Paulo : Nabii kwa Mataifa

Swahili
(Matendo 6, 7, 9, 11, 15 & 22)
Year: 
2017
Quarter: 
3
Lesson Number: 
1

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tunaanza somo jipya juu ya mojawapo ya vitabu vya muhimu sana vya Agano Jipya! Wakati vitabu vyote vya Biblia ni vya muhimu, kitabu cha Wagalatia ni cha muhimu sana katika uelewa sahihi wa wokovu wetu. Hata hivyo, kabla hatujachimba zaidi kwenye muktadha halisi wa kitabu cha Wagalatia, hebu kwanza tuangalie habari za mtu aliyekiandika. Kuuelewa muktadha huu inatusaidia kuelewa kitabu cha Wagalatia vizuri zaidi!

 

 1. Kuutangaza Ufalme?
  1. Soma Matendo 7:57-60. Huu ndio utangulizi wetu wa kwanza kwa Paulo. Anaonekana kama ni karani wa mahakama. Je, hivyo ndivyo tunavyopaswa kuhitimisha? (Hapana. Kwa dhahiri mashahidi wanaompiga Stefano kwa mawe wanamfahamu Sauli, maana Sauli ni mmojawao katika kundi lao kwa sababu wamemwachia nguo zao wanapoanza shughuli pevu ya kumwua Stefano.)

 

  1. Soma Matendo 6:8-10. Kundi hili liko makini kiasi gani linapojadiliana na Stefano? (Hawawezi kushindana naye.)

 

  1. Soma Matendo 6:11-14. Unaposhindwa hoja na mantiki ya Stefano katika kujadiliana, basi unaamua tu kusema uongo ili aweze kuuawa. Watu wa aina gani wanafanya kitendo kama hicho??

 

   1. Utakumbuka inaonekana kwamba Sauli anawafahamu hawa mashahidi. Je, wote kwa pamoja ni washiriki wa “Sinagogi la Mahuru?” (Kuna mjadala unaoendelea kuhusu kundi hili kwamba ni la namna gani, lakini kwangu mimi hii inaashiria kuwa Sauli ni mmojawao. Angalao baadhi yao katika kundi hilo wanadhani kuwa falsafa kadhaa za kidini ni za muhimu zaidi kuliko uaminifu.)

 

   1. Angalia tena Matendo 6:14. Utakumbuka kwamba mashtaka dhidi ya Stefano ni kwamba yeye ni sehemu ya kundi linalotaka “kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.”

 

  1. Soma Matendo 8:3 na Matendo 9:1-2. Je, Sauli amejiingiza kwenye vuguvugu la kuwaangamiza Wakristo? (Sasa haangalii tena nguo, bali ni kiongozi kwani anaongoza utekelezaji wa mateso kule Dameski.)

 

  1. Soma Matendo 9:3-5. Ikiwa unafahamu tu kile tulichokisoma kumhusu Sauli hadi hapa tulipofikia, unaweza kuhitimisha kwamba alikuwa mtu mbaya? Tukio hili linatuonesha nini? (Mungu ana maslahi na Sauli. Hata kama tunaweza kuona upande mbaya wa Sauli, wito wa Yesu hapa ni wa kidini. Yesu anajifungamanisha na wale wanaoteswa. Yesu anaamini kuwa tatizo la Paulo lina kasoro ya kiteolojia, sio kasoro ya kitabia.)

 

   1. Kitu gani kingekuwa kinaendelea mawazoni mwako endapo ungekuwa Sauli?

 

 

  1. Soma Matendo 9:6-9. Kwa nini hali? (Sauli anapitia msongo mkubwa sana wa mawazo. Sio tu kwamba amepoteza uwezo wake wa kuona, ametambua kwamba anamdhuru Mungu, na si kwamba anamsaidia.)

 

  1. Soma Matendo 9:10-11. Unadhani Sauli anaomba juu ya nini? (Je, hii inaondosha fikira yako juu ya upande mbaya wa Sauli? Katika wakati wenye msongo halisi, anamgekia Mungu.)

