Somo la 10: Toba na Msamaha

(Mathayo 3 & 22, Luka 3)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
2
Lesson Number: 
10

Somo la 10: Toba na Msamaha

 

(Mathayo 3 & 22, Luka 3)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Yohana Mbatizaji na Yesu wanaonekana kuongoza kwa ujumbe wa kwamba wasikilizaji wao wanapaswa “kutubu.” Toba maana yake ni nini? Tulipojifunza Sala ya Bwana, tuliona kwamba Yesu anapendekeza kuwa tuombee mahitaji yetu kabla ya kuomba msamaha wa dhambi zetu. Ikiwa Yesu hatangulizi msamaha kwenye sala yake ya mfano, kwa nini toba ndio ujumbe wa kwanza kwa wote wawili, yaani Yohana na Yesu? Je, toba inahusu masuala mengine zaidi ya dhambi? Hebu tuzame kwenye Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu maana kamili ya toba!

 

  1.    Maana ya Toba

 

    1.    Soma Mathayo 3:1-2. Wazo kuu la hubiri la Yohana ni lipi? (Kutubu.)

 

    1.    Soma Mathayo 4:17. Yesu alianzaje hubiri lake? (Alisema, “Tubuni.”)

 

    1.    Ikiwa wote wawili, yaani, Yohana Mbatizaji na Yesu waliamini kuwa wanapaswa kuanza ujumbe wao kwa amri ya “kutubu,” unadhani hilo linazungumzia nini kuhusu umuhimu wa toba?

 

    1.    Angalia tena Mathayo 3:2 na Mathayo 4:17. Kwa nini Yohana na Yesu wanasema kuwa watu wanapaswa kutubu? (“Ufalme wa mbinguni umekaribia.”)

 

      1.    Hiyo inamaanisha nini? (Soma Danieli 7:13-14. Nadhani wasikilizaji wa Kiyahudi walielewa hili kumaanisha kwamba sasa Masihi angeanzisha ufalme wake wa duniani.)

 

      1.    Hilo lingehusianaje na toba?

 

    1.    Hebu tuweke pembeni dhana ya Yesu kuja kama mfalme mshindi, na kutafakari upande wa kiroho wa ujumbe huu. Uelewa wao wa wokovu ulipaswa kubadilikaje kwa kuzingatia kuwa sasa Yesu amefika? (Neno la Kiyunani lililotafsiriwa kama “toba” kimsingi linamaanisha “kubadili mawazo ya mtu” au “kufikiri tofauti baada ya hapo.” Wasikilizaji wanapaswa kuufikiria wokovu kwa utofauti.)

 

      1.    Badiliko gani la msingi la fikra ambalo wasikilizaji wa Yohana na Yesu wanapaswa kulifanya baada ya kujifunza habari za Yesu? (Ujio wa Yesu utafunua kwa uwazi mpya kwamba wokovu umejengwa juu ya neema. Maisha makamilifu ya Yesu, kifo chake kwa ajili yetu, na kuongoza kwake njia ya kwenda mbinguni vinapingana kabisa na dhana ya haki kwa matendo. Wasikilizaji wanaombwa kubadili kabisa njia yao ya wokovu.)

 

  1.   Imani ya Uongo

 

    1.    Soma Mathayo 3:9. Baadhi ya wasikilizaji walikuwa na mwitiko gani kwenye ujumbe kwamba wanapaswa kutubu? (Walidhani walikuwa sawa kwa sababu walikuwa na “Ibrahimu kama baba [wao].”)

 

      1.    Hebu tutafakari kwa kina kuhusu dhana hiyo. Je, hii leo kuna Wakristo wanaodhani kuwa hawana haja ya toba ya dhambi kutokana na uhusiano wao na Yesu? (Ninaona mfanano mkubwa kati ya wale wanaosema kuwa wameokolewa kwa neema pekee (jambo ambalo ni ukweli), na hivyo kuamini kuwa hakuna kingine wanachotakiwa kukifanya. Kimsingi, baadhi ya wasikilizaji wa Yohana walisema, “Kama Ibrahimu ni baba yetu, basi tuna kila kitu kinachotakiwa.”)

