Pamoja na Matajiri na Watu Mashuhuri
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Fedha ni kitu kigumu sana kukabiliana nacho. Majuma kadhaa yaliyopita nilikuwa nikirejea kitabu cha Kumbukumbu la Torati 28, kinachofundisha kuwa watu wanaoshika amri za Mungu watabarikiwa kwa kupata mali. Kanuni hii ya maisha ndio iliyowafanya marafiki wa Ayubu kuhoji kwamba kupotea kwa utajiri wa Ayubu pamoja na matatizo mengine kulitokana na Ayubu kushindwa kumtii Mungu. Hata Ayubu aliamini hivyo, ndio maana kitabu cha Ayubu 31 kinaelezea utii wake na madai ya kutaka kusikilizwa ili Mungu aweze kumjibu malalamiko yake. Kwa upande mwingine, katika Mathayo 19:24 Yesu analinganisha fedha na kushindwa kuingia mbinguni. Utii unawezaje kuleta utajiri, halafu tena utajiri huo ukutenge na mbingu? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!
- Mtawala Tajiri
- Soma Mathayo 19:16-17. Kama mtu akikuuliza swali hili, utajibuje? (Ningesema “Hakuna jambo jema unaloweza kulitenda ili kuingia mbinguni. Badala yake, unatakiwa kutegemea kile Yesu alichokitenda kwa ajili yako.”)
- Je, Yesu alijibuje? (Kimsingi nadhani Yesu alisema kitu kile kile – Mungu pekee ndiye mwema kwa hiyo usiniulize mambo mema unayoweza kuyatenda.)
- Baadhi ya tafsiri za Biblia zinasema, “Bwana Mwema” au “Mwalimu Mwema,” lakini tafsiri nyingi nilizozisoma hazijumuishi neno “mwema” kumwelezea Yesu. Tatizo la kutafsiri jambo hili kama “Bwana Mwema” ni kwamba Yesu anaonekana kujibu kuwa Mungu pekee ndiye mwema na yeye (Yesu) si Mungu. Je, hilo linawakilisha tatizo gani? (Yesu ni Mungu! Namna ambavyo tafsiri ya NIV, pamoja na tafsiri nyingine nyingi, zinavyotafsiri jambo hili inaendana na fundisho la jumla la Biblia kuhusu Utatu Mtakatifu.)
- Utabaini kwamba licha ya kile nilichokiandika, kwa wazi kabisa Yesu anasema, “Zishike amri.” Je, lengo letu linapaswa kuwa ni kuzishika amri? (Ndiyo, kwa hakika kabisa.)
- Soma Mathayo 19:18-19. Angalia orodha ya Yesu ya amri. Upekee wa hizo amri ni upi? (Yesu anaorodhesha tu wajibu wetu kwa watu wengine. Haorodheshi wajibu wetu wowote kwa Mungu.)
- Swali la mtawala tajiri linachukulia kwamba kuzishika baadhi ya amri kunatosha, na Yesu anajibu kwa kuorodhesha mambo machache. Je, kuzishika baadhi ya amri kunatosha? Yakobo 2:10-11 inatuambia kuwa ukiukwaji wa sheria moja ni ukiukwaji wa sheria yote.)
- Soma Mathayo 19:20-21. Je, huu ndio ufunguo wa kuingia mbinguni? Kuuza vitu vyetu na kuwapatia maskini kunatufanya kuwa wakamilifu?
- Soma Mathayo 19:22-25. Ninafahamu kwa nini ninashangazwa na mazungumzo ya Yesu na mtawala tajiri, kwa nini wanafunzi “walishangaa mno?” (Walikuwa na uelewa wa mambo kwa mujibu wa Kumbukumbu la Torati 28 – huyu kijana alikuwa amebarikiwa kwa sababu alikuwa mwema. Kwa kuongezea, mtawala tajiri alisema kuwa alikuwa mtiifu.)
- Soma Mathayo 19:26. Hatimaye tunapata jibu kutoka kwa Yesu linaloonekana kuendana na Biblia yote. Hebu tutafakari maswali kadhaa:
- Je, fikra makinifu ya mtawala tajiri ilikuwa ipi? (Kwamba utii utampeleka mbinguni -- na alikuwa mtiifu.)
- Je, katika yote hayo tunajifunza nini kumhusu mtawala tajiri? (Kwamba asingeweza (au hakuweza) kutii. Hakuwa radhi kuviuza vyote alivyokuwa navyo.)
