Somo la 9: Wito wa Paulo wa Kichungaji

Swahili
(Wagalatia 4:12-20)
Year: 
2017
Quarter: 
3
Lesson Number: 
9

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, umewahi kuwa na marafiki ambao kwa ghafla tu si marafiki wako tena? Katika zama hizi za Facebook, hilo linatutokea sisi sote! Huenda kwangu mimi uzoefu mchungu kabisa wa kirafiki ulitokana na sababu za kiteolojia. Mke wangu ananiambia kuwa mimi ndiye nilikuwa na makosa. Anaweza kuwa sahihi, lakini sina uhakika kwa sababu sikupenda kusitisha uhusiano na rafiki wangu. Mjadala wa Paulo juma hili unahusu Wagalatia “kusitisha urafiki wao na Paulo” kutokana na tofauti za kiteolojia. Anawataka waendelee kuwa marafiki, lakini anataka urafiki huo uendelee kuwepo kwa vigezo vya (Mungu) wake. Je, jambo hilo linaonekana kuwa la kawaida? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1. Uinjilisti Usio Sahihi

 

  1. Soma Wagalatia 4:12. Paulo anawaambia Wagalatia wafanye nini? (Wawe kama yeye.)

 

   1. Sababu ya kufurahisha (hoja) ni pale Paulo anapotoa sababu kwa nini wanapaswa kufanana naye. Sababu ya kwanza ni kwamba amefanana nao. Unaweza kuelezea hoja hiyo? “Tafadhali iweni kama mimi kwa kuwa mimi nimekuwa kama ninyi.” (Katika hali ya kawaida haina mantiki yoyote.)

 

    1. Ni kwa jinsi gani Paulo “alifanana” na Wagalatia? (Kumbuka jinsi ambavyo, katika Wagalatia 2:11-13, Paulo anaelezea kuwa Petro aliungana na kula pamoja na Mataifa? Paulo anasema kwamba aliachana na tamaduni za Kiyahudi zilizonitaka nikae mbali na Mataif Nikaungana nawe.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:13. Hapa tunaona sababu ya pili ya Paulo. Kwanza alisimama kwenye mji wao kwa sababu alikuwa mgonjwa. Kwani Paulo hasemi kwamba, “niliwahubiria kwa isivyo bahati? Sicho nilichokidhamiria.” Ni kwa jinsi gani hoja hiyo ina ushawishi kiasi cha kuwa sababu ya wao kupaswa kufanana na Paulo? Inawezekana Paulo anasema kuwa Roho Mtakatifu aliweka mazingira yaliyomleta Paulo kwa Wagalatia. Uamuzi huu ulifanywa mbinguni, haukufanywa na Paulo.)

 

   1. Tafakari kidogo hoja mbili za Paulo. Kwa kuwa tunaweza kuchukulia kwamba bado wanakula pamoja, je, Paulo amebadili jambo gani kiasi cha kuwataka Mataifa wabadilike? Wanapaswa waige jambo gani kutoka kwa Paulo? (Paulo amebadilika kutokana na sababu za kiteolojia (Wagalatia 2:15-16) pamoja na ukweli kwamba Yesu alikabiliana naye alipokuwa akielekea Dameski (Matendo 9:3-6). Paulo anawataka Wagalatia kuwa watu walio radhi kufuata maelekezo ya Mungu maishani mwao.)

 

 

  1. Soma Wagalatia 4:14. Hii inaashiria sababu nyingine ya Paulo kubainisha ugonjwa wake. Ugonjwa wake unajengaje hoja ya Wagalatia kufanana naye? (Paulo anawaza kwamba kabari imewekwa kati yake na Wagalatia kwa sababu wanaigeukia sheria kama njia ya wokovu. Kimsingi Paulo anasema, “Tulikuwa na uhusiano mzuri sana. Hata nilipokuwa mgonjwa, na nikawa mzigo kwenu mlinisaidia na wala hamkunidhuru. Paulo anasema, “nilikuwa rafiki mhitaji sana, na bado mlitaka pawepo na uhusiano wa karibu sana na mimi.”)

