Somo la 2: Ujumbe wa Msalaba

(1 Wakorintho 1:17-31)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
3
Lesson Number: 
2

Somo la 2: Ujumbe wa Msalaba

 

(1 Wakorintho 1:17-31)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Kwa juu juu, somo letu juma hili linaonekana kuwa la ajabu sana. Juma lililopita tulijifunza kwa nini Paulo alikuwa na haki ya kujiita “mtume.” Lakini historia yake haikufanana kabisa na historia ya wanafunzi kumi na wawili wa Yesu. Paulo alikuwa na elimu ya juu ya kiteolojia (Matendo 22:3), alikuwa Mfarisayo, na aliandika vitabu vingi vya Agano Jipya kuliko mwandishi mwingine yeyote. Gavana wa Kirumi wa Yudea, Festo, katika Matendo 26:24, alibainisha “elimu ya juu” ya Paulo. Paulo alikuwa mtu mwenye akili nyingi na aliyeelimika sana. Licha ya hayo, somo letu juma hili, lililoandikwa na Paulo, linashambulia waziwazi hekima na elimu ya kidunia. Linawapendelea wasio na hekima, wapumbavu, na wale wenye fikra dhaifu. Nini kinaendelea hapa? Je, injili ni kwa ajili ya watu wenye uwezo mdogo wa kufikiri? Je, ni kwa ajili ya watu wasioelimika? Hebu tuzame kwa kina ili kujaribu kuelewa kile hasa Paulo anachotufundisha!

 

  1.    Upumbavu

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:17-18. Paulo anatuambia kuwa kazi aliyopewa na Yesu ni kuhubiri injili. Ni njia gani anayoitumia na ipi asiyoitumia katika kuhubiri? (Hatumii “hekima ya maneno” kuhubiri injili. Badala yake, njia ya Paulo inajikita kwenye nguvu ya msalaba.)

 

      1.    Hiyo inamaanisha nini? Je, ungehubiri vipi “nguvu ya msalaba?” (Soma 1 Wakorintho 2:2. Hii inabainisha kuwa Paulo alihubiri habari za “Yesu Kristo na kusulubiwa kwake.”)

 

        1.    Je, kuna nguvu katika ujumbe huo? (Niliipenda huduma ya injili ya Billy Graham. Lakini mara zote nilidhani kwamba mahubiri yake yalikuwa mepesi sana. Aliona maono ya mtazamo wa Paulo, “Jikite kwenye hubiri la Yesu na kujitoa kwake kwa ajili yetu.”)

 

    1.    Angalia tena 1 Wakorintho 1:18. Wale wanaopotea, ikimaanisha wale wanaohitaji injili, wanalichukulia “neno la msalaba” kuwa “upuuzi.” Neno lililotafsiriwa kama “upuuzi” ni moria, kutoka kwenye mzizi ule ule wa Kiyunani unaotoa neno ambalo “moron” limetokana nalo. Lakini Paulo hasemi kwamba tatizo ni uwezo mdogo wa akili. Anasema kuwa, kwa hekima ya kibinadamu isiyoamini, msalaba unaonekana kuwa jambo lisilo na maana. Ikiwa ulimwengu unadhani kuwa ujumbe wa msalaba hauna maana, hiyo inawezaje kuwa njia sahihi?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:19-20. Paulo anasema nini kuhusu hekima ya kidunia? (Anasema kuwa wenye hekima ya kidunia ndio wapuuzi wa kweli (wapumbavu).)

 

      1.    Ulimwengu unadhani kuwa injili ni ya kipuuzi, na wale wanaomfuata Yesu wanajua kuwa ulimwengu ni wa kipumbavu. Tunawezaje kutatua tatizo hili kubwa kabisa?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:21. Sulhisho la Mungu kwa tatizo hili ni lipi? (Ni mpango wa Mungu kwamba ulimwengu hautaongolewa kupitia “hekima.” Badala yake, Mungu atawaongoa wapagani kupitia “upuuzi wa lile neno linalohubiriwa.”

