First Things First (Haggai)
Utangulizi: Je, inaonekana kana kwamba mfuko wako wa suruali umetoboka? Huwezi kupata maendeleo na kamwe huweki akiba? Inapoonekana kuwa utapata fedha za ziada, inatokea kwamba mahitaji mapya yanajitokeza yanayokurudisha nyuma hadi kule ulipokuwa kabla! Kama jibu lako ni, “ndiyo, hii inayaelezea maisha yangu,” basi fuatilia kitabu cha Hagai kwa makini kabisa. Somo letu juma hili linawahusu watu walioachiwa kutoka utumwani Babeli, lakini mambo hayawaendei vizuri maishani mwao. Hebu tuzame kwenye Biblia ili tubaini sababu!
I. Ujumbe Kuhusu Vipaumbele
A. Soma Hagai 1:1. Watu wa Mungu waliporejea kutoka utumwani Babeli walijikita katika kuijenga upya Yerusalemu. Walizijenga kuta, hekalu, na nyumba zao. Majirani wao wa Samaria hawakupenda jambo hili, kwa hiyo walimshawishi Artashasta kusitisha ujenzi mpya wa hekalu. Hata hivyo, Mfalme Dario alipoingia madarakani kule Uajemi, aliwaruhusu Wayahudi kuendelea na ujenzi mpya wa hekalu. Je, ungefanyaje kama ungekuwa unaishi katika nyakati hizo na Mfalme Dario amekupa ruhusa ya kuendelea na ujenzi wa hekalu?
B. Soma Hagai 1:2. Je, watu wa kipindi hicho walisemaje? (Muda haujawadia wa kulijenga upya hekalu.)
1. Je, hilo linawezekanaje? (Soma Yeremia 25:11 na Danieli 9:2. Danieli alitabiri kwamba Yerusalemu itaangamizwa kwa miaka sabini na miwili. Maoni ya Jamieson, Fausset na Brown yanasema kwamba miaka sabini bado ilikuwa haijaisha, na kwa hiyo watu walisema, “Tunapaswa kusubiri.” Nukuu za Barnes zinasema kuwa miaka sabini ilikuwa imekwishapita zamani, na watu walikuwa wakicheza na tarehe ili waweze kuzima juhudi za ujenzi mpya.)
C. Soma Hagai 1:3-4. Ni kitu gani kinachoonekana kuwa kizuizi mahsusi cha ujenzi mpya wa hekalu la Mungu? (Watu walikuwa wakikazania nyumba zao wenyewe.)
1. Je, Mungu anajiingiza kwenye mjadala wa kipindi ambacho unabii wa miaka sabini ulikuwa umekwishapita? (Hapana.)
2. Je, dhana ya Mungu ni ipi? (Watu hawakujali masuala yaliyomhusu Mungu.)
a. Je, jibu kwa swali la Mungu ni lipi? (Hapana! Watu walidhani kwamba ilikuwa ni muda wa kuzijenga upya nyumba zao, kwa nini muda haukuwa muafaka kwa ajili ya ujenzi wa hekalu.)
3. Je, jibu hilo linahusikaje maishani mwetu hivi leo?
D. Soma Hagai 1:5-6. Je, Mungu atatufanya tuwe na matatizo ya kifedha kama hatutakuwa wakarimu kwenye kazi yake?
1. Soma 2 Wakorintho 9:7. Je, jambo hili linaendanaje na mjadala wetu? Vipi kama watu hawa wangekubaliana na suala la ujenzi wa hekalu, na kufanya uamuzi kuwa muda ulikuwa muafaka? Je, hilo lingekubaliana na lugha ya “kila mtu na akusudie?”
a. Kama hivyo ndivyo, kwa nini watu hawa wanaadhibiwa?
2. Je, Mungu anawalipa watu waliopuuzia hekalu lake?
3. Angalia tena Hagai 1:5-7. Utabaini kwamba mara mbili Mungu anasema, “Zitafakarini njia zenu.” Je, hiyo inaashiria nini kuhusu nia ya Mungu? (Mungu anajaribu kuvuta umakini wa watu. Anamtuma Hagai kupeleka ujumbe, na anakatisha tamaa mafanikio/ustawi wa watu. Utabaini kwamba 2 Wakorintho 9:7 pia inaanza kwa maelekezo ya kuitafakari hali yako: “kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake…”)
E. Soma Hagai 1:8. Tunapojenga makanisa mazuri, tunapoiendeleza kazi ya Mungu, je, Mungu anajisikiaje? (Anafurahia pale tunapomheshimu.)
F. Soma Hagai 1:9-11. Hapo kabla Mungu alisema, “Tafakari ni kwa nini hustawi/hufanikiwi.” Tulijadili kile tulichodhani kwamba Mungu alikuwa akikifanya. Sasa Mungu anatoa jibu lake kuhusu kile anachokifanya. Je, ni kitu gani hicho? (Kwa uwazi kabisa Mungu anasema kwamba anakatisha tamaa juhudu zao za mafanikio kwa sababu hawakuyatilia maanani mahitaji ya Mungu.)
II. Ujumbe Wapokelewa
A. Soma Hagai 1:12-15. Je, watu wanauchukuliaje ujumbe wa Mungu? (Wanaanza kuifanyia kazi nyumba ya Mungu.)
1. Mafungu yanaposema kwamba Mungu “akaziamsha roho” za viongozi, je, hiyo inamaanisha nini? (Roho Mtakatifu aligusa roho zao.)
a. Je, inamaanisha nini kwa kusema kuwa “roho zao?” Je, hiki ni kitu kingine zaidi ya Roho Mtakatifu? (Soma Yohana 14:15-17 na Warumi 8:9. Roho Mtakatifu wa Mungu ataishi ndani yetu na kuongoza njia zetu. Kuwa na uelewa mzuri zaidi wa Roho Mtakatifu ni eneo langu jipya ninalolifurahia. Bado sijalielewa jambo hili kwa ukamilifu, lakini nina uhakika kwamba ubongo wetu sio tu mlundikano wa nyama. Kihisia tunafahamu kwamba tunafanana (kwa Kihebrania ni: “ruwach”), na mafungu haya yanaashiria kuwa kwa namna fulani hivi tunaweza “kuunganisha” roho zetu na Roho Mtakatifu ili tuweze kuishi maisha yanayoongozwa na Roho. 1 Wakorintho 6:19 inasema, “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe.”
