Utambuzi: Kinga ya Uamsho
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mojawapo ya karama za Roho Mtakatifu ni utambuzi wa roho. 1 Wakorintho 12:10. Kwa nini Mungu alitoa hii karama? Ama kwa hakika, ni kwa sababu sio roho zote ni njema. Katika Mathayo 24:24 Yesu anaonya kwamba makristo wa uongo na manabii wa uongo watatenda miujiza kwa lengo la kuwadanganya Wakristo. Hii inamaanisha kuwa tunapaswa kuwa makini na wale wanaodai kuwa na uwezo wa Roho Mtakatifu. Wakati huo huo, Yesu anatuonya juu ya hatari ya kuhusianisha matendo ya Roho Mtakatifu na ya Shetani. Mathayo 12:32. Hebu tuzame kwenye somo letu ili tuone kile ambacho Biblia inafundisha kuhusu jinsi ambavyo utambuzi unavyoweza kulinda ushindani ndani ya kanisa!
a. Je, unaweza kulielezeaje jaribio la Yohana kwa kutumia lugha ya siku hizi? (Je, yeye ni mshiriki wa kanisa letu?)
-
Tahadhari Watambuzi!
- Soma Mathayo 12:22-23. Yesu anatenda muujiza mkubwa, je, watu wanauliza jambo gani? (Soma Yohana 7:41-42 na Isaya 35:4-5. Watu walifahamu kwamba Isaya alitabiri kuwa Masihi atatenda muujiza wa aina hii. Waliamini kuwa Masihi atakuja kupitia uzao wa Mfalme Daudi, kwa hiyo wanauliza, “Je, huyu ndiye Masihi aliyetabiriwa?”)
- Soma Mathayo 12:24. Je, viongozi wa dini wana maoni gani juu ya tendo la muujiza la Yesu? (Wanasema kuwa miujiza ya Yesu inatokana na roho wa uongo, inatoka kwa Shetani.)
- Soma Mathayo 12:25-26. Je, hoja ya kimantiki ya Yesu dhidi ya mawazo ya viongozi wa dini ni ipi? (Shetani hawezi kumtoa Shetani. Akifanya hivyo, ufalme wake utaanguka.)
- Soma Mathayo 12:27-29. Je, Yesu anajenga hoja gani ya kimantikia juu ya mtu kumfunga mwenye nguvu? (Yesu anaondoa pepo. Inawezekanaje kuondoa pepo isipokuwa tu kama utafunga vichwa vya pepo – Shetani?)
- Soma Mathayo 12:30. Je, hii inatufundisha nini kuhusu utambuzi wa roho? (Tunaiangalia taswira pana. Je, mtu huyu anauendeleza Ufalme wa Mungu?)
- Soma Mathayo 12:31-32. Je, tunapewa onyo gani kali kwa kuiita kazi ya Roho Mtakatifu kuwa ni ya Kishetani? (Ni dhambi ambayo haiwezi kusamehewa!)
- Je, ungependelea kupewa zawadi kubwa isiyo ya hatari kuliko utambuzi wa roho?
- Roho Mtakatifu ni sehemu moja tu ya Utatu Mtakatifu, kwa nini kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu ni mbaya zaidi kuliko kumkufuru Yesu? (Yohana 16:7-8 inatuambia kuwa Roho Mtakatifu anatuhakikisha dhambi zetu. Kama hatuwezi kumtambua Roho Mtakatifu dhidi ya nguvu za pepo, basi tutakuwa kwenye tatizo kubwa inapokuja suala la kuielewa dhambi.)
- Soma Mathayo 12:9-13. Utakumbuka kuwa jambo hili lilitokea kabla Mafarisayo hawajadai kwamba Yesu alitenda miujiza kwa uwezo wa Shetani. Je, Sabato ina wajibu gani kwenye maoni ya Mafarisayo juu ya muujiza wa Yesu? (Yumkini Mafarisayo walidhani kuwa muujiza wa Yesu ulitoka kwa Shetani kwa sababu ya tofauti zao za kiteolojia kuhusu Sabato.)
