Somo la 10: Paulo na Uasi

Swahili
(Warumi 5, 1 Wakorintho 3 & 12)
Year: 
2016
Quarter: 
1
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kanisa lina umuhimu gani? Huwa ninasikia madai yanayosema kwamba, kuwa katika hali ya asili ni jambo jema, kama si bora zaidi, kuliko kuwa kanisani. Kuna baraka halisi katika hali ya asili, lakini baraka hiyo ni tofauti kuliko kwenda kanisani mara kwa mara. Juma hili tunajifunza kuwa kwa pamoja sote tupo dhambini, na tunatakiwa kuwa pamoja kwenye mapambano dhidi ya dhambi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 1. Suluhisho la Dhambi
  1. Soma Warumi 5:12. Huyu “mtu mmoja” ni nani? (Adamu, kama tutakavyoona kwa jinsi tutakavyoendelea kusoma.)
   1. Je, ulifanya uchaguzi wa kutenda dhambi? (Ndiyo: “Wote wamefanya dhambi.” Hata hivyo, hii inaashiria jambo zaidi – kwamba uamuzi wetu wa kutenda dhambo moja kwa moja ulitupatia kifo kutokana na uamuzi wa awali wa Adamu.)
  2. Soma Warumi 5:13-14. Inamaanisha nini kusema kuwa “dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria?” (Fungu lote linasema kuwa tulikufa kabla sheria haijatolewa, hata wale ambao “hawakutenda dhambi kwa kuvunja amri.” Kwa hiyo, hii haiwezi kumaanisha kuwa adhabu ya dhambi haikuwepo. Badala yake, lazima inamaanisha kuwa dhambi haikuchukuliwa kwa namna hiyo. Adamu na Hawa walipewa amri mahsusi, nao waliikiuka. Kabla Amri Kumi hazijatolewa, watu walikufa hata kama hawakuwa na amri mahsusi ya kuivunja.)
   1. Kuna jambo gani la kujifunza kivitendo kwa ajili yetu? (Amri Kumi zina lengo la kubainisha dhambi. Hazibadili ukweli kwamba sisi ni wadhambi.)
  3. Soma Warumi 5:15-17. Kwa kiwango rahisi kabisa tunaweza kuona kuwa “karama sio kama kosa” kwa maana ya kwamba mtu mmoja alituingiza dhambini na kwenye kifo na mwingine “alileta kuhesabiwa haki” kutoka dhambini. Je, taarifa ya ziada inamaanisha nini kuhusu “hukumu ilifuata baada ya dhambi moja kutendwa,” bali “karama ilizifuata dhambi nyingi.?” (Sisi ni waathirika wa dhambi ya Adamu. Dhambi yake ilitudhuru. Lakini, tayari kila mtu binafsi alishachagua kutenda dhambi Yesu alipotatua tatizo letu la dhambi kwa kutuhesabia haki.)
  4. Soma Warumi 5:18-19. Hii inaonekana kusema kuwa kuhesabiwa kwetu haki hutokea moja kwa moja kwa njia ya Yesu. Je, ni sahihi? (Nadhani hii inapaswa kumaanisha kuwa kuhesabiwa haki hutokea moja kwa moja. Hoja ya Paulo inahusu jinsi dhambi na neema vinavyoakisiana, na Paulo anabainisha kuwa kila mtu alitenda dhambi yeye binafsi.)
  5. Soma warumi 6:1-4. Hii inaongezea nini kuhusu endapo tunahitaji kuchagua neema? (Inatuambia kuwa katika ubatizo tunaingia kwenye kifo cha Yesu na ufufuo wake kutoka kwenye mauti. Tunaingia kwenye maisha mapya. “Sisi pia tunaweza kuishi maisha mapya.”)
   1. Mafungu haya yanatufundisha nini kuhusu jamii? (Kwa pamoja sote tupo kwenye jambo hili. Tumo dhambini pamoja na tumo ndani ya neema pamoja. Hebu tuangalie jambo hili kivitendo katika sehemu inayofuatia.)
