Wokovu na Wakati wa Mwisho

(Yohana 14, Warumi 10, Ufunuo 22)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
4

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Jambo gani linautofautisha Ukristo na mifumo mingine ya imani za kidini hapa duniani? Ni kwamba Wakristo wanaelewa kuwa wanaokolewa kwa imani pekee, na si kwa matendo yao. Mifumo ya dini nyingine inahusisha aina fulani hivi ya matendo ili “kutakasa” maisha yako au kumfurahisha mungu unayemtumikia. Ukristo wa kweli ni mgumu kwa watu wanaoishi kwenye utamaduni unaoamini kwamba bidii ya kazi itapata zawadi ya mafanikio. Unawezaje kuwa na falsafa ya kazi inayopingana sana na teolojia yako? Ni vigumu. Ndio maana Wakristo wengi sana wanamtumikia Shetani pasipo kujua pale wanapoandika makala zinazoashiria kwamba Wakristo wasiofikia viwango vigumu vya dini zao wamepotea. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze tofauti kati ya wokovu na mwenendo wa Kikristo kuuelekea utakatifu!

 

  1.    Njia Kuuelekea Wokovu

 

    1.    Soma Yohana 14:1-4. Endapo ungekuwa unamsikiliza Yesu, ungepaswa kujiuliza nini mara moja? (Kimsingi ningefanya uchunguzi ili kuhakikisha kuwa, ninafahamu “njia inayoelekea mahali” ambapo Yesu anakwenda.)

 

    1.    Soma Yohana 14:5. Unatoa alama ngapi kwa swali la Tomaso? (Ninampatia alama ya “A.” Umegundua kwamba mwanafunzi asiyejidai anauliza swali ambalo limo akilini mwa wanafunzi wote waliosalia?)

 

    1.    Soma Yohana 14:6. Tomaso anaamini kuwa jibu la swali lake linazungumzia mahali halisi. Hivyo ndivyo ambavyo ningehitimisha kama ningekuwa nimekaa pembeni mwa Tomaso. Yesu anasema kuwa “njia iendayo mahali ninapokwenda” ni ipi? (Si mahali, bali ni mtu. Njia ya kwenda mbinguni ni kupitia kwa Yesu.)

 

    1.    Soma Warumi 10:1-2. Je, Waisraeli hawa walikuwa na bidii ya kazi? (Ndiyo! Ungewaangalia na kusema kuwa “wako makini.” Wapo kwenye “njia sahihi.”)

 

      1.    Je, kuna ubaya wowote katika jambo hili? (Hawajaelimishwa kikamilifu. Hawazielewi njia za Mungu.)

 

    1.    Soma Warumi 10:3-4. Kuna kasoro gani kwenye maarifa ya hawa wafuasi wa Mungu wanaomfuata kwa moyo? (Wanadhani kuwa haki inatokana na matendo yao.)

 

      1.    Je, wao ni waasi kwa Mungu? (Ndiyo. Kwa namna ya kushangaza jinsi inavyoonekana, Biblia inatuambia kuwa “hawakujitia” chini ya “haki ya Mungu.”)

 

      1.    Je, kuishika sheria ndio njia ya kuifikia haki? (Hapana. Hii inasema kuwa “Kristo ni mwisho wa sheria,” hivyo hiyo haiwezi kuwa njia ya kuifikia haki. Badala yake, Biblia inasema kuwa “ili kila aaminiye ahesabiwe haki.” Imani kwa Yesu ndio njia ya kuifikia haki.)

 

    1.    Soma Warumi 10:9-11. Hii imani inayotuokoa inaelezewaje? (Unakiri kwamba Yesu ni Mungu. Unaamini kwamba kwa maisha, matendo na ufufuo wa Yesu unaokolewa. Kukiri huku na imani hii ndio njia ya kutufikisha mbinguni. Ukimtumaini Yesu kwa ajili ya wokovu wako, “kamwe hutatahayarika.”)

