Roho Mtakatifu, Neno na Maombi

Swahili
(Warumi 8, Waefeso 3, Mathayo 7, Marko 11)
Year: 
2017
Quarter: 
1
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Kuna wakati huwa tunapata ugumu kuhusianisha ahadi za Biblia na uzoefu wetu. Kwa mfano, katika sehemu kadhaa Biblia inatuambia kuwa ikiwa tutamwomba Mungu tutapewa kile tunachokiomba. Angalia, kwa mfano, Mathayo 7:8. Katika Mathayo 18:19 tunaahidiwa kuwa watu wawili wakipatana “katika jambo lolote watakaloliomba” basi “watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.” Je, ahadi hizi zimetendeka kwako mara zote ulipoziomba? Ikiwa jibu ni hapana, kwa nini? Hivi karibuni kabisa, nilisoma mahali kwamba ikiwa nitanufaika kutokana na maombi yangu, basi hiyo itakuwa ni “nia mbaya” itakayobatilisha ombi langu. Bila shaka mwandishi wa kauli hiyo alidhani kwamba kitendo hicho kinaelezea sababu ya baadhi ya maombi yetu kutojibiwa. Nia ya ubinafsi inawezaje kubatilisha maombi yangu Yesu anaponiambia kuwa ninapaswa kuomba kuwa “Utupe leo mkate wetu wa kila siku?” Mathayo 6:11. Kwa dhahiri, tunahitaji kujifunza zaidi juu ya hii mada! Hebu tuchimbue somo letu kuhusu Roho Mtakatifu na maombi!

 

 1. Roho Mtakatifu na Maombezi

 

  1. Soma Warumi 8:26-27. Hii inatufundisha nini juu ya umahiri wetu katika kufahamu nini cha kuomba? (Vifungu vinasema kuwa hatujui kile tunachotakiwa kukiomba.)

 

   1. Mkristo mwenye kutumia akili ya kawaida anaweza kuhitimisha kwamba ikiwa Mungu haonekani kujibu maombi yake, basi lazima tatizo litakuwa upande wetu kwa namna moja au nyingine. Je, kifungu hiki kinaonekana kuthibitisha tatizo hilo?

 

   1. Roho Mtakatifu anatusaidiaje kuomba maombi “sahihi?” (Anatuombea.)

 

   1. Jambo gani linatujia mawazoni mwetu tunapozungumzia maombezi ya wanadamu? (Kwa dhahiri, ninawafikiria wanasheria. Mwanasheria anafahamu, kutokana na mafunzo na uzoefu, jinsi ya kuyaweka maombi ya mteja wake katika mlolongo sahihi. Tunaambiwa kuwa Roho Mtakatifu ana namna anayotumia kufanya mawasiliano ambayo ina ufanisi mkubwa zaidi kuliko maneno.)

 

    1. Unawezaje kuita maombezi ya Roho Mtakatifu “kuugua?” Hilo linawezaje kuwa na ufanisi mkubwa kuliko maneno?

 

    1. Kwa nini tunamhitaji Roho Mtakatifu ili kuyaboresha maombi yetu? Kwani Mungu haelewi? Kwani Roho Mtakatifu sio Roho wa Mungu?

 

   1. Nani ambaye ni “na Yeye” katika Warumi 8:27 aichunguzaye mioyo yetu? (Soma Yeremia 17:10. Nadhani inamzungumzia Mungu Baba.)

 

 

  1. Angalia tena sehemu ya mwisho ya Warumi 8:27. Ukweli kwamba Mungu aijua nia ya Roho Mtakatifu una msaada gani kwenye maombi yetu? (Mungu anaijua mioyo yetu na anafahamu jinsi Roho Mtakatifu anavyofikiri. Mambo yote haya yanatusaidia kujua nini cha kuomba na jinsi ya kuomba. Kwa nini? Roho Mtakatifu anagusa hiyo misukumo yetu inayoumba maombi “sahihi,” kisha anaiwasilisha kwa Mungu kwa namna inayoendana na mapenzi ya Mungu. Hii inaonesha kwamba tatizo halitokani na uelewa wa Mungu, bali linatokana na asili ya maombi yetu.)

