Mtakuwa Mashahidi Wangu

(Matendo 1)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
1

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, umewahi kukabiliana na hali ya wasiwasi mkubwa maishani mwako ambapo mtu fulani alikuangusha? Ulikuwa na mpango fulani kwa ajili ya siku zijazo, lakini ghafla mipango yako yote ikabadilika. Je, unaukumbuka msukosuko uliokutinga mawazoni mwako? Hukujua uamini nini na hukujua mustakabali wako. Nadhani hapo ndipo tunapokutana na wanafunzi katika somo hili. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 1.    Mtazamo Potofu

 

  1.    Soma Marko 10:35-36. Je, mtu amewahi kukwambia kuwa, “Utanitendea jambo fulani?” au “Una nafasi siku ya Jumanne usiku?” Je, unayajibu maswali hayo, au badala yake unauliza swali lako mwenyewe: “Kwa nini?” (Ninafahamu maswali hayo kwa kiwango kikubwa huwa yanataabisha, hivyo siyajibu isipokuwa tu kama nimegundua wanachokiwaza. Tunaona kwamba Yesu pia anachukua tahadhari.)

 

  1.    Soma Marko 10:37-39. Yesu anawaambia kuwa hawajui wanachokiomba. Hii ni kweli pasipo na shaka yoyote. Unadhani kwa nini waliamini kile walichokiomba? (Walizungumzia “utukufu.” Walidhani Yesu atakuwa Mfalme na walitaka kuwa na nafasi za juu kwenye ufalme wake hapa duniani.)

 

  1.    Soma Matendo 1:6-7. Je, Yakobo na Yohana ndio wanafunzi pekee wanaodhani kuwa Yesu “ataurejesha ufalme Israeli?” (Hapana! Hata katika hizi nyakati za mwisho, muda mfupi kabla ya Yesu kurudi mbinguni, bado wanafunzi wana mtazamo potofu juu ya mustakabali wao.)

 

  1.    Soma Matendo 1:4-5 na Marko 10:32-34. Hiki ndicho alichokisema Yesu kabla Yakobo na Yohana hawajauliza swali lao na wanafunzi hawajauliza swali lao. Unaelezeaje kushindwa kwao kuwa makini? (Wangepaswa kujikita kwenye ujio wa Roho Mtakatifu au ukweli ambao Yesu ameusema, kwamba anakaribia kuuawa. Badala yake, walizingatia kile walichotaka kitokee, na inaonekana hawakuzingatia kile ambacho kimsingi Yesu alikisema.)

 

 1.   Mtazamo Sahihi

 

  1.    Soma Matendo 1:8-9. Yesu alikuwa na mustakabali gani kwa ajili ya wanafunzi? (Watakuwa mashahidi duniani, na si watawala.)

 

   1.    Kama ungekuwa mwanafunzi, ungefanyaje kwenye hayo mabadiliko ya mipango?

 

   1.    Yesu anaweka mpango gani wa jumla kwa ajili ya kushuhudia? (Mahala pao pa kushuhudia palikuwa pakubwa sana, kiasi cha kujumuisha ulimwengu wote.)

 

   1.    Wanafunzi walipouliza kuhusu kurejesha “Ufalme kwa Yerusalemu,” unadhani walimaanisha Israele pekee, au kwamba Israeli itautawala ulimwengu?

 

  1.    Soma Matendo 1:10-11. Wanafunzi walikuwa wanafikiria nini Yesu alipopaa kwenda mbinguni?

 

   1.    Walikuwa na mawazo gani malaika walipowaambia kuwa Yesu atarejea?

 

  1.    Soma Luka 24:44-52. Huu ni mwonekano mwingine wakati Yesu aliporejea mbinguni. Inataarifiwa kuwa wanafunzi walijawa “furaha kuu.” Hilo lilitokeaje, tukichukulia kwamba muda mfupi hapo kabla walikuwa wamechanganyikiwa kuhusu mustakabali wao?

 

   1.    Kitendo hicho kilitokeaje wakati nina uhakika lazima walikuwa wamesikitika sana kwa kutokuwa watawala hapa duniani? (Sina uhakika kama walielewa kikamilifu, ila nafikiri walidhani kuwa ikiwa walitimiza malengo yao ya kushuhudia, Yesu angerudi na kuusimika Ufalme wake. Hilo liliwapatia furaha. Ilikuwa tu ni furaha iliyocheleweshwa.)

 

 1. Ulimwengu Halisi

 

  1.    Soma Matendo 1:12-14. Ikiwa maisha yanakwenda mrama, au ikiwa unachanganyikiwa kuhusu mustakabali wako, unapaswa kufanya nini? (Sali! Hicho ndicho walichokifanya wanafunzi na marafiki wa karibu wa Yesu pamoja na familia yake.)

