Kuutumaini Wema wa Mungu (Habakuki)

(Habakuki 1-3)
Swahili
Year: 
2013
Quarter: 
2
Lesson Number: 
8

Utangulizi: Je, ungependa maamuzi yako ya zamani ambayo yalikuwa na walakini yawe siri yako? Je, ni mara ngapi unatamani watu wengine wasikukosoe? Je, unapendelea pale ambapo watu wanataka kujadili makosa yako uliyoyafanya siku za nyuma? Isipokuwa tu pale ambapo unajivunia dhambi zako, je, unapendelea kuzungumzia dhambi za zamani? Isipokuwa tu kama wewe ni mtakatifu usiyekuwa wa kawaida, jibu kwa haya maswali yote ni kwamba hatupendi kuulizwa, kukosolewa au kukumbushwa dhambi zetu. Mungu wetu wa ajabu yupo tayari kujadiliana nasi kuhusiana na maamuzi yake. Mungu aliyetuumba yu radhi kwa mjadala wa jinsi anavyotutendea. Kitabu cha Habakuki kinamfunua Mungu aliye tayari na muwazi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu maamuzi ya Mungu!

  1. Malalamiko
    1. Soma Habakuki 1:1-2. Tafsiri ya NIV inatafsiri neno la “oracle” kumaanisha kuwa “mzigo” au kitamathali ni kama “ujumbe wenye giza.” Je, ujumbe huu unatoka kwa Mungu? (Ujumbe wa giza unaonekana kutoka kwa watu wanaomlalamikia Mungu.)
      1. Je, umewahi kuwasikia wanao au mwenzi wako wakisema, “Hunisikilizi!” “Huwa hunisaidii”? Je, unapenda aina hiyo ya malalamiko?
      2. Je, unadhani ni kwa nini Mungu anachapisha malalamiko haya dhidi yake kwenye Biblia? (Anataka tujifunze jambo fulani.)
    2. Soma Habakuki 1:3. Je, hapa malalamiko ni yapi? (Mungu anavumilia vitendo visivyokuwa vya haki. Mungu anavumilia vurugu na uangamivu.)
    3. Soma Habakuki 1:4. Kwa nini mjadala kuhusu sheria unahusika? (Kwa kawaida, mfumo wa kisheria unaohusu haki ni njia ambayo vurugu, uangamivu na vitendo visivyo vya haki vinashughulikiwa. Hizi ni njia za wanadamu za kutatua haya matatizo. Malalamiko ni kwamba wanadamu wala Mungu hawafanyi lolote kuhusu vitendo visivyo vya haki.)
  2. Jibu la Mungu
    1. Soma Habakuki 1:5. Hili ndilo jibu la Mungu. Je, Mungu anadhani kwamba jibu lake litapokelewaje? (Mungu anasema, “nafahamu halitaaminiwa.”)
    2. Soma Habakuki 1:6-7. Je, ni jambo gani lisilo la kuaminika alilo nalo Mungu mawazoni mwake? (Atawatumia watu waovu, wasiotenda haki na wenye kujigamba (Wababeli) kutimiza utume wa Mungu.)
    3. Soma Habakuki 1:8-11. Pamoja na kuwa waovu, je, ni jambo gani jingine tunaloweza kulisema kuhusu Wababeli? (Wana jeshi lenye nguvu.)
  3. . Jibu
    1. Soma Habakuki 1:12-13. Je, matatizo ya dhahiri kwenye mpango wa Mungu ni yapi? (Mungu ni mkamilifu. Kwa nini awatumie waovu? Mungu anaamini katika haki, kwa nini awatumie wadanganyifu? Zaidi ya yote, kwa nini Mungu awatumie waovu waliokubuhu kuwaadhibu waovu wa kawaida?
    2. Hebu tujadili jambo hili kidogo. Je, kweli Mungu anawajali waovu waliokubuhu? (Tuliposoma kitabu cha Yona tulijifunza kwamba Mungu anawapenda na kuwafuatilia waovu waliokubuhu.)
      1. Kwa nini asiwatumie waovu wa kawaida kuwaadhibu waovu waliokubuhu? (Hili ni somo la msingi kwa Wakristo. Mungu hawasifii waovu wa kawaida. Hatuwezi kufikiri kwamba tunadaiwa kitu fulani na Mungu kwa kuwa waovu wa kawaida.)
      2. Je, umewahi kusema kuwa, “Kwa nini uliniadhibu? Huyu mtu mwingine ni mbaya zaidi?” “Afande, kwa nini unaniambia niegeshe gari pembeni mwa barabara, wakati hili gari jingine limenipita – unapaswa kumsimamisha yeye badala ya kunisimamisha mimi!
      3. Hebu tuzungumzie jambo hili kwa muktadha wa siku za leo. Je, Mungu angemruhusu Shetani au malaika walioanguka kutuadhibu?
        1. Je, Shetani anataka kutudhuru? (Ndiyo!)
        2. Je, adhabu ya Mungu inakaa pembeni tu, na haizuii uovu?
        3. Je, umegundua kwamba inaonekana sheria ya dunia nzima inasema kuwa matendo maovu huleta matokeo ya kiovu? Unampiga mtu ngumi na kuna uwezekano kwa mtu huyo kulipiza kwa kukupiga ngumi pia. Je, itakuwa sahihi kuhitimisha kwamba mara nyingi uovu una adhabu yake ya asili, na Mungu anaamua aidha kuingilia au kutoingilia kati na kuepusha adhabu?
    3. Soma Habakuki 1:14-16. Je, kuna tatizo gani jingine kwa Mungu kuwatumia waovu waliokubuhu kuwadhibu waovu wa kawaida? (Waovu waliokubuhu wanaisifu miungu yao ya uongo.)