 

   1. Ikiwa tunadhani kwamba Mungu hajibu maombi yetu, je, tatizo linaweza kuwa ni kwamba hatumwombi Roho Mtakatifu msaada?

 

  1. Soma Waefeso 3:16-17. Jambo gani ambalo linaimarisha “utu wetu wa ndani” pamoja na kumruhusu Yesu kukaa ndani ya mioyo yetu? (Roho Mtakatifu.)

 

  1. Soma Waefeso 3:17-19. Yesu akaapo ndani yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu, anatusaidia nini katika kuuelewa upendo wa Mungu? (Kukaa kwa Yesu ndani yetu hutusaidia kuelewa asili ya upendo wa Mungu.)

 

  1. Soma Mathayo 7:9-11. Hii inatuambia nini juu ya njia ya Mungu ya kujibu maombi yetu? (Je, unawapatia watoto wako kila wanachokuomba? Hapana. Unafahamu kuwa kuwapatia baadhi ya vitu inaweza kuwa na madhara. Unafahamu kwamba muda wa karama yako ni wa muhimu.)

 

  1. Soma Mathayo 7:12. Je, Yesu anatoa kauli za kweli bila kufuata utaratibu maalumu? Au, je, hii inaungana na mada ya kumwomba Mungu kutupatia haja zetu? (Kauli ya Yesu inaonekana kuhusiana kwa namna mbili. Kwanza, uamuzi wa Mungu juu ya maombi ya kuyajibu inaakisi upendo wake katika hali chanya – kama ambavyo kuwatendea watu wengine jinsi ambavyo tungependa tutendewe kunavyoakisi upendo. Pili, maombi yetu yanatakiwa kuhusisha athari zake kwa watu wengine.)

 

  1. Hebu tupitie tena suala la Mungu kujibu maombi yetu. Tumejifunza kwamba Mungu anajibu maombi yetu kama mzazi mwenye upendo ajibuvyo. Pia tumejifunza kuwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu anatusaidia kuelewa namna ya upendo wa Mungu. Tukichukulia hayo mambo mawili ya muhimu, Roho Mtakatifu anatusaidiaje kwa maombi yanayojibiwa? (Kwa kuuelewa upendo wa Mungu, tunaelewa kile tunachopaswa kukiomba kinachoendana na upendo wake kwetu.)

 

 1. Roho Mtakatifu na Uombaji

 

  1. Soma Mathayo 7:7-8. Je, kuna vigezo vyovyote kwenye hizi ahadi? (Ndiyo, kwa maana ya kwamba tunatakiwa kuomba, kutafuta na kubisha. Inamaanisha kuwa tunatakiwa kuchukua hatua.)

 

  1. Soma Mathayo 18:19-20. Kwa nini ni muhimu sana kwa watu wawili kukubaliana? (Ikiwa unatakiwa kumwambia mtu mwingine kile ulicho nacho mawazoni mwako, kinaweza kufanya maombi yako yawe na kiasi. Ikiwa unataka mtu wa pili akubali, huo ndio ukomo wa maombi yasiyo na mantiki.)

 

   1. Kwa nini Yesu anaongezea kwa kusema kwamba Roho Mtakatifu atakuwepo mahali ambapo watu wawili au watatu watakuja pamoja katika jina la Yesu? (Uongozi wa Roho Mtakatifu kwenye suala la maombi yetu, kama tulivyojadili hivi punde, ni jambo la muhimu sana.)

 

  1. Soma 1 Yohana 5:14-15. Je, kauli hii ya kwamba “sawasawa na mapenzi yake” ni kigezo cha maombi kujibiwa?

 

 

   1. Utaona kwamba 1 Yohana 5:15 inaonekana kusema jambo tofauti, kwamba Mungu anasikia “chochote tuombacho.” Je, kuna ukinzani kwenye hivi vifungu viwili? Kwanza tunaambiwa kuwa Yesu anasikia pale tu tunapoomba sawasawa na mapenzi yake, kisha tunaambiwa kuwa anasikia chochote kile bila kujali kile tumwombacho? (Namna ya pekee kusoma vifungu hivi ni kwamba Yesu “anasikia” maombi yanayoendana na mapenzi yake. Kwa yale maombi yanayoendana na mapenzi yake, anayajibu kama yalivyoombwa.)

