Yesu Ndani ya Yerusalemu

(Mathayo 21 & 22)
Swahili
Year: 
2016
Quarter: 
2
Lesson Number: 
10
 1. Utangulizi: Kumkubali kiongozi kuna matokeo yake. Ukubali wako unamaanisha kwamba unamkubali mtu huyo aweze kuongoza na kufanya maamuzi ya msingi. Mathayo anaendelea na mwendelezo wake wa kuthibitisha kwamba Yesu ni Masihi, Yesu ni Bwana. Sasa Mathayo ananukuu matokeo ya kukataa kumfuata Yesu kwa dhati. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

   

  I.                    Kuingia

   

  A.                Soma Mathayo 21:1-3. Je, ungetilia mashaka maelekezo haya endapo Yesu angekupatia hayo maelekezo? (Ningepata ugumu sana kuchukua vitu vya thamani kwa msingi kwamba nitamwambia mwenye navyo “Bwana anawahitaji.” Hata hivyo, ikiwa Yesu anaweza kuyaona mambo yajayo, ninawezaje kutilia shaka jambo lolote analolisema?)

   

  B.                 Soma Mathayo 21:4-5. Mathayo anathibitisha jambo gani hapa? (Kwa mara nyingine, Mathayo anathibitisha kuwa Yesu anatimiza unabii kwamba yeye ni Masihi. Utaona kwamba anakuja kwa upole.)

   

  C.                 Soma Mathayo 21:6-9. Soma Mathayo 16:20. Jambo gani limetokea? (Sasa ni wakati wa kutangaza kuwa Yesu ni Masihi.)

   

  1.                  Makutano wanasema nini kumhusu Yesu? (Kwamba Yesu ni “Mwana wa Daudi,” Yeye ajaye “kwa jina la Bwana,” na “Hosana.”)

   

  2.                  Soma Zaburi 118:25-26. “Hosana” maana yake ni “utuokoe sasa” au “tafadhali tuokoe.” Je, Zaburi 118 inatufundisha jambo gani la ziada kuhusu makutano kupaza sauti? (Kwamba Yesu ndiye anayekuja kuwaokoa. Kitendo hiki kinatangaza kwamba Yesu ni Bwana na Masihi aliyeahidiwa.)

   

  D.                Soma Mathayo 21:10-11. Je, jibu hili lilisababisha matatizo? (Soma Mathayo 2:3-6. Ikiwa watu walikuwa wana ufahamu juu ya unabii wa Masihi, kusema kwamba Yesu alikuwa anatokea Nazareti kungesababisha mtafaruku.)

   

  1.                  Je, ungefanya nini endapo ungekuwepo mahali pale ukisikiliza jambo hili? (Natumaini ningefanya uchunguzi zaidi!)

   

  II.                  Hekalu

   

  A.                Soma Mathayo 21:12-13. Tulisikia wanachokisema watu wengine kumhusu Yesu. Tumefuatilia mfululizo wa uthibitisho wa Mathayo kumhusu Yesu. Yesu anajizungumziaje hapa? (Analiita hekalu kuwa ni “nyumba yangu” na anaonesha mamlaka juu ya kile kinachoendelea hekaluni.)

   

  B.                 Soma Mathayo 21:14-15. Je, viongozi wa dini wanaudhika kutokana na Yesu kuwaponya watu? (Soma Mathayo 21:16. Walikasirika kuhusu Yesu kuitwa “Mwana wa Daudi” na yeye (Yesu) kuenenda kama kiongozi wao.)


   

  C.                 Soma Zaburi 8:1-2. Hili ndilo fungu ambalo Yesu analinukuu. Fungu hili linabainisha jambo gani? (Kwamba Yesu ni Bwana, Kwamba Mungu anabariki sifa anazopewa kutoka kwa watoto, na sababu ya kufanya hivyo ni “kuwanyamazisha, kuwakomesha adui na mijilipiza kisasi!”)

