Sadaka za Shukrani

Swahili
(Luka 7, 1 Petro 4, 2 Wakorintho 9)
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.                           

 

 

Utangulizi: Inamaanisha nini kumtolea Mungu “sadaka?” Katika Agano la Kale, mara nyingi ilihusisha kutoa sadaka ya mnyama. Mawazoni mwangu, kauli ya “zaka na sadaka” inamaanisha kutoa fedha. Ninakumbuka mara nyingi nilipokuwa kwenye mimbara kanisani kwetu nikiwa pamoja na mchungaji wetu kwa upendo mkubwa. Ulipokuwa unafikia wasaa wa kutoa “sadaka,” nilimpatia dola moja atoe kwa sababu kamwe hakuwa akikumbuka kuchukua sadaka yake. Likawa suala la ucheshi kati yetu, kwamba moja kwa moja ilikuwa inatokea ninampatia dola moja. Juma hili tutaangalia aina tofauti ya sadaka, aina isiyohusisha viwango vidogo vya fedha, bali sehemu kubwa ya maisha yako. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 1.    Sadaka Itolewayo kwa Moyo

 

  1.    Soma Luka 7:36-38. Tunajifunza nini juu ya maisha ya nyuma ya mwanamke huyu? (Aliishi maisha ya dhambi. Kifungu hakiielezei dhambi hiyo. Wakati watu wengine wanasema kuwa mwanamke huyu ni Maria Magdalena, haileti mantiki yoyote kwamba Luka habainishi jina lake, kwa kuwa anamtaja kwa jina katika sura inayofuata (Luka 8:2).)

 

   1.    Unadhani kwa nini mwanamke huyu alimtendea hivi Yesu? (Muktadha unajenga hoja kwamba Yesu alikuwa amemtendea jambo la pekee kumtoa katika maisha yake ya zamani ya dhambi.)

 

    1.    Ikiwa Yesu amekusaidia kutoka dhambini, je, unayo shukrani au unayaangalia maisha yako ya zamani kwa kuyatamani?

 

  1.    Soma Luka 7:39. Je, unadhani Yesu aliyafahamu maisha ya zamani ya mwanamke huyu? (Tutakachokisoma katika sehemu inayofuata kinaonesha kuwa kwa hakika aliyafahamu. Hiyo inaunga mkono hoja kwamba hapo kabla Yesu aliingilia kati katika kumsaidia.)

 

  1.    Soma Luka 7:40-43. Je, unakubaliana na jibu la Simoni? (Nadhani, kwa sababu Yesu anatuambia kuwa hilo ndilo jibu sahihi!)

 

  1.    Soma Luka 7:44-46. Unadhani kwa nini Simoni alimkaribisha Yesu chakula cha usiku, lakini hakumwonesha ukarimu stahiki? (Simoni alikuwa anamdadisi Yesu. Hakuwa mwamini (muumini). Bila shaka alidhani kuwa alikuwa bora zaidi ya Yesu, na Yesu alipovumilia tabia (mwenendo) ya mwanamke huyu, ilimthibitishia zaidi Simoni hitimisho lake.)

 

  1.    Soma Luka 7:47-48. Kwa nini dhambi za mwanamke huyu zilisamehewa? (Kwa kuwa “alipenda sana.”)

 

   1.    Katika kisa cha Yesu, yule aliyesamehewa deni kubwa hupenda zaidi. Inakuwaje kwamba mwanamke huyu anampenda Yesu sana kabla dhambi zake hazijasamehewa? (Nadhani Yesu alikuwa amemsamehe dhambi zake hapo kabla au alimwonesha kwamba alimkubali. Hiyo iliamsha mwitiko wake kwa Yesu. Kufikia hapa Yesu anasema, “Umesamehewa dhambi zako” ili kuwaonyesha wale wanaomsikiliza kwamba yeye ni Mungu, yeye ni Masihi.)

 

  1.    Hebu tutafakari kisa hiki na jinsi kinavyohusika kwako na kanisani kwako. Je, viongozi wako wa sasa wa kanisa ni wale waliokuwa wadhambi wa kutisha huko zamani, au ni watu ambao kwa ujumla wamekuwa watiifu kwa Mungu sehemu kubwa ya maisha yao?

