Maneno ya Kweli

(Mithali 23 - 24)
Swahili
Year: 
2015
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, unataka kuufahamu ukweli? Mara nyingine huwa ni jambo la kufurahisha tunapokuwa tunajidanganya, lakini kwa ujumla huwa tunaupenda ukweli. Biblia inatuambia kwamba tunaweza kupumbazwa na kile kinachosemwa na watu wengine. Lakini, ikiwa tutajifunza kuangalia muktadha wa mambo kwa macho ya hekima, tutaweza kuuona ukweli. Hebu tuzame kwenye somo letu kuhusu hekima iliyojengwa juu ya Biblia ili tujifunze zaidi!

  1. Ulaji Mzuri
    1. Soma Mithali 23:1-3. Tunakula na nani kama ilivyoelezwa kwenye haya mafungu? (Mtawala. Mtu aliye na madaraka.)
      1. Je, huyu ni mtu wa kawaida tunayekula naye kila siku? (Hapana.)
      2. Mafungu haya yanaeleza kuwa jambo la muhimu zaidi ni lipi, je, ni kula chakula au kumfurahisha mtawala? (Lengo ni kumfurahisha mtawala, na sio kula kadiri ya uwezo wako.)
      3. Kwa nini chakula “kinatamanisha kwa hila?” (Mlo sio kwa ajili ya kuliwa, usijikite kwenye chakula.)
    2. Soma Mithali 23:6-7. Ninaogopa kwa kuwa ninahisi kwamba mimi ni mchoyo [mnyimi], lakini si mchoyo kama baadhi ya watu wengine (isipokuwa labda mtu mmoja) ninayemfahamu. Miaka mingi iliyopita, wanandoa fulani tuliokuwa tukila pamoja nao walikuwa wanaangalia kiasi cha bahshishi tulichompatia mhudumu (niliongezea kwenye kiasi ambacho wanandoa hawa walimpati yule mhudumu), na ikiwa niliweka “kiasi kikubwa,” walisema kuwa nimeweka kiasi kikubwa na walichukua sehemu ya kiasi cha bahshishi walichoweka! Unawezaje kufahamu kwamba mtu ambaye unakula nyumbani kwake ni mchoyo? (Unapokuwa na mashaka, chukulia kwamba mwenyeji wako ni mchoyo.)
      1. Kuna tatizo gani hapa? (Huwezi kuamini anachokisema mwenyeji wako. Anasikitika sana kwa kitendo cha wewe kula chakula chake chote. Anafikiria jinsi kile chakula kilivyomgharimu.)
    3. Soma Mithali 23:8. Tumepotezaje sifa zetu kwa mtu mchoyo? (Unaweza kuwa unasema maneno [mambo] mazuri kwa mwenyeji wako, lakini anachokifikiria huyu mwenyeji wako ni jinsi mambo yote haya yanavyomgharimu!)
      1. Inamaanisha nini kusema kwamba “utatapika kile kidogo ulichokula?” (Unafikiria kwamba chakula kinakunufaisha. Lakini, kinyume chake ni kwamba mwenyeji wako anafikiria kiasi cha fedha ambacho hakupaswa kukitumia kwa ajili ya chakula chako – hivyo, hisia mbaya alizonazo dhidi yako zinatangua uzuri wa chakula ulichokula.)
    4. Soma Mithali 24:3-4. Tumeona mifano miwili katika hali ambayo mtu anakifikiria sana chakula. Je, jambo hili linahusikaje na ujenzi wa nyumba? (Hekima inakufanya utafakari mambo katika mwanga wa kweli. Unapouelewa ukweli, basi utajenga “nyumba” utakayoishi maishani mwako na unaijaza vitu vya thamani na vya kupendeza.)
      1. Chukulia mfano wa kwanza: mtu anafurahia sana ulaji na hazingatii mazingira yaliyopo kwenye ulaji. Kitu gani kitajenga nyumba ya mtu huyu? (Kutafakari mambo makubwa zaidi ya chakula katika uhusiano wako na mtawala hukupatia hekima ya jinsi ya kuenenda.)
