Ungamo na Toba: Vigezo vya Uamsho
(Matendo 5, Zaburi 51)
Swahili
Year:
2013
Quarter:
3
Lesson Number:
6
Utangulizi: Je, mtazamo wako dhidi ya dhambi ukoje? Je, mara nyingi huwa unafikiria jinsi ambavyo watu wengine wanakuchukulia? Au, je, unajali sana jinsi dhambi zako zinavyomwathiri Mungu? Nilipokuwa nikikua, baba yangu alikuwa akihamasisha tabia njema kwa kusema, “Sijali kile wanachosema wavulana wengine, ninyi ni vijana wa Don Cameron!” Kama ujumbe wa baba ulikuwa ni kwamba dhambi ni jambo la mtu binafsi, hilo lisingekuwa jambo jema. Bali, kama alikuwa akisimama kwenye nafasi ya Baba yangu wa Mbinguni, basi ushauri wake ulikuwa mzuri. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kuhusu dhambi, ungamo na toba!
- Mitazamo dhidi ya Toba
- Soma Matendo 5:12-13. Je, ungependa kuungana na kundi linalotenda miujiza? Je, ungependa muujiza utendeke kwa ajili yako?
- Soma Matendo 5:14-16. Watu hawa wanataka muujiza na wanaungana na waumini! Je, hii inaashiria nini kuhusu maana iliyopo kwenye Matendo 5:13? (Wale wanaoutafuta muujiza walijiunga. Watu wa kawaida walikuwa wakiwaheshimu Wakristo, kwa hiyo lazima hii itakuwa inamaanisha kuwa wale walio kwenye nafasi za mamlaka za kidini hawakuthubutu kujitokeza kumwamini Yesu.)
- Soma Matendo 5:17. Je, ni kitu gani kinachowafanya hawa viongozi wa kidini wa ngazi za juu wawe na wivu? (Mungu anatenda kazi kupitia kwa wafuasi wa Yesu. Wanatenda miujiza na kuwabadilisha watu. Viongozi wa ngazi za juu wa kidini wanaona wivu, na viongozi walio chini yao wanaogopa kuwaudhi viongozi wao wenye wivu.)
- Soma Matendo 5:18-20. Ikiwa unakabiliana na mateso yanayotokana na imani yako, je, ni kitu gani kinachopaswa kukupa ujasiri?
- Kwenye mgongano kati ya mamlaka ya kiraia na mamlaka ya Mungu, nani ameshinda? (Hebu rukia kwenye mafungu ya mbele na usome Matendo 5:40. Ukweli kwamba mamlaka ya Mungu inashinda haimaanishi kuwa mara zote huwa tuna barabara nzuri isiyo na mabonde.)
- Soma Matendo 5:21-24. Je, ni kitu gani kinachopaswa kutokea hapa? Kama hili lilikuwa ni tukio la kawaida la uvunjaji wa gereza, je, viongozi hawa wasingejua cha kufanya? (Hakika wangejua cha kufanya.)
- Kwa hiyo, kwa nini mustakabali una wingu hapa? (Uvunjwaji huu wa jela sio wa kawaida.)
- Soma Matendo 5:25. Je, mitume waliofungwa wanaenenda kama wakimbizi? (Sio kirahisi namna hiyo.)
- Jiweke kwenye nafasi ya viongozi wa juu wa kidini. Wanaionea wivu kazi ya Mungu kupitia kwa mitume. Wanaona muujiza wa wazi kabisa ukionyesha kwamba jela lao haliwezi kuwahifadhi mitume. Je, wanapaswa kufanya nini?
- Soma Matendo 5:27-28. Angalia maneno ya Kuhani Mkuu. Je, viongozi wa kidini wanahofia nini?
- Soma Matendo 5:29-30. Je, Petro anaomba radhi kwa kuwaweka viongozi wa kidini kwenye nuru ya uongo? (Hapana! Anaweka mashtaka ambayo viongozi wa kidini wanayaogopa – kwamba wana hatia juu kifo cha Yesu. Kwa kuongezea, Mungu anapingana nao kwa sababu alimfufua Yesu kutoka katika mauti.)
