Kuishi Maisha Matakatifu

(1 Wathesalonike 4 :1 - 12)
Swahili
Year: 
2012
Quarter: 
3
Lesson Number: 
7

Utangulizi: Mara nyingine huwa ni vizuri kujipitisha pitisha kwenye ofisi, karakana, nyumba za watu au kanisani kwa watu wengine ili kujionea jinsi wanavyofanya mambo yao – jinsi wanavyofikiri na kutenda. Sehemu kubwa ya maisha yangu, niliamini kwamba neema ilikuwa upande mmoja wa Ukristo na matendo upande mwingine. Kwa uthabiti, kauli ya ninaokolewa bila kujali kile ninachokitenda, haikuwa na umakini sana kwa kile walichokitenda. Kwa uthabiti, suala la kwamba, kutokunywa kwangu pombe, kucheza muziki, kulalamika au kutembea na wale wanaofanya hivyo, havikuwa na umaana sana kwenye neema. Kazi yangu ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha Regent imenipatia dhima ya wazi kabisa katika mtazamo mwingine. Nimekumbana na watu wa madhehebu mbalimbali, walio thabiti sana kwenye suala la neema. Wanaamini kwamba mara mtu anapokuwa ameokolewa ni vigumu sana kupoteza wokovu wake kwa kufanya matendo mabaya. Wakati huo huo, kuishi maisha matakatifu ni jambo la muhimu sana kwao. Mchanyato wa ajabu namna gani! Wapo madhubuti sana kwenye wokovu wao, lakini mara kwa mara wanajiuliza kama wanauendeleza Ufalme wa Mungu kwa matendo yao. Hebu tuzame kwenye somo letu ili tuone kile Paulo anachotufundisha kuhusu wokovu na kuishi maisha matakatifu!

  1. Kumpendeza Mungu
    1. Soma 1 Wathesalonike 4:1. Je, Paulo alipendekeza aina gani ya maisha? (Maisha ya kumpendeza Mungu
      1. Mara ngapi unajiuliza kuwa, “Je, kile ninachokifanya kinampendeza Mungu?”
        1. Je, hiki kinapaswa kuwa kitu ambacho ni tabia maishani mwetu – kujiuliza kama kile tunachokifanya hivi sasa kinampendeza Mungu?
      2. Je, Wathesalonike wanayapimaje maisha yao? (Paulo anasema kwamba, kimsingi, wanaishi kwa kumpendeza Mungu.)
      3. Paulo anasema kwamba Wathesalonike wanawezaje kuboresha nyanja hii ya maisha yao? (Wanapaswa kufanya hivyo mara kwa mara.)
      4. Hebu angalia ukinzani wa wazi kabisa kwenye kile anachokiandika Paulo. Kwanza anasema kuwa “kimsingi” wanaishi kwa kumpendeza Mungu, na kisha anasema “wafanye hivyo zaidi na zaidi.” Je, “kimsingi” wanawezaje kufanya hivyo na pia wasifanye hivyo mara nyingine? Je, panawezaje kuwa na fursa ya “kufanya hivi tena?” (Hii inaakisi ujumbe wa Paulo wa “neema.” Kwa sababu ya kile alichotutedea Yesu, tumeokolewa. Sisi tu wakamilifu mbele za macho ya Mungu. Lakini, sisi wenyewe tu mbali sana na ukamilifu. Paulo anasema, “Endelea kulifanyia kazi. Endelea kuzingatia lengo lako la utakatifu.”)
    2. Soma 1 Wathesalonike 4:2. Je, ni kwa mamlaka gani Paulo anatoa maelekezo ya aina hii?
    3. Soma 1 Wathesalonike 4:3-5. Jiweke kwenye nafasi ya Paulo. Anawaandikia watu ambao hawajajifunza kuidhibiti miili yao. Watu wanaojiingiza kwenye uasherati. Je, utaanza kwa kusema kwamba mnaishi ili kumpendeza Mungu, lakini tafadhali jaribuni kufanya hivi mara kwa mara? Tafadhalini jitahidini mfanye vizuri zaidi?