 

      1.    Hilo linaweka jukumu la injili kwenye mabega ya nani? (Kwenye mabega ya Mungu.)

 

      1.    Dhana ya kwamba hekima inazuia kumjua Mungu inaonekana kutokuwa sahihi kabisa kwangu. Kadiri tunavyozidi kuuelewa ulimwengu wetu, ndivyo uwezo wa Mungu unavyozidi kufunuliwa. Hata Paulo anakiri hili katika Warumi 1:18-20. Hili linaweza kufafanuliwaje? (Tatizo si maarifa, elimu, au tafakari ya kina. Warumi 1 inafundisha kuwa uumbaji unamdhihirisha Mungu. Tatizo ni hekima ya kibinadamu bila msaada wa Mungu inayokataa ufunuo wa Mungu na kujaribu kuuhukumu msalaba kwa kutumia majivuno, uwezo na hadhi ya kibinadamu.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:22-23. Wayahudi na Wayunani wanashawishiwaje kuwa jambo fulani ni la kweli? (Wayahudi wanadai ishara na Wayunani wanatafuta hoja za busara zenye mantiki.)

 

      1.    Paulo anatoa nini badala yake? (“Kristo aliyesulubiwa.”)

 

      1.    Njia hiyo ina mantiki kiasi gani? (Paulo anakiri kuwa ni “kikwazo kwa Wayahudi na upuuzi kwa Wayunani.”)

 

      1.    Mara ngapi unasikia kwamba lazima tufanye kanisa “liendane na wakati?” mara ngapi unasikia kwamba lazima tubadilishe mafundisho ya kanisa ili yaendane na mtazamo au maadili ya dunia? Mara ngapi unasikia kwamba lazima tuendane na maendeleo ya zama za kisasa?

 

      1.    Je, Paulo anatuambia kwamba alikuwa na tatizo kama hilo katika utume wake wa injili? (Naam. Anasema kuwa injili hailingani na mtazamo na matarajio ya Wayahudi wala Wayunani.)

 

    1.    Soma Matendo 1:6. Tatizo la Wayahudi kutokuelewa injili lilikuwa kubwa kiasi gani? (Hata wanafunzi wa Yesu, mwishoni mwa muda wake pamoja nao hapa duniani, bado walikuwa na mtazamo wao wa awali wa Masihi kuja kwa uwezo.)

 

  1.   Wito

 

    1.    Tatizo kubwa la utume wa injili linaonekana kuwekwa wazi kabisa. Soma 1 Wakorintho 1:24. Ni nini kinachoshinda tatizo hili? (Wito.)

 

      1.    Unaelewa nini kuhusu “kuitwa?” Je, ni kuchaguliwa tangu awali? Je, ni Roho Mtakatifu? Je, ni sifa na vigezo vya kipekee?

 

    1.    Soma Mathayo 22:14 na pitia kwa haraka haraka Mathayo 22:1-13. Nani anayefanya uchaguzi? (Tunachagua kuitikia wito.)

 

      1.    Mfano huu una nafasi gani muhimu kwenye dhana ya kuitwa? (Mfalme aliwaita marafiki wake, kisha akamuita kila mtu. Marafiki hawakuitikia wito. Watu wengi wa kawaida waliitikia wito, isipokuwa yule aliyedhani kuwa mavazi yake yalikuwa yanatosha.)

 

  1.      Kinyume

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:25. Je, kuhubiri injili ni upumbavu wa kweli? Je, ni fikra dhaifu? (Hapana. Ni hekima na uwezo wa Mungu unaozidi hekima yoyote na uwezo wa wanadamu.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:26. Je, kuna habari njema katika hili? Au hili ni jambo la aibu tu? (Kanisa si klabu ambapo matajiri na werevu hukutana pamoja. Ni kwa ajili ya kila mtu.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:27. Kwa nini Mungu atake kuwaaaibisha wenye hekima au wenye nguvu? Hawa ni watu wanaaofanikisha mambo, si ndio? Wao ndio wanaojenga biashara na kuwaajiri wengine, si ndio?

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:28-29. Je, huu ndio ufunguo wa siri ya kwa nini Mungu anawaaibisha wenye hekima na wenye nguvu? (Mungu ndiye anayestahili utukufu wa kuwaongoa watu. Yeye ndiye nguvu ya injili.)

