Masomo Kutoka Patakatifu

(Kutoka 25 & 31, 1 Wafalme 8, Zaburi 73)
Swahili
Year: 
2013
Quarter: 
4
Lesson Number: 
4
 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, inamaanisha nini kuwa mtakatifu? Yumkini kwa namna fulani kinachokuja akilini ni mhudumu wa kanisa (padre/mchungaji/kasisi). Mtu aliyejitoa kikamilifu kwa kazi ya kidini. Kama nikikuambia kwamba unahitajika kuwa mtakatifu katika mambo yote uyatendayo, je, hiyo itamaanisha kwamba ubadilishe taaluma yako? Patakatifu panatufundisha jambo juu ya kuwa watakatifu, kwa hiyo hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

  1.  Mtakatifu
    
    1. Soma Kutoka 25:8 na Mambo ya Walawi 19:2. Gari la polisi linapokuwa nyuma yako, je, huwa unaendesha gari lako kwa umakini zaidi? Bosi wako anapokuangalia, je, huwa unafanya kazi vizuri zaidi? Wazazi wako wanapokuwepo nyumbani, je, unaenenda vizuri zaidi?
      1. Kama jibu lako kwa haya maswali ni “ndiyo,” je, unadhani hiyo ndio sababu ya Mungu kuwa pamoja nasi – ili tuboreshe tabia zetu, na kutusaidia kuwa watakatifu?
      2. Je, hiyo ndio sababu wazazi wanataka kuwa karibu na watoto wao – ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na mwenendo mzuri? (Hapana. Wazazi wanataka kuwa karibu na watoto wao kwa sababu wanawapenda.)
      3. Tuchukulie kwamba kile ninachokiamini ni cha kweli, Mungu anataka kuwa pamoja nasi kwa sababu anatupenda. Kwa nini anatuambia tuwe watakatifu kwa kuwa Yeye ni mtakatifu?
        1. Je, Mungu anatumaini kuwa hatutamfedhehesha? (Ukipitia Ayubu 1:6-11, mafungu yanaashiria kuwa Mungu anafurahia utiifu wetu. Kwa hiyo, kinyume chake pia kinapaswa kuwa kweli.)
    2. Soma Mwanzo 2:3. Je, inamaanisha nini kwa Sabato kuwa “takatifu?”
      1. Mungu anapotuambia tuwe watakatifu, je, hiyo inakufanya ujisikie vizuri, au inakufanya ujisikie kukata tamaa?
      2. Kama nikikuuliza “Unadhani siku gani ya juma inafanana nawe sana,” je, utajibuje? (Nani anataka kuwa Jumatatu? Kwa nini nisiwe Jumamosi, siku ambayo Mungu aliitenga na kuwa maalum.)
      3. Je, hiyo ni njia stahiki ya kuiangalia amri ya Mungu inayotutaka tuwe watakatifu, kwamba anatutaka tuwe wa kipekee kabisa?
        1. Iangalia tena Sabato. Je, ni kuwekwa kwake wakfu ndiko kunakoifanya kuwa takatifu au, je, kuna jambo jingine linalohusishwa? (Chukulia kwamba Sabato imekusudiwa kuyageuza mawazo yetu kwa Mungu. Hii inaashiria kwamba kuwa watakatifu ni sawa na kuwekwa wakfu, na kuufanya usikivu wetu uwe kwa Mungu.)
  2. Kazi Takatifu
    1. Soma Kutoka 31:1-5. Je, ungependa kuwa kama Bezaleli?
      1. Je, yeye ni mfanyakazi “za kiufundi’ au mfanyakazi “za ofisini?” (Yeye ni mfanyakazi za kiufundi, anafanya kazi kwa mikono yake.)
      2. Je, jambo la kwanza alilolifanya Mungu kumwezesha Bezaleli (nitamwita Bez kwa kifupi) kufanya kazi kwa mikono yake ni lipi? (“Nimemjaza Roho wa Mungu.”)
        1. Je, hiyo inaleta mantiki yoyote?
        2. Je, hiyo ina chochote cha kujihusisha na kuwa mtakatifu? (Kama kuwa mtakatifu ni kuwekwa wakfu, kuwa maalum, basi kwa wazi kabisa jibu ni, “ndiyo!” Hatua ya kwanza kwa Bez kuwa fundi mzuri ni kudhamiria kuwa wa kipekee, kutengwa dhidi ya wafanyakazi waliosalia.)
    2. Soma tena Kutoka 31:3-5. Je, Bez ana ujuzi gani? (Anajishughulisha na kazi za chuma, vito na mbao.)
      1. Nani aliyempa huo ujuzi? (Mungu anasema kuwa alimpa Bez “ujuzi, uwezo na maarifa.”)
      2. Tunamchukulia Mungu kuwapatia karama viongozi. Vipi kuhusu karama kwa watu wasioongoza? (Mungu anawapa karama kuwa watu wa kipekee. Kuwa wafanyakazi watakatifu – ikimaanisha kuwa na ujuzi dhidi ya watu wengine.)
      3. Je, ni sahihi kutamani kuwa bora zaidi ya wengine? Kuwa Sabato miongoni mwa kundi la wafanyakazi wa Jumanne, Jumatano na Alhamisi? (Hii ni sehemu ya kuwa mtakatifu. Mungu anakupatia karama ya kuwa mfanyakazi stadi. Mungu anakupatia matamanio ya kuwa bora zaidi!)
        1. Fungu linalofuatia tutakalolisoma linatuambia kuwa Bez anatumia ujuzi wake kutengeneza vitu kwa ajili ya mahali patakatifu. Tunapofikiria asili ya kazi ya Bez, je, tamaa yake ya kuwa bora zaidi inamletea utukufu yeye mwenyewe? (Anatengeneza vitu kwa ajili ya mahali patakatifu. Kwa hiyo, ufundi wake maridhawa unawafanya watu wengine wamfikirie Mungu. Anayabadilisha mawazo yao kwa Mungu. Hata hivyo, Bez pia anatafuta sifa.)
