Somo la 6: Kumtumainia Kristo Pekee

(Wafilipi 3:1-16)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
1
Lesson Number: 
6

Somo la 6: Kumtumainia Kristo Pekee

 

(Wafilipi 3:1-16)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, dhana ya kuhesabiwa haki kwa imani inaonekana kuwa na mantiki au ya kawaida kwako? Sivyo kwa upande wangu. Tukiweka kando imani yangu kwa baraka za Mungu, maishani mwangu mwote nimeamini na kupitia uzoefu wa kwamba kama nikifanya kazi kwa juhudi nitafanikiwa. Huu si tu mtazamo wangu; bali pia ni fundisho la Biblia. Soma Mithali 24:30-34 inayofafanua kuwa tunapaswa kujifunza kutoka kwa “mtu mvivu.” Kuwa goigoi hukufanya kuwa masikini. Bila shaka ndio maana nawe umeliona jambo hilo hilo. Ni kawaida kutumia mawazo haya kwenye kuhesabiwa haki. Lakini Biblia inatufundisha jambo tofauti kabisa. Kuhesabiwa haki ni thawabu ambayo hatuwezi kuifanyia kazi. Tukijaribu kuifanyia kazi, au tukidhani kuwa tumeshaipata, basi tumekiuka kanuni za wokovu. Hebu tuzame kwenye mjadala wa Paulo na Wafilipi kuhusu kuhesabiwa haki kwa imani pekee!

 

  1.    Furaha na Mbwa

 

    1.    Soma Wafilipi 3:1. “Furahini katika Bwana” ni maneno tunayoyasikia nyakati zote. Maoni ya John MacArthur yanataarifu kuwa Paulo anaandika kuwa tunapaswa “kufurahi,” lakini hii ni mara ya kwanza Paulo anaongezea “katika Bwana.” Je, kuna tofauti kati ya “furahini,” na “furahini katika Bwana?” (Ndiyo. Chanzo kimoja cha furaha kimahsusi kimefungamanishwa na Yesu.)

 

      1.    “Unafurahije katika Bwana?” (Ninafurahia katika wema wake kwangu.)

 

      1.    Je, unajisikia furaha ya jumla? Ikiwa sivyo, je, unaweza kufurahi katika Bwana na usiwe na furaha kwa ujumla?

 

    1.    Soma Wafilipi 3:2. Kama ungekuwa unamfahamu mtu ambaye mara zote anawatafuta “mbwa,” na “watenda maovu,” je, ungetarajia mtu huyo awe na furaha? (Hilo linaonekana kuwa giza tororo na si mtazamo unaohusiana na furaha.)

 

      1.    Watu wengi wanapenda mbwa. Paulo anazungumzia jambo gani? (Katika Mathayo 15 Yesu na wanafunzi wake wanaendewa na mwanamke Mkaanani anayeomba msaada kwa sababu binti wake amepagawa pepo. Soma Mathayo 15:25-28. Yesu anamuita mwanamke huyu na binti wake, “mbwa.”)

 

        1.    Je, Paulo anaandika kuhusu wasio Wayahudi anapoandika juu ya “mbwa?”

 

  1.   Mwili

 

    1.    Soma Wafilipi 3:3. Paulo anadai kuwa yeye ni “tohara.” Je, hii inathibitisha kuwa anawaita wasio Wayahudi “mbwa?”

 

      1.    Paulo anamaanisha nini anaposema kuwa “hautumainii mwili?” (Sasa taswira inakuwa bayana ili kutusaidia kuelewa Wafilipi 3:2-3. Paulo alikuwa mfungwa katika kupambana dhidi ya amri ya kwamba lazima waongofu wa Mataifa watahiriwe. Angalia Matendo 15. Kwa kujiita “tohara,” Paulo amekatilia mbali fundisho hili linaloamrisha tohara.)

 

      1.    Hebu tulivunjevunje hili. Paulo anamuita nani “mbwa,” “watenda maovu,” na wale “wajikatao?” (Anawazungumzia viongozi wa Kiyahudi wanaosisitiza juu ya tohara.)

 

        1.    Kwa nini kitendo hicho kiwe “kutenda maovu?” (Dhana iliyopo ni kwamba lazima mtu atende mambo haya ili kuwa na uhusiano sahihi na Mungu. Ni uovu kuamini kuwa unaweza kutenda jambo ili kuupata wokovu wako.)

 

    1.    Soma Warumi 2:29. Kifungu hiki kinaifafanuaje tohara? (Tohara mpya ni suala la moyo. Ni kumwabudu Roho Mtakatifu, kumtukuza Yesu na kile alichotutendea, na si kujiamini kwa matendo yetu.)

 

      1.    Kwa ufupi, unazielewaje kauli za Paulo kuhusu “mwili?” (Anaandika juu ya kutenda mambo ili kuupata wokovu.)

 

  1.      Shujaa Mkuu wa Matendo

 

    1.    Soma Wafilipi 3:4-6. Kwa nini Paulo anasema kuwa ana matendo mazuri zaidi kuliko wengine? (Mtu mvivu anaweza kutarajiwa kushangilia kuhesabiwa haki kwa imani pekee kwa sababu kukataa kufanya kazi ndio asili ya kawaida ya watu goigoi. Paulo anathibitisha kuwa alikuwa mtenda kazi asiye wa kawaida. Hatangazi imani ili kuficha udhaifu wake, bali anaisimamia imani kwa sababu huo ndio ukweli.)

