Kuwafanya Mataifa Kuwa Wanafunzi
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, unauelezeaje msisitizo mkuu wa kanisa lako? Je, msisitizo huo umejikita ndani ya kanisa au nje ya kanisa? Vipi kuhusu wewe – je, umejikita kwako mwenyewe au umejikita kwa watu wengine? Juma hili tunajifunza badiliko kubwa katika kazi ya Mungu hapa duniani. Badala ya kujikita kwenye taifa la Kiyahudi, msisitizo unabadilika na kutoka nje kwenye ulimwengu wote. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu mtazamo wetu binafsi na ule wa kanisa!
- Badiliko
- Soma Kumbukumbu la Torati 23:1-3. Aina gani ya watu katika makundi matatu hawakuruhusiwa “kujiunga na kanisa” la watu wa Mungu? (Matowashi, wana wa haramu, na wale ambao mababu wao hawakuwa wa msaada kwa watu wa Mungu.)
- Soma Isaya 56:1-2. Jambo gani “li karibu kuja?” (Wokovu wa Mungu. Haki yake (haki ya Yesu) itafunuliwa hivi karibuni.)
- Soma Isaya 56:3. Je, wageni na matowashi wametenda jambo gani ambalo halikutarajiwa? (Wameambatana na Bwana.)
- Je, hiyo inamaanisha nini? (Wameamua kumfuata Mungu wa kweli.)
- Soma Isaya 56:4-5. Hapo awali, matowashi wasingeweza kuwa sehemu ya kanisa. Je, jambo gani limebadilika? (Walikuwa na nafasi ndani ya hekalu. Wana “kumbukumbu na jina lililo jema kuliko kuwa na wana na binti.”)
- Je, aina gani ya kumbukumbu ambayo towashi angeweza kuwa nayo ambayo ingekuwa bora kuliko “wana na binti?” (Utakumbuka kwamba towashi alisema (Isaya 56:3) kuwa yeye ni “mti mkavu?” Hakuwa na uwezo wa kuzalisha. Atakapokuwa sehemu ya “kanisa” huzaa wafuasi wa Mungu – na kwa hiyo yeye ni “mwenye kuzaa sana” kuliko kuwa na wana na binti.)
- Soma Isaya 56:6-7. Je, mtu gani mwingine anayekubalika kwenye ushirika kama sehemu ya watu wa Mungu? (Wageni ambao hapo awali walikuwa wametengwa.)
- Angalia tena Isaya 56:7. Nani atakayekaribishwa katika nyumba ya Bwana? (Mataifa yote.)
- Jambo gani lililo la msingi kuhusu nukuu ya “kafara na dhabihu” na “maombi” kwa ajili ya hawa wageni? (Sio tu kwamba wanaweza kuzungumza na Mungu, bali wataweza kusamehewa dhambi zao kwa njia ya huduma ya patakatifu.)
- Utabaini kwamba Mungu anaweka vigezo vya kuwakubali wale ambao hapo awali walikuwa hawakubaliki. Soma tena Isaya 56:6. Jambo gani linalohitajika? (Wanakubali kumtumikia, kumpenda na kumwabudu Mungu. Wanaitunza Sabato na agano la Mungu.)
- Linaonekana kama jambo la kuhesabiwa haki kwa njia ya matendo! Kweli? (Neema ipo kwa ajili ya watu wote, lakini haikubaliwi na wageni wasiojali. Wale ambao hapo awali walikuwa wametengwa wanataka kuwa na uhusiano na Mungu. Sabato inamkiri Mungu kama Muumbaji na Mkombozi. Agano linawakilisha kile ambacho Mungu anakiwasilisha duniani – watu wanaompenda Mungu na majirani wao. Hivyo, watu hawa wanamwabudu, kumpenda na kumtumikia Mungu.)
- Unapoendelea kutafakari unabii huu kwa ujumla, je, unawezaje kuelezea kwa ufupi hizi habari njema? (Kwanza, nadhani watu wengi wanaosoma somo hili si Wayahudi. Kwa hiyo, hii ni habari njema sana kwetu. Mafungu haya yanamaanisha kuwa injili ipo kwa ajili ya watu wote wanaoitafuta.)
- Hivi karibuni nilisikiliza hubiri lililokuwa na mada isemayo kuwa ni muhimu zaidi kupenda kuliko kuwa sahihi. Nilikuwa na mawazo mawili nilipokuwa nimekaa mahali pale na kulisikiliza hubiri: kwanza, kwamba ninaweza kujifunza jambo kutokana na hili hubiri; pili, nilidhani kwamba hubiri hili halina ukweli. Je, upendo na kuwa na viwango [vigezo] haviendani? (Hilo ndilo jambo la kufurahisha linaloendelea kwenye haya mafungu katika kitabu cha Isaya. Mungu anasema kuwa viwango [vigezo] vya zamani vya kuwatenga watu vimepita, lakini watu wa zamani waliotengwa wanatakiwa kujitoa kikamilifu kuwa watiifu.)
- Badiliko Dogo
- Soma Luka 19:1-3. Matajiri walikuwa wakiheshimika katika kipindi hicho. Kwa nini Zakayo anapanda miti badala ya kusimama mbele mahali anapoweza kuona na kuonekana? (Watu walimchukia kwa sababu alikuwa mtosha ushuru mkuu wa Warumi.)
- Soma Luka 19:5-6. Je, huu ni mfano wa kile kilichotabiriwa katika Isaya 56? (Ndiyo. Wale ambao hapo awali hawakukaribishwa sasa wanakaribishwa.)
- Soma Luka 19:7. Watu walichukuliaje suala la Zakayo kukubalika? (Hawakulichukulia vizuri.)