 

  1.    Soma Matendo 1:15-17. Tafakari maneno ya Petro. Hebu niambie, unadhani mada ya maombi katika chumba cha orofani ilikuwa ni ipi? (Petro anazungumzia Maandiko na unabii. Anazungumza kuhusu Roho Mtakatifu. Nadhani walikuwa wanapitia unabii kumhusu Yesu, na kuomba mwongozo wa Roho Mtakatifu. Bila shaka ndio maana walitaka kufahamu walikosea mahala gani katika mipango yao ijayo. Bila shaka anguko la Yuda lilikuwa ni onyo makini kuhusu kukosa kuuzingatia mpango wa Mungu.)

 

  1.    Soma Matendo 1:18-20. Biblia inatoa mwongozo gani kuhusu uongozi ujao? (Inasema kuwa mtu fulani anapaswa kuchukua nafasi ya Yuda.)

 

  1.    Soma Matendo 1:21-22. Mwanafunzi wa kuchukua nafasi ya Yuda anapaswa kuwa na vigezo gani? (Mtu ambaye ni shahidi wa kazi yote ya utume wa Yesu, ikiwemo kufufuka kwake.)

 

   1.    Tafakari jambo hili. Kwa nini hiki ndio kile walichokihitaji kwa mwanafunzi mbadala? (Hii inaonesha wamepata maono sahihi kwa ajili ya mustakabali wao. Wanamtafuta shahidi, sio kiongozi wa kisiasa. Sasa wanauelewa mustakabali wao hapa duniani.)

 

  1.    Soma Matendo 1:23-26. Kwa nini Roho Mtakatifu anatakiwa kuchagua kati ya watu wawili ambao hapo awali walikuwa wamechaguliwa na kundi la waumini?

 

   1.    Kwa nini wasimwache Roho Mtakatifu afanye uchaguzi kutoka miongoni mwa waumini wote 120?

 

   1.    Bado baadhi ya makanisa yanawachagua viongozi kwa njia hii. Kwa nini isiwe kwa makanisa yote?

 

   1.    Hii inatufundisha nini kuhusu kufanya uamuzi maishani mwetu? (Tunaona kwamba katika taswira pana, tunaweza kukosea – na Mungu ataturekebisha. Lakini, pia tunaona kipengele kikubwa cha uamuzi na uchaguzi wa kibinadamu. Tunachokiona hapa ni mpango wa pamoja kati ya Roho Mtakatifu na wanadamu.)

 

  1.    Soma Matendo 13:1-3. Kwa nini Roho Mtakatifu anafanya uchaguzi wa upande mmoja hapa?

 

  1.    Soma Matendo 16:6-10. Hapa tunamwona Roho Mtakatifu akimzuia Paulo kivitendo (inaonekana hivyo) asihubiri katika maeneo fulani. Kwa nini asifanye uamuzi wa pamoja na Paulo?

 

   1.    Matendo 16:10 inaposema kuwa Paulo na wainjilisti wenzake walikuwa “wanahitimisha” kwamba Mungu aliwaita wakahubiri Makedonia, hiyo inazungumzia nini kuhusu uhakika wa uamuzi wao? (Hii inafanana sana nasi. Hatuna uhakika wa nini cha kufanya. Tunataka kuyafanya mapenzi ya Mungu. Baadhi ya njia tunazotaka kupita zimezibwa, lakini hatimaye tunaona ishara kwamba tunapaswa kupita kwenye njia fulani. “Tunahitimisha,” kwa kadri tuwezavyo, kile ambacho Mungu anakitaka. Hatuna uhakika tutakaokuwa nao na mambo ya Mungu au Roho Mtakatifu kutupatia ujumbe maalum.)

 

  1.    Vifungu hivi vinatupatia mwongozo gani katika suala la kuchagua viongozi wa kanisa na kuweka mipango ya baadaye kwa ajili ya kanisa? (Ikiwa tunamtazamia Mungu, ataongoza mipango yetu. Ni sawa kwetu, kutokana na maombi na mantiki ya kawaida, kuweka mipango. Lakini, tunatakiwa kumkaribisha Roho Mtakatifu kufanya mabadiliko madogo au makubwa kwenye mipango yetu ili kuutangaza Ufalme wa Mungu.)

 

  1.    Rafiki, je, unasikitika juu ya mustakabali wako? Je, mipango yako haikufanya kazi kama ulivyotarajia? Je, uliomba na kumkaribisha Roho Mtakatifu ili auongoze mustakabali wako? Ikiwa ulifanya hivyo, basi unapaswa kuanza na kile unachodhani kuwa unapaswa kukifanya, na umtafute Roho Mtakatifu ayaongoze mapito yako.

 

 1.   Juma lijalo: Pentekoste.