      1. Je, hawa Wathesalonike ni watu wa aina gani? (Ni Wakristo waliookolewa. Paulo hasemi kwamba wao ni wapagani. Hasemi kwamba wamepotea.)
      2. Je, lengo la hawa Wakristo waliookolewa ni lipi? (Lengo lao ni kuishi kwa namna iliyo “takatifu na yenye heshima.” Wanapaswa kutakaswa. Wanapaswa kuwa kwenye uelekeo wa kuwa watakatifu.)
  2. Tamaa ya Ngono
    1. Soma 1 Wathesalonike 4:6. Nilipokuwa kijana mdogo niliambiwa na kutumiwa na Wakristo aina zote za ujumbe unaohusiana na ngono. Baadhi walinielekeza kwenye “picha chafu,” na mienendo michafu na yenye unajisi. Wakati huo huo, wazazi wangu walinipeleka kwenye darasa la kujifunza masuala ya ngono/jinsia lililokuwa linafundishwa na mtu aliyeandika kitabu cha “Mungu Alianzisha Ngono.” Paulo harejei “tamaa ya ngono” kama kitu ambacho ni kichafu au kilianzishwa na Mungu. Je, Paulo anaona kuwa tatizo kubwa ni lipi? (Unatumia vibaya nafasi ya mtu fulani. Unamtendea mtu fulani vibaya.)
      1. Je, umeona filamu ya ngono, uzinzi na dhambi nyingine zinazoendana na masuala ya kujamiianai kwenye huu muktadha?
      2. Hivi karibuni nilikuwa msimamizi kwenye mkutano unaohusu biashara haramu ya usafirishaji wa watu. Mkutano huo ulinifumbua macho kwenye ukweli kwamba wengi wa watu wanaojihusisha na umalaya na kutengeneza filamu za ngono ni watumwa kwa namna fulani. Watu wengine wanawadhibiti/wanawamiliki. Je, uelewa huu unabadilije mtazamo wako kuhusu kujihusisha kwako na hii kazi? (Hoja ya zamani ni kwamba hii ni “furaha ya wasiokuwa wahanga” au “kosa lisilokuwa la wahanga.” Badala yake, hoja ina wahanga wengi – kwa ujumla vijana wadogo wanaoathiriwa kwa namna za kutisha ajabu.)
      3. Juma hili mama mmoja aliniambia kuwa mke wa kijana wake alimwacha mumewe na mtoto wao mdogo sana na kwenda kwa mwanaume mwingine. Kisa hiki kinaweza kurudiwa mara mamilioni. Je, ni “biashara” gani inayofanyika hapa? (Mwenzi anampata mtu mwingine aliye na vitu vya kufurahisha au kupendeza zaidi. Na mwenzi mwingine na watoto wanateseka. Mwanamke mzururaji ameichukulia familia yake kirahisi. Mwanaume mzururaji ameichukulia familia yake kirahisi. Ni ubinafsi wa hali ya juu.)
    2. Paulo anaandika katika 1 Wathesalonike 4:6 kwamba Mungu “atawaadhibu” wale wanaotenda dhambi za aina hiyo. Je, unawezaje kulinganisha hili na 1 Wathesalonike 4:1 inayosema kwamba wanaishi kwa namna inayopmendeza Mungu? (Sio adhabu zote za Mungu ni za upotevu wa milele. Matokeo ya chaguzi zetu za kiovu/zisizo na uadilifu ni kuishia kupata adhabu. Matokeo ya raha na furaha za “kutangatanga” ni kuwadhuru watu wengine, ambao hatimaye, wataishia kutudhuru.)
      1. Je, ni mara ngapi umeshuhudia ukweli wa kile nilichokiandika hivi punde? Wale waliodhani kwamba jambo hili lingekuwa la “kufurahisha,” waliishia kwenye mzigo wa maumivu na huzuni?
  3. . Dhambi Inayotenganisha
    1. Soma 1 Wathesalonike 4:7-8. Tuna tatizo kama lili lile tulilolijadili hapo kabla. Paulo anasema hawa watu wanaishi maisha yanayompendeza Mungu, na pia anasema kuwa wapo kwenye hatari ya kumkataa Mungu. Chukulia dhambi ya kujamiiana. Je, mtu anayefanya hiyo dhambi amemkataa Mungu au mtu huyo anaelekea kwenye maisha ya kumpendeza Mungu? (Kwa mshangao, inaonekana kwamba jibu ama linaweza kuwa moja. Kwa Wathesalonike, jibu, kwa mujibu wa Paulo, ni kwamba wanayaelekea maisha ya kumpendeza Mungu – wanapaswa tu kuimarika katika hilo.)
