Somo la 7: Maombi Halisi
Somo la 7: Maombi Halisi
(Mathayo 6 & 18, Luka 11, Waefeso 3)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Utangulizi: Je, uko tayari kujifunza zaidi juu ya kuwasiliana na Mungu? Juma lililopita tulijifunza vifungu kadhaa vya Biblia, ikiwemo onyo la Yesu katika Mathayo 6 kuhusu kuomba hadharani kwa lengo la kuwafurahisha watu wengine. Pia alionya juu ya “maneno matupu” na maneno mengi kwenye maombi kwa dhana potofu ya kwamba “maneno mengi ni bora zaidi” linapokuja suala la maombi. Yesu pia alituambia kuwa Mungu anajua tunachohitaji kabla hatujaomba. Bwana wetu anaendelea katika Mathayo 6 kujadili Sala ya Bwana. Fuatana nami kwa kina kwenye mfano wa Yesu wa maombi!
I. Utangulizi wa Sala ya Bwana
A. Soma Mathayo 6:9. Kabla hatujaingia kwenye maeneo mahsusi kwenye maombi ya Yesu, tunapaswa kujadili jinsi tutakavyotumia sala yake ya mfano. Yesu anasema, “Basi ninyi salini hivi,” ikifuatiwa na sala yake ya mfano. Unadhani anamaanisha nini anaposema “salini hivi?” (Hivi punde tu Yesu amesema katika Mathayo 6:8 msisali kama “wao,” ikimaanisha wanafiki waliomo ndani ya sinagogi na Mataifa wenye “maneno mengi.” Hakuna hata njia moja kati ya hizo iliyo sahihi. Sasa Yesu anatoa njia sahihi ya kuomba.)
1. Unadhani Yesu anamaanisha jambo gani jingine kwa kutumia neno “na hao,” ambalo kwa Kiyunani linamaanisha “kwa mtindo huu?” Unadhani tunapaswa kukariri ombi la Yesu na kulirudia?
2. Kama tutalirudia ombi la mfano la Yesu, jambo gani litalifanya lisiwe aina ya urudiaji usio na maana ambao Yesu aliuonya?
a. Je, aina hiyo ya ombi itakuwa ya kimazungumzo sana? (Hapana. Lakini itatufanya tusitoke nje ya mada sahihi.)
B. Sura ya 11 ya kitabu cha Luka ina sehemu fupi ya Sala ya Bwana. Soma Luka 11:2. Hapa, Yesu anatumia neno tofauti na “na hao.” Tafsiri za ESV na KJV zinalitafsiri neno hilo, “semeni.” Kiyunani cha asili, kwa mujibu wa Strong, kinaweza kumaanisha “hotuba ya utaratibu au maelezo yaliyopangwa.” Je, hiyo inaongezea ufafanuzi zaidi na kuashiria kuwa tunapaswa kurudia ombi neno kwa neno?
C. Tafakari tena kwamba Mathayo 6:9 inasema ombeni “hivi” angalao kumaanisha “si kama” wanafiki na wapagani. Katika shule ya sheria tunawafundisha wanafunzi kuwa na “mpango wa utekelezaji (roadmap)” wanapokuwa kwenye ushindani wa hoja ya kukata rufaa. Je, Yesu anatupatia mpango wa utekelezaji? (Mifano isiyo sahihi ilihusisha kuomba ili kuwafurahisha wengine. Au kuomba kwa mtazamo kwamba Mungu hajui mazingira yako. Kwa hiyo, “ndiyo,” nadhani angalao huu ni mpango wa utekelezaji.
II. Undani wa Sala ya Bwana
A. Soma tena Mathayo 6:9. Kipengele cha kwanza cha ombi la mfano la Yesu ni kipi? (Kumtukuza Mungu.)
1. Hebu tuendelee na mjadala wetu wa jinsi ya kutumia mfano wa Yesu. Kama Yesu alikuwa anatupatia mpango wa utekelezaji, je, kungekuwa na uwezekano mkubwa kwamba angesema, “Anza kwa kumsifu Mungu?”