 

   1.    Ikiwa ndivyo, tunao watu katika uongozi wanaompenda Yesu kidogo?

 

  1.    Je, watu waliofanikiwa kanisani kwako (katika macho ya kidunia) ni wale waliokuwa wadhambi wa kutisha siku za nyuma? (Yumkini hapana. Kumbuka masomo yaliyopita ambapo tulijifunza kwamba Mungu anatupatia amri zake ili kuyaboresha maisha yetu. Hivyo, wale walioishi maisha ya utii yumkini wana mafanikio zaidi.)

 

   1.    Ikiwa niko sahihi, je, hiyo inamaanisha kuwa wale wenye fedha nyingi na karama ya kutoa kwa ajili ya kazi ya Mungu ni watu ambao wana hamasa ndogo ya kutoa?

 

  1.    Kauli zangu zinazohusisha utii na mafanikio ni kauli za jumla, na mara zote kauli hizo si sahihi kwa baadhi ya watu. Lakini, kama unaliona tatizo la jumla ninalolielezea, je, utafanya nini ili kulitatua? Au, je, ni jambo ambalo haliwezi kutatuliwa? (Farisayo katika kipindi cha Yesu anaonekana, angalao kwa juu-juu, kuwa mtiifu. Hii inayaelekeza mawazo yetu kwenye tatizo la majivuno na kujitegemea (kujitosheleza). Yumkini tunahitaji mafundisho zaidi kwenye dhambi zisizo za dhahiri zaidi ili washiriki wengi zaidi wawe na upendo zaidi.)

 

  1.    Soma Luka 7:48-50. Yesu aliwafanya watu hawa watafakari jambo gani aliposema, “Umesamehewa dhambi zako?” (Kwamba yeye ni nani. Huu ndio ujumbe mkuu wa injili: Yesu Kristo ni nani? Mungu pekee ndiye awezaye kusamehe dhambi, na huo ndio ujumbe wa Yesu.)

 

   1.    Mwanamke amekuwa akifanya mambo mengi ambayo Simoni hakuyafanya. Je, hiyo ndio “imani” iliyomwokoa? (Hapana. Mtazamo wake ulikuwa tofauti kabisa na ule wa Simoni. Alikuwa na shukrani kwa Yesu. Shukrani yake ilijidhihirisha kwenye zawadi yake na matendo yake.)

 

    1.    Matokeo ya mtazamo wako kwa Yesu ni yapi?

 

 1.   Utoaji wa Karama

 

  1.    Soma 1 Petro 4:10. Wanadamu wamepokea karama gani kutoka kwa Mungu? (Petro haorodheshi karama za roho kama alivyofanya Paulo katika maandiko yake (1 Wakorintho 12), lakini ukisoma muktadha wa hiki kifungu Petro anabainisha upendo, ukarimu, mazungumzo na huduma.)

 

   1.    Wajibu wetu ni upi kutokana na hizi karama? (Kuzishiriki na watu wengine! Kuzitoa sadaka.)

 

  1.    Mtu anapokuhamasisha kumtolea Mungu sadaka (kanisani), je, unafikiria tu kwamba wanataka fedha?

 

   1.    Ikiwa ndivyo, kwa nini wanataka fedha? (Lengo la fedha ni kununua mahitaji na kulipia huduma.)

 

   1.    Je, karama yako ya kutoa huduma itakuwa mbadala wa fedha? (Ikiwa lengo la fedha ni kulipia huduma, basi kutoa huduma hiyo ni njia fupi tu ya huo mchakato wa kutoa huduma.)

 

 1. Malipo

 

  1.    Soma Mathayo 6:2-4. Inamaanisha nini kwamba wale wanaotangaza karama zao “wamekwisha kupata thawabu yao kamili?”

 

   1.    Ikiwa hapa tutafuata anachokipendekeza Yesu, je, thawabu yetu kutoka kwake itakuwa ya siri? (Inaonekana ni vigumu kuamini kwamba itakuwa ni ya siri.)