 

    1.    Hebu turejee nyuma na tusome kifungu tulichojifunza hivi karibuni. Soma ufunuo 22:12-15. Ni jambo gani ambalo wenye haki, wanaoshikilia tiketi ya kuingia mbinguni, wamelitenda? (Wamezifua nguo zao. Ufunuo 7:14 inadhihirisha kikamilifu kabisa maana ya jambo hili: “Wamefua mavai yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.” Waliyategemea maisha makamilifu na kifo cha upatanisho cha Yesu.)

 

      1.    Angalia tena Ufunuo 22:15. Waovu wamefanya nini? (Orodha kubwa ya dhambi.)

 

      1.    Je, wanaoshikilia tiketi ya kwenda mbinguni wametenda mambo hayo hayo? Je, mambo haya yanaweza kuwaelezea? (Kwa hakika hili halina maana kwa kuwa Biblia haisemi chochote. Hatujui dhambi mahsusi “zilizosafishwa” kwenye nguo za wenye haki. Tunaambiwa mambo mawili: matendo haya yanakustahilisha mauti ya milele. Kuyafua mavazi yako kwenye haki ya Yesu (bila kujali hali halisi ya nguo yako) hukupatia tiketi ya kwenda mbinguni. Waliookolewa wanaelewa na kulikubali jambo hili. Angalia Warumi 10:2-3.)

 

    1.    Soma Mathayo 7:21. Je, kifungu hiki kinatilia shaka uelewa wetu juu ya kile ambacho tumekuwa tukikisoma? (Inawezekana. Hivyo, tunatakiwa kukielewa.)

 

    1.    Soma Mathayo 7:22-23. Je, watu hawa, watakaozuiwa kuingia mbinguni, wote wataongea? (Hapana. Wamefanya kazi nzuri. Matendo haya ni ya kufurahisha zaidi kuliko matendo ya Wakristo wengi ninaowafahamu!)

 

      1.    Watu hawa waliopotea wangetakiwa kufanya nini? (Kumjua Yesu.)

 

      1.    Hebu tupitie mazungumzo ya Yesu na Tomaso. Soma tena Yohana 14:6-7. Tatizo la Tomaso ni lipi? (Hamjui Yesu. Haelewi kwamba “mtu haji kwa Baba ila kwa kupitia Mimi.” Huendi kwa Baba kutokana na matendo yako mazuri. Hiyo ndio sababu Yesu anawaambia wale wanaodai matendo yao (makuu) kama msingi wa wokovu, kwamba hawamjui Yesu. Hawaelewi kuwa njia ya kuupata wokovu inapitia kwa Yesu pekee.)

 

  1.   Kuielewa Njia Inayoelekea Kwenye Utakatifu

 

    1.    Hebu tuendelee na mazungumzo ya wanafunzi na Yesu. Soma Yohana 14:9-14. Hivi ni vifungu virefu kuvisoma, lakini nadhani tunatakiwa kusoma vifungu hivi pamoja ili kuyaelewa maelekezo ya Yesu. Lengo la miujiza aliyoitenda Yesu ni lipi? (Kutia msukumo imani kwamba Yesu ni Masihi, Mwana wa Mungu.)

 

      1.    Ikiwa miujiza hii inalenga kuthibitisha kwamba Yesu ni Masihi, kwa nini Yesu anasema kuwa wafuasi wake watatenda “mambo makubwa kuliko haya?” Je, tunawaonyesha watu kwamba sisi tu pamoja na Mungu? (Hiyo si maana yake. Kifungu cha 13 kinatuambia kuwa matokeo ya miujiza tunayoitenda ni ili “Baba” atukuzwe ndani ya “Mwana.”)

 

    1.    Soma Yohana 14:15. Unadhani kwa nini jambo hili ni kweli? Niliwapenda wazazi wangu, lakini wakati mwingine sikuwa nikiwatii. (Angalia muktadha. Yesu anajadili jinsi tunavyoweza kumpatia Mungu utukufu. Kuzitii amri za Mungu humpa Mungu utukufu. Kama unampenda Mungu, utapenda kumpa utukufu.)

