Siku ya Bwana

Swahili
(2 Petro 3:1-18)
Year: 
2017
Quarter: 
2
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Mambo yamebadilika. Usiku uliopita niliwaambia wanafunzi wangu darasani kwamba baadhi ya mambo yamebadilika sana katika kipindi cha miaka 30-40 iliyopita. Mojawapo ya mambo hayo ni mtazamo juu ya uvutaji wa sigara. Nakumbuka, miongo kadhaa iliyopita, nilikuwa mahakamani kwenye kesi pakiwepo na mahakimu na wanasheria kadhaa. Sio tu kwamba mimi pekee ndiye nilikuwa ninawawakilisha wateja wangu, bali pia mimi pekee ndiye sikuwa nikivuta sigara. Anga lilikuwa la bluu kutokana na moshi wa sigara. Petro anatuambia kuwa katika siku za mwisho watu watasema “vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo tangu mwanzo wa kuumbwa.” Kwa hakika haiwezekani kuwa “vitu vyote.” Mtu gani huyu asiye na uelewa asemaye hivyo? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kuhusu madai ya watu “wasiobadilika!”

 

 1. Manabii Wenu

 

  1. Soma 2 Petro 3:1-2. Utakumbuka kuwa Petro anatumia unabii wa Agano la Kale kuthibitisha kwamba Yesu ni Mungu. Petro anaongezea nini kwenye haya mamlaka? (“Manabii wenu.” Sasa Petro anasema kuwa mafundisho ya Yesu kwa mitume yanajenga aina nyingine ya mamlaka ya kidini. Sasa Petro pamoja na mitume wengine wamesimama katika kiwango kimoja na manabii wa Agano la Kale – wanawasilisha maneno ya Mungu.)

 

  1. Soma 2 Petro 3:3. Petro anaandika nini hapa? (Kwa dhahiri huu unaonekana kufanana na unabii wa siku za mwisho. Unaweza kuona mageuzi anayoyafanya Petro? Sasa anatupatia unabii wake mwenyewe wa siku zijazo – siku ambazo anadai kuwa na mamlaka nazo kama mtume wa Yesu.)

 

 1. Hukumu ya Siku ya Mwisho

 

  1. Soma 2 Petro 3:4-6. Je, mambo yapo vile vile kama yalivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa? (Hapana. Petro anasema gharika liliingilia kati na kubadili kila kitu. Petro anapingana, wala hakubaliani, na wale wanaosema “hakuna kilichobadilika.” Kimsingi Petro anazungumzia mabadiliko makubwa, sio mitazamo inayohusu uvutaji wa sigara.)

 

   1. Inamaanisha nini kusema “kusahau kwa makusudi?”

 

    1. Je, hilo linatokea leo? (Hivi karibuni nilitazama makala inayohusu maelezo ya Mwanzo na habari za mtu asiyekubali kupokea mambo mapy Inaonekana wanasayansi wanataka kutunga kila sababu juu ya kutokubali mambo mapya tofauti na gharika lililotokea duniani kote. Wamelisahau gharika kwa makusudi.)

 

    1. Kwa nini wanasayansi wanaepuka jambo la dhahiri – historia ya kale maarufu sana inayohusu gharika lililotokea duniani kote ambalo pia lingeweza kuweka kumbukumbu ya jambo jipya tofauti? (Kwa sababu maelezo hayo yanasema kuwa Mungu aliumba gharika ili kuwaadhibu wanadamu kutokana na dhambi zao. Hawataki kukiri kipengele cha kisa hicho.)

 

 

   1. Maelezo ya gharika yanatufundisha nini juu ya dhambi? (Kwamba Mungu aliingilia kati na ataendelea kuingilia kati mambo yetu katika dunia hii ili kukabiliana na dhambi.)

 

  1. Angalia tena 2 Petro 3:5. Petro anarejea tukio gani? (Tukio la Uumbaji!)

 

   1. Soma 2 Petro 2:10-1 Unakumbuka nilipendekeza kwamba kuwakashifu viumbe wa mbinguni inajumuisha kuzikataa siku sita halisi za uumbaji zinazochukua nafasi ya nadharia ya uibukaji inayojumuisha mamilioni ya miaka? Petro anazungumzia nini kuhusu maelezo ya Uumbaji? (Anasema kuwa Mungu alizungumza na dunia ikapata kuwepo “kutokana na maji,” na kwamba Mungu aliuangamiza ulimwengu kwa kutumia “haya maji.” Matukio yote mawili yanaakisi uwezo na mamlaka ya Mungu.)

