Kuishi kwa Imani

(Mithali 28 & 29)
Swahili
Year: 
2015
Quarter: 
1
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mada mbili tutakazozijadili juma hili zinahusu sheria na uwazi. Unaweza kubashiri hii maana yake ni kwamba, “Wale wanaoishi kwenye nyumba zenye madirisha ya vioo hawapaswi kutupa mawe.” Lakini, unaweza usiwe sahihi. Badala yake, “uwazi,” maana yake ni kuwafanya watu wayaone yale yote uyatendayo. Hakuna siri. Hii inakusaidia uishi kutokana na viwango vyako ulivyojiwekea. Ikiwa sheria ya Mungu ndicho kiwango ulichojiwekea, basi kama unaamini kwamba jambo fulani linapaswa kuwa siri, hicho ni kiashiria kwamba kile unachotaka kukifanya kiwe siri ni jambo ambalo hutakiwi kulitenda. Hebu tuzame kwenye somo letu la Mithali!

  1. Serikali na Sheria
    1. Soma Mithali 28:2. Je, ungependa kuishi kwenye nchi yenye “watawala wengi?”
      1. Kama hupendi, kwa nini? (Inaonekana kwamba uwepo wa watawala wengu huendana na sheria (kanuni) nyingi – na zinaweza kukinzana.)
      2. Namna bora ya kuendesha (kutawala) nchi ni ipi? (Kuishi kwa utawala wa sheria. “Mtu mwenye ufahamu na maarifa hudumisha utii wa sheria.”)
        1. Je, kanuni hii pia inahusika kwenye maisha yetu binafsi? (Sheria ya Mungu inapaswa kuwa “kanuni” katika maisha yetu.)
    2. Soma Mithali 29:4. Rushwa zinaendanaje na utawala wa sheria? (Haziendani. Mfalme anayepokea rushwa anapindua utawala wa sheria kwa manufaa yake binafsi.)
      1. Matokeo yake kwa nchi ni yapi? (Inaharibu usitawi na kuivunja nchi vipande vipande.)
    3. Soma Mithali 28:3. Utagundua kwamba tafsiri ya Biblia ya Kiingereza ya NIV inatafsiri fungu hili tofauti na tafsiri nyingi za Biblia. Tafsiri ya NIV inasema “Mtawala anayekandamiza….” Mvua isiyosaza chakula ni ipi? (Fursa isiyotumika! Ikiwa mtawala hatendi haki kwa maskini, matokeo yake yanatisha. Ikiwa maskini hawawatendei haki maskini, wao pia wanaitumia fursa vibaya.)
    4. Soma Mithali 28:4. Je, tunaona makundi gani mawili ya watu kwenye hii mithali? (Wale waishikao sheria na wale wasioishika.)
      1. Tabia ya wale wasioshika sheria inafananaje? (Wanawasifu waovu.)
      2. Tabia ya wale wanaoishika sheria inafananaje? (Wanashindana/wanapingana na waovu.)
      3.  
      4. Kuna mjadala unaoendelea nchini Marekani kuhusu wajibu wa imani za dini katika siasa. Je, fungu hili linapendekeza jambo gani? (Wenye haki wanawajibika kupingana na waovu.)
        1. Je, hapa tunazungumzia sheria gani? Sheria ya Mungu au sheria ya nchi? (Sheria ya Mungu, lakini kunapaswa kuwepo uhusiano kati ya sheria ya Mungu na Sheria ya mwanadamu. Soma Warumi 13:1-2.)
    5. Soma Mithali 28:5. Tumeona kwamba watu waovu hawaiungi mkono sheria. Kwa nini? (Hawaielewi haki.)
    6. Soma Mithali 28:15-16. Unaelezeaje jambo hili, kwamba, mara nyingine Mungu huwafanya waovu na madikteta (wadhalimu) kuwa watawala? (Mungu ndiye mtawala, lakini anawapa wanadamu uhuru wa kuchagua. Mara nyingine wanadamu wanawaweka madarakani viongozi waovu na madikteta – au wanashindwa kukabiliana nao.)
    7. Soma Mithali 28:12. Inamaanisha nini “kwenda kujificha?” (Kila mtu anataka kuepuka kukabiliana na mtawala mwovu. Lakini, pia inaweza kumaanisha kwamba uovu unaruhusiwa kuendelea kuwepo na watu ambao ni waoga kupaza sauti zao. Katika jambo hili tunapaswa kuwa makini. Rejea onyo dhidi ya uasi katika Warumi 13:2.)
  2. Maskini
    1. Soma Mithali 28:6-7. Tumesoma mithali nyingi zinazotuambia kwamba kuna uhusiano chanya kati ya kuwa mwenye haki na kupata mafanikio. Je, mithali hii inasema nini kuhusu uhusiano huo? (Si kweli mara zote. Mara nyingine matajiri ni wakaidi na wapotovu na maskini hawana hatia.)
      1. Je, hii inaashiria nini katika nia yetu ya kumtii Mungu? Je, tunapaswa kutenda hivyo kwa ajili ya kupata fedha? (Utii una thawabu yake. Bila kujali kama tuna fedha au hatuna, mtu mtiifu anaishi maisha bora – maisha yanayomuakisi yeye au wazazi wake.)
    2. Soma Mithali 28:9. Je, Mungu anasikia maombi ya waovu? (Soma Mathayo 9:10-12. Yesu alipokuwepo hapa duniani alielezea suala la kutumia muda na wadhambi. Ni vigumu kutafakari kwamba jambo hilo limebadilika.)
