa nani? (Sasa ni mjukuu wa Farao!)
      1.    Utaona kwamba mamaye Musa kibaiolojia alimlea Musa hadi “alipokuwa mkubwa.” Unadhani hiki kilikuwa kipindi cha miaka mingapi? (Soma Waebrania 11:24. Hii inatuambia kuwa Musa “alipokuwa mtu mzima” alikataa kuitwa “mwana wa binti Farao.” Hii inabainisha kuwa Musa alikuwa na wazazi wake halisi kwa muda mrefu, kwa kipindi kirefu kiasi kwamba alijinasibisha nao na si mamaye aliyemuasili.)
      1.    Tafakari jinsi jambo hili litakavyojitokeza katika makazi ya Farao. Unadhani binti Farao alibainisha kuwa alimwokoa mtoto wa kiume wa Kiebrania? Je, hii ni aina ya uasi unaoutarajia kutoka kwa mabinti wadogo?
        1.    Je, kifungu cha Waebrania 11:24 kinabainisha kuwa Musa pia alikuwa muasi katika makazi ya kifalme?
        1.    Farao amefanya uamuzi gani juu ya jambo hili? (Kwa kuwa Musa aliishi, tunafahamu alimkubali Musa angalao kwa kiwango fulani.)
    1.    Soma Kutoka 6:20. Hii si tu kwamba inatuambia majina ya wazazi halisi wa Musa, bali pia inatuambia kuwa Haruni ni nduguye. Amramu na Yokebedi waliwezaje kumwokoa Haruni asiuawe? (Lazima itakuwa alizaliwa kabla ya amri ya kifo.)
    1.    Soma Kutoka 28:1-3. Utakumbuka kwamba hapo awali niliuliza kama kuzaliwa Mlawi kulikuwa na umuhimu wowote. Hii inatuambia nini? (Haruni na wanaye walikuwa makuhani wa Israeli.)
    1.    Hebu tutafakari kidogo. Je, Mungu ameingilia kati ili kuyaokoa maisha ya Musa?
      1.    Je, Mungu ameingilia kati ili kumfanya Musa kuwa mjukuu wa Farao?
      1.    Unadhani ni nini lengo la Mungu kwa Musa? (Ninadhani Mungu alimkusudia awe Farao na kuwaweka huru watu wa Mungu kutoka utumwani Misri. Mpango unaonekana kuwa wa dhahiri.)
  1.    Kosa Jingine?
    1.    Soma Kutoka 2:11. Unadhani Musa alipokea mafunzo ya aina gani alipokuwa akikua?
      1.    Je, mafunzo ndio yatakayomsaidia kuwaongoza watu wake kurejea katika nchi aliyoahidiwa Ibrahimu?
    1.    Soma Kutoka 2:12. Je, Musa alidhani kuwa anachokifanya si sahihi? (Ndiyo! Alitaka kuwa na uhakika kuwa hakuna mtu aliyeyashuhudia mauaji. Alizika ushahidi.)
      1.    Musa alikuwa mtu muhimu. Je, angeweza kufanya Mmisri akamatwe? Je, angeweza kumtishia Mmisri?
    1.    Soma Kutoka 2:13-14. Kwa nini Musa anajihusisha kwenye mgogoro huu? Hii inatuambia nini kuhusu hulka yake?
    1.    Soma Mithali 26:17. Hii inatufundisha nini kuhusu kuingilia ugomvi usio wetu?
      1.    Unadhani Musa alifikaje umri aliokuwa nao bila hapo kabla kuingilia kati kwa niaba ya watu wake dhidi ya manyanyaso ya Wamisri?
    1.    Soma Kutoka 2:15. Kwa nini Farao afanye uamuzi wa kumwua mjukuu wake mwenyewe juu ya tatizo na mmojawapo wa mabwana wa watumwa wake wa Kimisri? (Lazima hii itakuwa inaakisi concern ya jambo la muda mrefu kuhsu kumuasili Muebrania au ninachokidhani chenye uwezekano mkubwa ni kwamba, Musa hakuwa mtu wa kuaminika lilipokuja suala la Waebrania.)
      1.    Unadhani Musa alipaswa kumwua Mmisri? (Kama lingekuwa suala lenye utetezi, basi Musa asingejaribu kuficha mauaji.)
      1.    Je, Musa ametenda kosa la kutisha ambalo si tu kwamba linabadilisha mwelekeo wa maisha yake, bali pia linazuia mpango wa Mungu kumfanya achukue mamlaka na kazi ndani ya mfumo wa kuwaweka huru Waebrania?
    1.    Soma Mwanzo 50:14. Maoni ya watu wengi yanasema kuwa safari ya kurudi Kaanani ilikuwa umbali wa maili 300 (kilomita 480). Kumbuka kwamba nduguze Yusufu walifanya safari hii angalao mara mbili ili kununua nafaka. Fikiria kama Musa angekuwa Farao na kuweka mipango ya Waebrania kurejea katika nchi aliyoahidiwa Ibrahimu. Je, hiyo ingekuwa njia bora kabisa ya kurejea?
      1.    Unadhani Waebrania wangeondoka kwa hiari kama wasingekuwa wamefanywa kuwa watumwa?
    1.    Soma Kutoka 2:23-25. Kwa nini sasa hivi? Kwani hapo kabla watu hawakumwomba Mungu kuwaokoa?
    1.    Rafiki, ninayaona makosa yaliyotendwa na watu wa Mungu na Musa. Ninaweza nisiwe sahihi, lakini kama niko sahihi, je, unaweza kuona jinsi walivyoyafanya maisha yao kuwa mabaya zaidi? Je, utamwomba Mungu aziongoze hatua za maisha yako ili yawe bora?

 

  1.   Juma lijalo: Kichaka Kinachowaka Moto.