Kristo, Sheria na Maagano
Title: Somo la 10: Kristo, Sheria na Maagano Bible Text: (Mwanzo 9, 15, 17 & 31, Wagalatia 3)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: “Agano” si neno linalotumika sana siku hizi. Neno la kisasa linalotumika ni “mkataba.” Biblia inatumia “maagano” kati ya Mungu na wanadamu kwa kurudiarudia. Kwa kawaida mikataba huingiwa baina ya pande mbili ambazo zina maamuzi yanayolingana. Je, “mkataba” utakuwa sahihi tunaporejea makubaliano kati ya Mungu na wanadamu? Je, tunaweza kuingia mkataba na Muumba wetu, ambaye anatupatia riziki mara kwa mara? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kukigundua!
- Sehemu za Wanyama na Miamba
- Soma Mwanzo 15:9-10. Je, unaweza kulitafakari hili mawazoni mwako? Abramu anawakata wanyama vipande viwili na kuvipanga vipande hivi kwa kutazamana. Unadhani jambo gani linaendelea? (Soma Yeremia 34:18-19. Mafungu haya yanatusaidia kuelewa. Neno la Kiebrania la “agano” linamaanisha “kugawanya” au “kukata katika vipande viwili” kwa mujibu wa Kamusi ya Biblia ya Fausset. Watu walikuwa wakiwakata wanyama vipande viwili na kisha walipita katikati ya vipande hivyo. Hiyo ilimaanisha kuwa waliingia mkataba.)
- Je, unaweza kuhusianisha mantiki ya tukio hili na mikataba ya leo? (Ndiyo! Kwa ujumla pande mbili zinaingia makubaliano ambayo wanagawana majukumu. Kila upande unaahidi jambo. Jambo hili linaitwa “uzingatiaji” na ni muhimu kwenye mkataba halali. Nitakujengea nyumba ikiwa utanilipa kiasi fulani cha fedha. Wajibu wako ni kulipa na wajibu wangu ni kujenga.)
- Soma Mwanzo 31:44-45 na Mwanzo 31:48-49. Je, hapa ishara ya mkataba ni ipi? (Nguzo ya mawe.)
- Unadhani kwa nini walitumia mawe kwa ajili ya mkataba?
- Kuna uhusiano gani, kama upo, ambao sehemu za wanyama zinajihusisha na mawe? (Lengo la mawe ni kutoa ishara au kumbukumbu ya makubaliano. Nadhani kumkata mnyama vipande viwili na kupita katikati ya vipande hivyo pia ni ishara ya makubaliano ya kimkataba.)
- Je, kuna jambo gani linalofanana na hilo tulilonalo leo? (Tunaandika mikataba yetu, na kila upande unasaini jina lake. Maandishi yanafananishwa na mawe – kwa hiyo una uthibitisho wa makubaliano. Saini yako inakuwakilisha, ni utambulisho wako binafsi kwenye mkataba – kama vile kutembea katikati ya vipande vya mnyama.)
- Soma Mwanzo 15:9-10. Je, unaweza kulitafakari hili mawazoni mwako? Abramu anawakata wanyama vipande viwili na kuvipanga vipande hivi kwa kutazamana. Unadhani jambo gani linaendelea? (Soma Yeremia 34:18-19. Mafungu haya yanatusaidia kuelewa. Neno la Kiebrania la “agano” linamaanisha “kugawanya” au “kukata katika vipande viwili” kwa mujibu wa Kamusi ya Biblia ya Fausset. Watu walikuwa wakiwakata wanyama vipande viwili na kisha walipita katikati ya vipande hivyo. Hiyo ilimaanisha kuwa waliingia mkataba.)
- Upinde wa Mvua
- Soma Mwanzo 9:8-11. Je, hapa mkataba ni upi? (Mungu hataiangamiza dunia na uhai uliomo ndani yake kwa gharika litakalotokea duniani kote.)
- Soma Mwanzo 9:12-15. Ishara ya mkataba huu ni ipi? (Upinde wa mvua mawinguni.)
