Somo la 4: Manabii wa Agano Jipya

(Kumbukumbu la Torati 18, Matendo 21, 1 Wakorintho 14)
Swahili
Year: 
2026
Quarter: 
4
Lesson Number: 
4

Somo la 4: Manabii wa Agano Jipya

 

(Kumbukumbu la Torati 18, Matendo 21, 1 Wakorintho 14)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2026, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani.

 

Utangulizi: Unapowafikiria manabii wa Agano la Kale, akilini mwako unaweza kusikia maneno haya, “asema Bwana.” Imani iliyopo ni kwamba manabii hawa walizungumza kwa niaba ya Mungu kwa namna ya kipekee. Ikiwa sivyo, Kumbukumbu la Torati 18:20-22 inasema kuwa nabii wa uongo anapaswa kufa kwa kuwakilisha vibaya neno la Mungu. Hata kama nabii wa uongo angeepuka adhabu ya kifo, Israeli iliambiwa isiogope kile ambacho alikisema baadaye. Mjadala wa Agano Jipya kuhusu karama ya unabii unaonekana kuwa tofauti kabisa. Unabii si karama ya juu kabisa ya Roho Mtakatifu. Mjadala wa Paulo kuhusu kauli za manabii unachukulia kwamba si kila kauli ya mtu mwenye karama ya unabii haina uwezekano wa kukosea. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi kuhusu mada hii ya kuvutia na muhimu!

 

  1.    Kutoka kwa Musa hadi kwa Yesu

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 18:15-17. Nani anayeandika “nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi?” (Huyu ni Musa akiongea na Waisraeli baada ya kuondoka Misri.)

 

      1.    Kwa nini Musa anajiita nabii? (Anawakumbusha watu kuwa waliogopa kusikia kutoka kwa Mungu moja kwa moja. Walidhani wanaweza kufa.)

 

      1.    Je, watu walikuwa sahihi? (Mungu anasema watu wako sahihi na anathibitisha jukumu la Musa kuwa mtu wa kati kati ya Mungu na watu.)

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 18:18-19. Huyu nabii ajaye anayefanana na Musa ni nani? (Soma Matendo 3:22-26. Petro anatumia unabii huu kwa Yesu.)

 

      1.    Je, inaonekana kuwa jambo la ajabu kumwita Yesu kama “nabii” tu na kudai kuwa Musa anafanana na Yesu? (Jibu ni “ndiyo” kwa namna nyingi, na mojawapo ya sababu kuu ni kwamba Yesu ni Mungu. Lakini jibu ni “hapana” kwa namna nyingine nyingi. Fikiria jinsi Musa alivyokuwa kiungo cha moja kwa moja kati ya Mungu na watu walipokuwa katika safari yao kwenda Nchi ya Ahadi. Yesu ni kiungo cha moja kwa moja kinachotuelekeza kwenye nchi ya ahadi ya milele.)

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 18:20-22. Mjadala unaoendelea kuhusu Musa na Yesu kuwa manabii unaweka kipimo gani kigumu kwa manabii wa aina hiyo? (Unakufa ikiwa utataarifu kwamba Mungu alisema jambo ambalo hakulisema. Unatakiwa kuwa sahihi kila wakati, la sivyo unapaswa kupuuzwa.)

 

  1.   Karama ya Unabii

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:27-31. Je, hii ni orodha ya karama za roho zilizopangwa kulingana na umuhimu wake? (Kwa hakika inaonekana hivyo.)

 

      1.    Inawezekanaje manabii wanakuwa kwenye nafasi ya pili? Kwa nini inaonekana kwamba kuna manabii wengi? (Kwa dhahiri inaonekana manabii wa nyakati za sasa hawatekelezi aina ya huduma ya kiunabii ya kipekee na yenye mamlaka kama ile inayohusishwa na Musa.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 12:7-11. Je, karama ya unabii iliyotajwa hapa inaonekana kuwa katika ngazi moja na kazi ya Musa au Yesu?

 

    1.    Soma Waefeso 4:11. Hapa manabii wako kwenye nafasi ya ngapi? (Nafasi ya pili. Tuliona katika 1 Wakorintho 12:31 kwamba kwamba huu ni mpangilio halisi wa vyeo kwa sababu Paulo anaandika “takeni sana karama zilizo kuu.”)

 

  1.      Agabo

 

    1.    Soma Matendo 21:10-13. Agabo anamuonya Paulo asiende Yerusalemu lakini bado Paulo anaamua kwenda. Je, Paulo hamtii Mungu?

