Roho Mtakatifu na Tunda la Roho

(Yohana 15, 1 Wakorintho 13, Warumi 14, Wagalatia 6)
Swahili
Year: 
2017
Quarter: 
1
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Juma lililopita tulihitimisha somo letu kwa wazo la kwamba ikiwa tutabatizwa kwa Roho Mtakatifu, maisha yetu yanapaswa kuakisi matunda ya Roho Mtakatifu. Matunda ya Roho Mtakatifu kwa kiasi kikubwa ni mitazamo: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili uaminifu, upole na kiasi. Wagalatia 5:22-23. Kinyume chake ni kwamba upande mwingine, kuishi maisha yanayoongozwa na asili yetu ya dhambi hutusababishia matendo maovu. Wagalatia 5:19-21. Hebu tuchimbue Biblia yetu ili tuone jinsi maisha yetu yanavyoweza kumilikiwa na matunda ya Roho Mtakatifu!

 

  1. Muunganiko wa Mzabibu

 

    1. Soma Yohana 15:1-4. Hapa Yesu hazungumzii chochote kuhusu Roho Mtakatifu. Anamtaja Baba pamoja na yeye (wawili peke yao). Baba ana wajibu gani? (“Kuondoa” matawi yasiyozaa na “kusafisha (kupogolea)” matawi yazaayo matunda.)

 

      1. Je, hiyo inakufanya utetemeke? Nilipokuwa kijana mdogo mimi pamoja na kaka yangu tulikuwa tunapogolea miti ya rasiberi (raspberry). Tulikuwa tunapogolea miti hiyo tukiwa pande mkabala katika mti wa rasiberi. Ninakumbuka kutetemeka (na kupiga kelele) kaka yangu alipozungushia kichongeo (kisu) chake kwenye mojawaapo ya vidole vyangu!

 

      1. Unadhani inamaanisha nini “kupogolewa?” Je, ni kama kile kilichotokea kwenye kidole changu?

 

    1. Angalia kwa makini Yohana 15:3. Inamaanisha nini kuwa “safi?” (Inamaanisha kuwa umepogolewa.)

 

      1. Wanafunzi “walipogolewaje?” (Kwa kutumia maneno ambayo Yesu alikuwa amezungumza nao.)

 

      1. Hii inatusaidiaje kuelewa upogoleaji? (Katika huu mfano, sio jambo la kutisha tulilolipoteza maishani. Badala yake, ni kuyaelewa na kuyafuata maneno ya Yesu ili tuweze kuimarisha maisha yetu ya Kikristo.)

 

    1. Soma Yohana 15:5. Tunakaaje ndani ya Yesu? (Yesu hamaanishi Roho Mtakatifu kimahsusi, lakini hivi ndivyo ambavyo “tunavyokaa” ndani ya Yesu. Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu na hivyo tunao huu muunganiko wa kwenye “mzabibu.”)

 

      1. Unadhani ni jambo la nasibu kwamba Wagalatia 5:22 inarejea “tunda la Roho” na Yohana 15:4-5 inarejea juu ya kukaa ndani ya Yesu na kuzaa “matunda?” (Hapana. Hivyo ndivyo tunavyofahamu Yesu anarejea muunganiko wa Roho Mtakatifu.)

 

 

    1. Soma Yohana 15:6. Hii inaonekana kutia uchungu. Haionekani kama kunoa mtazamo wetu katika msingi wa kulielewa vizuri neno la Mungu. Kama wewe ni mtaalamu wa kupogolea, je, unapogoa “tawi” la namna gani? (Kwa uzoefu wangu mdogo, ninaondoa vitu ambavyo tayari vimeshakufa. Ninafuata mwelekeo uliokwishachukuliwa na mmea, kwa kukatilia mbali chakula cha mmea kwenye maeneo ambayo hayawezi kutumia chakula hicho.)

 

      1. Kuna fundisho gani la kiroho tunaloweza kujifunza kutoka kwenye jambo hili? (“Tukikatiliwa mbali” basi ni kwa sababu tumeshachukua uamuzi wa “kufa.”)