 2. Suluhisho la Kanisa
  1. Soma 1 Wakorintho 3:10. Paulo anajenga “msingi” gani? (Soma 1 Wakorintho 3:5-9 ili kupata maelezo. Paulo anazungumzia kuhusu “ujenzi” unaowahusisha wafuasi wa Yesu.)
  2. Soma 1 Wakorintho 3:10-15. Hii inawaambia nini wale wanaofanya kazi kuliboresha kanisa? (Kwamba tunapaswa kuwa “makini” jinsi tunavyojenga na tunatakiwa kuwa makini kutumia nyenzo/malighafi bora.)
   1. Kila ninaposoma fungu hili mara moja huwa ninafikiria kuhusu kufundisha, na hitaji langu la kujitahidi kuwa mwalimu wa “kiwango cha dhahabu.” Lakini, huu ni mtazamo finyu sana. Wale wanaoshughulika na watoto kanisani ndio wajenzi, wale wanaojihusisha kumsifu Mungu ndio wajenzi, wale wanaowatembelea wagonjwa ndio wajenzi, wale wanaohudumia mahitaji ya kanisa ndio wajenzi. Swali ni hili, ikiwa wewe ni mjenzi, je, mara zote unajitahidi kufanya kazi yenye “kiwango cha dhahabu?” Je, unajitahidi kuwa bora zaidi?
   2. Hebu tuangalie jambo hili kwa mtazamo tofauti. Tuchukulie kwamba mwalimu anajenga kwa kutumia “madini ya fedha” au nyenzo/malighafi hafifu. Je, hiyo inamaanisha kuwa tunatakiwa kuwapinga? (Tunatakiwa kujizuia kuwakosoa wale ambao wanaweza wasiwe wanafanya mambo kwa usahihi (kwa mtazamo wetu). Tunatakiwa kuendelea kusimamia kazi kwa kiwango cha dhahabu kwa sababu hatuhitaji “hitilafu,” bali tunatakiwa kutambua kwamba kuna wajenzi wengine wengi, hata kama kazi yao si ya kiwango cha dhahabu.)
  3. Soma 1 Wakorintho 3:16. Hekalu la Mungu ni lipi, kwa kuzingatia muktadha wa kile ambacho tumekuwa tukijifunza? (Wakristo wenzetu. Ni kanisa.)
   1. Je, unawafahamu watu ambao hata si “wajenzi watumiao mabua/wasiofanya maandalizi kamili,” ambao ni waangamizaji wa kanisa?
    1. Nani atakayetatua hili tatizo? (Mungu atamwangamiza.”)
  4. Soma 1 Wakorintho 12:12-13. Nilipokuwa ninakua, palikuwepo na madhehebu yangu pamoja na madhehebu mengine yaliyosalia ambayo “hayakuwa safi.” Sasa nimekuwa mtu mzima na kufanya kazi kwa karibu na Wakristo wengine, nimetambua kwamba Wakristo wengine wanaokulia kwenye madhehebu mengine wana mtazamo huo huo kuhusu kanisa lao – kimsingi, inawezekana madhehebu yangu yalijihisi hivyo machoni mwao! Nani alifahamu hivyo? Fungu hili linasema nini kuhusu huu mtazamo “wao na sisi” miongoni mwa Wakristo? (Linasema kuwa sisi ni “mwili mmoja” katika Roho Mtakatifu na tunanyweshwa kwa “Roho mmoja.”)
   1. Hii inatufundisha nini kuhusu washiriki wa kanisa wanaoyadharau madhehebu mengine? (Bado hawajanywa vya kutosha kutoka kwa Roho Mtakatifu.)
  5. Soma 1 Wakorintho 12:14-17. Kanisa langu lina utume maalum wa kutangaza ujumbe wa Ufunuo 14:6-12. Je, ni sahihi kuchukulia kuwa ujumbe huu ni wa “jicho?” Ikimaanisha kwamba, je, ni sehemu tu ya ujumbe wa jumla uliowasilishwa na kila madhehebu katika kanisa kuu la Kikristo?