   

  III.              Mtini

   

  A.                Soma Mathayo 21:17-19. Je, hili ni jambo jema au baya? Je, Yesu anauangamiza mti kutokana na hasira?

   

  1.                  Mtini umetenda jambo gani lililosababisha uangamizwe? (Majani yake yanakudanganya na kukufanya udhani kuwa una matunda.)

   

  2.                  Je, hili ni fundisho kwa Wakristo wanaojiita kuwa ni Wakristo?

   

  B.                 Soma Mathayo 21:20-22. Hivi karibuni nilitazama sinema iliyoonesha miujiza kadhaa isiyo na maana (ya kipuuzi). Watu waliota meno ya dhahabu, vito vya bandia vilitengenezwa bila kutumia rasilimali yoyote, nk. Asili ya kipuuzi ya miujiza hiyo ilinifanya nishangae na kutafakari asili yake. Je, tunashughulika na miujiza isiyo na maana katika Mathayo 21: kuufanya mtini unyauke na kuhamisha milima? (Mti ni fundisho kwa wanafiki. Milima inaweza kuwa inawakilisha changamoto na matatizo yaliyopo maishani mwako. Yesu anatuambia kuwa imani ndio jibu kwa changamoto za maisha.)

   

  IV.              Shamba la Mizabibu

   

  A.                Soma Mathayo 21:33-36. Wapangaji wanaweza kujenga hoja gani kutokana na mwenendo (tabia) wao? (Hawana kisingizio kwa ajili ya jambo hili.)

   

  B.                 Soma Mathayo 21:37-39. Nia ya kumwua mwana wa mwenye shamba ni ipi? (Mali. Uroho/ulafi. Wizi.)

   

  C.                 Soma Mathayo 21:40-43. Yesu anasema huu ni muujiza kuhusu viongozi wa dini na watu watakaomwua (Yesu). Walitaka mali gani? Shamba lao la mzabibu lililoibwa ni lipi? Mungu alitarajia taifa lake teule kuzaa matunda ya roho. Badala yake, walijielekezea faida na kujisifu wao wenyewe.)

   

  D.                Fikiria tena kuhusu mtini ulionyauka. Je, kweli huo ni muujiza wa kipuuzi? Uangamivu wa kipuuzi? (Hii ilielezea sababu ya taifa la Kiyahudi lililomkataa Yesu litakavyoangamizwa hivi karibuni.)

   

  E.                 Soma Mathayo 21:44. Je, hizi ndizo chaguzi zetu mbili maishani?

   

  F.                  Soma Mathayo 21:45. Je, walengwa wa mjadala wa Yesu wana mashaka? (Hapana. Mathayo anabainisha jambo hili kwa dhahiri kabisa.)

   

  V.                Harusi

   

  A.                Soma Mathayo 22:1-5. Kwa nini wale walioalikwa harusini hawaji? (Wametingwa na shughuli nyingi sana.)

   

  1.                  Kisingizio chao kinafananaje na nia ya wale waliotaka kuiba shamba la mzabibu? (Makundi yote mawili yalikuwa yanatafuta kujipatia fedha. Walikuwa wanataka kuongeza mali zao.)

   


  2.                  Harusi ni ya muhimu kiasi gani kwa mfalme?

   

  B.                 Soma Mathayo 22:6-7. Je, hii ni haki? (Wao ni wauaji! Walimdhihaki na kumkasirisha mfalme wao.)

   

  1.                  Je, si kitendo kikubwa kupita kiasi kuwaua watu kwa sababu wamekudhihaki na kukukasirisha? (Kwa mara nyingine, tafakari muktadha uliopo. Hapo awali Mathayo alielezea kisa cha mtini na kisa cha shamba la mizabibu. Kuwa mnafiki, kuipinga injili, kuwatendea vibaya na kuwaua wafuasi wa Mungu, na kumkataa Mungu kuna matokeo yake.)