- Je, unadhani viongozi wa kidini waliamini kile alichokisema Petro?
- Soma Matendo 5:31. Tunapata kiini cha suala hili. Je, hawa viongozi wa kidini walihitaji nini? (Walihitajika kutubu ili wasamehewe “hatia ya damu ya [Yesu]” Matendo 5:28.)
- Je, kitu gani kiliwazuia hawa viongozi wa kidini wasitubu ili waweze kusamehewa?
- Soma Matendo 5:32. Kwa nini Petro analazimika kuwarejea mashahidi? (Mojawapo ya suala walilokuwa nalo viongozi wa kidini ilikuwa ni endapo wangeweza kuamini kile alichokisema Petro. Hawakutaka kukiamini.
- Kwa nini walipaswa kuamini? (Kwa sababu ya ushuhuda wa mitume na miujiza iliyotendwa kupitia uwezo wa Roho Mtakatifu.)
- Ni kwa namna gani mitume na Roho Mtakatifu wanakuwa mashahidi? (Sio tu kwamba mitume walimwona Yesu mfufuka, bali waliona uvunjwaji wa gereza na ukweli kwamba mitume wapo nje wakifundisha tena. Roho Mtakatifu sio tu kwamba aliwezesha miujiza iliyowafanya viongozi wa kidini washikwe wivu, bali Roho Mtakatifu alikuwa akitenda kazi na mioyo ya viongozi wa kidini!)
- Soma Matendo 5:33. Je, toba inaendeleaje? Kwa nini walikasirika? (Majivuno. Walipaswa kukiri kuwa walikuwa na makosa – na wauaji!)
- Yesu na Toba
- Hebu turejee nyuma na tusome tena Matendo 5:31. Je, Yesu “anawapaje toba na msamaha wa dhambi Waisraeli?” Hebu kwanza tuangalie toba. Je, Yesu anatupatiaje toba?
- Soma tena Matendo 5:30. Je, haya pia ni mashtaka dhidi yako? (Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Dhambi zetu ndizo zilizomwua. Kama vile kondoo alivyotolewa kafara kwa ajili ya dhambi za mtu katika Agano la Kale, vivyo hivyo Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Angalia Waebrania 9:6-14.)
- Je, Yesu anatupatiaje msamaha? (Soma Warumi 8:1-4.)
- Je, tunapokeaje toba na msamaha? Je, ni suala linalotokea lenyewe? (Hebu waangalie viongozi wa kidini. Walikuwa na utibitisho mkubwa kabisa na waliusikia ujumbe wenye ukweli wa wazi kabisa, lakini bado walikataa kutubu au kusamehewa. Hii inaonyesha kuwa toba na msamaha ni zawadi, lakini hazipokelewi “automatically.”)
- Hebu turejee nyuma na tusome tena Matendo 5:31. Je, Yesu “anawapaje toba na msamaha wa dhambi Waisraeli?” Hebu kwanza tuangalie toba. Je, Yesu anatupatiaje toba?
- Hatia na Toba
- Soma Zaburi 51:3. Je, unajisikia kama anavyojisikia Mfalme Daudi?
- Je, viongozi wa kidini tuliowajadili kwenye Matendo 5 walipaswa kujisikia kama alivyojisikia Mfalme Daudi?
- Juma lililopita nilipokuwa nikifundisha, mshiriki wa darasa aliuliza kama hatia ni jambo zuri. Je, wewe unafikirije?
- Hebu tuangalie kwa kina zaidi hali aliyonayo Mfalme Daudi. Soma Zaburi 51:1-2. Je, Daudi anashughulikaje na dhambi yake? (Anataka kuwa huru dhidi ya dhambi.)
- Soma Zaburi 51:5-6. Je, hali ya kibinadamu ni ipi? (Tunazaliwa dhambini, lakini Mungu anatutaka tutamani kuwa huru dhidi ya dhambi.)
- Soma Zaburi 51:7. Je, Daudi anafikiri kuwa anaweza kusamehewaje? (Anaweza kusamehewa kabisa [kikamilifu]. Mungu anamsafisha. Mungu anamsamehe.)
