Mtafaruku Mbinguni

(Isaya 14, Ufunuo 12, Ezekieli 28, Mwanzo 3)
Swahili
Year: 
2016
Quarter: 
1
Lesson Number: 
1

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Dhambi ilianzaje? Biblia inaandika kwamba Adamu na Eva waliumbwa na Mungu. Kwa nini Mungu aliumba kitu chenye dosari, kitu kilichokuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na dhambi ndani yake? Biblia pia inaandika kuwa Adamu na Eva walisaidiwa kuingia dhambini. “Msaada” ulitokana na kiumbe mwingine aliyeumbwa na Mungu. Kwa nini kiumbe kilichoumbwa na Mungu kisaidie kuanzisha dhambi? Kwa kuwa dhambi inaonekana kuwepo kabla ya Adamu na Hawa, je, ilianzia wapi? Hebu tuchimbue somo letu la Biblia ili tuone vidokezo vinavyobainishwa!

  1. Dhambi Inaanza
    1. Soma Isaya 14:12. Huyu anaonekana kuwa mtu wa namna gani? (Mtu wa muhimu aliyetoka mbinguni, lakini “aliangushwa kutoka mbinguni” na kutupwa duniani. Mtu ambaye amesababisha matatizo kwa mataifa ya hapa duniani.)
    2. Soma Isaya 14:13-14. Sababu ya huyu mtu kutupwa kutoka mbinguni ni ipi? (Mtu huyu ana hamu ya kuwa juu ya watu wengine wote na kuwa sawa na Mungu.)
      1. Hiyo inaonekana kama tamaa ya kutaka makuu (malengo makubwa). Kuwa na malengo makubwa ni jambo jema, sawa? (Kiumbe aliyeumbwa anawezaje kutamani kuwa sawa na Mungu?)
    3. Soma Ufunuo 12:7-9. Je, kuna uhusiano wowote kati ya mtu anayeelezewa hapa na yule anayeelezewa katika Isaya 14:12? (Wote walitupwa kutoka mbinguni. Ufunuo inamwelezea mtu huyu kwamba anaudanganya ulimwengu wote, wakati Isaya inamwelezea mtu aliyewaangusha mataifa. Mazingira yanaonekana kufanana.)
      1. Nani mwingine alitupwa chini? (“Malaika zake.”)
      2. Mbingu ilitamani kwa kiasi gani kumwondosha mtu huyu? (Ilitamani sana kiasi cha kuingia vitani dhidi yake.)
    4. Soma Ezekieli 28:14-16. Tunajifunza nini kumhusu mtu huyu? (Pamoja na mambo mengine, alikuwa mtu wa muhimu mbinguni, alifukuzwa mbinguni (kutoka kwenye mlima wa Mungu), na ana tatizo la dhambi.)
    5. Je, tunajifunza kuhusu watu watatu tofauti, au matukio yote haya matatu yanamzungumzia mtu mmoja? (Si rahisi sana kwamba watu watatu wawe na hayo maelezo ya pekee yenye kufanana. Nadhani tunatakiwa kuchukulia kwamba maelezo yote hayo yanamhusu mtu mmoja.)
    6. Soma Ezekieli 28:11-13. Fumbo limefumbuliwa! Maelezo yote haya matatu yanamwelezea Mfalme wa Tiro, sawa?
      1. Ikiwa hii ni sawa na kutatua fumbo, kuna baadhi ya vipengele katika jambo hili ambavyo vinakinzana. Tunaposoma Ezekieli 28:13-14 tunajifunza huyu Mfalme wa Tiro alikuwa “kerubi wa mbinguni mwenye kutiwa mafuta afunikaye,” lakini pia alikuwepo Edeni. Je, unakumbuka nani alikuwepo Edeni? Je, baadhi ya tabia zilimjumuisha mtu mmoja anayeitwa Mfalme wa Tiro?
    7. Soma Mwanzo 3:1-4. Maelezo haya yanamzungumziaje mtu huyu ambayo yanaendana na maelezo tuliyoyasoma katika Ufunuo 12? (Anaelezewa kama nyoka. Hiyo tu inaendana na maelezo ya Ufunuo 12, lakini kuwepo huku katika Edeni pia kunaendana na maelezo ya Ezekieli 28.)
      1. Ikiwa kweli huyu ni mtu yule yule aliyeelezewa katika sehemu nne kwenye Biblia, unawezaje kumwelezea mtu huyu kuwa ni Mfalme wa Tiro? (Ikiwa nyoka aliyopo Edeni hakuwa nyoka halisi, lakini kiuhalisia zamani alikuwa kerubi mbinguni na sasa akijulikana kama Shetani, inawezekanaje sasa kueneza habari kwamba kweli Mfalme wa Tiro pia alikuwa Shetani? Huenda kama ambavyo Shetani alichukua umbo la nyoka pale Edeni, vivyo hivyo Shetani alimdhibiti Mfalme wa Tiro. Maoni ya Unger yanatuambia kwamba “Tiro [alikuwa] fisadi, mbinafsi, tajiri, na worldly wise city” ikiwa ni matokeo ya “kuchakaa na kuporomoka kimaadili” kwa “madhehebu ya Kikaanani.”)
    8. Soma Ufunuo 12:12. Tunajifunza kwamba mbingu zinashangilia kuwa Shetani amefukuzwa, lakini wale tunaoishi duniani tunatakiwa kuwa na wasiwasi sana kwa sababu Shetani ana hasira na “anafahamu kuwa muda wake ni mchache.” Unadhani kauli ya “muda wake ni mchache” inamaanisha nini?