    3. Soma Kutoka 31:6-11. Je, inatisha kuwa Oholiabu? Bez ni mzuri sana kiutendaji, bali Oholiabu ni msaidizi. (Unaweza kuwa msaidizi mzuri sana. Huenda siku moja Oholiabu atakuwa fundi mzuri kama Bez. Lakini, kazi yoyote inayowekwa mbele yetu, tunatakiwa kuifanya vizuri kabisa.)
      1. Kama msaidizi, je, kazi ya Oholiabu inayageuza mawazo ya Mungu? (Ndiyo, kwa sababu anafanya kazi pamoja na Bez ambaye naye anatengeneza vitu vinavyobadilisha mawazo ya Mungu. Ni kazi ya ushirikiano.)
    4. Angalia tena Kutoka 31:7-11. Je, ujuzi wa aina ngapi unaouona hapa?
      1. Je, kazi ya wafanyakazi wanaotengeneza hivi vitu ni ya msingi kiasi gani? (Wanatengeneza vifaa vitakavyotumika mbele za Mungu, na wanatengeneza vifaa vinavyowafanya wanadamu waakisi vitu vya mbinguni.)
        1. Je, kuhani anayetoa kafara madhabahuni ni wa muhimu zaidi kuliko mtu aliyetengeneza madhabahu?
  3. . Maisha Matakatifu
    1. Soma 1 Wafalme 8:31-32. Chukulia kwamba umeliacha gari lako nyumbani kwa rafiki yako kwa ajili ya usalama. Baadaye rafiki yako akapigia simu kwamba gari lako halipo. Je, kitu gani kinaweza kuwa kimetokea kwa gari lako? (Huenda gari lako limeibwa. Au, inawezekana limeuzwa na rafiki yako.)
      1. Hii ndio hali inayoelezewa katika 1 Wafalme 8:31-32. (Linganisha na Kutoka 22:10-11.) Mwenye gari hajui kilichotokea, kwa hiyo rafiki atakwenda madhabahuni katika mahali patakatifu na kuapa kwamba hakuliuza gari – hajui kilichotokea. Je, hili linajihusishaje na kuishi maisha matakatifu? (Kuishi mbele za Mungu kunatufanya tuwe waaminifu. Marafiki zetu wanaufahamu uaminifu wetu na wanautegemea.)
    2. Soma 1 Wafalme 8:33-34. Je, hii inatufundisha nini juu ya kuishi maisha matakatifu? (Kwamba tukitenda dhambi mbele za Mungu, maadui zetu wanaweza kutushinda.)
      1. Je, tumaini gani limewekwa kwa wale wanaotamani kuishi maisha matakatifu? (Kwamba hata pale tunapoanguka, Mungu yu tayari kutusamehe na kuturejesha.)
    3. Soma 1 Wafalme 8:35-36. Je, hili si jambo linalorejewa kama “Tendo la Mungu?” Je, hii inaashiria nini kuhusu matatizo yanaoonekana kutokuwa na utaratibu maalum? (Yanaweza kuwa na uhusiano na dhambi zetu.)
      1. Je, lipo tumaini gani kwa ajili yetu? (Kwa mara nyingine, tunamgeukia Mungu na anaponya tatizo.)
    4. Soma 1 Wafalme 8:41-43. Kama tunaishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu, je, inawezekana kuwa watu wengine wataona na kutaka kujifunza zaidi juu ya Mungu? (Hiki ndicho kiini cha kuwa watakatifu. Kufanya kazi kwa ustadi mkubwa kwa namna itakayowavuta watu kwa Mungu.)
      1. Je, Mungu atafanya nini katika hali kama hiyo? (Sulemani anaomba kwamba Mungu athibitishe katika maisha ya “mgeni” kwamba Mungu ni Mungu mkuu wa Mbinguni.)
    5. Soma Zaburi 73:1-3. Je, kitu gani kinaelezewa hapa kinachoonekana kupingana na mjadala tuliokuwa nao kwenye 1 Wafalme 8? (Nadharia iliyopo katika 1 Wafalme 8 ilikuwa ikisema kuwa endapo tungekuwa watiifu basi mambo mazuri yangetutokea na endapo tusingekuwa watiifu, mambo mabaya yangetokea. Hapa, waovu wanastawi.)
    6. Soma Zaburi 73:4-6 na Zaburi 73:12-14. Je, maisha yanamwendea huyu mtu mwema kwa namna ambayo maisha yanapaswa kuwa unapokuwa mtakatifu? (Hapana!)
    7. Soma Zaburi 73:15-17. Je, ni kwa jinsi gani kuyaacha mashaka yako yawe kwako peke yako na kisha kuingia mahali patakatifu kunajibu tatizo kwamba maisha hayaendi kwa namna yanavyopaswa kuwa kwa mtu mtakatifu? (Dhambi huleta mauti. Mungu alikufa kwa ajili yetu kwa sababu anatupenda sana. Hatimaye waovu watakufa, hata kama sasa hivi wanaonekana kusatawi. Wale wanaotafuta kuishi maisha matakatifu, maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu, wataishi milele na Mungu anayewapenda kwa kiwango cha juu kabisa!)
    8. Rafiki, je, utajitoa kumwomba Roho Mtakatifu akusaidie ili uishi maisha matakatifu? Maisha ambayo utatafuta ubora katika yote uyatendayo kwa lengo la kuwavuta watu wengine kwa Mungu?
  4. Juma lijalo: Upatanisho: Sadaka ya Utakaso.