Uumbaji na Injili
Utangulizi: Rafiki wangu wa Kiyahudi anamwelezea Yesu kama “yule mwalimu anayetembeatembea/anayezungukazunguka.” Haamini kwamba miaka 2,000 iliyopita Mungu alifanyika mwanadamu na kwa mamlaka yake alikabiliana na tatizo la dhambi. Je, jibu la Mungu kwa mashtaka ya aina hii ni lipi? Je, ni mara ngapi umekaa nyumbani kwako na kutafakari kwamba nyumba yako ilijengwa kutokana na miti iliyopo jirani kutokana na dhoruba ya upepo? Vipi kuhusu miaka milioni tano ya dhoruba? Vipi kama palikuwepo na matetemeko ya ardhi machache? Hakuna wanaofikiria kwamba nyumba zao nzuri zilipatikana kwa bahati tu. Kimsingi Mungu anasema “nilikuumba wewe pamoja na dunia, kwa hiyo unaweza kuamini kwamba ninao uwezo wa kuwa mwanadamu na kuishinda dhambi.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kuhusu uhusiano kati ya Uumbaji na wokovu wetu!
- Supu ya Dhambi
- Soma Mwanzo 2:15-17. Je, umewahi kuona alama ya barabarani inayobainisha adhabu endapo utakamatwa ukiendesha gari kwa mwendo wa kasi? Je, adhabu “iliyoandikwa na kubandikwa” kutokana na kula tunda kutoka kwenye mti wa ujuzi wa mema na mabaya ni ipi? (“Utakufa hakika.”)
- Soma Mwanzo 3:8-11. Je, jibu kwa swali la Mungu ni lipi? (Ukisoma mafungu ya kwanza ya Mwanzo 3, utaona kwamba wote wawili wamekula tunda la mti waliokatazwa wasile.)
- Unadhani ni kwa nini wanadamu wanajificha? Je, ni kwa sababu wako uchi? Au, ni kwa sababu wanakumbuka adhabu iliyowekwa kwa kula tunda la mti uliozuiliwa?
- Soma Mwanzo 3:12. Maelezo ya kawaida ninayoyasikia kwa Adamu kula tunda lililokatazwa ni kwamba hakutaka kumpoteza Hawa. Kama unaamini kile alichokisema Adamu, je, jibu lake kimantiki ni lipi? Je, Hawa anapaswa kuuawa? (Ndiyo.)
- Soma Mwanzo 3:13. Je, unalichukuliaje jibu la Hawa? (Angalao yeye hamlaumu Adamu. Kumuua nyoka sio jambo litakalomsababishia maumivu.)
- Soma Mwanzo 3:14. Je, Mungu anamwamini Hawa? (Ndiyo. Kwa hakika kabisa Mungu alifahamu kilichotokea.)
- Kwa nini adhabu ni kitu kingine zaidi ya kifo?
- Soma Mwanzo 3:15. Je, hii ni adhabu ya kifo? (Ndiyo. Kuponda kichwa kutasababisha kifo.)
- Soma Mwanzo 3:16. Je, hii ni adhabu ya kifo? (Hapana, walao sio ya papo kwa papo.)
- Soma Mwanzo 3:17-19. Je, hii ni adhabu ya kifo? (Ndiyo na hapana. Kama kwa Hawa na nyoka, kuna adhabu ya papo kwa papo kwa jambo tofauti na kifo, na hatimaye kifo. “Tunarejea ardhini.”)
- Tuliangalia adhabu “iliyobandikwa” kuhusu kutokuwa na utii, na tuliiangalia adhabu halisi. Je, hii inatufundisha nini kumhusu Mungu? (Mungu anasema ukweli kuhusu hukumu. Lakini, anaonyesha neema.)
- Neema
- Soma 1 Wakorintho 15:21. Je, ni nani ambaye kifo kilikuja kupitia kwake? (Adamu.)
- Kwa nini fungu halisemi kuwa ni “Hawa?”
- Soma 1 Wakorintho 15:22-23. Je, Adamu na Yesu wanahusianishwaje? (Adamu alituletea kifo. Yesu anatupa uzima.)
- Ni lini Yesu atatupa uzima? (“Atakapokuja.”)
- Ili kuuelewa huu uhusiano, je, tunatakiwa kuamini katika uumbaji? Je, ukweli kwamba tunaamini katika Adamu inatusaidia kuamini katika Yesu Kristo?
- Soma Warumi 5:12-14. Je, Adamu ameyabadili maisha yangu kwa jinsi gani? (Alileta mauti. Hata kama kamwe hatukukiuka amri mahsusi, bado tungekabiliana na kifo. Hata hivyo, sisi sote tumetenda dhambi kila mtu kwa nafsi yake, kwa hiyo sote tumepewa adhabu ya kifo.)
- Soma Warumi 5:6-9. Je, Yesu alitupaje uzima? (Kumbuka kwamba adhabu ya dhambi ni mauti. Yesu alilipa adhabu kwa ajili yetu.)
- Je, ni adhabu gani nyingine tuliyoiepuka? (Ghadhabu ya Mungu.)
- Soma Warumi 5:10-11. Je, Yesu alituokoaje dhidi ya ghadhabu ya Mungu? (Kifo cha Yesu kilitupatanisha na Mungu Baba.)
- Angalia tena Warumi 5:8. Je, ni kwa namna gani Mungu anaweza kutupenda na kuwa na hasira dhidi yetu? (Kwa sababu ya dhambi. Mungu anachukia dhambi. Hatuchukii. Dhambi yetu ilitufanya tuwe maadui wake.)