   1. Nilipokuwa mdogo, nilifundishwa kuwa madhehebu yaliyokuwa kongwe kuliko kanisa letu yalikuwa na ujumbe maalumu kila moja, na kila madhehebu yaliyofuatia yaliongezea uboreshaji zaidi hadi tulipopata madhehebu yangu (kanisa langu) yaliyokuwa yakitangaza umakini/uadilisho wa mwisho. Je, kuna msingi wowote wa Biblia kwenye huo mtazamo? Au, je, maelezo mazuri zaidi yanapatikana kwenye sura tunayojifunza, kwamba kila “sehemu” ya kanisa la Kikristo hupeleka ujumbe wake wa pekee na wa muhimu?
   2. Ikiwa pendekezo langu liko sahihi, je, hii inasaidia kuleta mantiki kuhusu makanisa yote ya Kikristo? Badala ya kulalamika kwamba madhehebu yote yanaonesha udhaifu kwenye umoja, vipi kama madhehebu yote ni sehemu ya mwili wa Kristo, yote yakiwa na nyongeza ya pekee katika kweli? Unaweza kuufikiria mguu usemao, “Tuna sehemu nyingi za mwili kupita kiasi hapa, hali hii inaonesha upungufu wa umoja?”
  6. Soma 1 Wakorintho 12:18-20. Nani anawajibika kwa wajibu wa pekee wa kila sehemu ya kanisa la Kikristo? (Mungu ndiye anayewajibika!)
   1. Angalia huu mfano: babu yangu, mjomba wangu na binamu yangu walikuwa watumishi kwenye Kanisa la Jeshi la Wokovu. Ndugu zangu wengi ni washiriki wa hayo madhehebu ya pekee. Je, Kanisa hilo lina wajibu wa pekee katika mwili wa Kristo unaoweza kuubainisha? (Ndiyo, kanisa hilo linajulikana kwa huduma yake kwa masikini na watu wasio na makazi.)
   2. Nilipokuwa mdogo, na mjinga, nilikuwa ninajivunia kile nilichodhani kuwa ni uelewa mahiri wa teolojia kuliko mjomba wangu ambaye alikuwa mtumishi kwenye kanisa la Jeshi la Wokovu. Hii ni sawa na sikio kujiona bora zaidi kuliko pua! Sidhani kama kamwe nitafikia kiwango cha upendo na kumtumaini Mungu vilivyodhihirishwa katika maisha ya mjomba wangu. Alikuwa mtu wa pekee wa Mungu! Unadhani unaweza kujifunza nini kutoka kwa washiriki wa makanisa mengine?
    1. Tunawezaje kushirikiana nao ili kuutangaza Ufalme wa Mungu, mwili wa Kristo?
  7. Soma 1 Wakorintho 12:21-26. Nimetoa maoni yangu kwamba unapaswa kuangalia kama maneno ya Paulo yanahusika kwa madhehebu yote tofauti tofauti ya Kikristo. Yanaweza kutumikaje kwa namna nyingine?
   1. Je, yanaweza kutumika kwenye vikundi vidogo ndani ya madhehebu yetu?
   2. Je, yanaweza kutumika kwenye kanisa mahalia, kwenye kundi la kanisa lako?
   3. Ikiwa yanaweza kutumika kwenye madhehebu mengine, kwenye vikundi ndani ya kanisa letu na ndani ya kundi lako la kanisa, unayaelewaje maoni ya Paulo kuhusu sehemu ambazo “hazina heshima,” na “visivyo na uzuri?” (Ninaposoma maoni kwenye mtandao wa intaneti kutoka kwa watu wanaodhaniwa kuwa ni washiriki wa kanisa langu, mara nyingine huwa ninadhani kuwa “siwahitaji!” Paulo ananisahihisha na kusema kuwa “tunapaswa kuwa na mtazamo wa usawa kwa kila mtu.”)
  8. Rafiki, tunatakiwa kuhusiana na washiriki wengine wa kanisa. Tunawahitaji watu walio na karama tofauti za roho, talanta tofauti na mitazamo tofauti. Ikiwa huendi kanisani mara kwa mara, kwa nini usidhamirie kuanza kwenda katika Sabato hii inayokuja?
 3. Juma lijalo: Petro na Pambano Kuu.