Roho Mtakatifu na Karama za Roho

(1 Wakorintho 12, Mathayo 12, 1 Yohana 4)
Swahili
Year: 
2017
Quarter: 
1
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Ni mbaraka wa ajabu kiasi gani kuwa na Roho Mtakatifu! Majuma mawili yaliyopita tulijifunza kwamba Roho Mtakatifu huyaongoza mawazo yetu ikiwa tutamwomba. Juma lililopita tulijifunza kuwa Roho Mtakatifu hubadili mitazamo yetu ili tuweze kuwa na uzoefu mzuri wa upendo, furaha na amani. Juma hili tunajifunza jinsi ambavyo kila mmoja wetu anapewa angalao karama moja kutoka kwa Roho Mtakatifu ili aitumie kujenga mwili wa waumini. Je, unapenda karama? Hebu tuzame mara moja kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi juu ya karama ambazo Roho Mtakatifu anazo kwa ajili yetu!

 

  1. Jambo la Dhahiri

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:1-3. Paulo anatufundisha mada gani? (Karama za roho!)

 

      1. Jambo gani la kwanza ambalo Paulo anataka tulijue kuhusu karama za roho? “Msingi” wa fundisho lake ni upi kuhusu hizi karama? (Sote tunapata ushawishi kutokana na mambo yanayotuzunguka. Paulo hataki “tuingizwe upotevuni” kwa ushawishi mbaya. Kama ilivyo kwa ushawishi sahihi, ushawishi uelezeao endapo mtu anafanyia kazi karama ya Roho Mtakatifu ni jambo jepesi – ikiwa anasema “Yesu ni Bwana” (tofauti na “Yesu alaaniwe”), basi unajua kwamba jambo hili linatoka kwa Roho Mtakatifu.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:4-6. Kwa nini Paulo anatuambia kuwa kuna karama tofauti tofauti, huduma na utendaji kazi, lakini Roho Mtakatifu yule yule ndiye yuko nyuma ya mambo yote hayo? (Hili ni onyo jingine – tusihukumu karama za roho za watu wengine. Kwa kuwa tu mtu fulani ana karama tofauti, huduma tofauti, au utendaji kazi tofauti, hatupaswi kusema kuwa vinatoka kwa Shetani. Roho Mtakatifu anatenda kazi kwa njia tofauti tofauti kwa Wakristo tofauti tofauti.)

 

    1. Soma Mathayo 12:22 na Mathayo 12:24-26. Yesu anasema nini kuhusu wazo la mtu kutumia uwezo wa Shetani kutenda jambo jema? (Yesu anasema kuwa kitendo hicho hakina mantiki.)

 

    1. Soma Mathayo 12:31-32. Hapo awali tulijifunza kutoka kwa Paulo kwamba kutambua kama jambo linatoka kwa Roho Mtakatifu ni kitendo cha dhahiri. Kisha anatuonya tusihukumu pale watu wengine wanapokuwa na karama ambazo tunaweza tusiwe nazo au tunaweza tusizielewe. Kwa nini Yesu anatuambia kuwa hili ni jambo zito sana? (Ikiwa tutaiita kazi ya Roho Mtakatifu kuwa ni kazi ya Shetani, tunakuwa tumemkufuru Roho Mtakatifu! Kibaya zaidi ni kwamba hii ni dhambi isiyosameheka!)

 

 

      1. Kwa nini kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu haisameheki na kufuru dhidi ya Yesu inasameheka? Wote wawili ni sehemu ya Mungu Baba! (Fikiria jambo hili. Yesu alimpeleka Roho Mtakatifu ili akae nasi, atuongoze, abadili mitazamo yetu, na kutupatia karama. Ikiwa hatuwezi kutenganisha kazi ya Roho Mtakatifu na kazi ya Shetani, basi tunalo tatizo kubwa sana!)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:10 na 1 Yohana 4:1. Muda mfupi uliopita tumejifunza kuwa kuhukumu kimakosa katika masuala ya roho (utambuzi au “kutofautisha roho mbalimbali”) ni jambo la hatari sana. Kimsingi, utambuzi wa roho ni karama wapewayo baadhi ya watu. Je, tunapaswa kusita kufanya uamuzi (kuhukumu) juu ya jambo hili, kwa kuwa adhabu ya kukosea kutoa hukumu sahihi ni ya kutisha sana?