 

  1.    Soma 2 Wakorintho 9:6. Kifungu hiki kinatoa ahadi gani kuhusiana na utoaji wetu? (Kwamba Mungu atatupatia thawabu. Ama tunapata thawabu ndogo (tunapokuwa wabahili) au tunapata thawabu kubwa (tunapokuwa wakarimu). Je, hii inafanya asili ya utoaji wetu iwe bayana kwa wote? Je, inaubainisha ukarimu wetu kwa watu?

 

   1.    Unaelezeaje tofauti kati ya mwelekeo wa “ifanye kuwa siri yako”, na “ahadi ya mtapokea thawabu kubwa?” (Ni Mungu, wala si wewe, aliye chanzo cha sifa.)

 

  1.    Soma 2 Wakorintho 9:7. Katika mfululizo wa masomo haya tumeangalia kama mfumo wa utoaji zaka wa Agano la Kale, pamoja na kauli zake za Malaki 3:8-9 kuhusu wizi na laana, bado unatumika kikamilifu. Kifungu hiki kinaashiria nini? (Muktadha mahsusi ni kuwasaidia washiriki wenzetu, na sio kuwasaidia viongozi wa kanisa, lakini Paulo anaonekana kuzungumzia kwa nguvu kabisa kuhusu utoaji – si kwa “kulazimishwa.”)

 

  1.    Soma 2 Wakorintho 9:8-9. Hapa ahadi ya “malipo” ni ipi? (Kwamba “katika mambo yote siku zote” tutapata “yote tunayoyahitaji.” Kupata kile tunachokihitaji kunatufanya “tujitoe kwa kila tendo jema.”)

 

  1.    Soma 2 Wakorintho 9:10-11. Ni kwa namna gani ukarimu utatutajirisha? “Mtatajirishwa katika vitu vyote.”)

 

   1.    Je, Mungu anazungumzia fedha au baraka za kiakili tu? (Kifungu kinazungumzia “mbegu kwa mwenye kupanda,” “mkate” na “mavuno.” Hizi ni baraka za wazi, halisi na zenye kugusika. Hizi ni sawa na fedha.)

 

   1.    Je, unalitilia hili mashaka? (Watu wengi wanakataa ahadi ya baraka za kifedha. “Injili ya mafanikio” ndio alama hasi katika jambo hili. Pamoja na hayo, tumesoma kwa kurudiarudia, katika Agano la Kale na Agano Jipya, ahadi za baraka za kifedha kwa watu wanaotoa zaka kwa uaminifu au kwa namna inayofanana na hiyo watu hao ni wakarimu kwa Mungu.)

 

   1.    Kwa nini upinzani kwa baraka za Mungu? (Watu wengine wanasema kuwa Yesu hakuwa tajiri. Pia hakuwa na mwonekano mzuri wa sura (Isaya 53:2). Kuwa maskini na kuwa na mwonekano wa kawaida ilikuwa hivyo ili kila mtu aweze kusema kuwa Yesu alipitia uzoefu wa “masikitiko/huzuni” ambazo ni za kawaida kwa wanadamu. (angalia Isaya 53:4.))

 

   1.    Je, tatizo ni kwamba kila mtu ambaye si tajiri anasema, “sidhani kama hii ni kweli – kutokana na uzoefu wangu?” (Kuna majibu mawili kwa swali hili. Kwanza, tunatakiwa kuwa waaminifu na wakweli kama kweli tumekuwa wakarimu kwa Mungu. Pili, kuwa “tajiri” ni neno lisiloweza kuhitimishwa kwa asilimia zote kwamba ni kweli au si kweli. Angalia jinsi unavyolinganishwa na mambo mengi ya hapa duniani.)

 

  1.    Rafiki, je, utajitoa kwa moyo na kuwa na bidii ya ibada kwa Mungu wako na kumtolea Mungu thawabu? Matokeo yake ni kwamba anakurejeshea mambo mengi! Kwa nini usimjaribu leo?

 

 1.   Juma lijalo: Wajibu wa Uwakili.