Somo la 7: Kuishinda Dhambi

Swahili
(Warumi 6)
Year: 
2017
Quarter: 
4
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Majuma mawili yaliyopita tulijifunza kwamba Yesu alikufa ili kuwahesabia haki “waovu” (Warumi 4:5). Hiyo ni habari njema, lakini inaweza kutuelekeza kuhitimisha kuwa, “uovu una raha” (angalao kwa muda), hivyo ninaweza kuwa mwovu na nikaokolewa. Hilo si hitimisho ambalo Paulo anataka tulifikie. Kwa hakika hilo si lengo la Mungu kwetu. Mungu anatutaka tupige hatua kuielekea haki badala ya kugaagaa (kujiachia) dhambini. Hebu tuchimbue somo letu la Biblia juma hili na tujifunze zaidi!

 

 1. Maisha Mapya

 

  1. Soma Warumi 6:1. Unajibuje swali la Paulo? Utakumbuka kwamba katika Warumi 5:20, Paulo alituambia kuwa dhambi ilipoongezeka “neema pia iliongezeka zaidi.”

 

  1. Soma Warumi 6:2. Paulo anatoa jibu gani kwa swali lake? Je, Paulo analeta utata kwenye jibu? (Hapana, haleti utata na hapana, hataki “tuendelee kutenda dhambi.”)

 

  1. Soma Warumi 6:3-4. Unawafahamu watu wenye tatizo la kiafya la muda mrefu, na wanatakiwa kufanya mambo kama vile kupunguza uzito, kufanya mazoezi na kula kwa umakini zaidi? Hata hivyo, badala ya kufanya mambo kama hayo, wanatumia tu dawa ili kutatua tatizo la kiafya. Kama hilo linaleta mantiki, kwa nini tu basi kutoitegemea neem na kuendelea kutenda dhambi? Paulo anatupatia sababu gani tunayopaswa kuijali kuhusu tatizo lililopo, la dhambi maishani mwetu? (Tulipobatizwa, tulikufa pamoja na Yesu kwa ajili ya dhambi zetu. Tatizo ni kumalizana na dhambi, na kuishi maisha mapya.)

 

  1. Soma Warumi 6:5. Unalinganishaje kifo na ufufuo? Tofauti ni zipi? (Kifo ni tukio la kutisha. Kwa ujumla ndio mwisho wa uhai. Ufufuo ni mwanzo wa uhai. Ni tumaini na furaha. Tunataka hilo!)

 

  1. Soma Warumi 6:6-7. Kwa nini Yesu alikufa kwa ajili yetu? (Kutuweka huru dhidi ya dhambi na adhabu zake.)

 

   1. Unaweza kuona kwa nini kusalia dhambini hushinda lengo zima la kifo cha Yesu kwa ajili ya dhambi zako?

 

   1. Angalia kauli mahsusi anayoitumia Paulo, “kuitumikia dhambi.” Dhambi inatutumikishaje (inatufanyaje kuwa watumwa)? (Kijana mdogo ambaye binti yangu alikuwa na urafiki naye kimahusiano amefariki hivi karibuni kutokana na kutumia dawa za kulevya nyingi kupita kiasi. Hakuweza kuwa huru dhidi ya kutawaliwa kwake na dawa hizo. Alikuwa mtumwa, na utumwa huo uliyachukua maisha yake. Paulo anasema “ishi maisha mapya,” na si maisha ya kale ya utumwa wa dhambi.)

 

  1. Soma Warumi 6:8-9. Tunaona neno jingine ambalo huwa linahusishwa na utumwa, naloa.” Ni kitu gani ambacho hakimtawali tena Yesu? (Kifo.)

 

 

   1. Je, hiyo pia ni kweli kwetu?

 

  1. Soma Warumi 6:10. Yesu anaishije maisha yake baada ya ufufuo wake? (Amwishia Mungu.)

 

   1. Unapaswa kuishije baada ya ubatizo?

 

  1. Unadhani kwa nini Paulo anazungumzia sana habari ya kifo kwenye mjadala wa haki kwa imani? (Soma Warumi 7:1-2. Hii ndio mada ya Paulo. Tulipoifia sheria, haina tena mamlaka juu yetu. Vivyo hivyo, tulipokufa pamoja na Yesu kwa njia ya ubatizo, dhambi haina tena mamlaka juu yetu. Fanyia mazoezi uhuru wako na kataa dhambi!)