- Tunaona mambo kadhaa yenye kufanana katika kile ambacho tayari tumejifunza. Wanyama waliokatwa vipande viwili, mawe, na upinde wa mvua ni uthibitisho wa mkataba. Je, mgawanyo wa majukumu hapa ni upi? Tunaona sehemu (wajibu wa) ya Mungu, je, wanadamu wanafanya sehemu gani? Je, wanyama (Mwanzo 9:9-10) wanafanya sehemu gani? (Haya hayaonekani kuwa makubaliano ya kawaida ya pande mbili. Mungu ndiye anayetoa ahadi zote. Ikiwa wanadamu na wanyama wana chochote cha kuahidi, basi itakuwa ni kukiri kwamba Mungu ni Mungu wao.)
- Tohara
- Soma Mwanzo 17:1-2. Hii inatuambia nini kuhusu mkataba kati ya Mungu na Abramu? (Tayari ulikuwepo. Huu ni uthibitisho wa mkataba uliopo.)
- Soma Mwanzo 17:3-8. Mungu anaahidi nini katika upande wake wa makubaliano? (Atamfanya Ibrahimu kuwa “baba wa mataifa mengi,” atakuwa Mungu wa Ibrahimu na uzao wake, atawapatia nchi mahsusi “kama milki ya milele.”)
- Soma Mwanzo 17:9-13. Je, Ibrahimu anaahidi nini katika upande wake wa makubaliano? (Kila mwanamume … atatahiriwa.)
- Je, hii inaonekana zaidi kuwa ishara ya mkataba kisha makubaliano halisi?
- Je, mkataba huu unafanana zaidi na mkataba wa gharika/upinde wa mvua? Je, wanadamu wanaahidi chochote?
- Soma Wagalatia 3:6-9. Mafungu haya yanaangalia mjadala tuliousoma muda mfupi uliopita. Je, mafungu haya yanasema kuwa Ibrahimu aliahidi nini? Je, sehemu ya Ibrahimu katika mkataba ni ipi? (Kumwamini Mungu.)
- Je, hii inaashiria nini kuhusu mkataba wa gharika/upinde wa mvua? (Jambo lili lile – sehemu iliyopo katika upande wetu ni kumwamini Mungu.)
- Mikataba na Neema
- Soma Wagalatia 3:15. Mazungumzo haya yanaonekana kuwa ya kisheria. Je, unaelewaje jambo hili? (Mara unapokuwa na mkataba wa kiutekelezaji, hauwezi kusimikwa bila kuwepo kwa makubaliano ya pande mbili. Kwa kuongezea, upande mmoja hauwezi kuongeza majukumu ya upande mwingine.)
- Soma Wagalatia 3:16. Je, unaelewaje jambo hili? Jambo hili linaonekana kusema kuwa Ibrahimu na Yesu waliahidiwa kuhesabiwa haki kwa imani. Je, Yesu alihitaji neema? (Hapana! Jambo hili haliwezi kumaanisha kuwa Yesu aliokolewa kwa imani. Tunayategemea maisha yake makamilifu kwa ajili ya wokovu wetu.)
- Hebu turejee nyuma kidogo, na tusome fungu ambalo nililiruka. Soma Wagalatia 3:14. Fungu hili linasema kuwa sisi Mataifa tunapewaje mbaraka ulioahidiwa kupitia kwa Ibrahimu? (Kwa njia ya Yesu Kristo.)
- Je, hiyo inatusaidia kuelewa anachokimaanisha Paulo alipoandika kuwa “ahadi zilitolewa kwa Ibrahimu na mzao wake” na kwamba “mzao” unamaanisha “mtu mmoja, ambaye ni Kristo?” (Ndiyo. Ahadi ilikuwa kwa Yesu, kwa sababu ni kwa njia ya Yesu pekee sote tunapokea kuhesabiwa haki kwa imani. Yesu ndiye njia yetu katika kuingia kwenye uzima wa milele. Kwa hiyo, ahadi yetu huja kwa njia yake pekee!)
- Hebu turejee nyuma kidogo, na tusome fungu ambalo nililiruka. Soma Wagalatia 3:14. Fungu hili linasema kuwa sisi Mataifa tunapewaje mbaraka ulioahidiwa kupitia kwa Ibrahimu? (Kwa njia ya Yesu Kristo.)