- Je, inawezekana kwamba kwa maswali yake Yesu alikuwa “akicheza” na mtawala tajiri ili mtawala huyo aweze kuuona ukweli – kwamba hawezi kujitafutia/kufanyia kazi suala lake la kwenda mbinguni?
- Endapo Yesu alikuwa “akicheza” naye, kwa nini hakumwambia mtawala tajiri, “nilikuwa ninakutania tu, ufunguo wa mbinguni ni neema, hakuna unaloweza kulitenda ili uweze kuokolewa – ikiwemo kutoa fedha zako au maisha yako?” (Soma 1 Wakorintho 13:3 halafu ulinganishe.)
- Soma tena Mathayo 19:23-24. Ni vigumu sana jambo hili kuonekana kama Yesu anatania kuhusu suala la fedha kuwa tatizo. Je, unadhani Yesu anamaanisha nini? Je, kuna wazo moja kwenye huu mjadala wote? (Hitimisho la Yesu (Mathayo 19:26) ni kwamba wokovu hauwezekani kwa wanadamu, lakini unawezekana kwa njia ya Mungu. Tukifanyia kazi kuanzia hapo, tunaona kwamba huyu mtawala tajiri kwanza aliyategemea matendo yake na pili aliutegemea utajiri wake. Haya ni mambo yaliyokuwa ndani ya uwezo wake. Yesu alimwonesha mtawala tajiri kwamba alikuwa amekosea kuhusu matendo yake, na Yesu anatuonesha kwamba mtawala alikuwa akizitegemea fedha zake.)
- Je, mtawala tajiri anapaswa kumtegemea nani? (Mungu!)
- Kama hiyo ni kweli, je, kutoa fedha zake kulikuwa na lengo la kuwasaidia maskini au kumwokoa mtawala tajiri? (Yote yalimhusu mtawala tajiri. Suala lilikuwa ni endapo atamtumaini Mungu au fedha zake. Aliamua kuzitumainia fedha zake.)
- Je, mtawala tajiri anapaswa kumtegemea nani? (Mungu!)
- Soma Mathayo 19:27-28. Petro pamoja na wanafunzi wengine wanasema kuwa wameacha vyote na kumfuata Yesu. Je, Yesu anasema kuwa wanafunzi watapata nini? Vitu? (Hapana. Watapata uwezo/nguvu.)
- Soma Mathayo 19:29. Ninaona mambo mawili kwenye hii orodha yanayowakilisha utajiri – nyumba na mashamba. Je, inaonekana kuwa mjadala huu unahusu fedha? (Hapana! Mjadala huu unahusu kumpa Mungu kipaumbele – kumfanya Mungu kuwa wa kwanza. Kumtegemea Mungu.)
- Ngoja nikuulize tena, kwa nini ni vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu? (Jambo hili linahusu neema na utegemezi. Hatuwezi kuyategemea matendo yetu. Hatuwezi kuitegemea familia. Lazima tumtegemee Mungu pekee.)
- Soma Mathayo 19:16-17. Kama mtu akikuuliza swali hili, utajibuje? (Ningesema “Hakuna jambo jema unaloweza kulitenda ili kuingia mbinguni. Badala yake, unatakiwa kutegemea kile Yesu alichokitenda kwa ajili yako.”)
- Nikodemo
- Soma Yohana 3:1. Tunajifunza nini kumhusu Nikodemo? (Alikuwa mtu mwenye ushawishi. Katika siku za nyuma nilisoma vyanzo vya ziada zaidi ya Biblia vilivyoashiria kuwa Nyumba ya Nikodemo ilikuwa mojawapo ya nyuma za matajiri wakubwa.)
- Soma Yohana 3:2. Nadhani Nikodemo alidhamiria kumsifia Yesu. Endapo ungekuwa Yesu, je, ungesifiwa? (Hapana. Nikodemo anakuja wakati wa usiku, jambo linaloonekana kuwa hataki kuonekana akiwa na Yesu. Anasema kuwa Yesu ni mwalimu, hakiri kwamba Yesu ni Masihi.)
- Soma Yohana 3:3. Je, Yesu anayatendea haki “mazungumzo mafupi?” (Ndiyo. Anaingia kwenye jambo analotaka kuliwasilisha moja kwa moja.)