 

    1. Soma 1 Yohana 4:2-3. Je, tumefikia kwenye mzunguko kamili hadi pale tulipoanzia kwenye huu mjadala? Yohana anakubaliana na Paulo, kwamba kuzitambua roho ni jambo rahisi na la dhahiri. Hatuna haja ya kuwa na wasiwasi kukosea kuzitambua, ikiwa tutafuata hii kanuni rahisi – ikiwa Roho anasema Yesu anatoka kwa Mungu, kwamba Yesu ni Mungu aliyefanyika kuwa mwanadamu, basi huyo ni Roho Mtakatifu. Ikiwa roho anasema Yesu hatoki kwa Mungu, basi huo ni ushetani. Hili si jambo gumu. Kilicho kigumu kwa dhahiri ni kukubali kwamba Roho Mtakatifu anafanya kazi kwa Wakristo tofauti kwa namna tofauti tofauti!)

 

      1. Ikiwa hii ni rahisi sana, kwa nini tunahitaji karama ya roho ili kuitambua? (Utakumbuka hivi karibuni tulijifunza kisa cha Anania na Safira. Katika Matendo 5:3 Petro anasema kuwa Shetani ameujaza moyo wa Anania. Anania alikuwa anatoa fedha kanisani. Hakuna ushahidi kwamba alitilia shaka kuwa Yesu alitoka kwa Mungu. Pamoja na hayo, mtazamo wake haukuwa sahihi na Petro aliujua mtazamo huo. Roho Mtakatifu alimwambia Petro jambo kuhusu roho ya Anania ambayo haikuwa dhahiri. Nadhani hiyo ni karama ya kuzitambua roho – kutambua asili ya roho ya mwanadamu.)

 

  1. Karama kwa Ajili ya Watu Wote

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:7. Hebu tutafakari kifungu hiki kwa muda mfupi kidogo. Watu wangapi wanapokea “ufunuo” wa Roho Mtakatifu? (“Kila mmoja.” Hiyo inamaanisha kila mtu, ikiwa ni pamoja na wewe!)

 

      1. Kwa nini tunapewa angalao karama moja ya roho? (Kwa nia njema kabisa. Lazima hii inamaanisha kuwa ni kwa ajili ya manufaa ya waumini wenzetu katika Yesu.)

 

    1. Soma Matendo 2:38-39. Hii inatufundisha nini juu ya ahadi ya mtu mmoja mmoja ya karama ya Roho Mtakatifu kwa kipindi cha muda fulani? (Ahadi hiyo inaendelea kwa vizazi na vizazi.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:8-10. Je, inaonekana kuwa sote tunapokea karama za roho zinazofanana? (Hapana. Vifungu hivi vinaonekana tu kuzungumzia kinyume chake, kwamba waumini tofauti tofauti wanapokea karama tofauti tofauti. Sote tunapata karama, lakini ni vigumu karama hizo kuwa za kufanana kwa mtu aliyekaa pembeni yetu.)

 

      1. Endapo ungekuwa unalisimamia kanisa, vifungu hivi ambavyo nimevisoma hivi punde vingekufanya uhitimishe nini? (Kila mtu anayo angalao karama moja ya roho. Karama ni za pekee. Karama zinatolewa kwa manufaa ya kanisa. Hivyo, nitasimamia kazi ya kanisa kwa kumfanya kila mshiriki afanye jambo linaloendana na karama yake.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:11. Nani anayeamua yupi apate karama ipi? (Roho Mtakatifu.)