- Soma Zaburi 51:8-12. Hebu rurejee kwenye suala la kama hatia ni jambo zuri. Je, ni kitu gani tulichokisoma hadi sasa kinachotufanya tufikiri kuwa hatia ni jambo zuri? (Mfalme Daudi anasema dhambi zake zi “mbele yake daima.” Hiyo ni hatia.)
- Je, Daudi anataka aweje? (Msafi kabisa! Kisha Daudi anasema, “Unirudishie furaha ya wokovu wako.” Hatia njema inatuelekeza kwenye ungamo na toba. Wokovu wa Mungu huleta furaha!)
- Vipi kama bado unajisikia hatia baada ya toba na ungamo? (Soma Zakaria 3:1-2 na Ufunuo 12:10. Mashtaka yanayotolewa baada ya msamaha ni kazi ya Shetani. Hiyo hatia ni mbaya.)
- Hebu tuangalie mafungu mengine kuhusu hii mada. Soma 2 Wakorintho 7:8-10. Je, “hatia” itakuwa ni mbadala mzuri wa “huzuni” kwenye hili fungu? (Ndiyo. Hatia huleta huzuni. Hatia njema “huleta toba inayotuelekeza katika wokovu.” Huzuni ya dunia, hatia itokayo kwa Shetani, “huleta mauti.”)
- Soma Zaburi 51:3. Je, unajisikia kama anavyojisikia Mfalme Daudi?
- Toba Bandia
- Soma Zaburi 51:4. Niliruka fungu hili tulipokuwa tukiangalia hatia na toba ya Mfalme Daudi. Muktadha uliopo hapa unahusu uzinzi wa Daudi na Bathsheba. Daudi alisababisha kifo cha mumewe, Uria, ili afiche dhambi yake. Daudi anawezaje kusema kuwa amemtenda dhambi Mungu “peke yake?”
- Soma Ayubu 1:8-11. Je, dhambi yetu inamwathirije Mungu?
- Tukiunganisha kauli ya Daudi inayohusu dhambi kuwa “dhidi” ya Mungu, tukiiunganisha na kauli za Mungu kumhusu Ayubu, je, tunapaswa kuhitimishaje kuhusu dhambi zetu binafsi na toba ya kweli?
- Ili tuweze kuliweka suala hili kwenye mtazamo sahihi, hebu tujadili juu ya dhambi yako unayoipendelea. Kama kamwe hakuna mtu atakayeifahamu, je, utaendelea kuitenda? (Hii inatusaidia kuelewa toba ya kweli. Dhambi zetu tunazozitenda ni dhidi ya Mungu. Mungu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Mungu ni Mungu mtakatifu. Mungu anafedheheshwa na dhambi zetu kwa sababu dhambi ni uasi dhidi yake. Tukijikita kwenye kile ambacho dhambi zetu zinamaanisha kwa Mungu, badala ya kile inachomaanisha kwetu, tunayo taswira ya toba ya kweli.)
- Soma Waebrania 12:4-6. Mara nyingi dhambi zetu huwa haziwi siri. Je, huwa tunachukuliaje matokeo ya dhambi zetu kutokana na ukweli wa asili ya kutubu kwetu? (Fungu linasema “usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye.” Unapaswa kuikumbatia kama funzo kutoka kwa Mungu anayekupenda!)
- Soma Zaburi 32:1-2. Je, tunapata nini kutokana na ungamo na toba ya kweli? (Mungu hutusamehe na kusitiri dhambi zetu. Tunabarikiwa kwa msamaha wa Mungu.)
- Rafiki, viongozi wa kidini wa Kiyahudi walijali sana jinsi dhambi yao ambavyo ingewaathiri, na si kama Petro na mitume walikuwa wakiwaambia ukweli kuhusu wao kumwua Mungu na kuhafifisha kazi ya Mungu. Je, utajitoa leo kuiangalia dhambi kwa mtazamo mpya? Kuiangalia dhambi kama kizingiti cha mahusiano yako na Mungu aliyekufa kwa ajili yako, kuiangalia kama kizingiti cha furaha ya kweli ya msamaha?
- Juma lijalo: Umoja: Kiunganishi cha Uamsho.