 

  1. Soma Matendo 9:12-14. Anania anawaza nini juu ya kumrudishia Sauli uwezo wake wa kuona? (Anania ana uhakika kuwa Sauli ni mtu mbaya. Sauli ni adui wa injili. Anania anadhani kwamba Mungu haujui huu ukweli ulio wa muhimu. Sasa tunafahamu kwamba angalao sehemu ya maombi ya Sauli yanahusiana na kurejeshewa hali yake ya uoni.)

 

 1. Kazi Mpya

 

  1. Soma Matendo 9:15. Mungu ana kazi (utume) gani kwa Sauli? (Ni utume (kazi) mkubwa sana.)

 

  1. Soma Matendo 9:16. Unadhani Sauli ataichukuliaje kazi yake na hii kauli kwamba atapaswa kuteseka? (Kuna mantiki ya haki katika jambo hili. Sauli amekuwa akisababisha mateso miongoni mwa watu wa Mungu. Ninayo mashaka kidogo kwamba Sauli anataka kuutangaza Ufalme wa Mungu, lakini amekuwa akifanya hivyo kwa kutumia mbinu isiyo sahihi. Mungu anairejesha kazi (utume) ya Sauli kwenye njia sahihi.)

 

  1. Soma Matendo 9:17-19. Jambo gani ni la muhimu katika kazi mpya ya Sauli? (Anahitaji “kujazwa Roho Mtakatifu.”)

 

   1. Unadhani kwa nini Yesu alimpofusha Sauli? Kwa nini hakumfanya punda wake azungumze naye? Kwa nini asitumie maono? (Tafakari lugha ya ishara katika jambo hili. Kiuhalisia, Sauli haioni nuru. Badala yake, anaitesa nuru – kwa kujaribu kuizima. Katika hili tukio moja, sasa Sauli anauona ukweli. Magamba yanaanguka kutoka machoni mwake kiuhalisia na kiroho.)

 

   1. Kwa nini Sauli alibatizwa? Soma maelezo ya baadaye ya Sauli kuhusu tukio hili katika Matendo 22:13-16. Anataka dhambi zake zioshwe. Sauli ameshawishika kwamba alikuwa kwenye njia isiyo sahihi, na ameshawishika kumhusu Yesu.)

 

    1. Anania anatabiri unabii gani kuhusu Sauli na Yesu? (Atamwona Yesu (“Mwenye haki”) na kufundishwa naye.)

 

   1. Kwa nini Sauli anakula sasa hivi? (Mtafaruku wa mawazo, kiwewe, hatia, na mgogoro sasa vimetatuliwa. Anaweza kula.)

 

  1. Soma Matendo 22:17-20. Je, Sauli anabishana na Yesu? (Sauli anaamini kwamba historia yake kama mtesaji itawafanya wale waliokuwa wanakubaliana naye hapo awali waongoke na kuingia kwenye Ukristo. Yesu anamwambia Paulo kwamba hayuko sahihi kuhusu jambo hili.)

 

  1. Soma Matendo 22:21. Kazi ya kwanza ya Sauli ni ipi? (Kuondoka Yerusalemu na kwenda kuwahubiri watu wa Mataifa.)

 

   1. Je, jambo kama hili limekutokea? Unadhani kwamba una vigezo bora kabisa kuweza kufanya kazi fulani ya Mungu, na Mungu anakutuma kwenye jambo jingine tofauti kabisa?

 

 

  1. Soma Matendo 11:19-21. Mauaji ya Stefano yameitangazaje injili? (Yaliwafanya Wakristo wa awali waondoke Yerusalemu na kueneza ujumbe.)

 

  1. Soma Matendo 11:22-24. Viongozi wa Wakristo wanamtuma nani Antiokia kuitangaza injili miongoni mwa Wayunani? (Barnaba.)

 

  1. Soma Matendo 11:25-26. Je, Mungu alikuwa anamtumia Sauli hata kama alisaidia katika mauaji ya Stefano? (Soma Warumi 8:28. Mungu hakutaka Stefano auawe, lakini Mungu anafanya jambo zuri kutokana na hili tukio la kutisha kwa kulitumia kutangaza injili. Sasa tunajifunza kwamba hili janga linajenga msingi kwa kazi ya Sauli ya kuwaongoa Wayunani na kuwaleta katika injili.)