      1. Ikiwa Yesu anasikia maombi ya wadhambi, je, inamaanisha nini kwamba wale wasioifuata sheria maombi yao ni machukizo? (Kuna maana gani ya kufanya maombi? Ni ili Mungu akusaidie au awasaidie watu wengine, sawa? Kiini cha sheria ni kutusaidia. Kwa hiyo, ikiwa hatuitilii sheria maanani, kwa nini Mungu ayaangalie kwa huruma maombi yetu ya kuhitaji msaada wake?)
    3. Soma Mithali 28:10. Je, umewahi kuwaona watu wema wakipotezwa na watu wabaya? Kama umewahi, je, Biblia inasema kuwa hatima yake ni ipi? (Watu wabaya wataangukia kwenye mtego walioutengeneza, lakini hatimaye watu wema watatoka salama.)
    4. Soma Mithali 28:11. Je, hii inatufundisha nini kuhusu hekima na utajiri? (Tajiri huyu hana hekima, lakini maskini ana hekima.)
      1. Unadhani kwa nini jambo hili ni kweli? (Majivuno ya matajiri yanaweza kuwapofusha dhidi ya ukweli.)
      2. Kwa nini mtu maskini ana utambuzi/ufahamu? (Hapofushwi na majivuno. Na kwa kuongezea, mara kwa mara huwa tuna uwezo mzuri wa kuona dhambi za watu wengine kuliko uwezo tulio nao wa kuona dhambi zetu wenyewe.)
    5. Soma Mithali 28:27. Kwa nini uhusiano wetu na watu maskini unakinzana? (Sheria zinageuzwa kwa sababu kutoa maana yake ni kwamba tunapata zaidi. Kukataa kutoa maana yake ni kwamba tunaishia kupoteza.)
    6. Soma Mithali 29:7. Kwa nini waovu hawajali kuhusu kuwatendea haki maskini? (Haiwasaidii chochote kuwasaidia maskini. Kwa upande mwingine, wenye haki wanafahamu upendo wa Mungu kwa watu wote. Utabaini kwamba maskini wanahitaji vyote viwili, yaani haki na msaada.)
    7. Soma Mithali 29:13. Kauli hii inaonekana kuwa ya ovyo. Inamaanisha nini “kutia nuru macho?” (Wote wawili, yaani mkandamizwaji (mwenye kuonewa) na mkandamizaji (mnyanyasaji) wanaelewa kinachoendelea.)
      1. Kwa hiyo? (Hukumu ya mwisho ya Mungu inathibitika. Hakuna anayeweza kudai upumbavu.)
  3. Uwazi
    1. Soma Mithali 28:13. Kwa nini ungependa kuficha dhambi zako? (Majivuno - hutaki watu wengine wafahamu dhambi zako. Linaweza pia kuwa jambo la kujaribu kujiepusha na matatizo.)
      1. Je, kutubu dhambi zako kunakutendea nini? (Kunaziondoa dhambi zako hadharani kwa maana ya kwamba unaikiri dhambi.)
        1. Dhambi hizi ni za dhahiri kwa kiwango gani? (Tulijadili katika masomo yaliyopita dhana ya kwamba tunatubu dhambi kwa Mungu, sio kwa wanadamu wengine, isipokuwa tu kama tumewadhuru na kukiri huko kunaweza kuboresha mambo.)
        2. Vipi kuhusu wazo la kuishi maisha ya uwazi; je, jambo hilo linahusianaje na kutubu/kukiri dhambi? (Ikiwa utawafanya watu wengine waone jinsi unavyoishi, na ikiwa umeshiriki na watu wengine viwango vyako, hakuna uwezekano kwamba utatenda jambo linalokinzana na viwango vyako.)
    2. Pitia kwa haraka haraka Warumi 14 kisha soma Warumi 14:22-23. Hii inaashiria kwamba baadhi ya siri ni njema. Unawezaje kujua vipengele vya maisha yako vinavyopaswa kuwa vya wazi na vile vinavyopaswa kuwa siri? (Kanuni ya jumla inapaswa kuwa ni uwazi. Hata hivyo, ikiwa una uhakika mkubwa kabisa kwamba kile unachokitenda si dhambi, na unafahamu kwamba watu wengine kimakosa wanadhani kwamba ni dhambi, basi kwa manufaa ya watu wengine – si kwa manufaa yako – unapaswa kufanya jambo hilo liwe kati yako na Mungu.)
    3. Soma Mithali 28:14. Inamaanisha nini “kushupaza” moyo wako? (Kudhamiria kwamba utatenda kile unachokitaka, bila kujali sheria za Mungu.)
    4. Soma Mithali 28:25. Nini chanzo cha tatizo na “mtu mlafi?” (Ubinafsi. Anataka zaidi.)
      1. Kuna uhusiano gani wenye mantiki kati ya kuwa mlafi/mroho na kusababisha mfarakano/ugomvi? (Unatumia nguvu nyingi ili kuwa/kufika juu. Unataka watu watambue uwepo wako.)
      2. Kinyume chake, mtu mwenye hekima anafanya nini? (Anamtumaini Mungu.)
      3. Je, hii inahusianaje na uwazi? (Sasa tunafahamu kwamba wale wanaosababisha vurugu/ghasia maishani si watu wanaomtumaini Mungu.)
    5. Rafiki, somo letu linaonesha kwamba uadilifu, uwazi, utiifu wa sheria zilizowekwa, na kuwajali na kuwatendea haki maskini ni njia inayojielekeza kwenye maisha bora na nchi bora. Kwa nini usifanye mambo haya kuwa lengo lako?
  4. Juma lijalo: Unyenyekevu wa Wenye Hekima.