Mathayo 24 na 25

Swahili
(Mathayo 24)
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, ungependa kujua kuwa Yesu atakuja lini? Wanafunzi wa Yesu walitaka kujua! Tatizo lao ni kwamba hawakuwa wanasheria mahiri ambao wangeweza kuunda na kuuliza maswali ya wazi kuhusu wakati wa mwisho. Bila shaka Yesu alielewa mkanganyiko wao kuhusu ujio wake Mara ya Pili. Lakini, kwa sababu fulani fulani aliruhusu mkanganyiko wao uendelee kuwepo. Tatizo jingine la wanafunzi ni kwa wao kuwa na mawazo dhahania. Juma hili tunajifunza maoni ya Yesu kuhusu wakati wa mwisho ili tuone kile tunachoweza kukielewa. Tutaona kama tunaweza kuweka pembeni mawazo yetu dhahania. Hebu tuzame kwenye somo letu!

 

  1. Swali Lenye Mkanganyiko

 

A. Soma Mathayo 24:1-2. Jambo gani lingekuwa linaendelea mawazoni mwako endapo ungekuwa mmojawapo wa wanafunzi wa Yesu? (Hili lingekuwa janga la kutisha kuliko majanga yote ambayo wangeweza kuyafikiria. Taifa lao litaangamizwa. Mahali pao pazuri pa ibada pataharibiwa. Jambo hili liliwahi kutokea mara moja hapo kabla watu wa Babeli walipoiangamiza Yerusalemu. Kamwe maisha yao hayatakuwa kama yalivyokuwa hapo kabla.)

 

B. Soma Mathayo 24:3. Unalielewaje swali hili? Je, ni swali moja tu, au ni maswali mawili au zaidi? (Nina uhakika wanafunzi bado walikuwa na mshtuko, hivyo yumkini hawakuwa wakifikiri vizuri. Kiuhalisia haya ni maswali matatu: 1) Majengo ya hekalu yataharibiwa lini; 2) Ujio wa Yesu Mara ya Pili utatukia lini; na, 3) Mwisho wa dunia utakuwa lini? Kwa hili swali la mwisho, nadhani wanamaanisha mwisho wa ustaarabu.)

 

1. Je, haya maswali matatu tofauti yapo akilini mwako? (Nadhani yote ni maswali tofauti, lakini wanafunzi walidhani maswali yote matatu yalikuwa ni swali moja tu? Waliyaunganisha haya maswali matatu kuwa swali moja.)

 

II. Jibu

 

A. Soma Mathayo 24:4. Yesu anaonyesha kujali jambo gani? (Watadanganywa.)

 

1. Kwa nini Yesu hakusema, “Hebu subirini, mmeniuliza maswali matatu?”

 

2. Je, kukanganywa na kudanganywa kunafanana?

 

a. Kwa dhahiri Yesu aliwapenda. Unadhani kwa nini aliwajibu kama alivyojibu? (Kutokana na sababu fulani fulani Yesu hakutaka wawe na ubayana kamili kuhusu mustakabali wa siku zijazo. Wakati huo huo, hakutaka kutokuwa kwao bayana kuwafanye wadanganywe. Kutokana na hilo tunapaswa kuhitimisha kwamba maeneo ambayo Yesu anayaweka wazi ni ya muhimu sana kwetu kuyaelewa. Kwenye hayo maeneo asiyoyaweka bayana, ni muhimu kwetu kumtumaini.)

 

B. Soma Mathayo 24:5-8. Yesu anajibu swali gani hapa kati ya yale maswali matatu? (Kwa mahsusi anajibu kuhusu ujio wake Mara ya Pili na “wakati wa mwisho.” Hazungumzii kuhusu uharibifu wa Yerusalemu.)