 

      1.    Hebu tulitafakari hili kidogo. Je, Mungu anaonekana kutokuwa na mantiki katika kujichukulia utukufu?

 

      1.    Je, unaweza kuona hapa uhusiano wa imani katika kuhesabiwa haki kwa imani pekee? (Kwa upande wangu, haya ndio maelezo makuu wa kile kinachoonekana kuwa cha ajabu kwa haraka haraka. Yesu alifanya yote: alijitoa mwenyewe, akaja duniani, akaishi maisha makamilifu, akafa kifo cha mateso msalabani, na sasa anatoa uzima wa milele kwa wote wanaompokea. Ni Mungu na Mungu pekee ndiye anayestahili utukufu wote.)

 

    1.    Iwapo hili linaonekana kuwa la kinadharia, tafakari mabishano yanayoendelea kuhusu UVIKO-19. Maafisa wa serikali na mamlaka za kisayansi ziliendelea kuusisitiza umma kwa kurudiarudia kuiamini “sayansi,” lakini nyaraka za serikali zilizotolewa hivi karibuni zinaonesha kwamba migongano ya maslahi, utafiti wa kimaslahi, kujilinda kwa taasisi kulichangia kile ambacho umma uliambiwa. Mabishano hayo yanatukumbusha kuwa hekima ya kibinadamu, hata pale inapovikwa wasifu wa kuvutia, inaweza kupotoshwa na kiburi/majivuno, nguvu, kutokuwa na uaminifu, na maslahi binafsi.

 

    1.    Litafakari kanisa. Katika mapambano ya kulinda uhuru wa dini dhidi ya madai ya wale wanaounga mkono ndoa za jinsia moja, kanisa langu liliwasilisha hoja kwa Mahakama Kuu ya Marekani kuunga mkono uhuru wa kidini wa kujieleza. Kundi la washiriki wa kanisa, wanaojichukulia kuwa na hekima zaidi kuliko kanisa katika suala hili, waliwasilisha hoja ya kupinga. Wasomi hawa walitaka kulirekebisha kanisa mbele ya Mahakama Kuu! Jina la kesi hiyo ni 303 Creative dhidi ya Elenis (303 Creative v. Elenis). Uhuru wa dini wa kujieleza ulishinda katika kesi hii muhimu.

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 1:30-31. Hapa Paulo anasema nini kuhusu haki kwa imani pekee? (Anasema kuwa sasa, tunapokuwa ndani ya Yesu, tuna “hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi.”)

 

      1.    Tunaambiwa kuwa tunapaswa “kuona fahari juu ya Bwana.” Utafanyaje hivyo?

 

      1.    Chanzo cha tatizo katika hoja zinazopingana mbele ya Mahakama Kuu ni endapo mafundisho ya wazi ya Biblia kuhusu ndoa yatafungua njia kwa hekima ya kisasa kuhusu suala hilo. Je, una mtazamo wowote kwenye baadhi ya vipengele vya maisha unaopingana na mafundisho ya Biblia? Je, una marafiki wenye mitazamo kinzani?

 

        1.    Unadhani kitu gani kipo nyuma ya migogoro kama hii? (Kiburi/majivuno. Hili ndilo tatizo la msalaba. Ilikuwa njia ya kudhalilisha kabisa ya kufa. Unawezaje kujivunia kiongozi aliyekufa kwa namna hiyo? Je, si jambo la kawaida zaidi kutaka Masihi ambaye angekuwa mtawala wa Warumi?

 

    1.    Rafiki, tumetumia muda mwingi katika somo hili tukijiuliza kwa nini hekima na akili ya kidunia zilikuwa mbaya. Jibu sahihi ni kwamba kuwa na akili na kuelimika ni mambo mazuri. Tatizo linaibuka pale tunapotumia vipawa hivi kuhoji na kurekebisha mafundisho ya Mungu. Tatizo linaibuka pale tunapoitangaza injili kwa namna inayotukuza hekima na elimu ya kibinadamu badala ya nguvu ya msalaba. Hii inaakisi kiburi cha mwanadamu. Je, utadhamiria leo, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kujisalimisha kwa hekima ya Mungu? Kujivunia Bwana?

 

  1.   Juma lijalo: Umoja Katika Kristo.