 

  1. Unawafahamu Wakristo wanaosema kuwa wanaiamini Biblia, hawaamini tu mwanzo wa kuumbwa katika kitabu cha Mwanzo? Je, inaleta mantiki kudai kuwa Mkristo na unayeshadadia dhana ya uibukaji?

 

   1. Soma Mathayo 19:4-6 na 1 Wakorintho 15:45-48. Hizi kauli mbili zinatufundisha nini kuhusu maelezo ya uumbaji? (Yesu pamoja na Paulo sio tu kwamba waliamini na kunukuu kisa cha Uumbaji, bali pia teolojia yao imejengwa juu ya kisa hicho. Tunao Yesu, Paulo na Petro ambao wote wanaamini maelezo ya Uumbaji na wanadhani kuwa maelezo hayo ni ya kuaminika sana kiasi kwamba wanajenga hoja za kiteolojia juu yake.)

 

  1. Soma 2 Petro 3:7. Jambo gani linatupatia ujasiri na uthibitisho kwamba Yesu anakuja tena kutoa hukumu kwa waovu na kuiangamiza dunia na mbingu ya sasa? (Petro anatuambia kuwa na imani na maelezo ya Uumbaji na gharika (2 Petro 3:5-6), hutupatia ujasiri kwamba kwa neno la Mungu waovu wataangamizwa.)

 

 1. Kuchelewa

 

  1. Soma 2 Petro 3:8-9. Petro anatoa sababu gani za kuchelewa kwa Yesu kurudi Mara ya Pili? (Anatusubiria kwa uvumilivu mkubwa ili tuifikilie toba. Yeye anauzingatia muda kwa namna tofauti.)

 

   1. Hebu tuangalie sababu ya “kuvumilia ili kuifikilia toba.” Hii inazungumzia nini kutuhusu na uwezo wetu wa kushawishi muda wa ujio wa Mara ya Pili? (Inaashiria kwamba tunaweza kushawishi muda wa kuja kwake. Kama Mungu anatusubiria, tutakapochukua hatua naye atachukua hatua.)

 

  1. Soma 2 Petro 3:10. Wezi wanakuja wakati gani? (Wanakuja muda wanaotarajia kwamba huwatarajii.)

 

   1. Je, Petro anatupatia ujumbe mchanganyiko? Anasema kuwa muda wa Mungu ni tofauti, Mungu atakuja muda tusiotarajia, na tunaweza kushawishi muda wa ujio wa Mara ya Pili kwa kuwa Mungu anatusubiria. Je, huu ni mkanganyiko tu? Au, unaweza kutambua ujumbe wa wazi kutoka kwenye maelezo hayo? (Chukulia kwamba hatutabiriki katika kuifikilia toba. Ikiwa hali ndio hiyo, basi ujumbe hauna mkanganyiko. Ujumbe uliopo ni kwamba hatujui lini Yesu atakuja tena kwa sababu hatutabiriki.)

 

 1. Utayari

 

 

  1. Soma 2 Petro 3:11-12. Je, umejiandaa kwa wezi nyumbani kwako? (Mimi nimejiandaa. Ukweli kwamba muda wa ujio wa Mara ya Pili haujulikani inamaanisha kwamba tunatakiwa kujitayarisha nyakati zote.)

 

   1. Tunajiandaaje kwa ujio wa Mara ya Pili? Je, Petro anatuambia kuwa tunatakiwa “kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu” ili tuweze kuokolewa? Je, hicho ndicho kiwango kwa ajili ya hukumu? (Hiyo ni njia ya kuharakisha ujio wa Mara ya Pili! Tunaokolewa kwa neema na si kwa matendo yetu. Lakini, tunatakiwa pia kuwa werevu. Kumtii Mungu hutupatia maisha bora. Kumheshimu Mungu hutoa mfano duniani wa kwa nini kumchagua Mungu ni jambo bora. Huu ushuhuda unaharakisha ujio wa Mara ya Pili.)