 

      1.    Agabo anasema kuwa nani atamfunga Paulo? (Anasema kuwa Wayahudi watamfunga.)

 

      1.    Wayahudi watafanya nini baada ya kumfunga Paulo? (“Watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.”)

 

    1.    Soma Matendo 21:30-33. Je, unabii wa Agabo umetimia? (Paulo anafungwa, lakini Agabo amekosea kwenye taarifa za kina. Paulo aliokolewa na Warumi. Wayahudi hawakuwa wakijaribu kumwokoa Paulo, walikuwa wanajaribu kumwua Paulo.)

 

      1.    Je, kasoro hizi kwenye unabii wa Agabo zina umuhimu?

 

    1.    Soma Matendo 20:22-23. Paulo anaposema kuwa “amefungwa” na Roho Mtakatifu, je, anamaanisha kwamba Roho Mtakatifu anamwambia aende Yerusalemu? (Nadhani hicho ndicho kinachomaanishwa.)

 

      1.    Utaona kwamba Paulo anasema kuwa Roho Mtakatifu hakumwambia nini cha kutarajia kule Yerusalemu. Paulo anatarajia kuwa jambo gani linamngoja? (Roho Mtakatifu anasema kifungo kinamngoja “mji kwa mji.” Hiki ndicho kifungo alichokionya Agabo.)

 

    1.    Soma Matendo 21:4. Wanafunzi hawa, kwa njia ya Roho Mtakatifu, wanamwambia Paulo “asipande kwenda Yerusalemu.” Unauelezeaje ujumbe huu unaokinzana na kauli ya Paulo kwamba Roho Mtakatifu anamwambia kwenda Yerusalemu?

 

    1.    Angalia tena Matendo 21:13. Paulo anasema kuwa yuko tayari kufa “kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.” Je, haya ni mapenzi ya Mungu?

 

      1.    Unaielezeaje hali ya Paulo? Je, ana uchaguzi wa kuepuka kwenda katika mji? (Mara zote Paulo angekuwa na uchaguzi, lakini ninaamini Roho Mtakatifu anamwambia Paulo aende na baadaye anamwambia Paulo kile kinachomngoja.)  

 

      1.    Je, unaziona kauli mbalimbali zinazotolewa kwa Paulo, ambazo chanzo chake kinapaswa kuwa Roho Mtakatifu, zikiwa na mkanganyiko?

 

    1.    Soma tena Kumbukumbu la Torati 18:19. Hii inaashiria kuwa jambo gani litawatokea wale wasiowasikiliza manabii walio katika ngazi ya Musa? Mungu mwenyewe “atalitaka kwake.” Inaonekana kama kutokutii kunatakiwa kuadhibiwa. Kwa upande wa Paulo, kujua nini cha kufanya kunaonekana kutokuwa na uhakika kutokana na kauli zinazokinzana.)

 

    1.    Soma tena 1 Wakorintho 12:28. Kwa kuwa Paulo anajiita mtume, je, anatuambia kuwa yupo katika cheo cha juu kuliko manabii? (Ndiyo. Paulo hapuuzii sauti ya Mungu kwa sababu yuko radhi kuyatenda mapenzi ya Mungu. Kwa mara nyingine, tunawaona manabii wa nyakati za sasa ambao mamlaka yao hayapo katika ngazi ya Musa au Yesu.)

 

  1.   Nabii au Ujumbe

 

    1.    Hebu tufanye mapitio kwa kusoma Kumbukumbu la Torati 18:20. Je, hili linaelekezwa kwa mtu au kwenye ujumbe? (Mtu anayenena bila mamlaka ya Mungu anakufa.)

 

    1.    Soma 1 Wakorintho 14:29-32. Utaona kwamba katika huduma mojawapo ya kikanisa tuna manabii wengi. Baada ya wao kuzungumza, maneno “na wengine wapambanue hayo” yanamaanisha nini? Je, yanamaanisha kutafakari kwa makini kuhusu ujumbe huo?

 

    1.    Soma 1 Wathesalonike 5:20-21. Kifungu hiki kinasema kuwa tunapaswa kuwa tayari kupokea yale wanayoyasema manabii, lakini pia kwamba tunapaswa “kujaribu mambo yote.” Je, hiyo inamaanisha tutende zaidi ya “kutafakari kwa kina” kuhusu maneno yao?

 

      1.    Angalia maelekezo ya “kulishika lililo jema.” Je, hiyo inaashiria kuwa nabii yule yule, baada ya kujaribiwa, anaweza kusema mambo mema na mabaya?

 

    1.    Uchunguzi wa kina zaidi wa 1 Wakorintho 14:29 unatuambia kuwa neno lililotafsiriwa kama “kupima” halizungumzii juu ya kutafakari, bali kuhusu mashaka, kuhukumu, na kutenganisha. Tafsiri ya Biblia ya Mfalme Yakobo (The King James Version) inalitafsiri neno hilo kama “hakimu.” Vincent’s Word Studies inalihusisha na 1 Wakorintho 12:10 inayosema kuwa karama ya roho ni “kutofautisha roho.”)