 

   1. Hebu tuwe wahalisia hapa. Nakumbuka kuomba kwa hamasa tena kwa kurudiarudia kwamba wazazi wangu waishi hadi kufikisha umri wa miaka 85. Hilo halikutokea. Baba yangu alifariki akiwa na umri wa miaka 70 na mama yangu alifariki akiwa na umri wa miaka 80. Maombi yangu kwa wazazi wangu kurefushiwa uhai yanatofautianaje na mapenzi ya Mungu? (Sina nafasi ya kuelezea jambo hili kwa kina zaidi. Lakini, kwa kuwa sasa ninatafakari matukio haya, ninaamini kuwa muda wa Mungu ulikuwa sahihi na mkamilifu, kutokana na ukweli kwamba tunaishi kwenye ulimwengu uliojaa dhambi na usio mkamilifu. Endapo ningekuwa ninafahamu habari za mwanzo hadi mwisho (kama ambavyo angalao ninafahamu kwa sasa), ningekubaliana na muda wa Mungu kutenda mambo. Alitoa jibu la upendo mkubwa sana kwa kuzingatia matamanio yetu sisi watatu.)

 

 1. Roho Mtakatifu na Imani

 

  1. Soma Marko 11:22-24. Unaweza kufikiria jambo lolote lisilo na maana zaidi tofauti na kuung’oa mlima na kuutupa baharini? Baada ya mjadala wote huu wa jinsi Roho Mtakatifu anavyotusaidia kujua kilicho bora tunachoweza kumwomba Mungu, kwa nini Yesu anatumia mfano kama huu?

 

   1. Milima inawakilisha nini katika maisha halisi? (Milima ni vizingiti. Kuna ugumu kupita milimani. Milima ni changamoto.)

 

   1. Asili ya “changamoto” ya mlima inatuambia nini juu ya kile ambacho Yesu anakisema hasa kwenye kifungu hiki? (Bila kujali ukubwa wa tatizo maishani mwako, linaweza kutatuliwa kwa njia ya maombi yako.)

 

   1. Yesu anaposema “asione shaka moyoni mwake, ila aamini” je, anazungumzia jambo gani? (Hii inaturejesha kwenye uhusiano na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu ndiye afanyaye mambo haya yawezekane.)

 

  1. Soma Marko 11:25. Je, hiki ni kigezo kingine ili maombi yetu yaweze kujibiwa? (Yesu anakifanya kuwa kigezo cha kusamehewa. Yesu anasema jambo hilo hilo katika Mathayo 6:12. Hata hivyo, Yesu hahitimishi (hasemi kwa dhahiri kabisa) kwamba hiki ndicho kigezo cha maombi kujibiwa.)

 

   1. Ikiwa hicho si kigezo cha kujibiwa kwa maombi, kwa nini Yesu anakitaja hapa? (Kumbuka mjadala wetu wa awali jinsi Roho Mtakatifu anavyozingatia misukumo na mawazo yetu bora tunapoomba kwa msaada wake. Yesu anafanya vivyo hivyo hapa, anaizingatia misukumo yetu bora.)

 

  1. Je, unahisi kwamba unayo majibu ya sababu za kutojibiwa kwa baadhi ya maombi, na wakati huo huo Mungu anatupatia ahadi pana na tele kuhusu maombi? (Vifungu tulivyojifunza vinaashiria kuwa upendo ndio msingi wa majibu yote kwa maombi yetu. Mungu anatupatia majibu chanya tunapomwomba na maombi hayo yanalenga kuwa na manufaa bora kwetu. Mungu pia anaahidi Roho wake Mtakatifu kutupatia huo utambuzi, na kuamsha misukumo yetu, ili kuomba mambo yaliyo bora kabisa.)

 

 

  1. Rafiki, unamhitaji Roho Mtakatifu! Miongoni mwa mambo mengine, unamhitaji Roho Mtakatifu ayaongoze na kuyabariki maisha yako ya maombi. Je, utaendelea kumwomba Roho Mtakatifu mara zote ayaongoze mawazo yako na maombi yako?

 

 1. Juma lijalo: Kumhuzunisha na Kumpinga Roho.