      2. Chukulia mfano wa pili kutokana na mtazamo wa mwenyeji: anafikiria sana kuhusu gharama ya chakula. Tiba ya jambo hilo ni ipi? (Mwenyeji anatakiwa kutambua ubinafsi wake. Anapaswa kuwa na furaha kuwapatia marafiki wake zawadi nzuri. Ikiwa mwenyeji hatatibika, unapaswa kutoa msaada kidogo kwa kukilipia chakula.)
    5. Soma Mithali 23:12. Tunawezaje kuuelekeza moyo kusikiliza maneno ya hekima? (Kwa kujifunza hizi mithali. Ikiwa unajiona kwenye hii mifano (kama nilivyojiona kwenye mithali inayomhusu mtu mchoyo), basi unatakiwa kujifunza. Mtu mchoyo ni mbinafsi. Ikiwa unatambua ukweli halisi wa dhambi na kugeuka na kuiacha, basi utajenga nyumba yako!)
  2. Unene na Ulevi
    1. Soma Mithali 23:19-21. Hivi punde tumejadili juu ya ulaji mzuri. Lakini, kiuhalisia masomo hayo hayahusiani na ulaji. Je, mafungu haya yanahusiana na ulaji au la? (Yanahusu kuyaweka malengo yetu vizuri.)
      1. Kuna tatizo gani kula na kunywa kupita kiasi? (Inakuhafifisha. Inakufanya ujisikie usingizi. Inasababisha tatizo lile lile kama vile kulala kupita kiasi.)
      2. Bila shaka watu wenye uzito mkubwa kupita kiasi wanaosoma maneno haya watasema, “Hebu subiri kidogo! Mimi ninatembea kwa mwendo wa kasi. Niko sawa tu na ninafanya kazi zangu vizuri.” Wengine watasema, “Ninawafahamu watu wanene (au walevi) ambao wana mafanikio makubwa.” Unawezaje kuelezea huu ukinzani wa dhahiri? (Hii ni sawa na mafungu mengi tuliyojifunza kuhusu jinsi ambavyo kuwa mtu mwenye haki kunavyokutajirisha. Hizi ni kanuni za jumla. Ninadhani kwamba kila mtu aliyepunguza uzito “uliozidi” atakubaliana nami kwamba anajisikia mwepesi na kuwa na nguvu zaidi baada ya kupunguza uzito.)
    2. Soma Mithali 23:29-30. Je, “kukaa muda mrefu” kwenye mvinyo kunakutendea nini? (Kunafanya macho yako yawe mekundu pamoja na kuumwa kichwa wakati wa asubuhi. Unajikuta kwamba umejigonga kwenye vitu pasipo hata kutambua. Kunasababisha masikitiko [huzuni] na ugomvi.)
    3. Soma Mithali 23:33-35. Biblia inaelezea tatizo gani mahsusi hapa? (Kuona mambo mageni, akili kuchanganyikiwa, kuumia pasipo kutambua, kuamka ukiwa na pombe kichwani na kuhitaji [kutamani] “kinywaji kingine” ni ishara za ulevi. Huu ni ushahidi kwamba maisha yako hayajielekezi kufikia malengo yako.)
  3. Faida za Hekima
    1. Soma Mithali 23:22-23. Inamaanisha nini “kuinunua” hekima na wala si “kuiuza?” Ninagawa (kimsingi ninashiriki na watu wengine) hekima katika masomo haya! Je, hilo ni tatizo? (Fungu linasema kuwa uwe kama sponji [kijipande kidogo cha godoro] linapokuja suala la hekima. Mara zote jaribu kuipata kwa wingi zaidi. Kamwe usiache hekima uliyoipata. Uandishi wa haya masomo unanifundisha hekima zaidi!)
      1. Tunaweza kupata hekima kutoka kwenye chanzo kipi? (Wazazi wanaompenda Mungu.)
    2. Soma Mithali 22:17-18. Tuna njia gani nyingine za kuipata hekima? (Kumtafuta mtu mwenye hekima na kusikiliza kwa makini anachokisema mtu huyo. Yatumie mafundisho hayo maishani mwako na uyafanye kuwa sehemu ya fikra zako.)