 

 1. Mtazamo Mpya

 

  1. Soma Warumi 6:11-13. Paulo anazungumzia kuhusu kuitoa miili yetu kwa “dhambi” au kujitoa kwa “Mungu.” Nipatie mfano halisi wa jinsi utakavyojitoa kwa Mungu tofauti na kuutoa mwili wako kwa dhambi?

 

   1. Paulo anapotumia neno “kujitoa,” hiyo inatuambia nini kuhusu umuhimu wa chaguzi zetu? (Neema haitupatii ahueni ya kufanya chaguzi ngumu. Tunatakiwa kuchagua kufuata njia ambayo Mungu ameiweka mbele yetu.)

 

   1. Je, tuko peke yetu kwenye huu uchaguzi? (Roho Mtakatifu anasaidia kuongoza chaguzi zetu. Angalia, Yohana 16:7-11 na Wagalatia 5:16.)

 

  1. Soma Warumi 6:14. Hebu tuone kama tunaweza kuelewa kifungu hiki. Kwa nini neema inatusaidia zaidi kuliko sheria inavyotusaidia linapokuja suala la kuwa huru dhidi ya utawala wa dhambi na kifo? Je, sheria haibainishi kwa uwazi zaidi matatizo yaliyopo maishani mwetu? (Sheria inabainisha dhambi yetu. Bali, kama anavyosema Paulo, sheria “inafanya hasira” (warumi 4:15) tu. Tunapokuwa salama kwenye wokovu wetu, kutokana na neema ambayo Yesu anaitoa, basi tuko huru kufanya chaguzi sahihi zisizozongwa na hukumu ya sheria. Hatuzongwi kutokana na dhambi kuwa mtawala wetu.)

 

   1. Je, umewahi kujisikia kutatishwa tamaa kwa sababu kigezo cha mbingu kilikuwa juu sana, nawe ulikuwa chini sana ikilinganishwa na kigezo hicho? (Huo ndio mtazamo unaoondoshwa kwa kutumaini kuwa Yesu anakupatia haki kwa imani pekee. Dhambi na kifo si mtawala (bwana) wako tena.)

 

 1. Utumwa

 

  1. Soma Warumi 6:15. Je, hii inafanana sana na Warumi 6:1-2? Unadhani kwa nini Paulo anarudia wazo hili kwenye sura ile ile? (Anasisitiza kwamba neema haipaswi kuhamasisha utendaji wa dhambi.)

 

  1. Soma Warumi 6:16. Chaguzi zetu mbili ni zipi? (Hatimaye, chaguzi hizo ni mauti au haki.)

 

   1. Elezea njia ya kila moja? (Tunafanya uchaguzi wa “kujitoa” nafsi zetu ama kwa dhambi au kwa utii. Uchaguzi huo unatuweka kwenye njia ielekeayo ama kwenye mauti au haki.)

 

 

   1. Kwa nini Paulo anatumia kauli ya “uletao” mauti au haki? (Kwa sababu kipengele hiki cha maisha ya Kikristo ni mchakato. Neema ni ya papo hapo. Maisha ya kuchagua kutii ni mchakato.)

 

   1. Kuna jambo kubwa sana la fikra isiyo ya Kibiblia katika dunia ya sasa. Jambo moja linahusisha shambulizi kwenye mtazamo “wa aina mbili” (binary) wa ngono na jinsia. Badala ya “mwanaume na Mwanamke [Mungu] aliwaumba (Mwanzo 1:27), tunaweza kuchagua mapatano yoyote ya mwanaume na mwanamke kwa kadri tunavyotaka. Unaweza kuteteaje mtazamo wa “aina mbili” wa dhambi na utii? Hata wale waliookolewa kwa neema si wanatenda dhambi? (Kilicho cha namna mbili ni uchaguzi. Kama hufanyi uchaguzi wa kumtii Mungu, unachagua kutomtii. Umechagua dhambi.)

