Somo la 10: Kutimilika Katika Kristo

(Wakolosai 2)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
1
Lesson Number: 
10

Somo la 10: Kutimilika Katika Kristo

(Wakolosai 2)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
                
Utagulizi: Jaribu kujiweka kwenye nafasi ya watu ambao Paulo anazungumza nao kwenye barua yake kwa Wakolosai. Hivi leo, Ukristo ndio dini kubwa duniani. Fikiria kwamba hilo halikuwepo katika ulimwengu wako. Dini za kipagani zimejaa tele. Watu wengi muhimu wanaziamini dini hizo. Dini mpya kabisa, iliyojengwa juu ya maisha na kifo cha rabi wa Kiyahudi, inatoa madai kuwa hiyo ni dini ya kweli. Si dini mpya kabisa kwa sababu inadai kuwa inatimiza dini ya Kiyahudi (Judaism). Kufanya mambo kuwa magumu zaidi ni kwamba “wataalamu” kadhaa kwenye hii dini mpya wanafundisha mambo tofauti tofauti kuhusu dini hiyo. Sasa upo kwenye nafasi ya Wakolosai. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili kuelewa jinsi Paulo anavyojenga hoja kwa ajili ya Yesu na imani!

I.    Mpambano

A.    Soma Wakolosai 2:1-3. Kwa nini Paulo anapambana katika juhudi zake za kuwashawishi Wakolosai na Walaodikia juu ya ukweli? (Pamoja na matatizo yaliyobainishwa kwenye sehemu ya Utangulizi, Paulo hajaonana nao ana kwa ana.)

1.    Utaona katika kifungu cha pili Paulo anarejelea “siri ya Mungu.” Unadhani kwa nini Paulo anaiita injili kuwa ni siri? (Kila mtu anataka kuelewa watu wengine wanafanya nini. Tunapenda kujua majibu ya mambo ya siri.)

a.    Je, Paulo anaandika hili kama njia ya kuchochea hamasa? Au injili ndio siri halisi? (Kwa dhahiri Yesu si kama miungu ya kale. Yeye si mbinafsi. Hana wafuasi kwa ajili ya kumtumikia tu. Ni kinyume chake. Yesu anawatumikia (na aliwatumikia) wale wanaomfuata. Hii ni siri ya kina sana.)

2.    Paulo anaandika kuwa siri “ni Yesu.” Ni kwa namna gani hilo ni kweli? (Yesu anajumuisha siri. Yeye ndiye aliyejitoa nafsi yake kwa upendo wa kina kabisa usiopimika.)

B.    Soma Wakolosai 2:4. Ni nini iliyo hatari kwa hawa Wakristo wapya? (Kwamba watadanganywa. Watapotoshwa.)

1.    Kwa nini udanganyifu huu ni mgumu sana kuufikia na kuushinda? (Paulo anaziita hoja za wapinzani kuwa “zinakubalika.”)

a.    Je, unaona hoja “zinazokubalika” leo zinazohafifisha Neno la Mungu? (Nimesoma makala kubwa ya kanisa inayojenga hoja kuwa nadharia ya uibukaji haikinzani na maelezo ya Uumbaji ya kitabu cha Mwanzo. Makala hayo yaliandikwa kwa namna inayokubalika, lakini kwa dhahiri hitimisho lake ni la uongo. Biblia inasema kuwa Yesu alinena na ulimwengu ukawepo. Mwanzo 1; Yohana 1.)

2.    Ni nini jibu la hoja za uongo? (Soma Wakolosai 2:5. Kujiimarisha kiimani kwa Yesu, ikiwemo uwezo wake kama Muumbaji (Yohana 1) na Mkombozi wetu, yanajibu hoja za uongo.)

II.    Kristo na Maisha/Uhai

A.    Soma Wakolosai 2:6-7. Paulo anatuambia tufanyie kazi kivitendo kile tunachoamini. Kisha anasema kuwa tunapaswa kuwa na shukrani. Maelekezo ya kuwa na shukrani yana-assume jambo gani? (Kwamba tuna jambo la kushukuru.)

1.    Hebu tuchunguze assumption hii ya msingi. Je, kumtii Yesu kutayaboresha maisha yetu? (Hiyo ndio assumption ya msingi. Tunatenda kile tunachokiamini na matokeo yake ni maisha bora.)