- Je, funzo gani linaashiriwa hapo kwa watunza Sabato? (Hili ni onyo jingine.)
- Jaribu la Utambuzi
- Soma Marko 9:38-40. Je, huyu mtu alikuwa akiondoa pepo kwa kutumia roho gani? (Roho Mtakatifu.)
- Je, tunajuaje? (Yesu alitia mhuri wa ukubali wake kwa ajili ya kazi yake.)
- Je, Yesu alitumia jaribio gani kuzitambua roho, na Yohana alitumia jaribio gani kuzitambua roho? (Jaribio la Yohana lilikuwa “Je, yeye ni mmoja wetu?” Jaribio la Yesu lilikuwa “Je, alitenda muujiza kwa jina la nani?”)
- Angalia tena Marko 9:39-40. Je, tunapaswa kuhitimishaje kama mtu anatenda muujiza katika jina la Yesu? (Ukubali wa Yesu ni mpana sana. Hii ni mantiki ile ile aliyoitumia kusema kuwa Shetani hawezi kumwondoa Shetani: watenda miujiza wapo upande mmoja au ule mwingine.)
- Soma Isaya 8:19-20. Kwa dhahiri kabisa watu wanaowasiliana na mizimu na roho ni watu wenye roho wa uongo. Je, ni jaribio gani linalotumika hapa kutambua hilo? (Kuwasiliana na wafu ni dalili ya wazi. Jaribio pana litakuwa ni kama roho anazungumza kwa mujibu wa Biblia.)
- Soma Yohana 16:12-15. Je, mafungu haya yanasema nini kuhusu jinsi ambavyo Roho Mtakatifu atanena? (Atanena tu kwa mujibu wa washirika wenzake katika Utatu Mtakatifu. Tunaweza kumjaribu roho akizungumza nasi kwa kuuliza kama kwa ujumla ujumbe unaendana na Biblia.)
- Je, hili ni sambamba na kauli za Yesu kwamba watenda miujiza wapo kwenye upande mmoja au ule mwingine? (Hapa ndipo penye umuhimu wa Mafarisayo na uponyaji siku ya Sabato. Jaribio sio kama Wakristo wenzetu wanakubaliana nasi katika masuala yote ya mafundisho ya dini. Jaribio ni endapo utendaji wa miujiza unamwinua Yesu au la. Tukilifanya jaribio kuwa finyu sana, tunaweza kuona kuwa tunamkufuru Roho Mtakatifu!)
- Chukulia kwamba umemwona mtu akivuta sigara kubwa na amekwambia kuwa ameponywa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Je, uvutaji wake wa sigara utakuwa wa muhimu kwenye suala linalohusiana na uwezo uliomponya? (Hapana! Swali la msingi ni kama anamwinua Yesu, na sio suala dogo la kiteolojia kuhusu uvutaji wa sigara. Ni watu wangapi wanaoshindwa kufanya mazoezi, wanaokula vyakula vinavyodhuru afya, wana uzito mkubwa kupita kiasi, au wanashindwa kunywa dawa huomba kwa ajili ya uponyaji? Swali la msingi ni endapo mtu huyo anamwinua Yesu. Mungu ambaye anawaponya wale tu wanaofuata kanuni za afya kikamilifu atawasamehe wale tu ambao wanafuata sheria za kiroho kwa ukamilifu.)
- Soma Marko 9:38-40. Je, huyu mtu alikuwa akiondoa pepo kwa kutumia roho gani? (Roho Mtakatifu.)
- . Utambuzi wa Kiroho na Msisimko
- Soma Matendo 2:1-3. Kwa wale mnaofahamu kisa hiki, je, lengo la huu uzoefu wa Pentekoste kwa Kanisa la awali la Kikristo ni lipi? (Ni mwanzo wa safari ya uamsho baada ya Yesu kurejea mbinguni.)