 

  1. Soma Wagalatia 4:15. Je, umewahi kusikia kauli hii, “ningewapa mboni za macho yangu?” Nimewahi kusikia kauli ya kumpatia mtu shati, lakini kamwe sijawahi kusikia kauli ya mtu kutoa mboni za macho yake! Kwa nini Wagalatia wampatie Paulo macho yao? (Soma 2 Wakorintho 12:7-9. Wasomi na wachambuzi wa Biblia wanahisi kwamba “mwiba” wa Paulo ulikuwa ni tatizo la macho yake. Wagalatia 4:15 inatupatia msingi kamili wa makisio haya. Sababu pekee inayoweza kuwafanya Wagalatia watake kuyatoa na kuyagawa macho yao ni endapo Paulo alikuwa na tatizo la uoni hafifu.)

 

 1. Kuondoa Vikwazo

 

  1. Soma 1 Wakorintho 9:19-22. Vifungu hivi vinasema kuwa Paulo amekuwa kama kila mtu yeyote yule – angalao kwa muda mfupi. Je, hii inamaanisha kwamba Paulo hajajiwekea kanuni zozote, anafanya chochote chenye manufaa?

 

   1. Je, hiki ndicho wanachopaswa kukifanya Wagalatia ili wafanane na Paulo? (Paulo anabainisha ukweli muhimu sana wa kiteolojia – kuna mfumo wa mambo muhimu yenye manufaa. Jambo la thamani kubwa ni kupeleka injili kwa watu wasioijua injili. Paulo anasema kuwa ana tofauti za kiteolojia katika mitazamo yake kadhaa, lakini anaiweka kando ili kutekeleza lengo la msingi zaidi la kushiriki injili na watu wote.)

 

   1. Je, hili ni jambo la kiteolojia ambalo Wakristo wanalikosa mara kwa mara? (Siku hizi ninakwenda kwenye kanisa ambalo watu wanaohudumu mimbarani wanavaa kaptula na jeans za bluu. Wanafanya hivyo ili kuwahamasisha watu wengi “wahudhurie kanisani jinsi walivyo.” Mimi ni mtu ambaye nilikuwa nikiamini kwamba ni jambo la kumheshimu Mungu tunapovaa suti na tai kanisani. Wakati ambapo mimi si mmojawao wa wale waliopo mimbarani, sivai suti na tai, na ninaelewa ujumbe wa Paulo kwamba kuupata ulimwengu na kuuleta kwa Mungu ni jambo la muhimu zaidi.)

 

  1. Angalia tena 1 Wakorintho 9:20-21. Ipi kati ya hali hizi inaelezea tatizo la sasa la Paulo dhidi ya Wagalatia? (Walitaka kurejea chini ya sheria.)

 

   1. Niambie jinsi itakavyokuwa jambo la msaada kwao kwa wao kufanana na Paulo zaidi?

 

   1. Kwa nini Paulo asifanane nao zaidi? Hicho ndicho anachosema kuwa anakifanya! (Paulo anawataka Wagalatia warejee kwenye msitari sahihi. Lakini, lengo kuu na la msingi ni kuwapata waongofu wapya. Ikiwa Wagalatia watasisitiza utekelezaji wa sheria na tamaduni za Kiyahudi kwa waongofu wapya wa Mataifa, watakuwa wamehatarisha lengo la kuleta waumini wapya.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:17. Hivi punde tumejadili jinsi Paulo asivyotaka vikwazo vyovyote kwa waongofu wanaokuja kanisani. Vikwazo gani vinamsumbua akili kwenye kifungu hiki? (Hataki vikwazo kati ya washiriki wa kanisa. Anagundua kwamba lengo la upinzani ni “kuwatenganisha” Wagalatia na Paulo.)

 

 

   1. Je, hili ni tatizo lililopo kanisani kwako? Wale wanaodhani kuwa wana njia “bora” wanajaribu kujenga utengano?

 

   1. Je, kuna wakati ambao ikifikia hatua hiyo basi ni lazima kuchukua msimamo dhidi ya jambo baya? Paulo anachora msitari pahala gani? (Kwa dhahiri, anapingana na wale wanaotaka kuwarejesha Wagalatia kwenye dhana ya kuhesabiwa haki kwa njia ya matendo.)

 

  1. Hebu tuangalie vifungu kadhaa vinavyozungumzia vikwazo na uchoraji wa msitari. Soma Ufunuo 2:1-2 na Ufunuo 2:4-5. Kanisa la Efeso linafanya nini katika suala la uchoraji msitari?