   

  C.                 Soma Mathayo 22:8-10. Hapa kigezo cha kuwachagua watu ni kipi? Je, kuna wanafiki na watu wabaya katika kundi hili? (Mwaliko ulikuwa kwa ajili ya watu wote. Watu “wabaya” (pamoja na wema) waliutikia mwaliko. Kigezo cha kuchaguliwa ni kuukubali mwaliko.)

   

  D.                Soma Mathayo 22:11-12. Kuna jambo gani la kushangaza kuhusu kutokuwa na mavazi sahihi? Watu hawa walitolewa kutoka sehemu mbalimbali za mitaa, walikuwa wamevaa mavazi ya kuendea sokoni na kufanya manunuzi mengineyo, mavazi ya kazini, na mavazi kwa ajili ya mapumziko ya kawaida!

   

  1.                  Unadhani kwa nini mtu mmoja pekee ndiye hakuwa amevaa mavazi sahihi? (Hii inatusaidia kujaza mashimo katika kweli zisizoepukika. Lazima kila mtu alikuwa na upungufu kwenye suala la mavazi, sio mtu mmoja pekee. Hivyo, tunajifunza kuwa lazima mfalme atakuwa aligawa mavazi rasmi ya harusi kwa wageni wote, lakini mtu huyu aliyakataa.)

   

  a.                   Hebu tuangalie mantiki hapa. Mwishoni mwa fungu la 12 linatuambia kuwa mtu yule “alitekewa.” Je, tunaweza kuongezea kweli zipi nyingine? (Mfalme hana makosa. Ikiwa mfalme aliwatoza fedha kwa ajili ya kupata mavazi maalumu, ikiwa mavazi hayo hayakuwatosha, ikiwa mtu yule hakufahamu lolote kuhusu mavazi maalumu, basi angetoa kisingizio. Kwa namna fulani alidhani kwamba alikuwa sahihi kuyakataa mavazi ya mfalme.)

   

  b.                  Jambo gani linaweza kuwa lilimfanya mtu huyu adhani kuwa yuko sahihi kukataa kuvaa vazi maalumu la harusi lililotolewa na mfalme? (Aliyapenda mavazi yake zaidi. Hakuhitaji ukarimu wa mfalme, alikuwa mtu mwenye kujali sana suala la mavazi.)

   

  (1)               Vipi kuhusu wewe? Je, unajivunia kazi zako?

   

  E.                 Soma Mathayo 22:13. Jambo gani linamtokea mtu huyu? (Anafungwa na kutupwa gizani.)

   

  1.                  Hebu tujikite mwishoni mwa fungu hili. Hisia gani zinasababisha kulia na kusaga meno? (Ilikuwa rahisi sana kuyakubali mavazi ya mfalme. Anawezaje kufanya kosa kama hilo katika kufanya uamuzi?)

   


  F.                  Soma Mathayo 2:14. Tuliona kuwa kila aliyetajwa kwenye kisa alikaribishwa. Yesu anamaanisha nini kwa kusema “wateule ni wachache?” Mtu mmoja pekee ndiye anayeonekana kushangaa kuikosa harusi. (Jibu pekee lenye mantiki ni kwamba Yesu anarejea (anazungumzia) uchaguzi binafsi. Wageni wote walioalikwa waliukataa mwaliko wa mfalme kwa sababu walikuwa na shughuli nyingi sana kiasi cha kushindwa kuwa wasikivu. Hawakuwa marafiki wa mfalme. Kwa dhahiri hawakutaka kuja harusini kwa sababu waliwatendea vibaya watumwa wake.)

   

  G.                Rafiki, vipi kuhusu wewe? Je, una shughuli nyingi sana, maisha yamekusonga sana kiasi cha kushindwa kushughulikia mwaliko wa kumpokea na kumkubali Yesu kama Bwana na Mwokozi wako? Au, je, u miongoni mwa watu wachache wanaodhani kwamba haki yao inatosha kabisa? Kwa nini usiwe msikivu, ukatubu na kulipokea vazi la haki ya Yesu sasa hivi?

   

  VI.              Juma lijalo: Matukio ya Siku za Mwisho.