Somo la 12: Kuishi kwa Roho

(Wagalatia 5:16-25; Warumi 8)
Swahili
Year: 
2017
Quarter: 
3
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Miaka mingi iliyopita nilikuwa ninazungumza na mtu ambaye ndio kwanza alikuwa ameielewa neema. Tulikuwa tunazungumzia kuhusu sheria ya Mungu na aliniambia kuwa sheria haina na matumizi. Tulikubaliana kutokubaliana katika jambo hilo. Takribani mwaka mmoja au miwili baadaye nilikutana naye tena. Baada ya kukumbuka mazungumzo yetu, nilimuuliza juu ya maoni yake kwa sasa. Mawazo yake yalikuwa yamebadilika kwa kiasi kikubwa sana. Bado aliamini katika neema, lakini pia alitambua umuhimu wa utii. Somo letu juma hili linahusu utii. Yesu alilipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu. Tulikufa (katika Yesu) kwa ajili ya dhambi zetu tulipobatizwa. Lakini, kufunguliwa kutoka kwenye adhabu ya kifo haimaanishi kwamba tuipuuzie neema. Jambo hili linatokeaje? Ukomo unawekwa wapi na kwa namna gani? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

  1. Roho Dhidi ya Asili ya Dhambi (Mwili)

 

    1. Soma Wagalatia 5:16. Baada ya kuwa tumeokolewa kwa neema, je, bado tuna tamaa ya dhambi? (Ndiyo! Paulo anaandika juu ya “tamaa” za mwili ambazo zinakinzana na uongozi wa Roho Mtakatifu.)

 

      1. Lengo letu ni lipi? (“Kutozitosheleza” tamaa za mwili.)

 

      1. Je, hii haionekani kuwa kama kipindi tulipokuwa chini ya sheria? Sheria ilituelekeza tuishi kwa namna fulani, na miili yetu ilituambia tuishi kwa namna nyingine.

 

    1. Soma Wagalatia 5:17. Tunataka kufanya nini? (Kile ambacho miili yetu inakitamani.)

 

      1. Hilo linawezekanaje? Nilidhani kwamba Roho Mtakatifu ametupatia mtazamo mpya? (Nadhani mara zote tutauhisi ugomzi/mgongano. Mara zote tutauhisi mvuto wa majaribu.)

 

    1. Soma Warumi 7:14-20. Paulo yu mahsusi zaidi kwenye hivi vifungu. Tatizo gani halisi tunaliona maishani mwetu? (Tunaona kwamba tunatenda mambo ambayo hatutaki kuyatenda.)

 

    1. Kanisa la kwanza ambalo nilifundisha darasa la kujifunza Biblia lilikuwa na mjadala mzuri miongoni mwa wanadarasa kuhusu neema. Nakumbuka mwanadarasa mmoja “aliyepata” neema. Alikuwa na furaha kubwa sana kwa sababu alisema kuwa kwa ghafla alijisikia huru – huru dhidi ya sheria. Je, hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa? (Soma Warumi 8:1-2. Ndiyo. Hakuwa tena chini ya hukumu ya sheria. Lakini, nadhani alijisikia kwamba hahitajiki tena kuwa makini juu ya “mvuto” wa dhambi. Neema “haiui” asili yetu ya dhambi. Dhambi inaendelea kujikita akilini mwetu.)

 

 

    1. Soma Warumi 8:3-4. Je, bado tunaweza “kuishi kwa kufuata mambo ya Roho,” na bado tukawa tunapambana na hiki anachokielezea Paulo? (Nadhani hiyo ndio hali halisi kwa Wakristo wengi walio dhati.)

 

    1. Soma Warumi 8:5-9. Biblia inatuambia tufanye nini ili tuweze kuishi kwa kufuata mambo ya Roho? (Kuyaweka mawazo yetu kwenye kile ambacho Roho anatamani tukitende. Tunafanya chaguzi, na hili ndilo jambo la muhimu.)

 

      1. Je, huu ni ushikiliaji mno wa sheria? Je, hii ni dhana ya kuhesabiwa haki kwa njia ya matendo, isipokuwa tu kwamba mara hii matendo ni suala la uchaguzi? (Sijui ni kwa jinsi gani neema inaweza kuwa nyepesi zaidi ya uchaguzi.)