 

      1. Utagundua kwamba nimekuwa nikitumia neno “kupogolewa,” neno ambalo Yesu analitumia kwanza. Yesu anabadilije msamiati wake katika Yohana 15:4, 6 & 7? (Yesu anazungumzia sisi “kukaa” ndani yake. Hii inaonesha kuwa huo ni uchaguzi wetu ikiwa tutaungana na Yesu au la.)

 

    1. Soma Yohana 15:7-8. Yesu anatoa ahadi gani isiyo na kifani kwa wale wanaounganika naye kwa njia ya Roho Mtakatifu? (Kwamba Mungu atakupatia kila unalolitamani.)

 

      1. Vipi kama unatamani kuwa na gari aina ya Mercedes Benz? (Mazungumzo yote yanahusu tunda la Roho. Nadhani Yesu anatuambia kuwa ikiwa kwa mahsusi tutaomba kuwa na upendo, furaha, amani, uvumilivu, au tunda jinginelo, atatupatia!)

 

    1. Soma Yohana 15:9-11. Utakumbuka juma lililopita nilisema kwamba ikiwa lengo lako ni kuzishika amri basi “una lengo la kiwango cha chini kabisa?” Je, hii inakinzana na kile nilichokipendekeza? Kwa mahsusi, je, Yesu anasema kuwa ikiwa tutazishika amri zake, hiyo inaonesha kuwa tunampenda? Hivyo basi, kuzishika amri ni uthibitisho wa upendo wetu kwa Yesu? (Hapana. Hii inazungumzia jambo tofauti kabisa. Yesu alitupatia Amri Kumi (pamoja na amri nyinginezo zote) kwa faida yetu. Amri hizo zilikusudia kuyabariki maisha yetu. Zilitolewa kwa kuwa Yesu anatupenda. Katika Yohana 15:9 Yesu anatuambia “tukae katika pendo lake.” Ikiwa unazifuata amri zake, jambo linaloshiria upendo wake kwetu, basi “unakaa” katika pendo lake.)

 

    1. Soma Yohana 14:15. Hebu subiri kidogo! Je, kifungu hiki hakizungumzii kwa mahsusi kwamba ikiwa unampenda Yesu utazitii amri? (Ukisoma muktadha, Yohana 14:15-21, utaona kwamba Yesu anazungumzia juu ya kumpeleka Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu. Hivyo, Yesu hazungumzii “amri,” anazungumzia juu ya sisi kuishi maisha yanayoongozwa na Roho, na sio maisha yanayoongozwa na tamaa yetu ya dhambi. Tunatakiwa tutazame mbali zaidi badala ya kusaga meno yetu na kudhamiria kuzitii amri.)

 

  1. Kutembea Katika Pendo

 

    1. Hivi karibuni Bob Goff alitembelea kampasi ya Regent. Ikiwa kumbukumbu yangu iko sahihi, alisema, “Ishi katika neema, tembea katika upendo. Kuzishika Amri Kumi ni kutembea katika ulinzi wa upendo wa Mungu. Je, inaweza kumaanisha jambo gani jingine? Hebu tusome 1 Wakorintho 13:4. Ikiwa ulikuwa mvumilivu, mpole, mwenye kuridhika, usiye na majivuno na kujikweza, je, maisha yako yangekuwa na tofauti gani? (Bila shaka ungekuwa mtulivu zaidi, mwenye kuridhika zaidi.)

 

      1. Je, watu wengine wangefurahia zaidi kuwa karibu yako?

 

    1. Soma 1 Wakorintho 13:1-3. Unaweza kuelezeaje kunena kwa lugha, karama ya unabii na imani? (Haya ni matunda ya Roho Mtakatifu.)

 

 

      1. Hii inazungumzia nini juu ya tunda la upendo dhidi ya matunda mengine? (Upendo ni wa muhimu. Upendo ni msingi.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 13:5. Je, unalipiza “kisasi?” je, unatunza kumbukumbu ya watu waliokutukana?