 

  1. Soma Warumi 6:17-18. Paulo anashukuru kwa utii wa namna gani? (Utii wa moyo mkunjufu.)

 

   1. Kwa kuwa tunafahamu dhambi haikomi tu pale tunapobatizwa, Paulo anamaanisha nini anaposema “tumewekwa huru mbali na dhambi?” (Ukichagua dhambi, basi wewe ni mtumwa wa dhambi. Ukichagua utii, basi wewe si tena mtumwa wa dhambi.)

 

   1. Fikiria jambo hili katika muktadha wa kisiasa. Ama unaunga mkono au hauiiungi mkono nchi unayoishi. Ukichagua kutoiunga mkono nchi, bado unaishi katika nchi hiyo, basi unakuwa muasi wa kanuni zake. Ukichagua kumtii Mungu, je, uko kwenye uasi dhidi ya kanuni za dhambi?

 

  1. Soma Warumi 6:19. Unadhani Paulo anamaanisha nini anaposema kuwa anaweka hoja yake “kwa jinsi ya kibinadamu?” Angeweza kuiweka hoja hiyo kwa namna gani nyingine? (Utumwa ulikuwa jambo la kawaida katika nyakati za Paulo. Paulo anailinganisha jamii yetu na utumwa, ingawa Paulo anatambua kwamba hii sio njia kamilifu ya kulinganisha haya mambo mawili.)

 

   1. Hebu tujaribu kile anachokisema Paulo dhidi ya uzoefu wako mwenyewe. Paulo anapozungumzia “uovu unaozidi kuongezeka,” je, hii ni dhana unayoielewa? Je, dhambi gani inazoeleka sana na inaendelea kuongezeka hatua kwa hatua na kuwa kama kilevi?

 

    1. Kama umesema, “ndiyo,” huo ndio uzoefu wangu, hiyo inazungumzia nini kuhusu hoja juu ya uchaguzi tunaokabiliana nao ulio wa namna mbili? (Imethibitishwa kuwa kweli. Ikiwa uchaguzi mmoja unajielekeza kwenye uchaguzi mwingine unaofanana na huo wa awali, na kila uchaguzi unatupeleka mbali zaidi kwenye uchaguzi tuliouchagua, basi kweli tunazo chaguzi mbili pekee.)

 

   1. Je, unaweza kuthibitisha pia kwamba mara unapofanya uchaguzi wa kutii, uchaguzi unakuwa mwepezi baada ya muda fulani?

 

  1. Soma Warumi 6:20-22. Paulo anauliza swali zuri na la muhimu sana. Fikiria kipindi fulani maishani mwako ulipoichagua dhambi. Mambo yalikwendaje? Je, uliishia kuaibika kutokana na chaguzi zako? (Uchaguzi wetu una matokeo ya papo kwa hapo pamoja na ya muda mrefu. Kuchagua dhambi hutuelekeza kwenye kudhurika, aibu na mauti. Kuchagua kumtii Mungu kunatuelekeza kwenye haki, maisha yaliyoboresheka, na uzima wa milele.)

 

  1. Soma Warumi 6:23. Utakumbuka kwamba tulipojifunza Warumi 4:4-5, tulijadili tofauti kati ya ujira unaopatikana kutokana na kufanya kazi na karama (zawadi) ya bure. Je, tunapata mauti, na hatuupati uzima wa milele? (Ndiyo! Kifo si zawadi (karama). Tunakipata. Kwa upande mwingine, uzima wa milele ni karama (zawadi) ambayo hatuwezi kuifanyia kazi.)

 

 

  1. Rafiki, mustakabali wako uko mbele yako. Je, umechagua kuipokea karama ya neema? Vyema! Je, sasa utaendelea kwenye njia hiyo kwa kuchagua kuwa mtiifu badala ya kuchagua kuwa mtumwa kwa dhambi zinazoendelea kuongezeka? Kwa nini usichague utii?

 

 1. Juma lijalo: Ni Nani Aliye Mtu wa Warumi 7?