Somo la 10: Maagano Mawili

Swahili
(Wagalatia 4:21-31)
Year: 
2017
Quarter: 
3
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Jambo gani lilisababisha mjadala wetu juu ya kiwango ambacho Mataifa walipaswa kuikubali teolojia ya Kiyahudi ili waweze kuwa Wakristo? Je, haikuwa tohara? Angalia Matendo 15:1. Hii inawafanya Wakristo wengi waseme kuwa “sheria” ambayo Paulo anairejea mara kwa mara katika kitabu cha Wagalatia ni “sheria ya mapokeo,” na si Amri Kumi. Kimsingi tatizo la kimantiki kwenye hoja hiyo ni kwamba tohara haikutolewa kama sehemu ya sheria ya mapokeo. Ni amri iliyotolewa kwa Ibrahimu zamani. Mwanzo 17:9-10. Somo letu juma hili linazungumzia kauli ya dhahiri kwamba Paulo anapoirejea “sheria” anajumuisha Amri Kumi (pamoja na sheria ya mapokeo na tohara). Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi juu ya kauli hii ya wazi kabisa!

 

 1. Kile Sheria Inachokisema

 

  1. Soma Wagalatia 4:21. Paulo anauliza swali gani? (Unafahamu kile sheria inachokisema)?

 

   1. Utahitajika kufahamu jambo gani ili kuweza kujibu swali hili? (Inategemea na anachokimaanisha Paulo katika sheria. Ikiwa anamaanisha Amri Kumi, basi inazungumzia jambo tofauti na sheria ya mapokeo au sheria ya tohara.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:22-24. Agano (mkataba) gani lilitolewa katika Mlima Sinai? (Soma Kutoka 31:18.)

 

   1. Je, ahadi zilibadilishwa na Amri Kumi? (Soma Kutoka 19:3-9. Ndiyo! Kama ambavyo tumekuwa tukijifunza kwa majuma kadhaa kwamba “mkataba” kati ya Ibrahimu na Mungu ulikuwa kwamba Ibrahimu atamtumaini Mungu, naye Mungu atamhesabia Ibrahimu haki, vivyo hivyo kuna mkataba hapa kwamba Mungu atawafanya wana wa Israeli kuwa tunu yake ya thamani ikiwa watatii.)

 

  1. Soma Kutoka 32:1-4, Kutoka 32:15-16, na Kutoka 32:19. Watu wa Mungu walishika sehemu yao ya mkataba kwa muda gani? (Walivunja ahadi yao hata kabla Musa hajarudi akiwa na mbao ambazo Mungu aliandika Amri Kumi juu yake!)

 

   1. Soma tena Kutoka 19:5. Neno la Kiebrania lililotafsiriwa kama “utii” katika tafsiri ya Biblia ya NIV ni “kusikiliza kwa makini,” au “kusikiliza kwa busara.” Je, watu wa Mungu hata walimsikiliza yeye? (Nadhani Mungu anasema, “Kuwa makini kwenye makubaliano yetu na ufuate vigezo na masharti yake.” Badala yake tunachokiona ni kwamba hata kabla watu hawajasoma au kusikia kilichosemwa kwenye Amri Kumi, tayari walikuwa wameshajielekeza katika kuabudu miungu.)

 

 1. Kisa cha Hajiri

 

 

  1. Soma Mwanzo 16:1-4. Kwa nini Sarai (Sara) alimwambia Abramu (Ibrahimu) amwingilie Hajiri? (Alisema “Bwana amenifunga tumbo nisizae.”)

 

  1. Soma Mwanzo 15:4-6. Jambo gani lilitokea kwenye sura ya Biblia kabla tu ya kisa kilichofuatia cha Hajiri? (Tunayo ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu ya kuwa na uzao mkubwa, na “Abramu akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.”)

 

   1. Unachukuliaje kitendo cha Ibrahimu kukubali ushauri wa Sara? (Wawili hawa walidhani kwamba Mungu alihitaji msaada katika kutimiza ahadi yake.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:25. “Utumwa” ambao Hajiri anauwakilisha ni upi? (Pitia kile tulichojifunza majuma mawili yaliyopita: Wagalatia 4:1-5. Wale ambao hawajapokea kwa imani kile alichokitenda Yesu kwa ajili (niaba) yetu (kuishi maisha makamilifu, kulipa adhabu ya mauti kwa ajili ya dhambi zetu, na kufufuka katika uzima wa milele) wako kwenye utumwa wa sheria. Hajiri anawakilisha wale wanaoamini kwamba kwa kuitii sheria wanaweza kuokolewa. Hajiri anawakilisha wale wanaodhani kuwa Mungu anahitaji msaada!)

 

 1. Mwana wa Ahadi

 

  1. Soma tena Wagalatia 4:22-23. Mwana gani “alizaliwa kama matokeo ya ahadi?” (Soma Mwanzo 17:15-19. Isaka ndiye mwana wa ahadi. Ukisoma muktadha, unaonesha kwamba tohara ilianzishwa kama sehemu ya ahadi. Hivyo, unaweza kuona kwa nini wale wanaojenga hoja kutetea tohara wanavyoweza kukosea kile kinachomaanishwa kwa imani pekee.)

 

   1. Ni “agano” gani jingine analoweza kuwa analizungumzia Mungu katika Mwanzo 17:19? (Agano lililotolewa katika kitabu cha Mwanzo 15:4-6, mtumaini Mungu naye atakuhesabia haki.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:25-28. Paulo anatoa mlinganisho gani kati ya Hajiri, utumwa na “mji wa sasa wa Yerusalemu?” (Paulo anatuambia kwamba wale wanaosotea haki kwa matendo (watu wa Yerusalemu) wanajaribu kutufanya kuwa watumwa.)