- Soma Luka 19:8. Kwa nini watu walidhani kuwa Zakayo alikuwa mdhambi? (Bila shaka walidhani kuwa alikuwa akifanya udanganyifu katika kuwatoza ushuru.)
- Je, suala la Zakayo linaendanaje kwa uzri kabisa na unabii wa Isaya? (Zakayo anaelewa vizuri kabisa suala la tabia yake. Anaahidi kujirekebisha mara moja.)
- Je, tunajifunza lini leo? (Milango ya kuwa na ushirika na Mungu i wazi kwa kila mtu – wakiwemo wadhambi, lakini kujiunga na huo ushirika inamaanisha, kama kielelezo kilichotendwa na Zakayo, kujitoa kuwa watiifu. Upendo humaanisha kuwa na viwango.)
- Kuleta Badiliko
- Baada ya Yesu kufufuka, aliwatembelea wanafunzi wake. Hebu tusome Matendo 1:4-5 ili tujifunze zaidi juu ya mojawapo ya utembeleaji. Je, wanafunzi walipaswa kusubiri jambo gani? (Walitakiwa kusubiria Yerusalemu zawadi [karama] ya ubatizo wa Roho Mtakatifu.)
- Soma Matendo 1:6. Je, ni zawadi gani tofauti waliyokuwa nayo wanafunzi mawazoni mwao? Je, kusalia Yerusalemu kuliendanaje na mpango wao? (Walidhani kwamba Yesu alikuwa anakwenda kutangaza kuwa yeye ndiye Mfalme wa Israeli na hivyo kuivunja nira ya Rumi. Kitovu cha uwezo na nguvu kitakuwa Yerusalemu. Wao watakuwa kitovu cha huo uwezo na nguvu.)
- Soma Matendo 1:7-8. Kinyume chake ni kwamba mpango uliopo kwa ajili yao ni tofauti kabisa. Utagundua kwamba Yerusalemu bado ndio kitovu, lakini je, kazi inaishia wapi? (Walitakiwa kuwa kuwa mashahidi hata mwisho wa nchi.)
- Elezea kwa nini Yerusalemu ndio kitovu cha jambo hili? (Angalia jinsi jambo hili linavyoakisi kile tunachojifunza. Mungu alikuwa na mpango wa kushiriki injili na ulimwengu, na mpango wake ulianza na Wayahudi.)
- Ninaye rafiki wa karibu ambaye ni Myahudi aliyeniambia kuwa Wakristo “waliteka nyara” dini yake. Je, kuna ukweli kiasi gani katika wazo hilo? (Ni kweli kabisa kwamba Ukristo ulikua kutoka katika dini ya Kiyahudi. Lakini, Isaya anatufundisha kuwa watu wa Mungu waliukataa [waliutelekeza] mpango wake wa kuufikia [kuuendea] ulimwengu.)
- Angalia tena Matendo 1:6. Je, wanafunzi walikuwa wanatazamia nini? (Walikuwa wakiangalia mambo kwa ndani. Wao binafsi wangekuwa na uwezo wa kisiasa. Taifa lao lingeutawala ulimwengu.)
- Tunafahamu kwamba mpango wa Yesu wa awali kabisa ulikuwa tofauti sana. Je, jambo hili linalikereketaje kanisa lako? Je, kanisa lako linajikita kujifanyia urejeshwaji au linajikita kuyashuhudia mataifa yote?
- Nguvu ya Kubadili
- Kama jibu lako la dhati kwenye swali lililoulizwa hapo awali ni, “Ndiyo, kipaumbele chetu ni kushughulikia mambo ya ndani,” unadhani itakuwa vigumu kiasi gani kubadilika? Je, mtaanzia wapi?
- Soma Matendo 2:1. Unadhani muda kiasi gani ulipita kati ya Matendo 1:6 hadi kufikia kwenye hili tukio? (Soma Matendo 1:5 – ilikuwa si zaidi ya siku chache.)
- Soma Matendo 2:2-4. Unadhani lengo la kuzungumza kwa kutumia lugha nyingine ni lipi? (Soma Matendo 2:5-6. Walikuwa wameelekezwa na Yesu kuanzia Yerusalemu na kisha kupeleka injili hata mwisho wa nchi. Hii ilikuwa hatua kubwa kuelekea kutimiza jambo hilo.)
- Endapo unadhani kuwa kanisa lako (pamoja na wewe) mmejikita zaidi kushughulikia masuala ya ndani badala ya kujikita kutoka nje, je, kisa hiki kinatufundisha nini? (Badiliko linaweza kuja haraka sana.)
- Je, kitu gani cha muhimu kilileta badiliko la harakai? (Kumiminwa kwa Roho Mtakatifu! Matendo 1:4 inamwita Roho Mtakatifu kuwa ni “karama.” Hiyo inamaanisha kuwa mapenzi ya ufalme [enzi] wa Mungu yanahusika. Matendo 1:14 inaonesha kuwa watu wa Mungu walikuwa wakidumu katika kusali kwa ajili ya hii karama. Yoeli 2:28-29 inaashiria kuwa mkazo wa “kumimina” pia ni sehemu ya mapenzi ya ufalme wa Mungu.)
- Rafiki, je, utajikita kwenye mtazamo wa maisha yako au mtazamo wa kanisa lako? Kama unataka kuuangalia mtazamo wako upya, kwa nini usiombe sasa hivi, ili Roho Mtakatifu akujie maishani mwako na kanisani mwako kwa uwezo na nguvu kuu?
- Juma lijalo: Kuwafanya Viongozi wa Kiroho Kuwa Wanafunzi.