      1. Je, hii inatufundisha nini kuhusu asili ya dhambi? (Tunamtumikia Mungu Mtakatifu, lakini anavumilia dhambi kwa wale wanaodai haki ya Yesu. Sote tunafahamu kwamba dhambi ni endelevu. Inakuwa mbaya tunapogaagaa/tunapojiachia dhambini. Matokeo ya kuelekea uelekeo wa dhambi ni kwamba dhambi inaelekeza kwenye njia ya kumkataa Mungu na Roho Mtakatifu. Hapa ndipo mahali ambapo upotevu wa neema hutokea. Tunakuwa hatumkubali tena Mungu. Tunakuwa tumemkataa Mungu, tumeikataa neema yake, na kuukataa uwezo wa Roho Mtakatifu wa kutakasa!)
      2. Je, tunawezaje kujua pale tunapovuka msitari kutoka kwa mdhambi aliyeokolewa kwa neema hadi kuwa mdhambi aliyepotea? (Ni pale ambapo hatumchagui tena Yesu kama Mwokozi wetu. Pale ambapo hatujali tena tunapomkataa Mungu na maelekezo ya Roho Mtakatifu. Neema ni kitu cha undani sana. Neema inafunika dhambi nyingi. Lakini, mahala fulani dhambi inatutenga na Mungu kwa sababu inatufanya tumkatae Mungu.)
    2. Rafiki, je, unaweza kuona kile anachokisema Paulo? Unaweza kuwa salama kwenye wokovu wako maadam tu utachagua kusalia kuunganishwa na Mungu. Dhambi za kila siku tunazoangukamo hazitishii wokovu wetu – hata kama Shetani anajaribu kutuambia kwa udi na uvumba kwamba huo ndio ukweli. Badala yake, Mungu anatupa wito wa kuepuka dhambi, kuufukuzia/kuushikilia utakatifu kwa sababu Mungu ni mtakatifu na kwa sababu tunataka kuepuka adhabu inayoletwa na matendo mabaya hapa duniani. Wokovu wetu unapotea pale tu ambapo dhambi zitakuwa zimeponyoka mikononi kiasi cha kuishia kumkataa Mungu na kuyakataa maelekezo yake.
  4. Maisha ya Upendo
    1. Soma 1 Wathesalonike 4:9. Je, neema hii ya ajabu inatufundisha nini kuhusu kuwapenda watu wengine? (Paulo anasema tunafundishwa na Mungu kuwapenda watu wengine. Unapochukulia jinsi Mungu alivyo mwema kwako, unapokumbuka ni aina gani ya mdhambi jinsi ulivyo – na bado unaishi maisha ya kumpendeza Mungu – hii inabadilisha mtazamo wako dhidi ya wadhambi wengine wote wanaokuzunguka.)
    2. Soma 1 Wathesalonike 4:10. Je, ni upendo wa aina gani walio nao Wathesalonike? (Unaonekana kufanana na yale maisha yao ya kupendeza – wanahitajika kuufanyia kazi! Wanahitajika kupenda zaidi na zaidi.)
    3. Soma 1 Wathesalonike 4:11-12. Paulo amewaagiza Wathesalonike kuwa watiifu zaidi na kuwa na upendo zaidi. Je, lengo la utii na upendo mkuu ni lipi? (Watakuwa mfano chanya kwa wale wanaowazunguka. Watu watawaheshimu.)
    4. Rafiki, je, umejawa na furaha kwa kutambua kwamba wokovu wako u salama? Hebu acha hilo likuangazie! Angaza/nururisha upendo na matendo mema ili kwamba watu wengine wavutwe kwa Mungu wetu mkuu na mwenye neema! Je, utadhamiria kufanya hivyo hivi leo?
  5. Juma lijalo: Wafu Katika Kristo.