 

 

    1. Soma Warumi 12:6-8. Nani anayeamua kiasi cha karama za roho tupewazo? (Paulo anasema ni “kwa kadri ya neema tuliyopewa” na anasema “kwa kadri ya imani yake.” Hii inaashiria juhudu za pamoja: katika hali ya kawaida na ya asili Mungu anaamua aina na kiwango cha karama, na tunaweza kuongeza uimara wa karama kwa imani yetu.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:31. Katika 1 Wakorintho 12:27-30 Paulo anaorodhesha karama kadhaa za roho. Kisha anasema, “takeni sana karama zilizo kuu.” Hiyo inazungumzia nini juu ya wajibu wetu katika kupata karama ya roho ya ziada ambayo tungependa kuwa nayo? (Inaashiria kuwa pia tunao wajibu kwenye aina ya karama tunazopewa. Haina mantiki yoyote kwa Paulo kutuambia tutamani karama zingine ikiwa hatuwezi kuzipata.)

 

    1. Angalia tena 1 Wakorintho 12:11. Kama tulivyojadili hapo awali, hii inapaswa kuwa na athari kubwa kwa kanisa. Ikiwa tunasaidia tu kazi ya Roho Mtakatifu, je, hii inaashiria nini kuhusu kazi ya kanisa? (Tunataka Roho Mtakatifu awe kiongozi katika jambo hilo pia. Roho anaratibu na kuongoza.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:12-13. Lengo la taasisi hii ni lipi? (Umoja. Lengo ni kufanya kazi kama mwili mmoja.)

 

      1. Jambo gani lisilojalisha katika hii taasisi? (Kabila letu au hali yetu ya kiuchumi. Mipango ya Roho Mtakatifu ndio jambo linalotuunganisha.)

 

    1. Jiulize ikiwa Paulo analizungumzia kanisa lako mahalia au waumini wote? (Nilipokuwa ninakua, nilifundishwa kwamba kanisa langu lilikuwa ni sehemu ya maboresho ya hivi karibuni kabisa katika mfululizo wa maboresho mbalimbali ya mafundisho katika historia ya kanisa. Kwa mfano, Kanisa la Kilutheri lilikuwa ni maboresho juu ya mafundisho ya Kanisa Katoliki. Hili liliendelea tu na madhehebu yaliyofuatia.)

 

      1. Je, kuna ushahidi wowote wa Kibiblia kwenye wazo hili la siku zote juu ya huu mfululizo wa maboresho ya madhehebu ya makanisa? (Ufunuo sura ya 1-3 inaorodhesha makanisa yanayodhaniwa kuwakilisha historia ya kanisa katika vizazi na vizazi. Lakini, hii si mifululizo ya maboresho. Badala yake, fundisho la Biblia ni kwamba kila muumini (na huenda kila kundi la waumini) linajazilizia sehemu iliyosalia ya mwili wa Yesu.)

 

    1. Soma Warumi 12:3-5. Tunapewa onyo gani endapo tunadhani kuwa karama yetu (au huenda kanisa letu) ina hadhi ya juu kuliko karama (au makanisa) nyingine? (Hili ni suala linalohitaji “hukumu yenye busara.” Nadhani tunapaswa kuzingatia dhambi ya majivuno. Tunatakiwa kuelewa mapenzi ya Mungu kwa ukamilifu kwa kadri inavyowezekana. Tunatakiwa kushiriki na watu wengine uelewa ulioboreshwa zaidi kuhusu mapenzi ya Mungu. Lakini, hatimaye tunatakiwa kutambua kuwa washiriki wengine na makanisa mengine yanaweza kuwa yanafanya baadhi ya mambo kwa ubora zaidi kuliko vile tufanyavyo. Lengo ni umoja katika Kristo.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:27-28. Je, umeshabainisha karama ambayo au ambazo Roho Mtakatifu amekupatia? Je, uligundua kwamba kuwasaidia watu wengine ilikuwa ni karama?

 

    1. Rafiki, ikiwa umempokea Roho Mtakatifu, basi amekupatia angalao karama moja ya roho. Changamoto yangu kwako ni kuitafuta karama hiyo na kisha uitumie!

 

 

Juma lijalo: Roho Mtakatifu na Kanisa.