B.    Soma Wakolosai 2:8. “Kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu” inakinzana na mafundisho ya Yesu. Je, unaweza kutaja mafundisho ya ulimwengu? (Soma Mwanzo 3:4-5. Tunaona katika jaribu hili fundisho la kutoridhika. Eva alitaka kupata zaidi. Alitaka kuwa zaidi.)

1.    Utaona kwamba kifungu cha 8 kinarejelea “madanganyo matupu,” “falsafa,” na “mapokeo ya wanadamu.” Kwa dhahiri, udanganyifu si mzuri. Lakini tamaduni na falsafa vinaweza kuwa chanya. Hapa Paulo anazungumzia nini? (Kwanza, Paulo anaonya dhidi ya kuchukuliwa “mateka” kwa mambo haya. Hiyo itamaanisha kudhibitiwa na mambo hayo. Pili, uovu katika mambo haya hutokea pale tunapopingana na Yesu.)

C.    Soma Wakolosai 2:9-10. Paulo anaandika kuwa na utimilifu mara mbili. Uungu kamili unakaa ndani ya Yesu, nasi tumekamilika katika Yesu. Hilo litatusaidiaje kuepuka kuchukuliwa na mafundisho ya ulimwengu? (Tunapotimilika katika Yesu, hatuna nafasi ya kilicho cha uongo.)

1.    Hebu turejee kwenye makala inayounga mkono uibukaji niliyoibainisha awali. Makala ilipendekeza kuwa tunapaswa kuwa tayari kupokea sayansi mpya. Je, tunapaswa kufanya hivyo? (Tunapaswa kuwa tayari kupokea sayansi mpya ili kugundua jinsi inavyounga mkono Neno la Mungu. Hatupaswi kuacha nafasi kwa sayansi kuchukua nafasi ya Neno la Mungu.)

2.    Mojawapo ya hoja za kipuuzi iliyobainishwa kwenye makala ni kwamba sayansi inayohusu mianzo ni ya kuaminika kwa sababu inafuata nadharia ya kisayansi. Sayansi ya kweli inatambua jambo jipya na kisha inaizalisha upya kwa kuaminika. Je, hilo linawezekana kwa mianzo? (Hakuna mwanadamu aliyeshuhudia mwanzo wa ulimwengu wetu. Sayansi haiwezi kuumba au kuzalisha upya uhai kutoka katika hali ya kutokuwepo kabisa.)

D.    Soma Wakolosai 2:11-14. Mjadala wa Agano Jipya kuhusu tohara ulikuwa mkali. Tohara mpya kwa Wakristo ni ipi? (Ubatizo.)

1.    Unaweza kufafanua hili?

E.    Soma Warumi 4:11-12 na Mwanzo 17:9-11. Ni kwa jinsi gani tohara na ubatizo ni dhana zinazofanana? (Tohara na ubatizo ni ishara, alama (au muhuri) ya makubaliano kati ya Mungu na mwanadamu. Makubaliano hayo ni kumpokea Yesu kama mbadala wetu. Mbadala huo unatupatia uzima wa milele.)

F.    Angalia tena Wakolosai 2:12. Ni kwa jinsi gani ubatizo na kifo na ufufuo wa Yesu vinahusiana? (Kuzikwa ndani ya maji hushiriki katika kifo na maziko ya Yesu. Kuibuka kutoka kwenye maji ya ubatizo ni ushiriki katika ufufuo wa Yesu.)

G.    Soma Wakolosai 2:15. Watawala na mamlaka wanavuliwaje enzi zao? (Watawala wa giza walitaka tufe milele kwa ajili ya dhambi zetu. Yesu aliyachukua madai hayo kwa wale wanaompokea. Kwa kuonesha asili halisi ya Shetani na dhambi, Yesu alishinda dhidi ya dhambi.)

III.    Kuishi Maisha Kamili

A.    Wakolosai 2:10 inatuambia kuwa “tumetimilika” katika Yesu. Soma Wakolosai 2:16-17 na Wakolosai 2:23. Kifungu hiki ni muhimu kwangu kwa sababu ninaitunza Sabato ya siku ya saba. Je, msimamo wetu juu ya kile tunachokula au kunywa, sikukuu za Agano la Kale, au kuitunza Sabato unatuokoa? (Jibu la dhahiri ni, “Hapana.” Kinachotuokoa ni kutimilika katika Yesu. Kubatizwa katika Yeye.)