    3. Soma Mithali 24:1. Hatupaswi kufanya nini tunapoitafuta hekima? (Hatupaswi kuwasikiliza watu waovu.)
      1. Kwa nini hata tufikirie kuwaendea watu waovu ili kuchota hekima kutoka kwao? (Kwa sababu tunahusudu kile wanachomiliki au jinsi wanavyoishi.)
    4. Soma Mithali 24:21-22. Je, ni chanzo gani kingine cha taarifa tunachopaswa kukiepuka? (Maneno ya waasi. Kuasi dhidi ya mamlaka iliyopo ni tatizo kubwa. Kuwa na mtazamo wa uasi kuna athari kwenye usitawi wako.)
      1. Je, ni watu gani “wawili” watakaoleta “uharibifu wa ghafula” kwa waasi? (Mfalme na Mungu! Ninataka [ninatamani] kuwa upande wa Mungu!)
    5. Soma Mithali 24:5. Hekima inakupatia nini? (Uwezo na nguvu.)
      1. Hii inaonekana kukinzana na mtazamo wetu wa kawaida. Kwa kawaida huwa hatusemi kwamba kufikiri [kutafakari] kunakupatia nguvu. (Uwezo wa kweli hutokana na hekima na kujifunza.)
      2. Nilipokuwa shule, wanadarasa wenzangu walizingatia zaidi mchezo wa riadha badala ya masomo. Hakuna aliyetokea kuwa mwanariadha mahiri, lakini baadhi yao walipaata maarifa ya juu katika shahada za uzamivu. Tunalinganishaje mchezo wa riadha na udhamini wa masomo?
    6. Soma Mithali 24:10. Je, ni nguvu ya aina gani tunayoizungumzia hapa? (Hekima itokayo kwa Mungu. Tunapokabiliana na tatizo, hatupaswi kuangalia nguvu zetu wenyewe zilizo dhaifu, bali tunatakiwa kumgeukia Mungu ili kupata nguvu zake.)
      1. Je, ni jambo gani mahsusi unalomtaka Mungu alitende unapokabiliana na tatizo? (Mara kwa mara huwa tunatafuta uelekeo. Tunataka kufahamu nini cha kufanya. Mara nyingi, tayari Mungu ameshatuambia nini cha kufanya katika kitabu cha Mithali.)
    7. Soma Mithali 24:17-18. Huwa ninachekelea pale Mungu anapowashinda maadui wangu! Kuna tatizo gani na kitendo hicho? (Mungu amewashinda maadui wangu, hivyo basi kwa nini ninachelekea? Huu sio mtazamo tunaopaswa kuwa nao.)
    8. Soma Mithali 24:11-12. Je, tunapaswa kuwa na mtazamo gani dhidi ya watu wasio kwenye msitari sahihi? (Tunapaswa kujaribu kuwaokoa.)
      1. Je, kauli isemayo “wanaochukuliwa ili wauawe” inaongezea nini katika uelewa wetu kwenye juhudi za uokozi? (Inamaanisha kwamba watu waovu ndio wanawaongoza watu ambao hawako kwenye msitari sahihi. Tunaweza kukabiliana na upinzani kutoka kwa watu waovu.)
      2. Hili ni fungu zuri sana kwa watu wanaopinga kwa nguvu suala la utoaji mimba. Kisingizio gani ni batili? (Madai ya kijinga – wakati tulipaswa kufahamu ukweli.)
  4. Rafiki, ukweli ni kwamba tunatakiwa kuwa makini zaidi. Tunatakiwa kuwa makini kwenye suala la kula na kunywa, na kuwa makini na mazingira yanayotuzunguka. Kuwa na hekima hutusaidia kuufahamu ukweli. Je, utadhamiria leo kuutafuta ukweli kwa bidii ili kupata hekima zaidi?
  5. Juma lijalo: Nyuma ya Kinyago