- Soma Wagalatia 3:17-18. Tayari tumejifunza kwamba upande mmoja katika utekelezaji wa mkataba hauwezi kuongeza vigezo vya mkataba. Je, Paulo anasema kuwa jambo gani haliwezi kuongezwa hapa? (Utii wa Ahadi Kumi. “Miaka 430 baadaye” inarejea Amri Kumi na sheria nyingine zilizotolewa kupitia kwa Musa.)
- Soma tena Mwanzo 15:6. Kama tulivyojadili hapo awali, mkataba kati ya Ibrahimu na Mungu ulikuwa kwamba Ibrahimu aamini, na Mungu “akamhesabia jambo hili kuwa haki.” Je, Paulo anazungumza kuhusu Amri Kumi? (Kwa kuwa Ibrahimu na Mungu tayari walikuwa na mkataba wa kiutekelezaji, na kwa kuwa sisi ni warithi wa ule mkataba kwa njia ya Yesu, Mungu hawezi kubadili vigezo vya mkataba kwa kuongeza “Na, lazima mshike sheria ili muweze kuokolewa.”)
- Hebu turejee nyuma kidogo. Sehemu saba katika Biblia zinarejea “agano jipya.” Angalia, kwa mfano, Luka 22:20, 1 Wakorintho 11:25, na Waebrania 12:24. Tunawezaje kuwa na “agano jipya,” wakati Paulo ameelezea jinsi ambavyo mkataba halisi ni ule ule usioweza kuvunjika?
- Soma Kutoka 19:3-8. Je, ni kitu gani hiki? (Huu ni mkataba kati ya Mungu na watu wake wakati Amri Kumi zilipotolewa.)
- Je, mkataba huu unaendanaje na mjadala wetu? Hii ni nyongeza ya “miaka 430 baadaye” na Paulo anajenga hoja kuwa haikuwa nyongeza sahihi. Je, linawezekanaje jambo hilo? (Paulo anatuambia kuwa ahadi halisi ilitolewa kwa Ibrahimu na Yesu. Mungu alifahamu kwamba watu wake wasingeweza kushika Amri Kumi ili kuweza kuupata wokovu, lakini aliwataka watu wazishike ili waweze kuwa na uhusiano naye wa pekee. Yesu alipokuja baadaye, na kuishika sheria kikamilifu, hili lilikuwa jambo jipya. Katika kipindi hicho ahadi ya kuhesabiwa haki kwa imani ilitufikia sote kwa njia ya Yesu. Tunapata fursa ya kupata jambo “halisi,” mkataba halisi!)
- Soma Wagalatia 3:19. Kwa kuwa Amri Kumi haziwezi kuongezwa kwenye mkataba wa neema, kwa nini Mungu alizitoa? (Kwa sababu ya dhambi zetu!)
- Soma Wagalatia 3:23-25. Torati inatuongozaje kwa Yesu? (Tunayafahamu maisha yetu ya taabu na yasiyopendeza. Tunafahamu kuwa tunalo tatizo la dhambi. Hii inatufundisha kuwa njia pekee ya uzima wa milele ni kwa njia ya ahadi iliyotolewa kwa Ibrahimu na Yesu, ahadi inayosema kuwa imani hutupatia thawabu ya kuhesabiwa haki. Tunajinufaisha ahadi hiyo kwa njia ya Yesu pekee!)
- Je, jambo hili linatenda nini kwenye nadharia yangu inayosema kuwa Amri Kumi zinatukinga dhidi ya kudhuriwa na sheria ya asili? (Halitendi chochote. Bado ni ukweli kwamba Mungu alitupatia sheria kwa sababu ya upendo. Bado ni ukweli kwamba Mungu anawahitaji watu wanaotii sheria yake (kama ilivyokuwa pale Sinai). Lakini, pia ni ukweli kwamba kuhesabiwa haki huja kwa njia ya imani pekee – mkataba tunaoweza kujinufaisha nao kwa njia ya Yesu pekee!)
- Rafiki, je, kupitia kwa Yesu, utakuwa sehemu ya mkataba halisi wa kuhesabiwa haki kwa njia ya imani pekee? Kwa nini usimpokee Yesu sasa hivi?
- Juma lijalo: Mitume na Sheria.