 

   1. Paulo anatoa mlinganisho gani kati ya Isaka, mwana huru, na “Yerusalemu wa juu?” (Wale wanaoamini katika ahadi ya haki kwa imani wako “huru” na wana ufungamanifu na mbingu.)

 

   1. Ungependa kuwa nani, mtumwa au mwana huru? Je, ungependa kuhusianishwa na Yerusalemu ya duniani au Yerusalemu Mpya mbinguni?

 

    1. Je, unakubali kwamba uchaguzi ni kati ya haki kwa njia ya utii kwenye Amri Kumi na haki kwa imani?

 

 

  1. Hebu turejee pale tulipoanzia mjadala huu. Soma tena Wagalatia 4:21. Hatukushughulika na swali la Paulo mara moja kwa sababu nilikuuliza “Tunawezaje kusema kinachozungumziwa na sheria ikiwa hatufahamu Paulo anazungumzia sheria ipi?” Nadhani sasa tumeona sheria anayoizungumzia Paulo ni, angalau kwa kiwango kidogo, Amri Kumi. Unadhani kiuhalisia Paulo anauliza nini anaposema, “je, hamwisikii sheria?” (Je, hamjui kwamba haki kwa njia ya matendo huwafanya kuwa watumwa, kama ilivyokuwa kwa Hajiri? Je, hamjui ya kwamba haki kwa imani ni matokeo ya ahadi, na ukiipokea na kuikubali hiyo ahadi unakuwa mwana huru wa Mungu, kama ilivyokuwa kwa Isaka?)

 

 1. Mgogoro Kati ya Wana

 

  1. Soma Wagalatia 4:29 na Mwanzo 21:8-10. Kwa nini mwana wa Hajiri (Ishmaeli) anamdhihaki Isaka? (Ni jambo la kawaida kwa sababu nafasi yake inachukuliwa na huyu mwana mpya.)

 

   1. Je, dhihaka hii bado inaendelea? Je, wale wanaoshadadia wokovu kwa njia ya matendo wanawadhihaki wale wanaoamini katika haki kwa njia ya imani?

 

    1. Ikiwa ndivyo, unadhani kwa nini jambo hili linatokea? (Sizifahamu tamaduni zote, lakini tamaduni nyingi zinathamini bidii ya kazi na mafanikio. Ukifanya kazi kwa bidii na kujipatia kitu cha thamani, unasifiw Hii ni kinyume na haki kwa imani, ambapo huwezi kupata kitu chochote katika wokovu wako. Yote yanatokana na kazi ya Mungu. Hivyo, inaonekana jambo la kawaida kwamba “wafanyao kazi kwa bidii” wanapaswa kuwadhihaki “wavivu.”)

 

  1. Kabla sijaendelea, ninakutaka uangalie maneno yaliyopo katika Wagalatia 4:29. Kifungu hiki kinasema kuwa Isaka alizaliwaje? (“Kwa uwezo wa Roho.”)

 

   1. Je, hivyo ndivyo ambavyo maisha yako mapya ya neema yanavyowezeshwa na kutiwa nguvu? (Naam! Hatuitegemei bidii yetu ya kazi, tunautegemea uwezo wa Roho Mtakatifu.)

 

  1. Soma Wagalatia 4:30. Ukisoma kisa kinachopatikana katika Mwanzo 21:11-18, inahuzunisha kuona hisia za kibinadamu zinahusika. Kwa nini Paulo anasisitiza sehemu hiyo ya kisa hiki?

 

   1. Je, tunatakiwa “kuwafukuza” wale wanaoshadadia haki kwa njia ya matendo kanisani? Au, je, Paulo anapendekeza kuwa tunapaswa “kuondosha” mawazo ya haki kwa njia ya matendo kutoka akilini mwetu?

 

   1. Paulo anamaanisha nini anaposema “mfukuze” na “mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana?”

 

  1. Soma Wagalatia 4:31. Sisi ni watoto wa nani?

 

   1. Ikiwa wewe ni mwana wa Sara, mwana wa ahadi, je, unaenenda na vigezo hivyo? Au unaenenda kama mwana wa Hajiri?

 

   1. Angalia kipengele kingine cha jambo hili. Mojawapo ya jambo la kusikitisha juu ya kisa cha Hajiri na Ishmaeli ni kwamba hakuna hata mmoja kati yao aliyekuwa na uchaguzi kwenye jambo hili. Je, Isaka alikuwa na uchaguzi wowote katika kuzaliwa kwake kama mwana wa ahadi?

 

    1. Je, kuna fundisho lolote la kiroho katika jambo hili? (Hatukusababisha pambano la ulimwengu mzima kati ya Yesu na Shetani. Wale wanaotaka kuokolewa kwa matendo yao watatambua kwamba hawana udhibiti wa kutosha wa hali inayowakabili. Ndio maana ni bora zaidi kupokea tu ahadi ya Mungu. Kubali na pokea tu zawadi yake ya bure.)

 

 

  1. Soma maneno ya Yesu katika Yohana 6:28-29. Ni “matendo” gani ambayo “Mungu anatutaka” mimi na wewe tuyatende? (“Kumwamini Yeye aliyetumwa na Yeye.”)

 

  1. Rafiki, ikiwa huamini, kwa nini usichukue uamuzi huo sasa hivi? Kwa nini usiondoke utumwani hadi kuwa mwana wa Mungu aliye huru? Kwa nini usimtumaini Mungu kwa kumwamini Yesu?

 

 1. Juma lijalo: Uhuru Katika Kristo.