 

 1. Pambano la Wazi

 

  1. Soma Matendo 15:1. Kwa mujibu wa hawa watu, wokovu unategemeana na jambo gani? (Tohara.)

 

   1. Soma Mwanzo 17:9-1 Je, ni haki kuliita jambo hili “desturi iliyofundishwa na Musa?” (Watu wa Uyahudi wangeweza kutumia maneno makali zaidi – tohara ni ishara iliyoanzishwa na Mungu inayohusu agano kati ya Mungu na mwanadamu.)

 

  1. Soma Matendo 15:2-3. Kwa nini Sauli (sasa anaitwa Paulo) anakuwa upande wa wale waliopinga tohara? Kwa nini Wakristo wa Antiokia wanamtuma Paulo kujenga hoja dhidi ya tohara? (Paulo amekuwa akifanya kazi na Wayunani ili kuwaongoa. Unaweza kuona jinsi mazingira yanavyokusaidia kuelewa tatizo vizuri zaidi – na kuliangalia kwa huruma? Paulo anabadilika kutoka kuwa mtu anayedhani kuwa kubadili “desturi walizopewa na Musa” (Matendo 6:14) kunastahili adhabu ya kifo, hadi kuwa mtu anayetaka kubadili desturi hizo kutokana na hitaji la kuwaongoa watu wa Mataifa.)

 

  1. Soma Warumi 4:11. Hapa Paulo anasema kuwa tohara ni kitu gani? (“Muhuri wa haki.”)

 

   1. Je, hii inamaanisha kwamba watu wanaoshadadia tohara walikuwa sahihi kabisa? (Ukiangalia muktadha katika Warumi 4:9-12, Paulo anajenga hoja kwamba Ibrahimu alihesabiwa haki kwa imani kabla na baada ya kutahiriwa kwake. Hii ilikuwa ishara ya uwepo wa uhusiano sahihi na Mungu.)

 

  1. Soma Wakolosai 2:11-12. “Tohara” mpya ni ipi kwa mujibu wa Paulo? (Ubatizo!)

 

   1. Kwa kuwa ubatizo ulipaswa kufanyika siku nane baada ya kuzaliwa (Mwanzo 17:12), hii inaashiria nini juu ya tohara ya watoto wachanga? (Nilikuwa ninadhani kuwa ubatizo wa watoto wachanga ikifuatiwa na “kipaimara” mtoto anapokuwa mkubwa kiasi cha kuwa na uelewa wa mambo ni kinyume kabisa na Biblia. Ulinganifu huu kati ya tohara na ubatizo unanisaidia kuelewa kitendo hicho.)

 

  1. Soma Matendo 15:4-5 na Matendo 15:12. Kisha soma uamuzi wa Yakobo katika Matendo 15:19-21. Paulo anajenga hoja gani yenye ushawishi dhidi ya kutohitajika kwa tohara? (Uwezo wa Mungu ulidhihirishwa katika kazi yao kuwaongoa watu wa Mataifa.)

 

 

   1. Fikiria jambo hili kimantiki. Tunaamini Roho Mtakatifu anatenda kazi katika mioyo ya wale wanaoongolewa. Lakini, pia tunadhani kuwa waongofu wapya wanapaswa kubadilika baada ya kuongolewa. Uamuzi wa Yakobo umejengwa juu ya jambo gani? (Soma tena Matendo 15:19.  Yakobo anasema kuwa ni sahihi kuvunjavunja vizingiti vinavyowazuia watu wasimgeukie Mungu.)

 

    1. Utachora msitari mahala gani katika hili wazo? Je, panapaswa kuwepo na msitari wowote?

 

  1. Rafiki, yatafakari maisha ya Sauli. Alikuwa mnazi (shabiki) aliyekuwa radhi kuwadhuru watu ili kuitakasa dini ya Kiyahudi. Mungu aliyabadilisha maisha yake, na kumfanya (sasa Paulo) kuwa mtetezi kwa kuvunjavunja vitu ambavyo hapo awali alidhani kuwa vinamtakasa mtu katika muktadha wa kidini. Vipi kuhusu wewe? Je, unafanana zaidi na Sauli au Paulo?

 

 1. Juma lijalo: Mamlaka ya Paulo na Injili.