  2. Mafungu haya yanatupatia viashiria gani kuhusu asili ya dhambi? (Kwamba ilianzia mbinguni, na kwamba ilihusisha kuitamani nafasi ya Mungu, na kwamba hii tamaa kuu ilibadilika na kuwa vita halisi ambayo Shetani alishindwa. Shetani pamoja na washirika wake walifukuzwa – na ikawa ahueni kubwa na furaha mbinguni. Lakini, kitendo hiki kilileta machafuko makubwa katika sayari yetu!)
    1. Hebu turejee nyuma na tupitie tena kisa cha Edeni ili tuone kama tunaweza kurekebisha hitimisho letu. Biblia inatuambia kuwa hivi ndivyo ambavyo dhambi ilivyoingia katika dunia yetu. Soma Mwanzo 3:2-5. Kuna jambo gani limejificha ndani ya kishawishi hiki? (Kufanana na Mungu. Endapo Hawa atakula tunda, basi atafanana na Mungu.)
      1. Kutokana na kile tulichokisoma hadi sasa, nadharia yako ni ipi kuhusu jinsi ambavyo dhambi iliingia mbinguni? (Inaleta mantiki kwamba Shetani anatumia mbinu yoyote ambayo ingefanikiwa mbinguni kuleta dhambi duniani. Kwa kuwa Isaya anabainisha matamanio ya kutaka kufanana na Mungu kama sehemu ya tatizo halisi mbinguni, tunaona tatizo linalofanana na hilo kwa Eva. Hii inaashiria kuwa dhambi ilianza kwa sababu mmojawapo wa viumbe wa muhimu kabisa aliyeumbwa na Mungu alitamani nafasi ya Mungu.)
      2. Ikiwa ushauri huu uko sahihi, kwa nini Mungu aliuruhusu? Kwa nini aliwaumba watu mbinguni na duniani huku wakiwa na uwezo wa kutamani (Mungu aliwapa viumbe wake wote uhuru wa kuchagua.)
        1. Kwa nini Mungu alifanya hivyo ikiwa matokeo yake yalitisha: vita mbinguni na sasa vita duniani?
    2. Mada ya mfululizo huu wa masomo ni “Uasi na Ukombozi.” Je, unaweza kuichukulia tamaa ya kutaka kufanana na Mungu kuwa ya uasi zaidi kuliko uasi wenyewe? Vipi kama unataka kuchukua nafasi ya Mungu? Vipi ikiwa uko radhi kupambana na Mungu ili kupata nafasi ya juu? (Lengo kuu ambalo linaishia kwenye mapambano ya kuchukua nafasi ya Mungu ni uasi.)
      1. Je, leo hii wanadamu wanaweza kuwa na mtazamo kama huu? Je, inawezekana kwako?
  3. Mustakabali wa Vita
    1. Nilipokuwa mdogo, nilikuwa ninaangalia sana mpira wa miguu kuliko ninavyoangalia sasa hivi. Mojawapo ya tatizo ilikuwa ni kwamba kazi yangu ya uanasheria ilikuwa na shinikizo kubwa, na kutazama mechi nikiwa na matumaini kwamba timu yangu itashinda pia ilileta shinikizo kubwa zaidi. Kwa kuwa sikuhitaji mashinikizo mengi, nilirekodi mechi na kuitazama ikiwa tu timu yangu imeshinda. Hapo niliweza kuufurahia mchezo kwa uhakika kabisa huku nikifahamu hatma ya mchezo huo. Soma Ufunuo 12:10-11. Nani atakayeshinda vita duniani dhidi ya Shetani? (Sisi.)
      1. Tutashindaje? (Wokovu umekuja kwa njia ya mamlaka ya Masihi. Tunamshinda Shetani “kwa damu ya Mwana-Kondoo na kwa neno la ushuhuda wao.”)
      2. Wale wanadamu wanaoshinda vita wana mtazamo wa aina gani? (Wako radhi kufa. Hawayapendi maisha yao sana kiasi cha kutokuwa radhi kufa kwa ajili ya kushindana na dhambi.)
        1. Hiyo inalinganishwaje na mtazamo uliosababisha tatizo la dhambi hapo awali?
      3. Kama ambavyo yumkini unafahamu, rejea ya “Masihi” na “damu ya Mwana-Kondoo” ni kielelezo cha Yesu kufa kwa ajili yetu ili kulipa adhabu ya dhambi zetu. Ikiwa tunataka kuwa na mtazamo kama huu, hilo litatendekaje maishani mwetu? Hiyo itamaanisha nini kivitendo?
    2. Soma Yohana 12:31-33. Hapo awali tulijadili jinsi Shetani alivyotaka kuchukua nafasi ya Mungu na jinsi wanadamu wanavyoweza kutafuta namna ya kuchukua nafasi ya Mungu. Yesu anapomwita Shetani “mkuu wa ulimwengu huu,” je, Shetani amechukua nafasi ya Mungu? (Amechukua nafasi ya Mungu kama “mkuu” wa ulimwengu – na tunamsaidia Shetani kufanya hivyo tunapoichagua dhambi. Kila tunapomchagua Shetani dhidi ya Mungu tunakuwa tumechukua nafasi ya Mungu kwa kiasi fulani.)
      1. Yesu anasema kuwa atamfukuzaje Shetani? (“Atakapoinuliwa juu.” Hiki ni kielelezo cha mateso ya Yesu. Yesu anamshinda Shetani kwa “kuinuliwa juu,” lakini si kwa namna ambayo wanadamu wangependa kuinuliwa juu.)
    3. Rafiki, je, umeuchunguza mtazamo wako? Je, upo kwenye uasi dhidi ya Mungu? Je, unamchagua Shetani na hivyo kuchukua nafasi ya Mungu kama mtawala wa dunia yako? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu akusaidie uachane na mtazamo wako wa uasi na kujikweza?
  4. Juma lijalo: Mtafaruku Edeni.