 

    1. Soma Warumi 8:10-11. Ni kwa jinsi gani miili yetu “iliyokufa” inakuwa hai? (Kwa uwezo ule ule uliomfufua Yesu kutoka kaburini, uwezo wa Roho Mtakatifu.)

 

    1. Soma Warumi 8:12-14. Uchaguzi huu ni wa muhimu kiasi gani, uchaguzi wa kuishi kwa kufuata mambo ya Roho au kwa kuufuata mwili? (Tutakufa ikiwa tutaishi kwa kufuata mwili.)

 

    1. Soma Wagalatia 5:18. Tunao huu mvutano/mgogoro mawazoni mwetu kati ya uongozi wa Roho na matamanio ya mwili. Tunajuaje pale tunapokuwa tunamfuata Roho?

 

      1. Katika siku za nyuma sana baadhi ya magari yalikuwa na kipimo kisicho na hewa ambacho kilikuwa kinabadilika rangi na kuwa chekundu gari linapotumia mafuta mengi sana na kilikuwa kinabadilika rangi na kuwa cha kijani wakati mafuta kidogo yalipokuwa yanatumika kwa umbali mrefu. Je, isingekuwa vyema kuwa na kipimo kama hicho ili tuweze kujua wakati gani tunaishi kwa kufuata mambo ya Roho na wakati gani tunaishi kwa kuufuata mwili?

 

      1. Angalia jinsi Paulo anavyobainisha jambo hili. Hasemi kwamba tunaishi kwa kufuata majaribu yanayosababishwa na Shetani au mmojawapo wa mawakala wake. Paulo anasema “asili yetu ya dhambi” au “mwili” wetu ndivyo vinavyotuvuta dhambini. Je, umewahi kufikiri kwamba hazikuwa pepo, bali mwili wako ndio adui wako mkubwa linapokuja suala la utii?

 

    1. Soma tena Wagalatia 5:18. Ni kwa namna gani hatupo “chini” ya sheria tunapoishi kwa kufuata mambo ya Roho? (Hatupo chini ya hukumu ya sheria. Soma tena Warumi 8:6-7. Hii inaonesha kuwa ingawa hatupo tena chini ya sheria,  bado sheria ni alama (hata kama ni alama hafifu) kwa ajili ya kuishi maisha yanayompa Mungu utukufu pamoja na sisi pia.)

 

    1. Mjadala huu kuhusu uchaguzi unanifanya nitafakari kwamba tunazo chaguzi tatu. Tunaweza kuishi kwa kufuata miili yetu, tunaweza kuishi kwa kufuata mambo ya Roho, au tunaweza kujikaza kisabuni na kujaribu kuitii sheria. Unadhani kiuhalisia jambo hili linatendaje kazi? (Jambo la kwanza nitakalolifanya ili kuishi kwa kufuata mambo ya Roho ni kuomba kwamba Roho Mtakatifu ayaongoze mawazo yangu. Tuchukulie kwamba jaribu unalokabiliana nalo ni uzinzi. Unaweza kuchagua mtazamo wa, “Ninaweza kufanya jambo gani ili kumfurahisha mwenzi wangu leo?” Unaweza kuchagua mtazamo wa, “Ninaweza kufanya nini ili kumshawishi mtu aingie nami kwenye uhusiano usio sahihi?” Au, unaweza kuchagua mtazamo wa, “Hata sitajaribu kumwangalia mwanamke tofauti na mke wangu, hivyo sitaanguka kwenye kishawishi.” Nadhani chaguo la kwanza linaongozwa na Roho.)

 

  1. Kujichunguza

 

 

    1. Soma Wagalatia 5:19-21. Je, kuna tendo lolote kati ya hayo linalojidhihirisha maishani mwako?

 

      1. Kama jibu ni, “ndiyo,” je, hii inaashiria kwamba unaishi kwa kuufuata mwili (tofauti na kuishi kwa kufuata mambo ya Roho) na hivyo umepotea? Au, je, hii inaelezea tu kile ambacho Paulo amekikiri, kwamba anatenda mambo ambayo hakutaka kuyatenda?