 

C. Soma Mathayo 24:9-14. Vifungu hivi na vifungu vya awali vinasema kuwa jambo gani linahusishwa na ujio wa Yesu Mara ya Pili na wakati wa mwisho? (Makristo wa uongo, vita, njaa, matetemeko ya ardhi, mateso, vifo, chuki ya Wakristo, manabii wa uongo, kuongezeka kwa maovu na upendo kupungua. Injili itapelekwa ulimwenguni kote.)

 

1. Je, unayaona mambo haya duniani sasa hivi?

 

D. Soma Mathayo 24:15-20. Hapa Yesu anaelezea jambo gani? Anajibu swali gani? (Lazima hii itakuwa uharibifu wa Yerusalemu, kwa kuwa anafanya rejea ya eneo la kijiografia la Uyahudi.)

 

1. Angalia lugha iliyutumika kuhusu “chukizo la uharibifu.” Maneno hayo yanasema kuwa nani aliyetabiri hivi? (Danieli.)

 

a. Hebu tuchimbue baadhi ya vifungu kutoka kwenye kitabu cha Danieli. Soma Danieli 9:26-27. Je, hili ndilo chukizo lililotabiriwa linalosababisha uharibifu? (Inazungumzia “Mtiwa mafuta” “kukatiliwa mbali.” Inazungumzia “patakatifu” kuangamizwa. Haikuchukua muda mrefu sana baada ya Yesu kuteswa ambapo Rumi ililiangamiza hekalu mjini Yerusalemu kama alivyoonya Yesu. Unabii huu unakubaliana na utabiri.)

 

b. Soma Danielil 12:9-12. Hii ni rejea nyingine inayozungumzia chukizo linalosababisha uharibifu. Je, ni chukizo lile lile? (Lugha inaonekana kuzuia chukizo hili kuwa tukio lile lile kwani inazungumzia kipindi baada ya hekalu kuangamizwa na hivyo kukomeshwa kwa kafara ya kila siku.)

 

c. Kwa nini ni sawa kuliita jeshi la Rumi lenye ushindi kuwa “chukizo lililosababisha uharibufu?” (Liliangamiza jinsi ambavyo kihistoria watu wa Mungu walimjia Mungu ili dhambi zao ziweze kuondolewa.)

 

d. Hii inaashiria nini kuhusu chukizo la pili linalotokea baadaye? (Linaweza pia kuwa shambulio kwenye uwezo wetu wa kumwendea Mungu ili dhambi zetu ziweze kuondolewa.)

 

e. Hiyo inamaanisha nini baada ya kufufuka kwa Yesu? Hiyo inamaanisha nini kwetu leo? (Katika kipindi hicho na cha sasa hiyo inaashiria chukizo linalojaribu kuangamiza haki kwa njia ya imani.)

 

(1) Je, unaweza kufikiria nguvu inayoendana na maelezo hayo?

 

E. soma Mathayo 24:21-25. Swali gani linajibiwa hapa? (Rejea ya “dhiki kubwa” inaweza kuwazungumzia Wakristo waliokuwepo Yerusalemu wakati ilipoangamizwa. Utaona kwamba kifungu cha 21 kinaanza kwa kusema “Kwa kuwa,” inahusianisha dhiki hiyo na Uyahudi. Hata hivyo, dhiki inaweza pia kuzungumzia ujio wa Yesu Mara ya Pili. Angalia kauli ya “wakati huo,” inayohusishwa na makristo wa uongo. Kama tutakavyojadili katika sehemu inayofuata, hii ni rejea ya wazi ya ujio wa Mara ya Pili. Tunaambiwa kuwa hakuna wafuasi wowote waliohimili endapo Mungu asingeingilia kati.)

 

III. Maneno ya dhahiri

 

A. Soma Mathayo 24:26-27. Unawezaje kuelezea, katika hali chanya, ujio wa Yesu Mara ya Pili dhidi ya ujio wa uongo? (Ikiwa mtu atakutaarifu kuwa Yesu amekuja, basi huyo si Yesu!)