 

      1. Je, unafurahia pale watu wanapokumbuka matendo yako mabaya dhidi yao?

 

    1. Soma 1 Wakorintho 13:6. Inamaanisha nini kufurahi “pamoja na kweli,” kinyume na kufurahi katika uovu? (Tunafurahia pale watu wenye maadili wanapofanikiwa. Tunafurahi pale ukweli unapopata ushindi.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 13:7. Tafakari kila mojawapo ya matendo haya au hii mitazamo. Je, yote haya yanaakisiwa maishani mwako?

 

    1. Soma Warumi 14:12-16. Je, huu ni mfano wa kuishi katika upendo? (Ikiwa huelewi hoja ya Paulo, soma Warumi 14:1-11. Paulo anaandika kwamba kuwa sahihi katika mambo yenye kuibua mjadala si muhimu zaidi ya kuonesha upendo kwa waumini wenzako.)

 

    1. Soma Warumi 14:17-18. Kwa nini Paulo analinganisha kula na kunywa na “haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu?” (Tunapaswa kuwa na mtazamo sahihi maishani. Unawafahamu Wakristo wangapi ambao wanajikita kuangalia kama watu wengine wakula chakula sahihi na kutenda jambo sahihi, badala tu ya kuwapenda watu hao? Hata kama watu wengine wanatenda mambo tunayodhani kuwa si sahihi, je, tunaweza kuangalia namna ya kuonesha upendo bila kutenda dhambi?)

 

    1. Soma Warumi 14:19. Unapomwandikia Mkristo mwenzako kupitia kwenye ukurasa wako wa Facebook, je, unafuata ushauri huu?

 

    1. Soma Wagalatia 6:1-2. Hadi hapa tulipofikia mjadala wetu unatufundisha nini juu ya mtazamo wetu dhidi ya dhambi? Kifungu hiki kinazungumzia nini? (Tunapaswa kusimama dhidi ya dhambi. Lakini, pia tunaamriwa kumrejeza upya mdhambi kwa “roho ya upole.”)

 

      1. Kifungu kinamaanisha nini kinaposema “jiangalie nafsi yako?” (Tunaelekezwa kuonesha upendo na huruma kwa mdhambi. Tunaelekezwa kumrejeza upya kwa roho ya upole. Tunaelekezwa kuonesha busara kwenye masuala yenye kuibua mjadala (utata). Lakini, tunapaswa kuwa makini kwamba akili zetu hazichanganyikiwi juu ya dhambi. Hatupaswi kuvutwa na kuingia kwenye hiyo dhambi.)

 

    1. Soma Wagalatia 6:3-5. Kwa nini Paulo anatuonya dhidi ya majivuno?

 

      1. Je, umewahi kujiuliza kwamba unapojadili dhambi ya mtu mwingine ni kujihusisha zaidi na majivuno yako (kujisifu kwako), badala ya tamaa yako ya “kubeba mizigo” ya mtu mwingine?

 

      1. Hebu subiri kidogo! Paulo anatuambia “tuchukuliane mizigo” (Wagalatia 6:2) na kisha anasema “kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe” (Wagalatia 6:5). Je, huu ni mkanganyiko? (Sidhani. “Mzigo” wa mtu anayejihusisha na dhambi ya wazi ni kuacha kutenda dhambi. Mzigo wa mtu anayejaribu kusahihisha dhambi hiyo ni kuweka pembeni majivuno na kuonesha upendo. Kila mtu ana “mzigo.”

 

 

    1. Hadi kufikia hapa, je, unatikisha kichwa chako na kusema, “Hili ni jambo gumu sana?” Ikiwa ndivyo, kumbuka kwamba kuwa na mtazamo sahihi kunatokana na kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu!

 

    1. Rafiki, ikiwa umechunguza “tunda” lako na kugundua kuwa unapungukiwa, kwa nini usimkaribishe Roho Mtakatifu ili ayaongoze mawazo yako?

 

  1. Juma lijalo: Roho Mtakatifu na Karama za Roho.