2. Je, maneno anayoyatumia Yesu ni njia ya kimantiki ya kumkaribia Mungu wa Ulimwengu? (Naam. Tulipojadili kunukuu dhidi ya mpango wa utekelezaji, sikumaanisha kuashiria kwamba kunukuu maneno ya Yesu ni jambo baya. Ninahisi kwamba kwa kiwango fulani Yesu alidhamiria tunukuu sala yake. Sidhani tu kama kunukuu pekee ndio uelewa kamili au komavu zaidi wa kile ambacho Yesu anatufundisha. Ninapendelea zaidi njia ya mpango wa utekelezaji. Kwa mfano, ninadhani maneno ya ziada ya kumtukuza Mungu ni jambo zuri zaidi.)
B. Soma Mathayo 6:10. Linganisha na Luka 11:2. Jambo gani linafanana kwenye vifungu vyote viwili? (Yesu anatuambia tuombe kwa ajili ya kurejea kwake.)
1. Kuna tofauti gani? (Luka 11:2 haijumuishi ombi kwamba mapenzi ya Mungu yatimizwe duniani.)
a. Una wazo lolote kwa nini haiko hivyo? (Kama unaangalia marejeo na kanuni ya Yesu, itakuwa na mantiki kwako kutaka mapenzi yake yatawale mazingira yako ya sasa. Ungetaka kanuni yake iwe kanuni ya maisha yako.)
C. Soma Mathayo 6:11-12. Unadhani kwa nini Yesu anatuhamasisha tuombe kwa ajili ya mahitaji yetu kabla ya kutubu dhambi zetu? (Yesu anaashiria kwamba mahitaji yetu ya kila siku ni muhimu sana kwake. Mpangilio unavutia: anatukaribisha kuomba mahitaji kabla ya msamaha. Hiyo haimaanishi dhambi si muhimu, lakini Mungu anajali mambo yote maishani mwetu. Ilinichukua muda mrefu kulielewa hili. Kwa miongo kadhaa, mada ya kwanza ya ombi langu ilikuwa ni kuomba msamaha wa dhambi zangu. Nilitaka kuanza upya kwa rekodi mpya!)
1. Unaweza kufafanua kwa nini Mungu anaweka kipaumbele kwenye mahitaji yetu badala ya uvunjaji wetu wa sheria yake?
2. Kigezo gani kinawekwa kwenye msamaha wa dhambi zetu? (Kwamba tuwasamehe wale wanaotukosea. Hii ni mada ya muhimu sana ambayo tutairudia.)
D. Soma Mathayo 6:13 na Luka 11:4. Kuelewa ombi hili ni changamoto. Soma Yakobo 1:13. Yakobo anatuambia kuwa Mungu hatujaribu. Tunapaswa basi kuelewaje ombi la Yesu kwamba hatuongozwi na Mungu kuingia majaribuni? (Ufafanuzi bora ninaoweza kuuona ni kwamba Yesu anaomba kuhusu nyakati za majaribu kwetu. Kila mara Shetani na wasaidizi wake wanajaribu kutuhamasisha kuanguka. Ombi hili linamwomba Mungu atuepushe na mazingira magumu. Uelewa huo unaendana na sehemu iliyosalia ya kifungu cha Mathayo 6 kinachoomba kuokolewa kutoka maovuni.)
E. Soma Mathayo 6:14-15. Je, tumeiacha Sala ya Bwana? (Nadhani. Sasa Yesu anatoa maoni yake kwenye kipengele kimoja cha ombi lake, ambacho ni ombi letu kwa ajili ya msamaha. Katika sehemu inayofuata, hebu tuingie kwenye mjadala wa kina zaidi kuhusu wajibu wetu wa kuwasamehe wengine.)
III. Kuwasamehe Wengine
A. Soma Luka 11:4. Hapa Yesu anashughulikiaje suala la msamaha? (Hii inachukulia (assume) kwamba tunawasamehe wengine. Tuna mtazamo wa kusamehe.)
B. Luka 11 haitoi msisitizo wa kuwasamehe wengine kama sharti la msamaha wetu tunaouona katika Mathayo 6:14-15. Unadhani kwa nini Yesu anasisitiza hitaji la sisi kusamehe?
1. Mathayo 6:12 inazungumzia msamaha wa “deni” zetu, wakati Luka 11:4 inaendelea kwamba tumsamehe “kila tumwiaye.” Je, tunapaswa kuangalia dhambi na deni kama vitu viwili tofauti? (Mungu pekee ndiye anaweza kusamehe dhambi. Kwa sababu hatuwezi kusamehe dhambi, hii inatufundisha kwamba kwa ujumla tunahitaji kuwa na mtazamo wa kusamehe, bila kujali chochote tunachowiwa.)