- Kwa nini mwanzo huu unafanana hivi? (Unavuta usikivu wa watu.)
- Soma Matendo 2:5-8 na Matendo 2:12. Je, ni kitu gani ambacho kimsingi kilitokea kwa sababu ya sauti, moto na ndimi? (“Kundi lilikutana pamoja.” Kundi lililotaka kufahamu zaidi. Kundi lililokuwa likiuliza maswali.)
- Je, tunapaswa kufikiria jambo gani juu ya uamsho ambalo lina mambo ya kusisimua yanayotokea? (Linaendana na uamsho mkuu wa kwanza wa Kikristo.)
- Soma Matendo 2:13. Je, kundi hili lilidhani kuwa ni roho gai iliyokuwa nyuma ya sauti, moto na ndimi? (Mvinyo! Roho ya ulevi.)
- Soma Matendo 2:15-16. Je, Petro anaashiria kuwa jaribio gani litumike kwenye suala linalozungumzia aina ya roho iliyo nyuma ya hili tukio? (Anatumia mantiki – ni mapema mno kwa mtu kulewa. Kitu cha muhimu zaidi ni kwamba anaigeukia Biblia na kunukuu unabii wa Yoeli.)
- Soma Matendo 2:18-19. Je, Yoeli anatabiri kuwa nini kitatokea pale Roho wa Mungu atakapomwagwa katika siku za mwisho? (Ishara na maajabu. Mvuke wa moshi, moto na damu.)
- Kama tunaishi katika siku za mwisho, na uamsho wetu hauhusishi ishara na maajabu, je, tuhitimisheje?
- Soma 2 Wathesalonike 2:9-12. Je, Shetani atapanga mpango gani katika siku za mwisho? (Miujiza, ishara na maajabu ya bandia.)
- Je, hii inatufundisha nini juu ya ishara na maajabu? (Ishara na maajabu sio jaribio. Matumizi ya kweli na ya uongo ya ishara na maajabu.)
- Je, ni jaribio gani tunaloweza kuliona kwenye haya mafungu? (Dhana ya uamsho wa Shetani ni kutokuuamini ukweli na kujifurahisha kwenye uovu.)
- Kwa nini Biblia inarejea miujiza, ishara na maajabu ya bandia? (Hii inaonyesha kuwa kazi ya kweli ya Mungu pia ina miujiza, ishara na maajabu.)
- Angalia tena 2 Wathesalonike 2:10-11. Je, ni vigumu kiasi gani kutumia jaribio sahihi la utambuzi? Je, hii inasema nini juu ya watu wanaodanganywa? (Wanataka kudanganywa. Wanajifurahisha maovuni.)
- Soma Mathayo 24:23-24. Je, hapa jaribio ni gumu kiasi gani? (Yesu anasema kuwa huu ni udanganyifu mkubwa.)
- Hebu baini jambo fulani. Utakumbuka kwamba hapo awali tulihitimisha kuwa jaribio pana – la endapo mtu anamwinua Yesu – ndilo lililokuwa jaribio sahihi. Hapa tunalo hitimisho ambalo ni finyu zaidi. Je, hili linatufundisha nini? (Tunahitajika kuzifahamu Biblia zetu ili tuweze kuelewa vizuri kile kinachowinua Yesu na kile kisichomwinua.)
- Rafiki, je, utaomba kwa ajili ya kuwa na uwezo wa kuzitambua roho? Je, utaomba ili kwamba Roho Mtakatifu awezeshe juhudi zako za uamsho?
- Soma Matendo 2:1-3. Kwa wale mnaofahamu kisa hiki, je, lengo la huu uzoefu wa Pentekoste kwa Kanisa la awali la Kikristo ni lipi? (Ni mwanzo wa safari ya uamsho baada ya Yesu kurejea mbinguni.)
- Juma lijalo: Matengenezo: Matokeo ya Uamsho