 

   1. Jambo gani linaitokea dunia? (Kila kitu kinaungua na kuangamizwa.)

 

    1. Hii inaashiria nini kuhusu maandalizi yetu ya ujio wa Mara ya Pili? (Tunatakiwa tuzingatie kwamba tofauti na uwekezaji wetu kwa watu, hakuna kitu tunachokimiliki kitakachopon)

 

  1. Soma 2 Petro 3:13. Habari njema kuhusu “vitu” vyetu ni ipi? (Tutakuwa na makao mapya. Mbingu na nchi mpya zilizojaa watu wenye haki.)

 

  1. Soma 2 Petro 3:14-15. Dunia inajenga hoja juu ya jambo gani inapotoa madai yake ya “kutokuwepo kwa mabadiliko?” (Inajenga hoja kwamba mara zote hapatakuwepo na mabadiliko. “Kutokuwepo kwa mabadiliko” kunamaanisha kuwa kamwe Yesu hatakuja.)

 

   1. Petro anasema kuwa ucheleweshaji huo unamaanisha nini? (Unamaanisha kuwa tunayo fursa kubwa ya kuokolewa. Petro haoneshi tu kwamba hoja ya “kutokuwepo mabadiliko” haiko sahihi, bali pia anasema kuwa ucheleweshaji ni kwa faida yetu.)

 

  1. Petro anamnukuu Paulo kwamba anamuunga mkono. Soma Waefeso 2:3-5. Paulo anazungumzia nini kuhusu neema ya Mungu? (Paulo anakubali kwamba Yesu anatuonesha neema na anataka kutubadilisha.)

 

   1. Angalia tena 2 Petro 3:14. Petro anasema “fanyeni bidii ili mwonekane katika amani [na Mungu].” Paulo analielezeaje jambo hili katika Waefeso 2:3-5? (Hapo awali tulikuwa vitani na Mungu. Kwa asili “tulikuwa watoto wa hasira.” Lakini, kwa neema Yesu alituokoa – ili kwamba tuwe na amani na Mungu, na si vitani naye.)

 

   1. Soma Waefeso 2:8-10. Je, hii inatusaidia kujua anachokimaanisha Petro anaposema “fanyeni bidii?” (Hatufanyi bidii (hatufanyi kazi) ili tuokolewe, kwa kuwa wokovu haupatikani kwa njia ya matendo. Badala yake, “tuliumbwa katika Kristo Yesu ili kutenda matendo mema.” Unapotembea katika njia ya haki, matendo yako mema yanapaswa kuongezeka.)

 

  1. Soma 2 Petro 3:16. Unadhani Petro anafikiria nini mawazoni mwake anapoandika kuwa baadhi ya watu “huyapotoa” maandiko ya Paulo? (Nahisi hii inahusiana na dhana inayosema kwamba kwa kuwa tunaokolewa kwa neema, matendo yetu hayana maana yoyote. Matendo hayatupatii wokovu, ni zawadi kutoka kwa Mungu. Lakini, yana nafasi kubwa katika ufanisi wetu kwenye pambano kati ya wema na uovu. Yanahusika sana katika kuishi maisha yenye furaha zaidi.)

 

 

  1. Soma 2 Petro 3:17-18. Kosa la watu wasiotii sheria ni lipi? Jambo gani linaweza kutufanya tuanguke? (Kuamini kwamba Mungu hana mkono wake kwenye mambo ya wanadamu. Dhana ya kwamba Mungu si Muumbaji na hatakuja tena kutoa hukumu. Dhana ya kwamba Mungu hayuko hai katika pambano kati ya wema na uovu.)

 

  1. Rafiki, usikate tamaa. Mtumaini Mungu katika mambo madogo maishani mwako na katika mambo makubwa duniani ambapo Mungu anaongoza mustakabali wa mambo yajayo. Ishi maisha yaliyo muhimu katika pambano kati ya wema na uovu. Kwa nini usidhamirie sasa hivi kutumaini na kutii?

 

Juma lijalo: Mada Kuu Katika Petro wa 1 na 2.