B. Soma Hagai 2:1-3. Je, kuna habari gani njema hapa? (Kwamba watu walikamilisha ujenzi mpya wa hekalu la Mungu.)
1. Je, habari mbaya ni ipi? (Nyumba hiyo “si kitu” ikilinganishwa na utukufu wa hekalu la awali.)
2. Chukua muda mfupi na utafakari jambo hili. Je, watu walipewa changamoto ya kulijenga upya hekalu kwa kiwango cha utukufu wake wa awali? (Hapana. Walipewa changamoto ya kulijenga upya, na sio kuliacha kwenye uharibifu.)
III. Mwitikio wa Mungu
A. Soma Hagai 2:4-5. Je, Mungu hajafurahi kwa kuwa nyumba yake sio nzuri kama ilivyokuwa? (Hapana! Mungu aliwataka tu kuuangalia mtazamo wao dhidi ya hekalu la Mungu. Sasa anawatia moyo pale wanapokuwa wamekata tamaa kwa sababu hekalu lililojengwa upya linapungukiwa upungufu wa hekalu la awali.)
1. Je, ni kwa namna gani Mungu yu pamoja nao? (“Roho yangu i pamoja nanyi.”)
B. Soma Hagai 2:6-9. Watu walipokata tamaa kutokana na mwonekano wa hekalu jipya, je, lilikuwa na upungufu gani? (Lilipungukiwa fedha na dhahabu.)
1. Je, Mungu anasema nini kuhusu fedha na dhahabu? (Anazimiliki zote.)
a. Je, dhana ya Mungu ni ipi? (Tukiwa wabia na Mungu, ataleta “fedha na dhahabu” kwa ajili ya kazi yake.)
2. Je, fedha na dhahabu ndio mtazamo wa kile anachokitaka Mungu kwa ajili ya utukufu wake? (Hapana! “Vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja.” Utukufu wa kweli wa hekalu lililojengwa upya ni kwamba Yesu atasimama ndani yake!)
a. Je, tunajifunza nini katika jambo hili kwetu hivi leo? (Kama unataka kutumia kanisa lako kumpa Mungu utukufu, haijalishi ni zuri na limerembwa kiasi gani, bali ni kama Roho Mtakatifu ndiye anayelijaziliza.)
IV. Mfano wa Mafanikio
A. Soma Hagai 2:10-12. Je, unakubaliana na makuhani? (Ndiyo.)
B. Soma Hagai 2:13. Je, unakubaliana na jibu la makuhani? (Ndiyo.)
C. Soma Hagai 2:14. Je, hii inamaanisha nini? (Mtu au watu “wanaponajisiwa” (ikimaanisha kuwa nje ya upendeleo wa Mungu) wanatia unajisi chochote wanachokigusa. Kujikutanisha na watu wema hakuwafanyi kuwa watu wema.)
D. Kile kinachomaanishwa hapo hasa hakipo wazi sana, kwa hiyo hebu tuendelee kusoma ili tuweze kupata utambuzi mpana zaidi. Soma Hagai 2:15. Utabaini kwamba Mungu anasema kuwa tunahitajika kutafakari jambo hili zaidi, kwa hiyo hili linatuonyesha kwamba bado hatuuelewi mfano huu kwa ukamilifu.)
E. Soma Hagai 2:16-19. Mara tatu Mungu anasema, “zitafakarini kwa kina.” Je, ni kitu gani kinachotufanya kuwa wema, na kinachotubariki? (Watu walipoiacha nyumba ya Mungu kwenye uharibifu, Mungu aliingilia kati mibaraka yao. Watu walipojenga msingi kwa ajili ya kujenga upya nyumba ya Mungu, Mungu aliwabariki.)
1. Je, chanzo cha mibaraka ni kipi, kuwa na mawasiliano na watu wengine wema? (Hivyo ni vizuri, lakini chanzo cha kweli ni Mungu.)
F. Soma Hagai 2:20-23. Je, inamaanisha nini kubarikiwa na Mungu? (Anawashinda maaduo wako!)
G. Hagai anatufundisha kwamba tukiwa na utii tunafanikiwa. Kumbukumbu la Torati 28 inatufundisha kitu hicho hicho. Hata kisa cha Ayubu kinatufundisha kwamba utii huleta mafanikio. Je, unauelezeaje umaskini wa Yesu? Umaskini wa wanafunzi wake? (Soma tena Hagai 2:7-9. Utajiri wa kweli, utukufu wa kweli ni kuwa na Roho Mtakatifu ndani yako. Kama wewe ni mwaminifu, je, Mungu atakubariki kwa mali? Nadhani jibu ni “ndiyo,” lakini mbaraka wa kweli ni ule wa kujazwa Roho wa Mungu!)
H. Rafiki, je, “umetafakari kwa kina” vipaumbele maishani mwako? Je, u makini kuuendeleza Ufalme wa Mungu, na sio ufalme wako tu? Kwa nini usidhamirie hivi sasa kuufanya uendelezaji wa Ufalme wa Mungu kuwa kipaumbele maishani mwako?
V. Juma lijalo: Njozi za Tumaini (Zekaria).