    4. Soma Habakuki 2:1. Baada ya kuelezea malalamiko ya nyongeza, je, Habakuki anafanya nini? (Anasubiria jibu la Mungu.)
      1. Je, Mungu anapaswa kutoa jibu? Je, Mungu anapaswa kujielezea kwa viumbe vyake?
  4. Jibu la Mungu
    1. Soma Habakuki 2:2. Je, jibu la Mungu ni la msingi kwa kiasi gani? (Mungu anasema “Nataka kila mtu aelewe kile ninachotaka kukisema kuhusu haya malalamiko.” Hiyo inaashiria kuwa jibu ni la muhimu.)
    2. Soma Habakuki 2:3. Je, hili ni jibu la aina gani? (Mungu anasema, “Subiri.” “Muda ni wa msingi sana hapa. Nitatenda kile nilichokiahidi kwa wakati wangu.”)
    3. Soma Habakuki 2:4. Je, Mungu anasema kuwa ni aina gani mbili za watu zilizopo? (Wenye haki waishio kwa imani, na wenye kujisifu walio na matamanio yao maovu.)
    4. Soma Habakuki 2:5. Je, kuna tatizo gani kwa wale walio waovu? (Ni wachoyo na kamwe hawaridhiki.)
    5. Soma Habakuki 2:6-7. Je, jibu la Mungu ni lipi kuhusu mustakabali wa waovu? (Mungu anasema “malipo” yanakuja. Waovu watadharauliwa na kudhihakiwa. Watabadili mahali pa kuishi na kuwa wahanga.)
    6. Soma Habakuki 2:13-14. Ninaweka kumbukumbu ya muda kwa ajili ya kazi yangu. Siku moja kabla sijaandika somo hili lilitumia saa 11.4 za kazi. Je, Mungu anasema nini kuhusu kufanya kazi hadi kufikia kiwango cha kuchoka kabisa? (Vyote vitaangamizwa kwa moto!)
      1. Je, ni kitu gani kilicho cha muhimu maishani? (Kuyaendeleza maarifa ya utukufu wa Mungu. Kumpa Mungu utukufu. Ninapenda kutafakari kwamba kazi yangu kila siku ni kuuendeleza Ufalme wa Mungu badala ya kujenga tu kitu kitakachoishia kuangamizwa kwa moto.)
    7. Soma Habakuki 2:15-16. Je, huu unaonekana kuwa kama ushauri kwa masuala yanayotokea hivi sasa? (Fikiria idadi ya video zilizopo mitandaoni za vijana walevi wanaoendana na hii taswira.)
      1. Je, Mungu anatuambia nini? (Kwamba tukiwatumia watu wengine kwa faida yetu, tunaweza kutarajia watu wengine kututumia kwa faida yao. Mungu atamwaga kikombe cha aibu juu yetu.)
    8. Soma Habakuki 2:18-20. Tulianza sura hii kwa kusema kuwa Mungu atatoa jibu lake kwamba kwa nini waovu waliokubuhu wanatumika kuwaadhibu waovu wa kawaida. Mungu atatuambia kwa nini anaruhusu vurugu na kuvumilia vitendo visivyo vya haki. Je, ni majibu gani unayoyaona miongoni mwa mafungu tuliyoyasoma? (Jibu la Mungu linaonekana kuwa na sehemu kadhaa. Mosi, anawafahamu wenye haki waishio kwa imani na anawafahamu wenye kujisifu na wachoyo. Pili, Mungu anawafahamu wanaomtumaini na anawafahamu wanaotumaini mambo wanayoyafanya wao wenyewe. Mungu anasema muda unaweza kutofautiana, lakini waovu wataadhibiwa. Uovu na vurugu vitakoma. Mungu anasema, “Nipo kwenye kiti changu cha enzi – nitumainini!”)
  5. Sala ya Habakuki
    1. Soma Habakuki 3:1-2. Kutokana na kile Mungu alichomwambia Habakuki, je, Habakuki anaomba nini? (Fanya hivyo sasa hivi! Leta haki sasa hivi! Leta rehema sasa hivi!)
    2. Habakuki 3:3-16 inaghani uwezo mkuu na utukufu wa Mungu. Mungu anaweza kufanya jambo lolote!
    3. Soma Habakuki 3:17-18. Angalia kinyume chake. Mungu ni mwenye uwezo mkuu na anaweza kufanya jambo lolote. Hata hivyo, kama suala la kivitendo, sasa hivi maishani mwangu mambo yananiendea mrama. Je, ni mtazamo wa aina gani unaopaswa kuwa nao katika hali kama hiyo? (Tunapaswa kumfurahia Mungu na kuwa wenye furaha. Mungu anatutaka tuangalie mbele zaidi ya hali zetu na kutumaini kwamba atayafanya mambo kuwa sawa.)
    4. Soma Habakuki 3:19. Je, tumaini, imani na furaha katika Mungu vinabadilije maisha yetu? (Mtazamo wa kutumaini unatupatia mbawa! Unatupa nguvu na unatupa mwendokasi na unatupa uwezo wa kuyaona mambo kwa uwazi.)
    5. Rafiki, je, ungependa kuwa na mabawa? Je, ungependa kuwa na furaha, mwendokasi na mwenye kupenda uwazi/ubayana? Mtumaini Mungu. Pamoja na matatizo ya sasa maishani, Mungu yupo kwenye kiti chake cha enzi. Uwe na tumaini kwamba Mungu anawaona wale wanaoishi kwa imani na wale wanaompinga. Kwa wakati wake, Mungu atayafanya mambo kwa usahihi!
  6. Juma lijalo: Siku ya Bwana (Zefania).