 

   1. Soma Ufunuo 2:18-20. Kanisa la Thiatira linafanya nini katika suala la uchoraji msitari?

 

  1. Nadhani tunatakiwa kurejea nyuma na kwa mara nyingine tena tusome 1 Wakorintho 9:20-21. Je, Paulo anakiuka kanuni za kimaadili? (Utaona kwamba katika kila tukio, anaelezea msimamo sahihi wa kiteolojia. Halegezi masharti/haihitilafiani na ukweli.)

 

   1. Soma 1 Wakorintho 9:19. Paulo anamaanisha nini anaposema kuwa amejifanya “mtumwa wa wote?” Paulo anahitilafisha haki zake mwenyewe. Sidhani kama ni haki kuhitimisha kwamba Paulo anahitilafisha mtazamo wa Mungu juu ya kilicho sahihi na kisicho sahihi. Lakini, kumbuka kwamba tamaa kubwa ya Mungu ni kuwafanya watu wote wamwendee yeye ili waokolewe. Hilo ndilo linalopaswa kuwa lengo letu Paulo anaonekana kusema “Usiache malengo madogo yaingilie kati lengo kubwa.”)

 

 1. Njia ya Upendo

 

  1. Soma Wagalatia 4:19-20. Paulo anasema kuwa endapo angekuwapo pamoja nao angeweza “kuigeuza sauti yake.” Unaichukuliaje “sauti” anayoitumia Paulo kwenye hivi vifungu viwili? (Hii ni njia sahihi kabisa ya upendo. Paulo anawaita “vitoto vyangu” na anasema kuwa ana utungu kutokana na kuwajali kwake. Anasema kuwa amechanganyikiwa kimawazo juu ya tabia yao.)

 

   1. Vipi kuhusu “sauti” iliyopo katika Wagalatia 3:1? (Hakuna mtu anayependa kuitwa “mpumbavu.” “Kulogwa” hakuonekani kuwa sifa kwao.)

 

   1. Je, unaweza kuziunganisha hizi “sauti” mbili pamoja? (Tulikuwa tukiuita huu kuwa “upendo mgumu.” Unaonesha upendo na unasema ukweli.)

 

  1. Angalia tena kauli ya “kuzaliwa mtoto” katika Wagalatia 4:19. Je, unawafahamu watu wanaopenda kuwasahihisha washiriki wenzao wa kanisa? “Upendo wao mgumu” unamaanisha kwamba wanapenda kuwa ‘ngangari!’ Rejea ya Paulo ya “kuzaliwa mtoto” inatuambia nini juu ya mtazamo wake anapojaribu kuwarejesha Wagalatia kwenye mtazamo sahihi wa wokovu? (Kitendo cha kuzaa kina uchungu wa hali ya juu (ndivyo ninavyoelewa). Hii inaashiria kwamba bado hatujawa na udhibiti wa sehemu ya “upendo” ya “upendo mgumu” hadi tutakapogundua kwamba kuwasahihisha watu wengine ni jambo lenye maumivu makubwa sana kwetu.)

 

   1. Je, aina hii ya maumivu itakuwepo kwa mtu tunayemfahamu kwa juu juu? (Tunapotafakari kipengele halisi cha kupitia huu uzoefu wa maumivu, tunafahamu kwamba yanaweza tu kutokea kati ya watu walio marafiki wa karibu. Kuwasahihisha washiriki wa kanisa unaowafahamu kwa juu juu kwa ujumla sio jambo (wazo) zuri.)

 

 

  1. Kwenye utangulizi, nilitaja Facebook. Una mtazamo wa namna gani unapoandika ukosoaji kwenye ukurasa wa Facebook? (Naweza kuona kwamba sifuatilii kile tulichojifunza hivi punde kwenye kitabu cha Wagalatia! Ingawa mara kwa mara ninaandika juu ya masuala yanayohusu umma kwa ujumla kuliko masuala ya kiteolojia, nina wasiwasi kwamba ninaegemea upande wa “kulogwa” na “upumbavu” badala ya huruma ya utungu wa “kuzaa mtoto.”)

 

  1. Rafiki, ukijikuta unawasahihisha washiriki wenzako wa kanisa, na kama ilivyo kwangu ukajikuta kwamba mara zote umekuwa hufanyi hivyo kwa upendo stahiki, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu akubadilishe mtazamo wako?

 

Juma lijalo: Maagano Mawili.