- Soma Yohana 3:4-10. Nikodemo anakuja na kile alichodhani kuwa ni sifa. Je, Yesu anamsifia Nikodemo? (Hapana!)
- Je, hii inatufundisha nini juu ya kukabiliana na matajiri na watu mashuhuri? (Yesu anaushiriki ukweli na Nikodemo, lakini hauchanganyi ukweli ili kumfanya Nikodemo amuunge mkono.)
- Soma Yohana 3:11. Je, “enyi watu” ni maneno ya sifa? Je, akina nani hasa ambao ni “enyi watu?” (Huenda ni matajiri na viongozi wenye uwezo na nguvu.)
- Soma Yohana 3:12-15. Tulijadili hapo awali kuhusu suala la Yesu kukana kwamba alikuwa Mungu. Je, Yesu anasema nini hapa kuhusu uungu wake? (Anasema kuwa “alishuka kutoka mbinguni.”)
- Tofauti na mtawala tajiri, hatupewi hatma ya mwisho (jinsi alivyochukulia) ya Nikodemo kwenye huu mjadala. Je, Yesu anasema jambo gani linaloashiria kuwa huenda Nikodemo alikuwa anafikiria kama angemkubali Yesu kama Masihi? (Yesu anatabiri kwa ufasaha kabisa jinsi atakavyokufa. Huu ulikuwa uthibitisho mkuu kwa Nikodemo.)
- Soma Yohana 7:50 na Yohana 19:38-40. Je, hatimaye Nikodemo alifanya uamuzi gani kuhusu Yesu? (Tunaona kwamba Nikodemo alikuwa kinyume na kukamatwa kwa Yesu na kwamba alisaidia katika kuudai mwili wa Yesu na kuuandaa kwa ajili ya mazishi.)
- Hebu turejee kwenye kauli za mwisho za Yesu katika mazungumzo yake na Nikodemo. Soma Yohana 3:16-18. Je, kiwango cha hukumu ni kipi? (Imani. Kama humwamini Yesu, “umekwisha kuhukumiwa.” Kauli ya “umekwisha” inaashiria kuwa matendo yetu hayatupatii wokovu. Endapo huamini, hatuna haja ya kuingia kwenye suala la matendo yako.)
- . Mtazamo
- Soma Luka 16:13-15 na Kumbukumbu la Torati 8:17-18. Je, kuna mambo gani ya msingi ya kimtazamo kwa wale walio matajiri? (Mtazamo wa kuwa bora zaidi. Kwanza, mtazamo kwamba wanawajibika kwa utajiri wao, na pili, mtazamo wa kuupenda [kuuabudu] utajiri.)
- Je, jambo hilo linaendanaje na visa viwili tulivyojifunza: mtawala tajiri na Nikodemo? (Mtawala tajiri alikuwa akitafuta uthibitisho wa haki yake mwenyewe. Nikodemo, alichukizwa Yesu alipomwambia kuwa alihitajika kufanya jambo tofauti ili aweze kuokolewa.)
- Je, unatakiwa kuwa tajiri ili uweze kuipenda fedha? (Hapana. Wengine wanaipenda fedha (na wanawatamani matajiri) kwa sababu wao hawana utajiri wowote. Wao pia wanaipenda fedha.)
- Katika Mathayo 19:23 Yesu anaposema kuwa ni vigumu kwa mtu tajiri (mwanaume kwa mwanamke) kuingia katika ufalme wa mbinguni, je, sasa unadhani kuwa alimaanisha nini? (Kuingia mbinguni kunategemea neema, kumtegemea Mungu. Mara nyingi matajiri wana mtazamo wa kujitegemea wao wenyewe. Hii mitazmo miwili inasigana.)
- Rafiki, je, mtazamo wako dhidi ya fedha ukoje? Je, unaitegemea fedha? Kwa nini usijitoe leo kumtegemea Mungu – kwa ajili ya wokovu au kwa ajili ya mahitaji yako ya kila siku?
- Soma Luka 16:13-15 na Kumbukumbu la Torati 8:17-18. Je, kuna mambo gani ya msingi ya kimtazamo kwa wale walio matajiri? (Mtazamo wa kuwa bora zaidi. Kwanza, mtazamo kwamba wanawajibika kwa utajiri wao, na pili, mtazamo wa kuupenda [kuuabudu] utajiri.)
- Juma lijalo: Kuwafanya Wenye Nguvu/Uwezo Kuwa Wanafunzi.