1.    Wakolosai 2:17 inasema kuwa haya ni “kivuli cha mambo yajayo.” Hii inaongezea nini kwenye uelewa wetu wa kifungu cha 16? (Vyakula vya kimapokeo na unywaji, sikukuu (ambazo pia ziliitwa “Sabato”) vyote vilijielekeza kwa maisha yajayo, kifo na ufufuo wa Yesu.)

2.    Wakolosai 2:23 inazungumzia “kujinyima anasa na tamaa za mwili.” Hii inaendanaje na Wakolosai 2:16? (Ingawa ninaamini sikukuu zilikuwa kipindi cha furaha, kwa ujumla mambo yaliyobainishwa katika kifungu cha 16 yanahusisha masuala ya kujikana nafsi.)

B.    Soma Wakolosai 2:18-22. Kwa mara nyingine Paulo anaandika kuhusu anasa na sheria zinazotuambia msishike, msionje, au msiguse. Je, hii inaonekana kwako kama sheria za kimapokeo za Musa au jambo jingine? (Hii inajielekeza kwenye sheria ya mapokeo.)

C.    Bado hatujajadili kikamilifu suala la endapo Paulo anajumuisha Sabato ya kila juma kama jambo ambalo hakuna hukumu inayopaswa kutolewa. Maoni ya Adam Clarke kuhusu kifungu hiki yanajenga hoja ya nguvu kwamba Paulo haandiki juu ya Sabato ya kila juma. Clarke anasema, kwa kuendana na Mwanzo 2:3 na amri ya Kutoka 20:8-11, kwamba Sabato si sehemu ya sheria ya mapokeo. Ni “amri ya wajibu wa kudumu.” Je, unaichukulia yoyote kati ya Amri Kumi kama jambo ambalo Wakristo hawapaswi kutoa hukumu? Je, ni sawa kwa Mkristo kuua, kuiba, kuzini, au kutamani? (Ninahisi wengi watajibu, “Hapana, kukiuka Amri Kumi si sawa.”)

1.    Wakristo wengi hawazishiki sikukuu za Agano la Kale au sheria za vyakula. Lakini wanaadhimisha siku ya ibada ya kila juma. Kwa nini? Kama kweli Wakristo wanadhani kuwa Sabato ya kila juma imetupwa kwenye jalala la historia na Paulo, kwa nini kuendelea kuadhimisha siku moja ya kila juma? (Wakrissto wanaonesha kwa mienendo yao kwamba hawachukulii siku moja ya ibada ya kila juma kuwa sehemu ya sheria ya mapokeo na Paulo.)

2.    Kama unadhani kuwa kuiadhimisha siku moja ya ibada kwa juma bado ni sehemu ya kutimilika katika Yesu, kwa nini usiabudu kwenye siku mahsusi aliyoiamuru – Jumamosi? (Hakuna amri au vitendo vinavyoidhinisha siku nyingine ya pumziko. Yesu aliadhimisha pumziko la Sabato wakati wa juma la Uumbaji. Aliamrisha pumziko la Sabato katika Mlima Sinai. Yesu pamoja na wanafunzi wake waliitunza Sabato wakati Yesu akiwepo duniani. Na, yumkini la muhimu zaidi, aliadhimisha pumziko la Sabato katika kusherehekea ushindi wake wa dhambi kabla ya kufufuka kwake siku ya Jumapili. Ushahidi wa kutunza Sabato ni mkubwa kupita kiasi.)

D.    Rafiki, Paulo anaonesha kuwa Yesu amefanya yote kwa ajili yetu! Tunatakiwa kutegemea kile alichotutendea na kutimilika katika Yeye. Kutimilika katika Yesu kunajumuisha kuenenda kama alivyoenenda. Je, utampokea Yesu kama Mwokozi wako sasa hivi? Je, utajitoa, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kutembea pamoja naye?

IV.    Juma lijalo: Kuishi Pamoja na Kristo.