2. Mojawapo ya “sheria” za kutawala hisia (emotional intelligence) zilizojengwa juu ya Biblia ninazowafundisha wanafunzi wangu wa shule ya sheria ni kwamba tunapaswa kuthamini, wala si kuchukia, ukosoaji kwa sababu unaweza kutufundisha masomo muhimu. Je, kujifunza kupokea ukosoaji bila chuki ni moja ya hatua halisi kuelekea kuwa na roho ya kusamehe ambayo Yesu anaifafanua? (Ndiyo. Baadhi ya haya ni mambo magumu, si ndiyo?)
IV. Majibu ya Mungu kwa Maombi
A. Angalia tena Mathayo 6:10. Inajumuisha ombi kwamba mapenzi ya Mungu yatimizwe. Je, lazima maombi yetu yapatane na mapenzi ya Mungu? (Soma 1 Yohana 5:14. Hii inatuambia kuwa Mungu hujibu kwa upendeleo maombi yanayopatana na mapenzi yake.)
1. Kama ombi halijajibiwa, je, ni kwa sababu halikupatana na mapenzi ya Mungu? (Si lazima. Ombi linaweza kucheleweshwa, likajibiwa tofauti na tulivyotarajia, au likakataliwa kwa sababu Mungu anawazia jambo zuri zaidi.)
2. Je, ungependa jibu la ombi ambalo halikupatana na mapenzi ya Mungu?
B. Soma Waefeso 3:20-21. Tunapofikiria kuhusu kuomba kwa namna inayopatana na mapenzi ya Mungu, huenda tukadhani kwamba hiki ni katika maombi. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu mapenzi ya Mungu? (Kwamba mapenzi yake ni kutenda zaidi kuliko tunavyofikiria kumwomba. Tunatakiwa kutafakari nguvu ambayo Mungu anaileta kwenye maombi yetu.)
C. Soma Luka 11:9-13. Tunapaswa kutarajia nini kutoka kwa Mungu katika kujibu maombi yetu? (Anatupatia mambo mazuri. Hatupatii mambo mabaya tunapoomba.)
1. Ni zawadi gani bora ambayo Mungu anaweza kutupatia kama jibu la maombi yetu? (Roho Mtakatifu.)
V. Muktadha wa Mungu
A. Soma Mathayo 18:23-26. Hili ni deni kubwa kiasi gani? (John MacArthur anataarifu kuwa talanta “ilikuwa kiwango kikubwa zaidi cha fedha,” na “elfu kumi” ingeeleweka kuwa kiasi kisichoweza kuhesabika kwa urahisi au kilicho kikubwa sana kiasi cha kutoweza kufikika kwa urahisi. Kiwango hiki kilikuwa kikubwa mno!
B. Soma Mathayo 18:27. Maisha ya mdeni huyu yamebadilikaje? Je, maisha ya familia yake yamebadilika?
C. Soma Mathayo 18:28-30. Dinari mia moja ni sawa na mshahara wa miezi mitatu. Ni nini mwitiko wako kwenye kisa hiki?
1. Je, mwitiko wetu kwa mtumwa asiyesamehe ni taswira ndogo ya jinsi Mungu anavyotuangalia pale tunapokataa kuwasamehe wengine, ingawa Yesu aliyatoa maisha yake ili kutusamehe?
D. Rafiki, Yesu ametupatia mpangilio wa kuzungumza naye. Ingawa ninadhani kunukuu kwa kurudiarudia sala ya mfano ni jambo zuri, sidhani hilo ndilo lengo letu. Badala yake, kila kilichomaanishwa na Yesu ni mada ambayo tunapaswa kuijumuisha kwenye mazungumzo yetu na Yesu. Kwa kuwa tayari Mungu anajua kile tunachokihitaji, kurudiarudia tu bila kufikiri ni fursa iliyopotea ya kuwasiliana na Mungu Mkuu wa Mbinguni! Kwa nini usichukulie fursa hii, kwa kuanza sasa hivi?
VI. Juma lijalo: Kuwa na Imani.