 

    1.    Soma Yohana 14:16-17. Kwa nini Yesu anamzungumzia Roho Mtakatifu mara moja (immediately)? (Roho Mtakatifu ndiye anayetupatia utambuzi, mguso na uwezo wa kutii – kutenda kazi.)

 

    1.    Hebu turuke mafungu kadhaa ili tulifungamanishe jambo hili pamoja. Soma Yohana 14:26. Hii inaelezeaje wajibu wa Roho Mtakatifu maishani mwetu?

 

    1.    Soma Yohana 14:23-24. Jambo la thamani la ziada linalotokana na kumtii Mungu ni lipi? (Mungu atatupenda na kufanya makao yake pamoja nasi.)

 

      1.    Nilidhani kwamba Mungu anampenda kila mtu! Warumi 5:8 inasema kuwa Mungu aliwapenda sana “wadhambi” kiasi cha kuwafia. Unaielewaje Yohana 14:23? (Nadhani hii inamaanisha zaidi ya upendo wa jumla alionao Mungu kwa wadhambi wote. Hii inamaanisha kuwa Mungu atayabariki maisha yako kwa uwepo wake.)

 

      1.    Soma Zaburi 91:14-16. Hii inaongezea taarifa gani kwenye dhana ya kwamba uhusiano wetu wa upendo na Mungu huboresha maisha yetu?

 

    1.    Soma 1 Yohana 2:3-6. Unadhani kwa nini Yohana ametumia neno “kuenenda” kuelezea maisha ya mtu anayempenda Yesu? (Haya ni maisha yanayoendelea. Maisha ambayo unakua kuuelekea utakatifu.)

 

  1. Ihubiri!

 

    1.    Soma Ufunuo 14:6-7. Hii inasema kuwa jambo gani linapaswa kutendwa na “injili ya milele?” (Inapaswa kuhubiriwa kwa hao wakaao juu ya nchi.)

 

      1.    Malaika huyu anaielezeaje injili ya milele? (Kumcha na kumwabudu Mungu. Mungu Muumbaji ni Yesu. Yohana 1:1-5, 14.)

 

      1.    Malaika anatutaka tufanye jambo gani jingine? (“Tumpe Mungu utukufu.” Maisha yetu ya utii humpa Mungu utukufu.)

 

    1.    Soma Ufunuo 14:8. Waliopotea wanaelezewaje? (Wamekunywa “mvinyo’ wa uasherati – kukosa uaminifu kwa Mungu. Unaona jinsi huu ulivyo wito wa kufanya uchaguzi? Sio mjadala unaohusu endapo umetenda dhambi mahsusi. Msitari unaotenganisha wema na ubaya unahusiana na utiifu. Rejea mjadala wetu juu ya Warumi 10:9-10. Je, umemkiri Yesu kama Bwana na Mwokozi?)

 

    1.    Rafiki, elewa huu ujumbe vizuri. Unaokolewa kwa neema pekee – hakuna wokovu unaohusiana na matendo yako. Lakini, mara unapookolewa, ungependa kumpa Mungu utukufu kwa sababu unampenda. Unafanya hivyo kwa kuwa mtiifu. Jambo kubwa kuhusu utii ni kwamba unakubariki. Utii ni matokeo ya upendo wako kwa Mungu. Si ufunguo wa wokovu wako. Lakini, maisha yako yanapaswa kuakisi “mwenendo” wa utii mkubwa, mwenendo unaokuelekeza kwenye utakatifu! Je, unafahamu kwamba uhakika wa wokovu wako unategemea wewe kumpokea Yesu? Ikiwa ndivyo, tubu na umwamini Yesu sasa hivi! Kisha umwombe Roho Mtakatifu akusaidie uanze safari yako kuuelekea utakatifu.

 

  1.   Juma lijalo: Kristo Katika Patakatifu pa Mbinguni.