 

    1.    Soma Wafilipi 3:7-8. Hebu tujadili hili. Isipokuwa kwa kuwatesa Wakristo, mambo mengine yote anayoyabainisha Paulo ni mazuri. Anasema kuwa “hakuwa na hatia” katika kuishika torati. Kitendo hicho kinaonekana kuwa kikubwa isivyo kawaida kwa upande wangu. Hayo yanawezaje kuwa “hasara?” (Paulo anasema kuwa hayana thamani kwa kuzingatia msingi wa uzima wa milele.)

 

      1.    Litafakari hili kidogo. Mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka thelathini ya kufanya kazi na kijana wangu kuandika na kubandika (post) masomo haya kwenye mtandao wa Intaneti. Je, hiyo ni hasara? (Ndiyo, kwa namna mbili zinazohusiana na uzima wa milele. Kwanza, bidii hiyo ya kazi ya miongo kadhaa haifanyi chochote kabisa kuupata uzima wa milele kwangu au kwa mwanangu. Pili, inanishawishi kudhani kuwa juhudi zinanifanya niwe na haki.)

 

  1.   Haki kwa Imani

 

    1.    Soma tena Wafilipi 3:8 na uongezee Wafilipi 3:9. Paulo anatafuta haki gani? (Ile itokayo kwenye “imani kwa Yesu.” Uelewa huu ni muhimu kwa ajili ya uzima wa milele.)

 

      1.    Je, unayategemea matendo yako, utii wako, kama kigezo kitakachokupeleka mbinguni?

 

      1.    Je, ni jambo la fedheha kwamba wewe ni ombaomba, kama ilivyo kwa mdhambi yeyote?

 

      1.    Hebu turejee kwa Paulo na “mbwa” wake. Je, wale wanaoyafanya matendo kuwa kigezo cha kuupata uzima wa milele ni “mbwa?”

 

    1.    Soma Wafilipi 3:10-11. Tunafananaje na Yesu katika mauti? Ilikuwa muhimu kwamba Yesu aliishi maisha makamilifu, sawa? (Paulo anatufundisha kuwa Yesu alipokufa, baada ya kuishi maisha makamilifu, alitufungulia njia ya kupitia uzoefu wa ufufuo na kuingia kwenye uzima wa milele.)

 

      1.    Kwa nini Paulo anasema, “kwa njia yoyote,” wakati alitilia tu mkazo njia sahihi ya kuupata uzima wa milele? (Paulo anamwachia Mungu mambo ya ndani zaidi. Hotuba yote ya Paulo inakinzana na uelewa wa jumla (hata kutoka kwenye Biblia) kwamba unafanya kazi na kufanikiwa. Paulo anafafanua kuwa tunaacha kuyategemea matendo yetu, tunamtegemea Yesu pekee, na hilo linatupatia uzima wa milele. Mtazamo huu mbadala ndio unaoweza kuwa “kwa njia yoyote.”)

 

  1.    Kukazia Ukamilifu?

 

    1.    Soma Wafilipi 3:12-13. Hebu subiri kidogo. Ikiwa haki ni zawadi itolewayo bure ambayo siwezi kuifanyia kazi, Paulo anaandika juu ya jambo gani pale anaposema, “nakaza mwendo” na “nikiyachuchumilia yaliyo mbele?” Kukaza na kuchuchumilia yanaonekana kama mtazamo wangu wa zamani kuhusu jinsi ambavyo kufanya kazi kwa bidii huleta mafanikio! (Je, ni vigumu kwako kuachana na bidii yako yote ya kazi na mafanikio katika injili? Je, ni vigumu kwako kuacha kujitegemea mwenyewe? Ikiwa ndivyo, kaza mwendo na chuchumilia yaliyo mbele katika kuitegemea kwako haki kwa imani!)

 

      1.    Jiulize hili: ukikabiliana na tatizo lisilotarajiwa, akili yako inageukia wapi mara moja? (Mara moja ninajiuliza ninapaswa kufanya nini ili kutatua au kupunguza tatizo. Ninahisi hicho ndicho wengi wetu tunafanya. Tunahitaji badiliko la mtazamo. Tunatakiwa kulichukulia badiliko hili kwa dhati.)

 

    1.    Soma Wafilipi 3:14-16. Paulo anatuambia kuwa kama tumekomaa kiroho, tunapaswa kutafakari na “kukaza mwendo” kuielekea zawadi ya wito wa Mungu. Je, “kukaza mwendo” huku kunatoa wito wa bidii ya kazi kwa upande wetu? (Lazima mara zote tuzingatie uwezo wa Roho Mtakatifu wa kubadili mitazamo yetu. Hata hilo ninaliona kama pambano la kila mara. Ninapoona uovu unaongezeka, mara zote huwa ninatafakari jinsi ninavyoweza kuuibua na kuupinga. Ninahitaji Roho Mtakatifu anishawishi kutafakari kwanza nguvu ya maombi.)

 

    1.    Rafiki, kwa namna fulani wokovu ni rahisi, na kwa namna nyingine wokovu ni mgumu. Maishani mwangu nimejifunza somo kubwa kwamba bidii ya kazi ifanyikayo kwa werevu huleta mafanikio. Hilo ni kweli, lakini hiyo si njia ya uzima wa milele. Je, utaungana nami, sasa hivi, kumwomba Roho Mtakatifu abadili mtazamo wako ili kuamini na kutumaini kile pekee ambacho Yesu ametutendea ili kutupatia uzima wa milele?

 

  1.   Juma lijalo: Uraia wa Mbinguni.