 

      1. Angalia msitari usemao,“watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi Ufalme wa Mungu.” Hii inatuambia nini juu ya uwepo wa haya matendo maovu maishani mwetu? (Hatupendi matendo yoyote maovu maishani mwetu, lakini tatizo sio kuanguka dhambini mara moja moja, tatizo ni kuyafanya matendo haya kuwa mtindo wetu wa maisha. Ikiwa mara kwa mara tunaishi kwa namna hii, tunalo tatizo kubwa sana ambalo linaonesha kuwa hatujachagua kuishi kwa kufuata mambo ya Roho.)

 

    1. Soma Wagalatia 5:22-23. Orodha hii inatofautianaje na ile iliyotangulia? (Kwa dhahiri inaorodhesha mambo mazuri tofauti na mambo mabaya. Tofauti kuu ni kwamba kwa ujumla orodha ya pili inaorodhesha mitizamo, sio matendo.)

 

      1. Ukweli kwamba kwa ujumla orodha ya pili inaelezea mitizamo inakuambia nini kuhusu kuishi kwa kufuata mambo ya Roho? (Hiki ndicho kiini: ukichagua kuishi kwa kufuata mambo ya Roho, Romo Mtakatifu ataubadili moyo wako na atayabadili mawazo yako. Mtazamo wako dhidi ya dhambi utabadilika. Bado utaona asili yako ya dhambi ikishindana kupata usikivu wako, lakini mtazamo wako uliobadilishwa utaifanya dhambi isivutie sana.)

 

    1. Soma Wagalatia 5:24. Inamaanisha nini “kusulubisha mwili na sili ya dhambi?” (Kusulubisha inamaanisha kuiweka katika kifo cha kutisha.)

 

      1. Ikiwa asili yetu ya dhambi inasulubishwa, unaichukuliaje Warumi 7:15 ambapo Paulo anatuambia kuwa anatenda mambo ambayo hataki kuyatenda? Je, miili yetu inafanana na mhusika mbaya kwenye sinema ambaye mara kwa mara anarejea kuja kututisha? (Nadhani taswira bora ya jambo hili inapatikana kwa kusoma Warumi 7:19-8:4. Tunachokifahamu kwa hakika ni kwamba Yesu ametuweka huru dhidi ya “sheria ya dhambi na kifo.” Wajibu wetu ni kuendelea kuchagua kuishi kwa kufuata mambo ya Roho na si mambo ya mwili.)

 

    1. Soma Wagalatia 5:25. Hapo awali tulizungumza juu ya hii dhana ya “kuishi” kwa kufuata mambo ya Roho tofauti na kuishi kwa kufuata asili yetu ya dhambi. Dhana iliyopo ni kwamba inawakilisha mwenendowa maisha yetu, na si matendo ya wakati huo. Paulo anajengaje hoja kwenye jambo hili kwa kutuambia tuendelee “kuenenda kwa Roho?” (Maisha yetu ya Kikristo ni mwendo. Tunaelekea upande mmoja au mwingine. Hivyo, lengo letu ni kuenenda kwa mujibu wa uelekeo wa Roho Mtakatifu.)

 

  1. Taswira Pana

 

 

    1. Soma Mathayo 11:28-30. Yumkini hadi kufikia hapa unajisikia kukatishwa tamaa kwa sababu bado unapambana na sili yako ya dhambi. Yesu anasema nini kuhusu mzigo wa kumfuata Yeye? (Yesu anasema kwamba unapokabiliana na matatizo maishani kwa kutumia uwezo Wake, mzigo wako ni mwepesi. Fikiria tofauti halisi kati ya kujaribu kutii ili kuepuka mauti, na ushirika na Mungu ili kumpa Yeye utukufu na kuyaboresha maisha yako.)

 

    1. Rafiki, habari mbaya ni kwamba bado unajisikia kuwa na mvuto wa dhambi hata mara baada ya kuokolewa kwa neema pekee. Uko huru dhidi ya adhabu ya kifo inayotekelezwa na sheria, lakini bado unawajibika kufanya uchaguzi wa kuishi kwa mujibu wa uongozi wa Roho Mtakatifu. Je, utaamua sasa hivi, kwamba utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie “uendane naye” katika programu zake kwa ajili ya maisha yangu?

 

  1. Juma lijalo: Injili na Kanisa.