 

    1.    Soma Luka 3:3 na Luka 3:7-8. Yohana anawaambia nini wale waliokuwa wanamwendea kwa ajili ya ubatizo? Anawaambia nini wale walioweka imani yao kwa Ibrahimu kuwa baba yao? (Yohana anawaambia “Kutoa matunda yapatanayo na toba.”)

 

    1.    Soma Mathayo 3:8. Utaona tena kwamba Yohana anatumia maneno haya haya yanayotuambia kuwa kuna “tunda” linaloendana na toba. Ni tunda gani hilo? (Soma Luka 3:10-14. Yohana anabainisha “matunda” mahsusi. Matunda hayo ni kushiriki na wale walio wahitaji, kuwa waaminifu kwenye fedha, kutopata fedha kwa kutumia mabavu au mashtaka ya uongo, na kuridhika na mshahara wako.)

 

    1.    Soma Luka 3:9. Yohana anatumia neno “tunda” kama jambo linalotoka kwenye miti. Yohana pia anatofautisha mzizi wa mti na tunda la mti. Ikiwa tunawakilishwa na miti hii, je, Yohana anasema kuwa ikiwa hatuzai matunda tutakatwa na kutupwa motoni, ikimaanisha kuwa hatutaupata uzima wa milele? (Yohana hasemi kuwa lazima tuzae matunda ili Mungu atuokoe. Badala yake, anasema, kimsingi, kwamba, “Kama toba yako ni halisi, itajionyesha maishani mwako.” Kama toba yako si halisi, basi wewe si sehemu ya ufalme wa Mungu.”)

 

    1.    Soma Yohana 15:1-4. Mahitaji ya msingi ya kuzaa matunda ni yepi? (Kukaa ndani ya Yesu. Hii ndio sababu kwa nini kudhamiria tu kuachana na dhambi si toba halisi. Haifanyi kazi bila muunganiko huu.)

 

  1.      Kuikabili Dhambi

 

    1.    Soma Mathayo 22:1-6. Kuna uhusiano gani kati ya wageni waalikwa na mfalme? (Mitazamo yao iko tofauti kuanzia kumpuuzia mfalme, kuwa na shauku zaidi katika biashara kuliko kwa mfalme, hadi kuwa na uhasama na mfalme.)

 

      1.    Utaona kwamba kifungu cha 2 kinalinganisha kisa hiki na ufalme wa mbinguni. Maelezo haya ya wageni waalikwa yanaendanaje na mtazamo wako wa watu katika dunia ya leo?

 

        1.    Kama wanafanana na ulinwengu, kwa nini wao ni “wageni waalikwa?”

 

    1.    Soma Mathayo 22:7. Je, tunapaswa kuamini katika hukumu ya kudhamiria inayotekelezwa na Mungu?

 

      1.    Unadhani hukumu hii iliwajumuisha wale ambao hawakuwa tu na hamu ya harusi na hawakuwa na chuki? (Tunachokifahamu kwa uhakika ni kwamba hawakwenda kwenye karamu ya harusi.)

 

    1.    Soma Mathayo 22:8-10. Wageni wa awali “hawakustahili.” Unawaelezeaje waalikwa wapya? (Walikuwa mchanganyiko. Walikuwa “waovu na wema.” Lakini wote waliitikia wito.)

 

    1.    Soma Mathayo 22:11-12. Kwa kuwa wageni hawa wa sasa walipatikana barabarani, je, walikuwa wamevaa kwa ajili ya kuja harusini? (Kweli hizi zinatuambia kuwa hawakuwa wamevaa mavazi ya harusi. Walikuwa mitaani wakifanya shughuli tofauti tofauti. Hawakuwa wakisafiri barabarani ili kuja kwenye karamu ya harusi kwa ajili ya mwana wa mfalme.)

 

      1.    Unadhani kwa nini “rafiki” huyu alitekewa alipoulizwa juu ya kutokuwa na vazi lake la harusi? (Hakuwa na sababu za kujitetea alizodhani kuwa zingekuwa na mantiki.)