- Hebu turejee hatua moja nyuma kidogo na kutafakari jambo hili. Je, kuna namna yoyote ambapo Mungu anakuwa hana upande wowote (neutral) kuhusu dhambi?
- Kama jibu ni hapana, je, tunaweza kutokuwa na upande wowote kuhusu dhambi? (Ingawa tunaokolewa kwa neema, bado tunapaswa kuupigania/kuupania utakatifu.)
- Soma Yohana 1:1-5 na Yohana 1:14. Je, Muumba wa dunia ni nani? (Yesu.)
- Kwa nini Yohana anaonyesha kwanza kazi ya Yesu kama Muumba kwenye maelezo yake kuhusu Yesu kufanyika mwanadamu? (Tunaweza kuamini kisa cha “ajabu sana” kuhusu kufanyika mwili kwa sababu tuna uthibitisho wa dhahiri wa kisa cha “ajabu sana” jinsi ambavyo kila kitu kinachotuzunguka kilivyotokea/kilivyopata kuwepo.)
- Soma Warumi 5:18-19. Nani aliyerejea kutatua tatizo la dhambi na kulipa adhabu ya kifo kwa ajili yetu? (Yesu. Hakutuumba tu, bali “alituumba tena” alipotukomboa kutoka kwenye adhabu ya kifo. Haya ni majukumu yanayoendana. Yanafanana kiuaminifu, na yanafanana kimalengo.
- . Moyo Mpya
- Soma Mwanzo 3:4-6. Je, Hawa anajitafutia nini kwa juhudi zake mwenyewe? (Kuwa kama Mungu.)
- Soma Wagalatia 3:1-5. Paulo anauliza mfululizo wa maswali yanayowahusu Wagalatia. Je, jibu sahihi ni lipi? (Roho Mtakatifu, na uwezo wa Roho Mtakatifu huja kwa kuamini na sio kwa njia ya utii wa sheria.)
- Je, hii inasema nini kuhusu juhudi za Hawa? (Alipaswa kumwamini Mungu, na sio kujaribu kutaka kuwa kama Mungu kwa kutumia juhudi zake mwenyewe – juhudi ambazo zilizuiliwa moja kwa moja na Mungu.)
- Tunapojaribu kuzitii Amri Kumi, je, tunafanana na Hawa? (Kuna tofauti moja kubwa, Mungu alituambia kuzishika Amri Kumi, na alimwambia Hawa asile matunda ya mti uliozuiliwa.)
- Soma Wagalatia 3:10-14. Je, hii inabadili hitimisho letu kwamba Mungu alituambia tuzishike Amri Kumi? (Hapana. Angalia tofauti kati ya “kutegemea” na “kushika.” Tunatakiwa kuelewa tofauti hii vizuri. Hakuna tunachokifanya kinatufanya tuwe wenye haki mbele za Mungu. Hakuna hata kitu kimoja. Ukiutegemea utii wako ili uweze kuhesabiwa haki, uko chini ya laana kwa sababu sote tu wadhambi. Imani juu ya kile alichotutendea Yesu ndio njia pekee ya kupata wokovu. Wakati huo huo, Mungu anachukia dhambi. Tunatakiwa kuufukuzia/kuushikilia utakatifu – tukifahamu kwamba hauhusiki kivyovyote vile na wokovu wetu. Unajihusisha na kumpenda Mungu na kujipenda sisi wenyewe.)
- Soma Ezekieli 36:26-27. Utakumbuka kwamba Paulo aliwauliza Wagalatia jinsi walivyompata Roho Mtakatifu – kwa imani au kwa matendo? Je, Roho Mtakatifu ana jukumu gani kwetu sisi katika kuufukuzia/kuushikilia utakatifu? (Roho Mtakatifu akiwa anaishi ndani yetu anatusukuma kuachana na moyo wa mawe na kuwa na moyo wa nyama.)
- Soma Zaburi 51:10-12. Je, tunapaswa kuomba nini? (Kupata Roho Mtakatifu! Hii ndio taswira kamili. Tunaokolewa kwa neema pekee, hatuwezi kuupata wokovu kwa matendo yetu. Lakini, hata pale ambapo inatakiwa suala la kuishi maisha yanayoendana na mapenzi ya Mungu, bado hatujimudu/hatujiwezi. Ni zawadi ya bure ya Roho Mtakatifu inayotupatia moyo mpya, inayotupatia mtazamo wenye utayari/ulio radhi.)
- Soma Wagalatia 5:16-18 na 1 Wakorintho 3:16. Je, lengo letu kwa ajili ya kuwa na Roho Mtakatifu ni lipi? (Kuishi pamoja nasi! Kuongoza maamuzi yetu yote. Mungu pamoja nasi!)
- Rafiki, Mungu alituumba, Mungu alitukomboa, na Mungu ametupa Roho wake Mtakatifu ili aishi pamoja nasi. Hizi zote ni zawadi tusizostahili. Wewe, kama Hawa, unaweza kujaribu kufanya mambo fulani fulani kwa nguvu zako, lakini mwisho wake ni kushindwa tu. Kama Adamu na Hawa, utakuwa chini ya laana. Kwa nini usichague njia nyingine sasa hivi? Kwa nini usidai uzima, kifo na ufufuo wa Yesu kwa ajili yako? Kwa nini usimwombe Mungu amtume Roho Mtakatifu ili aishi ndani ya moyo wako?
- Juma lijalo: Uumbaji, Kwa Mara Nyingine Tena.