 

B. Soma Mathayo 24:28. Kwa nini Yesu anazungumzia tai? (Ukiwaona tai wanakusanyika angani, utajua kuwa kuna kitu kimekufa. Yesu anatuambia kwamba kuangalia juu kutatuepusha tusidananywe.)

 

C. Soma Mathayo 24:29. Je, hili ni tukio litakalotokea ulimwenguni kote? (Itakuwa hivyo, kutokana na muktadha uliotolewa. Ndio maana ninadhani baadhi ya mafundisho yaliyotolewa hapo awali na kanisa langu yalikuwa na kasoro pale yalipobainisha matukio yaliyotokea eneo la New England nchini Marekani kama utimilivu wa huu unabii.)

 

1. Unadhani inamaanishwa nini kwa maneno haya: “nguvu za mbinguni zitatikisika?” (Ufunuo 21:1 inatuambia kuwa mbingu ya kale itakoma na mbingu mpya itaundwa. Hii inaashiria kuwa uchanganuzi wa nguvu za mbinguni unaendelea. Hii inaleta mantiki kwa kuwa baadhi ya nyota zipo umbali mrefu sana. Gharika la kutisha linaendelea ulimwenguni.)

 

D. Soma Mathayo 24:30. “Ishara” ya Mwana wa Adamu ni ipi? Inatokea wapi? (Kwa mara nyingine, tunalo jambo linaloendelea angani kabla Yesu hajaja. Pasipo na shaka, jambo hili linavuta usikivu wa kila mtu.)

 

1. Yesu anakujaje? (Mawinguni na kwa nguvu na utukufu mwingi.)

 

 

2. Kwa nini mataifa yote “yataomboleza?” (Wenye haki hawaombolezi. Hii inatuambia kuwa watu wengi bado hawajampokea Yesu kama Mwokozi wao.)

 

E. Soma Mathayo 24:31. Wafuasi wa Yesu wanakaa wapi? (Wanaishi duniani kote. Huu ni uthibitisho zaidi kwamba hizi ishara za mbinguni si matukio ya kikanda.)

 

F. Soma Mathayo 24:32-35. Yesu anatuambia kuwa tunatakiwa kuwa makini na ishara hizi, na kwamba maneno yake ni ya kuaminika. Pia anasema kuwa kizazi hiki hakitapita. Tunapaswa kulielewaje jambo hili ikizingatiwa kuwa wasikilizaji wa Yesu walikufa miaka 2,000 iliyopita na Yesu hajarudi? (Kizazi kile hakikupita kabla Yerusalemu haijaangamizwa. Kimsingi swali lile ndilo swali la kwanza lililoulizwa na wanafunzi. Yumkini Yesu pia anasema kuwa kizazi kinachoona ishara hakitapita kabla hajarejea.)

 

G. Soma Mathayo 24:37-39. Je, huu ni ukweli wa kihistoria kwamba watu hawakujua chochote kuhusu ujio wa gharika? (Soma 2 Petro 2:5 na 1 Petro 3:19-20. Walifahamu kwamba Nuhu aliwaonya watu wakati alipokuwa akilijenga safina. Hivyo, lazima watu “wasiofahamu chochote” wawe wale wasiotamani kujua chochote.)

 

H. Soma Mathayo 24:42. Ukitafakari mambo yanayoonekana kuwa bayana na yale yasiyo bayana, unapaswa kuhitimisha nini kuhusu maandalizi yako ya nyakati za mwisho? (Ufinyu wetu wa kutoelewa mambo kwa ubayana unatushurutisha tuwe makini, kwamba tusalie kuwa waaminifu.)

 

I. Rafiki, je, utasalia kuwa mwaminifu? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, ili akusaidie uelewa wako wa matukio ya siku za mwisho, na akusaidie kusalia kuwa mwaminifu hadi katika kipindi hicho?

 

IV. Juma lijalo: Mwabudu Mwumbaji.