 

        1.    Ni zipi ambazo zingeweza kuwa sababu zake za kujitetea? (Hakuna aliyempatia vazi. Alichelewa hivyo hakupata vazi. Alikuwa mbali kimawazo lilipokuja suala la mavazi.)

 

        1.    Nilikutaka utafakari ambazo zingeweza kuwa sababu zake za kujitetea kwa sababu njema: lazima rafiki huyu alikuwa na sababu nyingine ambazo sasa anatambua hazitoshi kuzielezea. Unadhani zinaweza kuwa sababu gani hizo? (Alijivunia mavazi yake mwenyewe. Hakuhitaji vazi kutoka kwa mfalme. Haki yake binafsi ndio kwanza imekabiliwa na mfalme.)

 

        1.    Unadhani kwa nini mfalme alimwita kuwa “rafiki?”

 

      1.    Kichwa cha habari cha sehemu hii mi “Kuikabili Dhambi.” Je, mgeni huyu amekabiliana na aina ya mavazi yake dhidi ya vazi la mfalme? (Nafikiri mtu huyu alidhani kwamba hakuwa na haja ya kubadili vazi. Ni sawa na Luka 3:8, ambapo wasikilizaji walidhani kwamba kuwa na Ibrahimu kama baba yao ilitosha. Hawakuwa na haja ya kutubu, kumpokea Yesu, au kuzaa matunda.)

 

    1.    Soma Mathayo 22:13. Je, mtu huyu sasa anatendewa kama rafiki? (La hasha! Anafungwa na kutupwa katika giza la nje.)

 

    1.    Soma Mathayo 22:14. Watu gani katika kisa hiki waliitwa? (Watu wa awali walipokea mwaliko ambao waliudharau. Watu wa barabarani waliitwa na kuhudhuria kwenye karamu.)

 

      1.    Je, hii inamaanisha kuwa kuna angalao hatua mbili za kuchekecha? (Ndiyo.)

 

      1.    Mtu aliyetupwa nje anawakilisha ngazi ya tatu ya uchekechaji. Ni ipi hiyo? Jambo gani linahitajika ili “kuchaguliwa?” (Kuitegemea haki ya Yesu uliyopewa kama karama ya bure ndio msingi wa kuchaguliwa kwako.)

 

      1.    Je, “tunda” ni hatua ya uchekechaji? (Hapana. Lakini inabainisha kama umefungua mikono yako ili kuipokea neema.)

 

  1.   Msamaha

 

    1.    Soma 1 Yohana 1:6-9. Mungu atafanya nini kama tutakiri na kuziungama dhambi zetu? (Atazisamehe.)

 

    1.    Soma Zaburi 103:10-13. Ni nini mtazamo wa Mungu kwa wale wanaoomba msamaha? (Anaondoa “makosa” yetu. Hatutendei sawasawa na dhambi zetu.)

 

    1.    Soma Zaburi 103:14. Je, umemsikia mtu akisema, “Sisi ni wanadamu tu?” Je, hii inaakisi fikra ya Mungu? (Hicho ndicho kinachoonekana kusemwa kwenye kifungu hiki. Mungu anatambua kuwa sisi ni wanyonge.)

 

    1.    Soma 2 Wakorintho 2:5-8. Paulo anaandika juu ya mtu aliyetenda dhambi kuzidiwa na “huzuni ipitayo kiasi.” Je, unawafahamu watu kama huyu? Watu ambao huzuni yao kwa dhambi inapita kiasi?

 

      1.    Unapaswa kufanya nini ili kuwa wa msaada?

 

    1.    Rafiki, je, utatubu, kuipokea karama ya bure ya haki ya Yesu, kisha uishi maisha yanayoendana na neema ya Mungu? Kwa nini usijitoe katika hili sasa hivi na umwombe Roho Mtakatifu auimarishe na kuutia nguvu mustakabali wako?

 

  1.    Juma lijalo: Vikwazo.