 

      1.    Utaona kwamba ujumbe, na si mtu, ndio uliokuwa “unajaribiwa.”

 

      1.    Je, utakubaliana kwamba kipimo cha unabii katika Agano la Kale kilitofautisha kati ya mtu na mtu, na kipimo cha Agano Jipya kinatofautisha kati ya ujumbe na ujumbe?

 

    1.    Soma 1 Yohana 4:1. Je, wasiwasi kuhusu manabii wa uongo bado upo katika Agano Jipya? (Ndiyo!)

 

    1.    Hebu tuone kama tunaweza kufupisha fundisho la Agano Jipya kuhusu manabii wa nyakati za sasa. Je, kuna wakati nabii wa kweli anaweza kutoa unabii usio sahihi? (Hilo linatokana na 1 Wakorintho 14:29. Paulo hasemi kwamba kwanza tuamue ikiwa mtu huyu ni nabii wa kweli, na kisha tukubali chochote anachokisema nabii huyu. Badala yake, Paulo anasema kuwa tutathmini ujumbe na si hadhi ya mzungumzaji. Wakati huo huo, tunaonywa kwamba wapo watu wanaodai kuwa manabii lakini ambao kamwe hawakuwahi kuzungumza kwa niaba ya Mungu.)

 

    1.    Tafakari kama una upendeleo wa kitaasisi unaotokana na namna unabii unavyoshughulikiwa kanisani kwako.

 

      1.    Kwa mfano, Wakatoliki wanafundisha kwamba Papa anaweza kufundisha bila kukosea chini ya mazingira yaliyofafanuliwa kwa upekee na kwa mipaka maalumu, ambayo kwa desturi huelezwa kama kuzungumza ex cathedra.

 

      1.    Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linafundisha kwamba Joseph Smith alikuwa nabii ambaye kupitia kwake Mungu alizungumza, na kwamba Urais wa Kwanza wa sasa unaweza kuzungumza kwa niaba ya Mungu.)

 

      1.    Kanisa la Waadventista wa Sabato linafundisha kwamba Ellen White alikuwa nabii ambaye kupitia kwake Mungu alizungumza. Mifano hii mitatu inafanana sana na mfumo wa Agano la Kale, ingawa si Watakatifu wa Siku za Mwisho wala Waadventista wanaodai kwamba nabii wao anaweza kukosea. Na Waadventista wanaweka wazi kwamba Biblia ndio kipimo cha mwisho.

 

      1.    Kama wewe ni mshiriki wa Kanisa la Assemblies of God au kanisa jingine la kikarimastiki, kuna uwezekano kwamba mara kwa mara unawaona washiriki wakidai kuwa na unabii kutoka kwa Mungu. Hii inaonekana kuakisi maelekezo ya Paulo katika 1 Wakorintho 14:29-31 kwamba manabii wawili au watatu pekee ndio wanaoweza kuzungumza “mmoja baada ya mwingine.” Ninavyoelewa ni kwamba washiriki wa makanisa ya kikarimastiki wanajua kwamba manabii hawa hawawezi kukosea.)

 

      1.    Je, unakubaliana kwamba njia sahihi kibiblia ya kuwatathmini manabii wa nyakati za sasa ni kwa kuuhukumu ujumbe na si mtu?

 

  1.    Je, Idadi Ina Umuhimu?

 

    1.    Soma Matendo 21:8-9. Kwa nini Filipo alikuwa na mabinti wanne waliotabiri? Je, binti mmoja asingetosha kuwasilisha ujumbe wa Mungu?

 

    1.    Soma Yoeli 2:28-29. Biblia inaposema kwamba katika siku za mwisho Roho Mtakatifu atamimina roho yake katika “wote wenye mwili,” tunapaswa kutarajia nini katika mikusanyiko ya makanisa yetu mahalia? (Hii inaonekana kutopatana na mfumo wa Agano la Kale wa manabii wachache wanaozungumza moja kwa moja na kwa usahihi kwa niaba ya Mungu, huku adhabu ya kusema uongo kwa jina lake ikiwa ni kifo. Maneno “wote wenye mwili” yanaonekana kuwasilisha dhana ya kwamba watu wa aina mbalimbali wanawasilisha mapenzi ya Mungu. Hilo linafanya tahadhari ya kuupima ujumbe kuwa muhimu sana.)

 

    1.    Rafiki, Ninatumaini kwamba somo hili litaunda upya mtazamo wako wa manabii wa nyakati za sasa ili usipingane na unabii, bali upime ujumbe bila kumshambulia nabii.

 

  1.   Juma lijalo: Ufunuo na Uvuvio.